T

taifaleo.nation.co.ke

@taifaleo Wed, 22 Jul 2026 02:55:12

Ujuzi wake wa uchinjaji kuku kwa ubora wa juu umemdumishia soko tangu enzi za Corona

USTAHIMILIVU, ujuzi wa kuchinja na ukwasi wa kutambua hitaji la soko zimekuwa silaha kibindoni iliyomwezesha Douglas Sobera, 34, kubadili changamoto ya janga la Corona kuwa biashara ya mamilioni ya pesa mjini Kisii. Sobera ni mmiliki wa Maa Chicken, buchari inayochinja na kusambaza kuku kwa zaidi ya asilimia 80 ya hoteli kubwa na mikahawa mjini Kisii na viunga vyake. Yeye si mgeni kwenye tasnia ya nyama ya kuku. Alipata uzoefu wa miaka mitano kama mfanyakazi wa Quality Meat Packers (QMP) — kampuni ya kibinafsi humu nchini ya kuchinja na kusaga nyama. Akiishi Kajiado, mwaka 2019 alianzisha mradi mdogo wa kununua kuku kutoka kwa wafugaji na kuwauza kwa QMP. Wakati huo biashara ilikuwa ikinawiri. Lakini mwaka 2020 janga la Covid-19 lilipoteka ulimwengu mzima hoteli nyingi zilifungwa, QMP ikapunguza ununuzi kwa asilimia 70, na Sobero akalia na kuku zaidi ya 400 asijue la kufanya. Baada ya kutafiti soko alirejea nyumbani Kisii mwisho wa 2021. Aliona fursa na akaidandia, kama anavyoeleza: "Wakazi wa Kisii wanapenda sherehe kila wikendi. Hoteli zinajaa, lakini hakuna msambazaji wa kuku aliye na viwango vya ubora kama vya QMP. Niliona pengo na nikaja kulijaza." Februari 2022 alifungua buchari yake ya Maa Chicken katika soko la Marikiti mjini Kisii. Duka hilo liko katika kiingilio cha nyuma cha jumba la Uhuru Plaza ambalo ni maarufu sana katika mji huo. Maa ni jina la Kimaasai. Kwa kuwa Sobera alianza kazi yake ya uuzaji nyama ya kuku katika himaya ya jamii ya Maasai huko Kajiado, aliamua kuita biashara yake jina hilo kama njia ya kuweka kumbukizi alikoanzia. Leo hii Maa Chicken ni kitovu cha kuku Kisii. Mauzo ya wastani ni kuku 100 kwa siku, sawa na kilo 180-200 ambapo bei ni Sh420 kwa kilo. Haya ni mapato ya takriban Sh 75,600 kwa siku au Sh 2.2 milioni kwa mwezi. Maa Chicken huuza aina zote za nyama ya kuku: waliofugwa mahususi kwa nyama yao maarufu broila, ambao huuzia hoteli za bei nafuu; kienyeji walioimarishwa, ambao huuzia wateja wa kati; na kienyeji halisi, ambao huuzia hoteli za kifahari na kwa mteja anayetaka kwa ajili ya kupika kitoweo. Huduma ni kulingana na mteja: kuku mzima, au vipande vyake — paja, mbawa, kidari, maini, firigisi na sehemu zinginezo. Kila kitu hupimwa kutumia mizani ya kidijitali mbele ya mteja. "Hatuuzi kwa kubahatisha. Hoteli ikitaka nyama ya broila isiyo na mfupa kilo 20 saa kumi na mbili asubuhi, ni lazima zifike. Kuchelewa ni kupoteza mteja!"anasisitiza Sobera. Ili kuhakikisha hakosi kuku amejenga ushirikiano na wafugaji zaidi ya 30 wa kudumu kutoka Bonchari, Kitutu Chache, na Nyaribari. Anawalipa kwa bei nzuri papo hapo. "Uaminifu ni mtaji. Mfugaji akijua analipwa leo, hata mvua ikinyesha ataleta kuku," Sobera aongeza. Biashara yake imeajiri vijana 10 moja kwa moja: kuna wachinjaji, wasafirishaji wanaotumia pikipiki ili kufikia wateja chapchap, wauzaji na wasimamizi. Kwa kutumia ujuzi na desturi za ubora za QMP, Maa Chicken imeweka viwango vya juu vya usafi. Kuku huchinjwa na kusafirishwa hadi kwa mteja wakiwa freshi. Wafanyakazi huvalia magwanda na kofia spesheli zinazotumika ndani ya chumba cha kichinjio pekee. Nazo sakafu, meza na vifaa vingine vya matumizi husafishwa kila saa. Ana majokufu makubwa matatu ambayo humsaidia kuhifadhi nyama kwa nyuzi hasi 18 (yaani -18°C) ikisubiri wanunuzi. "Afisa wa afya akipita hapa hawezi kutufungia duka. Ndio maana hoteli za Daraja Mbili, Mwembe, Getare zinatuamini," anadeka Sobera. Kama wafugaji wengine wa kuku Sobera analia kuhusu gharama ya juu ya lishe ambayo imefanya wakuzaji wasizalishe mifugo hao kwa wingi. "Bei ya chakula cha kuku imepanda kwa asilimia 22 mwaka huu na kutupunguzia faida. Barabara duni za mashambani pia ni tatizo wakati wa masika," aliongeza. Sobera analenga kufungua matawi katika miji ya Nyamira na Migori kabla ya 2028, na kuweka bidhaa zake za Maa Chicken kwenye maduka ya jumla. "Corona ilinifukuza Kajiado, lakini Kisii imenipa ufalme. Kijana usiseme hakuna kazi - tafuta ujuzi, tafuta pengo, kisha ingia kwa hatua moja na uendelee kupiga ingine kwa ingine," anahitimisha.

read more
T

taifaleo.nation.co.ke

@taifaleo Wed, 22 Jul 2026 01:55:57

Stroberi za 'chandler' ni tamu pia kwa upande wa hela

MURAYA Mburu alipoacha kufanya kazi katika Kampuni ya Huduma za Maji na Usafi ya Nakuru (NAWASSCO) mwaka 2012 alijitosa katika kilimo shambani mwake Nyakiambi mjini Elburgon, Kaunti ya Nakuru. Tulipomtembelea majuzi tulimpata katika pilkapilka za kuvuna na kupakia mavuno ya matunda ya stroberi kwa ajili ya kuyauza. "Baada ya kuzalisha mahindi kwa miaka mitano nilififia kwani kilimo hicho hakikuwa kikienda vizuri. Baada ya kuuza mahindi makavu niliyokuwa nayo nilinunua kondoo dume 12 kwa kati ya Sh3,000 na Sh 5,000 kila mmoja kulingana na saizi. Nikawalea kwa mwaka mmoja kabla kuwauza Sh9,000 kila moja," alitanguliza Muraya kuhusu safari yake ndefu ya kilimo na ufugaji. Akapata ugumu kulea kondoo zaidi kutokana na uhaba wa malisho. [caption id="attachment_190380" align="alignnone" width="2560"] Muraya Mburu aonyesha stroberi alizopakia katika vikontena tayari kuuzwa, katika shamba Nyakiambi mjini Elburgon, Nakuru, wiki chache zilizopita. PICHA| JOHN NJOROGE[/caption] Ni wakati akikuna kichwa alipokumbuka makala katika chapisho la awali la Akili Mali, jinsi wakulima walikuwa wakistawi kwa kuuza bidhaa zao mtandaoni. Pitapita zake zikampeleka kwa kilimo cha stroberi. Akabaini ni rahisi kuanzisha, hakikuwa na kazi nyingi, na matunda yalichukua miezi michache kukomaa, tofauti na mahindi ambayo huchukua karibu mwaka mzima. Pia aligundua mauzo ya stroberi yalikuwa mazuri hata katika soko la mashinani. Muraya akafuatilia wakulima wa matunda hayo na kutembelea baadhi waliochapisha bidhaa zao mtandaoni. Ni kutoka kwa mmoja alijifunza kuhusu aina za stroberi zilizofaa maeneo mbalimbali. "Mnamo 2019 nilitembelea mkulima mjini Nyahururu, Kaunti ya Laikipia, nikanunua miche 800 kabla baadaye kuongeza 800 zaidi, kila moja ikiwa Sh30, kutoka kwa mtaji wa Sh120,000 niliokuwa nao," asema na kuongeza kuwa alihakikishiwa miche hiyo ilikuwa bora na ingenawiri eneo lake. Alitumia pesa zilizobaki kununua matangi ya maji, mabomba, kutayarish shamba, na nyavu ili kuepusha ndege wasifikie matunda shambani. Baada ya kukuza miche kwa mwezi mmoja aliipandikiza katika shamba lake la nusu robo. "Kwa kuwa sikuwa na mbolea ya kinyesi cha kondoo, ambayo ilikuwa bora kuchanganya na udongo wakati wa kupanda, niliweka ile ya kutokana na kinyesi cha ng'ombe baada ya wiki tatu," aeleza. Aliendelea kumwaga maji kwa miche hiyo kila asubuhi na jioni hasa wakati hakuna mvua, lakini baada ya miezi miwili alikuwa akitia maji mara mbili pekee kila wiki. Muraya anasema spishi ya chandler ambayo ndiyo anakuza katika shamba lake hustahimili hali ya anga ya eneo la Elburgon na Molo, ambayo mara nyingi ni baridi na mvua. Hata hivyo, atahadharisha kuwa mvua nyingi ni tatizo kwani matunda hupenda kiangazi wakati wa kukomaa. "Ningeomba serikali ya kaunti iimarishe mafunzo kwa wakulima kuhusu upanzi na soko la stroberi ili wapate mapato mazuri. Matunda haya ni matamu na utamu huo umefanya wateja kuongezeka, ikiwemo wakulima wanaonunua miche kwa upanzi," aeleza. Ni ombi ambalo Waziri wa Kilimo wa Kaunti ya Nakuru Leonard Bor, amelisikia kwani anasema maafisa wa kilimo nyanjani wako tayari kufika kokote katika kaunti ili kuhamasisha wakulima kuhusu masuala mbalimbali ikiwemo mifumo faafu ya kilimo, maradhi ya mimea, kudhibiti wadudu waharibifu na kadhalika. "Kama serikali ya kaunti tutaimarisha mipango ya kuhamasisha na kuwafikia wakulima wengi hususan siku za kilimo au kuwatembelea mashambani mwao ili kuendelea kufanikisha kilimo," alisema Bor na kuongeza kuwa wakulima pia huarifiwa wakati wa siku za kilimo kupitia ofisi za chifu katika maeneo yao. Muraya anahoji kwamba soko la matunda limeongezeka pakubwa katika maeneo ya Molo, Elburgon na Kuresoi tangu janga la corona kutokana na himizo la wataalamu wa afya kwamba matunda yana virutubishi ambavyo huimarisha kingamwili, na hivyo kusaidia kupambana na homa hiyo. Mavuno yake ya kwanza yalikuwa ya kuridhisha, lakini mwanzoni alipata changamoto kuyauza katika soko la mashinani kwani stroberi bado zilikuwa hazijachangamkiwa sana. Akaanza kupakia katika vikontena vidogo vya plastiki vya kuweka vyakula kavu [punnets kwa Kimombo] kwa wateja wa mijini na baadaye maduka makubwa ya jumla. Hata hivyo, aliendelea kuuza matunda yake reja reja kwa kutembea kutoka sehemu moja hadi nyingine kutokana kwamba baadhi ya wateja na maduka hayakuwa na friji za kuhifadhi matunda hayo katika vikontena. Sasa anafurahia matunda ya bidii yake kwani soko lake limeendelea kunawiri katika mji wa Elburgon na viunga vyake. Mkulima huyu hana majuto tangu alipozamia kilimo cha stroberi miaka saba iliyopita kwani amefanikiwa kumudu karo ya shule ya watoto wake na kukidhi mahitaji mengine ya kimsingi nyumbani. "Msimu mzuri ninavuna mara mbili kwa wiki, kati ya paneti 40 na 60 na kuuza kila kifurushi Sh150," alisema Muraya na kuongeza kuwa mpango wake ni kufuga kondoo ambao watamsaidia kupata mbolea asilia, ambayo ndiyo yeye hutumia shambani. Aidha, maono yake katika siku zijazo ni kupanua shamba hadi ekari tano akitumai soko la stroberi litaendelea kunawiri eneo hilo na kote nchini.

read more
T

taifaleo.nation.co.ke

@taifaleo Wed, 22 Jul 2026 00:55:35

Mwanamume aliyepatwa amemeza mihadarati alazimishwa kuitema

POLISI katika Kaunti ya Mombasa wanamzuilia mwanamume aliyepatikana amemeza madonge ya dawa za kulevya, akilenga kuyasafirisha hadi Dubai yakiwa ndani ya mwili wake. Mnamo Julai 15, wakati wasafiri wakisubiri kuabiri ndege ya saa saba mchana kutoka Mombasa kuelekea Dubai, wapelelezi katika Uwanja wa Kimataifa wa Moi jijini Mombasa walikuwa wakimfuatilia mwanamume huyo mwenye umri wa miaka 67. Taarifa za kijasusi zilikuwa zimemhusisha na mtandao wa kimataifa wa biashara ya dawa za kulevya, huku wachunguzi wakishuku kwamba alikuwa ameficha kokeini ndani ya mwili wake. Wapelelezi kutoka Kitengo cha Kupambana na Dawa za Kulevya cha Idara ya Kuchunguza Uhalifu (DCI), wakishirikiana na maafisa wa usalama wa uwanja huo wa ndege, walimkamata kabla ya kuabiri ndege. Operesheni hiyo baadaye ilihusishwa na mtandao wa kimataifa wa biashara ya dawa za kulevya ambao umekuwa ukichunguzwa kwa miezi kadhaa. [caption id="attachment_190364" align="alignnone" width="2560"] Polisi wapata mihadarati kutoka kwa msafiri mmoja aliyekuwa anaelekea Dubai Picha|Kevin Odit[/caption] Walanguzi hao wa kimataifa hutumia Mombasa kama kituo cha kupitisha dawa za kulevya kuelekea nchi nyingine za nje. Mshukiwa alikamatwa na kupelekwa katika kituo maalumu cha kutengwa kwa ajili ya uangalizi wa kimatibabu. Baadaye alipelekwa katika Hospitali ya Port Reitz, ambapo madaktari na wahudumu wa afya walimweka chini ya uangalizi wa karibu ili kusaidia kutoa dawa hizo alizokuwa amemeza kwa njia salama. Polisi walisema wataalamu wa matibabu walifanikiwa kutoa vidonge 44 vilivyofunikwa kutoka tumboni mwake kwa njia iliyolenga kuvizuia kupasuka. "Dawa hizo za kulevya zitatumika kama vielelezo mahakamani," alisema Kamanda wa Polisi wa eneo la Pwani Ali Nuno. Kulingana na wachunguzi, kumeza dawa za kulevya ili kukwepa ukaguzi wa usalama ni mojawapo ya njia hatari zaidi za kusafirisha dawa hizo, kwa sababu vikipasuka ndani ya mwili vinaweza kusababisha maafa. Polisi walifichua kwamba kukamatwa kwa mwanamume huyo kulitokana na operesheni inayoendelea ambayo hadi sasa imesababisha kukamatwa kwa washukiwa wengine kadhaa, wakiwemo wanaodaiwa kuwa walanguzi wakuu wa dawa za kulevya. Kwa jumla, dawa za kulevya zenye thamani ya karibu Sh151 milioni zimepatikana na polisi katika kipindi cha karibu miezi minne iliyopita. Operesheni hiyo pia ilifanikisha kukamatwa kwa mshukiwa mwingine ambaye wapelelezi wanaamini alikuwa kinara wa biashara hiyo haramu. Wakati wakiendeleza uchunguzi, maafisa walivamia nyumba iliyoshukiwa kutumiwa kama maficho na kituo cha muda cha kuwahifadhi wasafirishaji wa dawa za kulevya. Upekuzi huo ulisababisha kupatikana kwa vipande vingine 16 vinavyodhaniwa kuwa na kokeini. Uchunguzi unaendelea kubaini ukubwa kamili wa mtandao huo na kuwatambua washukiwa wengine. Takwimu zilizotolewa na Kitengo cha Kupambana na Dawa za Kulevya cha DCI zinaonyesha kwamba wapelelezi wamekamata kilo 37 za heroini zenye thamani ya takriban Sh111.846 milioni katika miezi minne iliyopita. Pia wamekamata gramu 1,336 za kokeini zenye thamani ya takriban Sh5.344 milioni. "Jumla ya watu tuliowakamata kuhusiana na dawa za kulevya ni washukiwa 27. Kati yao, watano ni wafanyabiashara wakubwa wa dawa za kulevya bila shaka yoyote, 10 ni wasafirishaji na 12 ni wauzaji," alisema Bw Nuno. Ripoti hiyo pia inaonyesha kwamba maafisa walikamata gramu 204 za methamphetamine, inayofahamika zaidi kama meth, yenye thamani ya takriban Sh1.632 milioni katika operesheni zilizofanywa katika kipindi cha miezi minne iliyopita. Bangi bado ndiyo dawa ya kulevya inayokamatwa zaidi katika eneo hilo, polisi wakiripoti kukamata kilo 10,747.84 zenye thamani ya takriban Sh32.243 milioni katika kipindi hicho. Kwa jumla, thamani ya dawa zote za kulevya zilizokamatwa katika operesheni za kupambana na biashara hiyo katika eneo la Pwani ni takriban Sh151.065 milioni.

read more