taifaleo.nation.co.ke
@taifaleo Mon, 09 Nov 2026 04:55:01
UN yatenga Sh387m kusaidia wakimbizi wanaoendelea kutorokea Kenya mpakani Moyale
AFISI ya Umoja wa Mataifa ya Kuratibu Masuala ya Kibinadamu (UNOCHA) imetenga zaidi ya Sh387 milioni kusaidia maelfu ya watu waliokimbia makazi yao kutokana na mapigano nchini Ethiopia. Naibu Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa anayeshughulikia masuala ya kibinadamu, Tom Fletcher, alisema fedha hizo zitatumika kutoa chakula, maji, makazi na huduma za afya kwa waathiriwa. Fedha hizo zimetolewa kupitia Hazina ya Umoja wa Mataifa ya Kukabiliana na Dharura (CERF) na zinalenga kuwafikia zaidi ya watu 50,000 waliovuka mpaka kuingia Kenya. Ufadhili huo unakuja siku chache baada ya mashirika ya UN kutoa ombi la Sh1.16 bilioni kusaidia waathiriwa wa mapigano hayo. Ripoti ya UNOCHA inaonyesha kuwa wanawake na watoto ndio wengi miongoni mwa waliowasili, pamoja na wazee na watu wenye ulemavu. "Wengi walikuwa wamejisitiri katika majengo ya umma, maeneo ya wazi na kando ya barabara, hali iliyoongeza hatari za kiusalama na kiafya. Watu wenye magonjwa sugu pia walikuwa katika hatari ya kukosa dawa muhimu," inasema ripoti hiyo. Inaongeza kuwa jamii zinazowazunguka wakimbizi zimeendelea kuwasaidia, lakini ongezeko la idadi yao linaweka shinikizo kwa huduma za kijamii na linaweza kusababisha mivutano kutokana na uhaba wa rasilimali. Ripoti hiyo inataja maji, vyoo na huduma za usafi kuwa miongoni mwa mahitaji ya dharura katika kambi saba zinazohifadhi wakimbizi. "Inakadiriwa kuwa vyoo vingine 410 vinahitajika katika maeneo manne, vikiwemo 342 kambini. Mahitaji mengine ni pamoja na kusambaza maji kwa magari, vifaa vya kunawia mikono na matangi ya kuhifadhi maji," inasema ripoti hiyo. Katika eneo la Arosa pekee, lita 19,650 za maji zinahitajika kila siku, huku familia 9,768 zikihitaji msaada wa chakula na lishe. UNOCHA pia imetaja watu 313 waliokimbia makazi yao katika Kaunti ya Mandera kuwa wanahitaji msaada wa kibinadamu. Nchini Ethiopia, mapigano hayo yamesababisha kufungwa kwa shule 200. Shirika la Msalaba Mwekundu la Ethiopia (ERCS) linasema zaidi ya watu 200,000 wamehama makazi yao katika Moyale na maeneo jirani. "Limetoa msaada wa makazi ya dharura na vifaa visivyo vya chakula vyenye thamani ya takriban Sh24 milioni kwa familia 1,000 zilizoathiriwa na mapigano ya hivi majuzi katika mji wa Moyale na maeneo yanayouzunguka." Ikasema shirika hilo kwenye taarifa yake. Hapa nchini, Shirika la Msalaba Mwekundu na mashirika mengine yamewafikia zaidi ya watu 13,000 kwa kuwapa chakula na huduma za afya katika siku 18 zilizopita. Wakati huohuo, Ubalozi wa Uingereza Ijumaa ulitoa tahadhari kwa raia wake dhidi ya kufanya safari zisizo za lazima kuenda Moyale kutokana na mapigano kati ya vikosi vya maeneo ya Oromia na Somali.
read moretaifaleo.nation.co.ke
@taifaleo Mon, 09 Nov 2026 05:55:50
Kunaswa kwa mihadarati ya Sh3.6 bilioni kwaibua hofu ya Kenya kuwa kitovu cha ulanguzi
POLISI wamegundua mtandao unaoshukiwa kujihusisha na ulanguzi wa mihadarati kimataifa kupitia mpaka wa Kenya na Tanzania. Hii ni baada ya mshukiwa aliyekamatwa nchini Tanzania kuwaongoza wapelelezi wa Kenya hadi kwenye shehena ya mihadarati yenye thamani ya Sh3.6 bilioni katika Kaunti ya Kwale. Mkurugenzi wa Idara ya Kuchunguza Uhalifu (DCI), Bw Mohamed Amin, alithibitisha kukamatwa kwa washukiwa watatu katika operesheni ya pamoja ya mashirika mbalimbali ya usalama. Operesheni hiyo ilisababisha kupatikana kwa kilo 454 za dawa za kulevya katika eneo la Msambweni. Washukiwa hao watatu, ambao ni raia wawili wa Tanzania na mwanamke mmoja raia wa Uganda, wanazuiliwa na polisi wakisubiri kufikishwa mahakamani. Duru zilisema mihadarati hiyo inashukiwa kuwa methamphetamine, huku uchunguzi wa kuthibitisha ukisubiriwa. Operesheni hiyo, iliyoanza kwa kukamatwa kwa mshukiwa mmoja nchini Tanzania Novemba 5, ilifichua watu wengine wanaoshukiwa kuhusika katika biashara hiyo katika vijiji viwili vya Kwale. Kwa mujibu wa DCI, maafisa wa Tanzania walimkamata mshukiwa wa kwanza akiwa na kilo 259 za mihadarati katika shehena tofauti, inayoshukiwa kuwa ni methamphetamine na kokeni, kabla ya kumkabidhi kwa maafisa wa Kenya katika kituo cha mpakani cha Lunga Lunga-Horohoro. Wapelelezi walisema mshukiwa huyo aliwaongoza maafisa hadi Kijiji cha Shirazi, katika eneo la Kingwede Shirazi, ambako walipata makazi ya mshukiwa wa pili. Baada ya mahojiano zaidi na ufuatiliaji, kikosi hicho kilielekea Kijiji cha Ganja La Simba, katika eneo la Kinondo, ambako maafisa walipata kilo 454 za mihadarati na kumkamata mshukiwa wa tatu. Vijiji hivyo viwili viko karibu na Bahari Hindi, hali inayofanya wapelelezi kushuku uwezekano kuwa ulanguzi ulifanywa kwa boti au dau lililodhaniwa kuwa la uvuvi. Magari mawili na pikipiki moja pia zilikamatwa katika operesheni hiyo, ambayo DCI imesema bado inaendelea. DCI imesema operesheni hiyo inaonyesha umuhimu wa ushirikiano wa kushiriki taarifa za ujasusi kati ya vyombo vya usalama vya Kenya na Tanzania, ikiwa ni sehemu ya juhudi za kuvunja mitandao ya uhalifu wa kupangwa inayovuka mipaka ya nchi. Tukio hilo limeibua upya wasiwasi kuhusu kuongezeka kwa uwezekano wa Kenya kutumiwa na mitandao ya kimataifa ya biashara haramu ya dawa za kulevya, hasa ile inayojihusisha na usafirishaji wa methamphetamine. Mwaka uliopita, meli iliyokuwa imebeba methamphetamine yenye thamani ya Sh8.2 bilioni ilizuiliwa katika Bahari Hindi na washukiwa sita raia wa kigeni wakakamatwa. Jeshi la Wanamaji nchini lilinasa meli ya MV Mashallah ikiwa imebeba zaidi ya kilo 1,024 za methamphetamine baharini. Haijabainika wazi dawa hizo zilikuwa zikielekea wapi, huku kesi dhidi ya washukiwa ikiendelea na mihadarati hiyo kuteketezwa kwa amri ya mahakama. Katika mwaka wa 2014, meli ya MV Amin Darya ilikamatwa ikiwa na dawa za kulevya zenye thamani ya Sh1.3 bilioni. Ingawa wafanyakazi wake walihukumiwa kifungo cha maisha awali, Mahakama Kuu baadaye ilibatilisha hukumu hizo baada ya kubaini kutokuwepo kwa ushahidi usiotiliwa shaka, ikiwemo kutokuwa na uhakika kuhusu eneo ambalo meli hiyo ilikuwa wakati ilipokamatwa.
read moretaifaleo.nation.co.ke
@taifaleo Mon, 09 Nov 2026 06:55:45
Hussein: Sijutii katu Mariga kufurushwa, alikuwa na ulafi wa mamlaka!
RAIS wa Shirikisho la Soka la Kenya (FKF), Hussein Mohamed, amemshutumu aliyekuwa naibu wake McDonald Mariga akidai alikuwa na tamaa ya madaraka na kutaka kumpokonya mamlaka mwezi mmoja tu baada ya wawili hao kuchaguliwa kuongoza shirikisho hilo. Akizungumza siku moja baada ya Mariga kuondolewa mamlakani pamoja na wajumbe wengine saba wa Kamati Kuu ya Kitaifa (NEC), Mohamed alisema hajutii uamuzi wa wajumbe katika Mkutano Spesheli wa FKF, akisisitiza kuwa uhusiano wake na Mariga ulikuwa umesambaratika kiasi cha kutotengenea. "Mambo yalianza kuharibika katika mkutano wa kwanza wa NEC uliofanyika Januari 2025, mwezi mmoja tu baada ya kuchaguliwa katika nyadhifa zetu. Mariga alitaka kuwa rais na alikuwa na nia ya kunisukuma pembeni ili ajitwalie kila kitu. Sijutii yaliyompata na wenzake," Mohamed akaambia Taifa Leo kwenye mahojiano. Mohamed alidai Mariga alitaka kudhibiti karibu kila shughuli ya shirikisho hilo na kumwacha kama kiongozi butu asiye na usemi kuhusu lolote kwenye shirikisho. "Alitaka kudhibiti timu za taifa, ligi, usimamizi na hata ufadhili na alitaka awe kila kitu. Mimi ndiye nilichaguliwa kuwa rais na yeye alikuwa naibu wangu. Kwa nini ningekubali hilo? Mariga alisafiri katika karibu ziara zote za timu za taifa, ambazo baadhi nilizifadhili kwa pesa zangu mwenyewe," akasema. Aliongeza kuwa Mariga alitaka kuwa katika kila kamati ili kutimiza maslahi yake binafsi. "Hivi majuzi alidai kuwa hakuwa akilipwa mshahara. Lakini nilipaswa kupata wapi pesa za kumlipa mshahara, walinzi, katibu wa afisi na dereva wa kudumu aliokuwa akitaka? Je, alikuja FKF kuongoza soka au kujinufaisha binafsi?" akauliza Mohamed. Pia alidai Mariga hakufurahishwa tangu mwanzo na uteuzi wa Harold Ndege kuwa Afisa Mkuu Mtendaji (CEO) wa FKF, akisema naibu huyo wa zamani alikuwa akimpendelea mgombea mwingine. Hata hivyo, Mohamed alidokeza kuwa Mariga na Ndege walikuwa wameridhiana hivi karibuni na sasa walikuwa wakishirikiana kumpinga. Alitaja pia madai ya juhudi za Mariga na washirika wake za kusitisha mashindano ya Chapa Dimba mwaka huu kuwa mojawapo ya mambo yaliyomkasirisha zaidi. Mohamed alisema alijaribu kutatua tofauti zao kwa mazungumzo na kukubali baadhi ya matakwa ya Mariga, lakini baadaye akatambua kuwa alikuwa akisukumwa na tamaa na majitapo. Alisisitiza kuwa Mariga, ikiwa alitamani urais, alipaswa kusubiri uchaguzi wa 2028 na kuwania nafasi hiyo badala ya kujaribu kubadilisha mamlaka ndani ya uongozi uliochaguliwa. Aidha, alimshutumu Mariga na mrengo wake kwa kukiuka maagizo ya FIFA kwa kupeleka malalamishi yao mahakamani, kwa Idara ya Upelelezi Nchini (DCI) na Bungeni. Alisema hatua hizo zinalilemaza usimamizi wa soka na kuenda kinyume na maelekezo ya FIFA.
read moretaifaleo.nation.co.ke
@taifaleo Mon, 09 Nov 2026 07:55:59
Mwalimu ambaye anatumia taarabu kama chombo cha kufunza Kiswahili
UNAPOKARIBIA lango la Shule ya Upili ya Wasichana ya Kakenya Girls Dream School, iliyoko Enoosaen, Kaunti ya Narok, unasikia midundo ya taarabu ikivuma. Muziki huo wenye asili ya Pwani umegeuka kuwa nyenzo ya kipekee ya kufundishia Kiswahili na kubadili mtazamo wa wanafunzi kuhusu lugha hiyo. Mwalimu Chimoli Bibiana ndiye aliyeanzisha mbinu hiyo, akitumia nyimbo, mashairi na maonyesho ya jukwaani kuwavutia wanafunzi. Anasema alipowasili shuleni humo, Oktoba 2022, aligundua kuwa wengi hawakupenda Kiswahili kwa kuwa walikichukulia kuwa kigumu na lugha ya watu wa Pwani. Wanafunzi wengi, ambao wanatoka katika jamii ya Wamaasai, walikuwa na dhana kwamba Kiswahili hakikuhusiana na utamaduni wao. Hali hiyo ilimchochea Bibiana kubuni njia ya kuwafanya wajifunze lugha hiyo kwa furaha na kujiamini. "Nilitafuta mbinu ya kuwavutia na kuwafanya waipende lugha hii. Ndipo nilipoamua kutumia taarabu, ambao umekuwa kivutio kwa wanafunzi na jamii inayozunguka shule," anasema. Kwa mujibu wake, mbinu hiyo imeboresha uwezo wa wanafunzi kuzungumza na kuandika Kiswahili, pamoja na matokeo yao katika somo hilo. Pia imeimarisha uhusiano na ushirikiano wao. Tangu aanzishe mfumo huo, ameshuhudia mabadiliko makubwa katika kipindi cha miaka minne, huku wanafunzi wakizidi kutumia lugha hiyo kwa ufasaha. Mbali na kufundisha lugha, Bibiana hutumia nyimbo na mashairi kuwapa wanafunzi mafunzo ya malezi, nidhamu na kufanya maamuzi yanayofaa. Anasema jukumu la mwalimu halipaswi kuishia kutekeleza mtaala, bali linahusisha pia kuwashauri wanafunzi, kuwajengea kujiamini na kuwasaidia kutambua uwezo wao. Anawahimiza walimu kutumia ubunifu, uvumilivu na kujitolea wanapokabili changamoto za ufundishaji. Pia anashauri shule kutenga nafasi na rasilimali za kukuza vipaji kupitia michezo na shughuli nyingine za ziada. Anasema michezo huwafundisha wanafunzi nidhamu, kufikiri kimkakati na kushirikiana kama timu, stadi zinazowasaidia kukabiliana na changamoto hata nje ya shule. Katika miaka minne aliyohudumu shuleni humo, anasema amewaongoza wasichana kwa karibu, akilenga kuwaona wakistawi na kuwa viongozi wa kesho. Anasisitiza kuwa walimu wanapaswa kutambua vipaji vya wanafunzi na kuunda mazingira yanayowapa nafasi ya kuvikuzia, badala ya kuzingatia alama za mitihani. Bibiana alianza masomo katika Shule ya Msingi ya Likhobero, eneo bunge la Ikolomani, Kaunti ya Kakamega, kisha akaendelea na Shule ya Upili ya St John Museno. Mwaka 2019 alijiunga na Chuo Kikuu cha Kibabii, Bungoma, kusomea Shahada ya Sanaa katika Elimu, na kuhitimu 2022. Oktoba mwaka huo, alipata kazi yake ya kwanza ya ualimu katika Kakenya Girls Dream School, ambako bado anafundisha Kiswahili. Kupitia taarabu, anaendelea kuvunja dhana potovu na kuwajengea wasichana mapenzi kwa lugha hiyo.
read moretaifaleo.nation.co.ke
@taifaleo Mon, 09 Nov 2026 10:33:17
Ruto aambia wakazi wa Gusiiland kususia upinzani kwa 'kukosa ajenda'
RAIS William Ruto jana aliwakejeli viongozi wa upinzani kutokana na mivutano yao ya ndani, akisema utabiri wake kwamba umoja wao ungesambaratika kabla ya uchaguzi mkuu wa 2027 umetimia. Akicheka kuhusu malumbano ya hivi majuzi miongoni mwa viongozi hao, Rais alisema migogoro hiyo inathibitisha madai yake kuwa hawana ajenda ya kuwatumikia Wakenya. Akihutubia wakazi wa Nyamira katika vituo mbalimbali wakati wa ziara yake eneo la Gusii, Dkt Ruto alisema ana uhakika atawashinda wapinzani wake kutokana na rekodi yake ya maendeleo, huku akiutaja upinzani kuwa usiokuwa na mwelekeo. Nyamira ni ngome ya kisiasa ya Kiongozi wa Jubilee na mgombea mtarajiwa wa urais wa upinzani, Dkt Fred Matiang'i, aliyekuwa Nyeri, ambako alisisitiza kuwa upinzani utaendelea kuwa na umoja katika azma yao ya kumwondoa Rais mamlakani. Rais alisema kazi kuu ya upinzani ni kumkosoa na kumtusi kwa majina kama Kasongo na kueneza chuki. "Watu hao hawajui barabara zitajengwa vipi, nyumba zitakuzwa vipi au bima ya afya itatolewa vipi. Hawana mpango, hawana ufahamu kuhusu hali yetu ya sasa, hawana mpango wa kesho wala maono ya mustakabali wetu," akaongeza. Aliwataka wakazi wa Nyamira wasichezee mustakabali wa nchi kwa kuwaunga mkono viongozi ambao hawana mwelekeo. Rais yuko katika ziara ya siku nne eneo la Gusii, kuanzia Jumapili hadi Jumatano, akitafuta uungwaji mkono wa muhula wake wa pili. Alisema viongozi wanaowania nyadhifa za kisiasa lazima waeleze rekodi yao ya maendeleo na mipango yao kwa wananchi badala ya kuwahadaa. Katika ziara hiyo, alihudhuria ibada ya pamoja katika uwanja wa Nyamaiya kabla ya kuzindua kituo cha kidijitali cha eneobunge la Mugirango Magharibi. Pia alizindua ujenzi wa barabara ya Bondeni-Magombo na mradi wa kusambaza umeme katika maeneo ya mashinani. Pia alizindua ujenzi wa barabara ya Tombe-Isinta-Mokomoni katika eneobunge la Mugirango Kaskazini. Ziara hiyo inafanyika wakati muungano wa upinzani unakabiliwa na migawanyiko kutokana na kutokubaliana kuhusu mgombeaji mmoja wa urais, maslahi ya maeneo na mikakati ya kisiasa.
read moreRight Column Content