T

taifaleo.nation.co.ke

@taifaleo Sun, 08 Nov 2026 10:55:30

Safari ya mapenzi haiishi na ndoa, harusi ni mwanzo tu

Mwanaume anapaswa kuelewa kuwa kumpata mwanamke anayempenda si mwisho wa safari ya mapenzi, bali ni mwanzo wa jukumu la kumtunza, kumheshimu na kuendelea kumthamini. Kuna mambo mengi kuhusu mwanamke ambayo mwanaume anapaswa kujifunza ili kudumisha uhusiano wenye furaha.  Kwanza, mwanamke anayempenda mwanaume kwa dhati anaweza kuhisi upweke na huzuni anapokuwa mbali naye. Uwepo wa mpenzi wake humpa faraja na kumfanya ajihisi salama. Hata hivyo, kupata imani ya mwanamke si jambo la siku moja. Huchukua muda kujenga uaminifu, lakini mwanaume anapovunja imani hiyo kwa uongo, usaliti au tabia zisizofaa, inaweza kuwa vigumu sana kuirejesha. Wataalamu wa mahusiano wanasema mwanaume anapaswa pia kuelewa kuwa mwanamke ni kama shule ambayo masomo yake hayaishi. Kadiri unavyoishi naye, ndivyo unavyoendelea kugundua mambo mapya kuhusu tabia, hisia, ndoto na matarajio yake. "Usidhani kuwa cheti cha ndoa ni ruhusa ya kuacha kumtongoza na kumfurahisha. Badala yake, ni kama kibali cha kuendelea kujifunza kuhusu mwenzi wako. Kumwonyesha mapenzi, kumpeleka matembezini, kumsifia na kumjali kunapaswa kuendelea hata baada ya miaka mingi ya ndoa," asema mtaalamu wa mahusiano Nelly Ikinya. Anasema mwanamke anaweza kukasirika leo na kufurahi kesho. "Jinsi unavyomchukulia wakati wa hasira inaweza kuamua kama atajihisi kupendwa au kuumizwa zaidi. Epuka matusi, vitisho na maneno ya kumdhalilisha," aeleza. Kumbuka kuwa baadhi ya wanawake hukumbuka sana maumivu waliyopitia. Hivyo, kuwa mwangalifu na maneno yako. Unapokosea, omba msamaha badala ya kutafuta sababu za kujitetea. Pia, usihukumu hisia zake kwa mwonekano wake. Mwanamke anaweza kuonekana mwenye nguvu na furaha mbele ya watu, ilhali moyoni anapitia wakati mgumu. Kuwa rafiki yake wa karibu, msikilize na umpe nafasi ya kueleza yanayomsumbua bila kumkatiza au kumhukumu. Wanawake wengi pia hupenda kujihisi wa pekee. Mambo madogo kama kumuuliza hali yake, kumshukuru kwa juhudi zake, kumshika mkono au kumwambia anapendeza yanaweza kuleta tofauti kubwa katika uhusiano. "Usisubiri hadi mwanamke akose nyumbani ndipo utambue umuhimu wake. Uwepo wake unaweza kuwa umefanya maisha yako kuwa rahisi kwa namna ambazo huzitambui. Anapoondoka, ndipo unaweza kugundua mchango wake katika maisha yako," asema mshauri wa masuala ya ndoa, Jimmy Petu. Anaongeza kuwa mwanamke anayekupenda anaweza kujitahidi kukufurahisha kwa njia mbalimbali. Hata hivyo, usitumie mapenzi yake kumlazimisha kufanya mambo asiyoyataka. Mapenzi ya kweli yanahitaji hiari, heshima na kuelewana. Katika masuala ya fedha, asema Petu, mwanaume hapaswi kusubiri mwenzi wake aombe msaada ndipo aone mahitaji yake. Kuwa tayari kumsaidia pale unapoweza, bila kumfanya ajihidi kama ombaomba. Vilevile, msaada wa kifedha haupaswi kutumiwa kama njia ya kumdhibiti. "Mwanamke anayekupenda na kusimama nawe katika nyakati nzuri na ngumu ni hazina inayopaswa kuthaminiwa. Usimwumize kwa kudhani kuwa atavumilia kila kitu. Upendo unahitaji juhudi za watu wawili," asema Kinya.

read more
T

taifaleo.nation.co.ke

@taifaleo Sun, 08 Nov 2026 09:55:52

SHERIA: Ni kosa kuishi kwenye ndoa isiyosajiliwa rasmi

Ndoa si sherehe, pete wala kuishi pamoja chini ya paa moja. Ni muhimu kuhakikisha imefanywa kwa mujibu wa sheria na kusajiliwa ili kulinda haki za wanandoa na watoto wao. Watu wengi huingia kwenye ndoa kwa kufanya sherehe za kifamilia, kidini au kimila, kisha kuendelea na maisha bila kuhakikisha kuwa ndoa hizo zimesajiliwa rasmi. Wengine huona usajili kama jambo la urasimu lisilo na umuhimu, mradi tu wamekubaliana kuishi pamoja kama mume na mke. Lakini kupuuza hatua hii kunaweza kuibua matatizo makubwa wanandoa wanapofarakana, mmoja wao anapofariki au kunapozuka mzozo kuhusu urithi, mali na haki za mwenzi aliyebaki. Sheria ya Ndoa ya Kenya ya mwaka 2014 inaweka wazi wajibu wa kusajili ndoa na kutambua aina mbalimbali za ndoa zinazoweza kufungwa nchini, zikiwemo za kiraia, Kikristo, Kiislamu, Kihindu na kitamaduni. Hata hivyo, kufungwa kwa ndoa na kusajiliwa kwake ni hatua mbili ambazo hazipaswi kuchanganywa. Wanandoa wanapaswa kuhakikisha kuwa ndoa yao imeunganishwa na mtu aliyeidhinishwa na kwamba taratibu za kisheria za usajili zinafuatwa. Kutosajili ndoa kunaweza kuhatarisha uhalali wake. Sehemu ya 42 ya Sheria ya Ndoa inaelekeza mtu anayefungisha au kusimamia ndoa kuwasilisha nakala ya cheti cha ndoa kwa Msajili wa Ndoa ili maelezo yake yaingizwe katika sajili rasmi. Sheria hiyo pia inaweka adhabu kwa mtu anayeshindwa kusajili ndoa. Akipatikana na hatia, anaweza kutozwa faini isiyozidi Sh5,000. Jambo muhimu zaidi ni kwamba sehemu ya 12 ya sheria hiyo inasema ndoa inaweza kubatilishwa ikikosa kusajiliwa rasmi. Hii ina maana kuwa wanandoa hawapaswi kudhani kuwa sherehe waliyoifanya pekee inatosha kuwahakikishia ulinzi kamili wa kisheria. Katiba ya Kenya, katika Ibara ya 45, inatambua familia kama msingi wa jamii na kuipa ulinzi wa Serikali. Pia inahakikisha kuwa wanandoa wana haki sawa wakati wa kufunga ndoa, wanapoishi pamoja na ndoa inapovunjika. Haki hizo zinapaswa kuambatana na kufuata taratibu za kisheria ili kuepusha hali ambapo mmoja wa wanandoa analazimika kutumia muda na fedha nyingi kuthibitisha uhusiano wake. Ndoa za kitamaduni hazijaachwa nyuma. Baadhi ya Wakenya hudhani kuwa ndoa za kimila hazihitaji kusajiliwa kwa sababu zinatambuliwa na wazee na familia za wahusika. Lakini Sheria ya Ndoa imeweka utaratibu maalumu kwa ndoa hizo kusajiliwa. Sehemu ya 44 inataka wahusika kuarifu Ofisi ya Msajili wa Ndoa ndani ya miezi mitatu baada ya kukamilisha taratibu na sherehe zinazotambulisha muungano wao chini ya mila husika. Aidha, sehemu ya 55 inawataka wanandoa kuwasilisha maombi ya cheti cha ndoa ndani ya miezi sita baada ya kukamilisha taratibu za kimila. Wote wawili wanapaswa kufika mbele ya Msajili ili kukamilisha usajili. Hivyo basi, kulipa mahari, kufanya sherehe ya kitamaduni na kutambuliwa na wazazi au wazee wa jamii hakupaswi kuwa mwisho wa safari. Hatua za usajili ni muhimu pia. Wanandoa wanaoishi nje ya nchi pia wanapaswa kuchukua tahadhari. Sheria haijawasahau Wakenya wanaofunga ndoa nje ya nchi. Sehemu ya 39 inaruhusu Wakenya kufunga ndoa za kiraia katika balozi za Kenya katika mataifa ya kigeni, mradi masharti yaliyowekwa yatimizwe. Aidha, sehemu ya 40 inatambua ndoa ya kiraia iliyofungwa katika nchi nyingine ikiwa ilifungwa kwa mujibu wa sheria za nchi hiyo na wahusika walikuwa na uwezo wa kisheria wa kuoana chini ya Sheria ya Ndoa ya Kenya. Sehemu ya 58 ya Sheria ya Ndoa ya Kenya inaruhusu Mkenya aliyefunga ndoa nje ya nchi kuomba ndoa hiyo isajiliwe na Msajili wa Ndoa nchini Kenya. Sehemu ya 59 ya Sheria ya Ndoa inaeleza kuwa ndoa inaweza kuthibitishwa kwa kutumia cheti cha ndoa, nakala yake iliyothibitishwa au taarifa zilizomo kwenye sajili rasmi ya ndoa. Hii ni muhimu hasa panapotokea migogoro ya kifamilia. Mjane anaweza kuhitaji kuthibitisha uhusiano wake na marehemu katika masuala ya mirathi. Vivyo hivyo, wanandoa wanapogawana mali baada ya kutengana, uthibitisho wa ndoa unaweza kuwa sehemu muhimu ya mchakato huo. Kwa wale ambao hawajasajili ndoa zao, hatua ya kwanza ni kuwasiliana na Ofisi ya Msajili wa Ndoa ili kufahamu utaratibu unaofaa kulingana na aina ya ndoa yao. Huduma za usajili zinapatikana pia kupitia tovuti ya eCitizen. Ujumbe muhimu ni kwamba cheti cha ndoa si pambo la kuweka kwenye droo, bali ni stakabadhi muhimu ya kulinda haki za wanandoa. Ni bora kuhakikisha kila kitu kiko sawa wakati uhusiano unaendelea vizuri kuliko kusubiri msiba au mzozo ndipo mtu aanze kutafuta ushahidi wa ndoa yake.

read more
T

taifaleo.nation.co.ke

@taifaleo Sun, 08 Nov 2026 08:55:41

Upinzani unavyojitoa pumzi kwa kulumbana hadharani

Viongozi wa upinzani wanaotaka kumwondoa Rais William Ruto mamlakani katika uchaguzi wa 2027 wanaonekana kutumia nguvu nyingi kujibizana hadharani, huku tofauti kuhusu nani atakayepeperusha bendera ya muungano na namna ya kugawana mamlaka zikizidi kujitokeza. Wachanganuzi wa siasa wanasema badala ya kuonyesha umoja na kuelekeza nguvu zao katika kuandaa ajenda mbadala ya taifa, baadhi ya vinara hao sasa wanashambuliana kwa maneno, wakilaumiana kwa kuwa na kiburi, ubabe na kujaribu kumiliki uongozi wa upinzani. "Badala ya kuonyesha ushirikiano wao unapata nguvu kuelekea muungano, wanarushiana cheche za maneno hadharani. Wanabomoa Imani ya wafuasi wao kwao," asema mchanganuzi wa siasa Daniel Kioko. Kulingana na kiongozi wa Jubilee Jeremiah Kioni, migawanyiko hiyo inaweza kumpa Rais Ruto nafasi ya kunufaika na kura kati ya wagombeaji wengi wa urais. Akizungumza katika mahojiano na kituo cha redio Alhamisi, Novemba 5, Kioni alisema viongozi wanaowania urais katika vyama tofauti wanahatarisha azma ya kuwa na mgombeaji mmoja wa kumkabili Rais Ruto. "Ni njia gani bora ya kumpa muhula wa pili? Hiyo ndiyo njia bora kabisa. Kwa kweli, atafurahi," alisema Kioni, akirejelea uwezekano wa vinara wa upinzani kuingia katika uchaguzi ujao wakiwa kadhaa. Alitaja aliyekuwa Waziri wa Usalama wa Ndani Fred Matiang'i, aliyekuwa Naibu Rais Rigathi Gachagua, kiongozi wa Wiper Kalonzo Musyoka na Seneta wa Nairobi Edwin Sifuna miongoni mwa wanasiasa ambao misimamo na matarajio yao yanaweza kuathiri mazungumzo ya kuunda muungano. Mvutano huo ulijitokeza wazi baada ya Gachagua kupendekeza muungano unaowaleta pamoja yeye, Sifuna na Kalonzo, akisema viongozi hao wana idadi ya kutosha ya wapiga kura kumkabili Rais Ruto. Katika mahojiano na runinga ya Inooro, Gachagua alidai kuwa anaweza kuleta kura milioni 10, Sifuna milioni nne na Kalonzo milioni tatu. Alilinganisha mpango huo na ushirikiano wa kisiasa kati ya marehemu Mwai Kibaki na Kijana Wamalwa uliosaidia upinzani kushinda uchaguzi wa 2002. Hata hivyo, pendekezo hilo lilionekana kuwaacha nje baadhi ya vinara wengine, akiwemo Matiang'i, Martha Karua, Eugene Wamalwa na Justin Muturi. Matiang'i alijibu kwa kulaumu Gachagua kwa kutumia kiburi na majivuno yanayoweza kuvunja upinzani. Alipinga pia siasa zinazotegemea hesabu za kikabila badala ya sera, uwezo na rekodi za viongozi. "Uongozi na mustakabali wa nchi yetu haupaswi kuamuliwa kwa kugawanya watu kwa misingi ya makabila. Nilidhani huu ni ushindani wa mawazo, sera za maendeleo, rekodi, uwezo na sifa," alisema Matiang'i. Aliongeza kuwa yuko tayari kumuunga mkono mgombeaji yeyote atakayechaguliwa kupitia mchakato shirikishi na unaokubalika, lakini akapinga viongozi wachache kuwalazimisha wengine kukubaliana na chaguo lao. "Hakuna Mkenya anayepaswa kuachwa nyuma. Lazima tuwashirikishe wote," alisema katika mahojiano na NTV. Gachagua, hata hivyo, alijitetea dhidi ya madai ya kiburi, akisema kuwa baadhi ya wanasiasa humchukulia kuwa mkorofi kwa sababu anasema ukweli. Alisisitiza kuwa kampeni za urais zinahitaji kuzingatia idadi ya kura na uwezo wa kuunganisha maeneo yenye wapiga kura wengi. Mzozo huo pia umehusisha Muturi, ambaye alimtaka Gachagua kuelewa kuwa hakuna jamii moja inayoweza kumuingiza mtu Ikulu bila ushirikiano kitaifa. Kwa mujibu wa Muturi, muungano wa upinzani unapaswa kujengwa kwa kuheshimiana badala ya vitisho, ubabe na mashindano ya kuonyesha nani ana nguvu zaidi. Changamoto nyingine ni kukubaliana kuhusu mgombeaji wa urais. Hadi sasa, mazungumzo ya viongozi hao hayajazaa makubaliano ya mwisho kuhusu atakayebeba bendera ya upinzani, huku baadhi wakitaka uamuzi ufanywe mapema ili maandalizi ya kampeni yaanze. Kwa sasa, Kioni na Matiang'i wanaonya kuwa muda unaotumika katika malumbano unaweza kuathiri juhudi za kujenga timu moja. Hata hivyo, wachanganuzi wa siasa wanasema kwamba suala linalowakabili viongozi hao si kuchagua mgombeaji pekee, bali pia kukubaliana kuhusu sera, uwakilishi wa maeneo mbalimbali na namna ya kushirikiana bila mmoja kuhisi ametengwa. "Huku uchaguzi wa 2027 ukikaribia, swali kubwa ni iwapo vinara hao wataweza kuweka kando tofauti zao na kufikia makubaliano, au wataendelea kulumbana huku kila mmoja akijaribu kuthibitisha ubabe wake wa kisiasa," asema mchanganuzi wa siasa Deborah Muyaki.

read more
T

taifaleo.nation.co.ke

@taifaleo Sun, 08 Nov 2026 07:55:09

Kamari ya urais ya Ndidi Nyoro akikaidi Gachagua mlimani

Mbunge wa Kiharu Ndindi Nyoro amejipata katikati ya vita vya kisiasa katika Mlima Kenya tangu alipotangaza azma ya kuwania urais, akipuuza chama cha UDA na kujiunga na People's Party of Kenya (PPK). Mbunge huyo anayehudumu muhula wa pili amekuwa akishambuliwa na washirika wa aliyekuwa Naibu Rais Rigathi Gachagua, ambao wanadai ni kibaraka wa serikali ndani ya upinzani, anayetaka kugawanya kura za eneo la Mlima Kenya. Lakini Nyoro anasema hana mpango wa kugawanya eneo hilo na yuko tayari kumuunga mkono mgombea yeyote atakayechaguliwa na upinzani kwa makubaliano. Katika mahojiano maalumu na Taifa Leo , alisema alijiunga na upinzani akiwa na ajenda ya kubadilisha nchi, wala si kwa mwaliko wa kiongozi yeyote. "Ikiwa ni Gachagua, nitamuunga mkono. Wakinichagua mimi, ninatumai naye ataniunga mkono. Kwa hivyo, ni kura gani ninazogawanya?" aliuliza. Alikanusha pia madai kuwa PPK ni mradi wa kumsaidia Rais William Ruto kugawanya kura za Mlima Kenya, akisema chama hicho kilianzishwa mwaka 1996, kabla ya Jubilee na DCP. Alisema alichukua usimamizi wa chama hicho mwaka 2024 na kujiunga rasmi miezi miwili iliyopita ili kupata nafasi ya kutekeleza ajenda yake bila kutegemea maamuzi ya viongozi wengine. Nyoro, ambaye zamani alikuwa mshirika wa karibu wa Rais Ruto, alisema uhusiano wao ulianza kuzorota wakati wa mchakato wa kumuondoa Gachagua mamlakani mwaka 2024. Alisema kutoshiriki kwake katika mchakato huo kulimfanya kuwa adui wa Rais, na baadaye akavuliwa uenyekiti wa Kamati ya Bajeti ya Bunge la Kitaifa. Alikanusha madai ya kupokea Sh30 milioni ili kukosa kikao cha kumuondoa Gachagua mamlakani, akisema hahitaji kuhongwa ili kufanya maamuzi ya kisiasa. Pia alimtaka Seneta wa Nyandarua John Methu kuthibitisha madai hayo, akidai kuwa yeye mwenyewe alimsaidia kifedha wakati wa uchaguzi mdogo wa Ol Kalou. Licha ya mzozo huo, Nyoro alisema bado ana uhusiano mzuri na Gavana wa Murang'a Irungu Kang'ata, akisisitiza kuwa tofauti za kisiasa hazipaswi kugeuzwa uhasama wa kibinafsi. Kuhusu uhusiano wake na kiongozi wa Jubilee Fred Matiang'i, alisema mazungumzo yao yanalenga mustakabali wa nchi, wala si kugawana mamlaka. Alisema yuko tayari kufanya kampeni pamoja na Gachagua, Kalonzo Musyoka au kiongozi mwingine yeyote wa upinzani, lakini hatakubali kulazimishwa kumfuata mtu. "Asiyetaka kufanya kazi nami, ni uamuzi wake," alisema. Nyoro anasema azma yake ya kuwania urais haikutokana na msukumo wa ghafla. Alisema amekuwa akijiandaa kwa muda kwa kujifunza kuhusu changamoto za nchi na kujiendeleza kitaaluma. Mbunge huyo ana shahada za uzamili katika uchumi kutoka Chuo Kikuu cha Nairobi na Chuo Kikuu cha Kenyatta, na amehudhuria kozi za uchumi na maendeleo katika London School of Economics. Pia alisema alihitimu na cheti cha juu cha uchumi wa maendeleo kutoka Chuo Kikuu cha Harvard Aprili mwaka huu. Alisema uongozi mzuri unahitaji nia njema pamoja na uwezo wa kutekeleza majukumu. Mbali na siasa, Nyoro amekuwa akijenga jina katika biashara na uwekezaji. Alisema alianza kujifunza kuhusu soko la hisa akiwa mwanafunzi wa Chuo Kikuu cha Kenyatta. Alisema alianza kununua hisa za Kenya Power kuelekea uchaguzi wa 2017, wakati hisa moja ilikuwa ikiuzwa kwa Sh1.50 na kampuni hiyo ikipata hasara. Alitumia takriban Sh46 milioni kununua hisa hizo hatua kwa hatua. Kwa sasa, alisema anamiliki hisa milioni 27 kupitia jina lake na kampuni zake mbili, Limpopo Capital na Sahara, za thamani ya takriban Sh594 milioni kwa bei ya Sh22 kwa hisa. Alikanusha madai kuwa anashikilia hisa hizo kwa niaba ya Rais Ruto, akisema uwekezaji wake ulianza kabla hajawa mbunge. Nyoro pia alitetea rekodi yake ya kusimamia hazina ya maendeleo ya maeneo bunge (CDF) Kiharu, akisema siri ni kutumia wafanyakazi wa eneo husika badala ya wakandarasi wakubwa. Alisema mfumo huo umesaidia kuboresha shule zote 120 za msingi za umma, huku taasisi 70 zikiwa na sakafu za cabro. Shule nyingine 20 zinatarajiwa kunufaika Desemba. Kupitia mpango wa Kiharu Masomo Bora, wanafunzi 12,000 katika shule za upili za kutwa 65 hupata chakula kwa kuchangia Sh500 kila muhula. Mpango huo pia unawapa chakula wanafunzi wanaohudhuria masomo ya ziada Jumamosi. Hata hivyo, Nyoro alisema changamoto kubwa ya uchumi wa Kenya ni deni la taifa, akidai Sh80 kati ya kila Sh100 za matumizi ya serikali huenda kulipa madeni. Alionya kuwa hali inaweza kuwa mbaya zaidi kabla ya Rais Ruto kuondoka mamlakani. Pia alikosoa kile alichokiita mfumo wa upendeleo katika biashara, ambapo viongozi hutumia mamlaka yao kujinufaisha katika sekta mbalimbali. Licha ya kujitetea dhidi ya tuhuma za kuwa kibaraka wa serikali, Nyoro anakabiliwa na mtihani wa kuwashawishi wapinzani kuwa azma yake ya urais inalenga kuimarisha upinzani, si kuudhoofisha. Anasema lengo lake ni upinzani kupata mgombea mmoja wa urais kupitia makubaliano ya haki na ya wazi, na yuko tayari kumuunga mkono atakayechaguliwa, iwapo hatakuwa yeye.

read more