T

taifaleo.nation.co.ke

@taifaleo Sun, 08 Nov 2026 05:55:30

Walimu walio na umri wa miaka 40 na zaidi waendelee kupuuzwa katika ajira ya TSC

Maelfu ya walimu waliohitimu mafunzo ambao hawakuajiriwa Tume ya Huduma kwa Walimu (TSC) wanahofia kufikisha umri wa kustaafu bila kupata nafasi ya kufundisha katika shule za umma. Walimu walio na umri wa zaidi ya miaka 45 ndio walioathirika zaidi, huku baadhi yao wakilazimika kufanya kazi za vibarua, kufundisha katika shule za kibinafsi kwa mishahara midogo au kuacha kabisa ndoto ya kuwa walimu. Hii ni licha ya serikali ya Rais William Ruto kuajiri zaidi ya walimu 100,000 katika kipindi cha miaka mitatu iliyopita. Walimu hao sasa wanangoja utekelezaji wa ahadi ya Rais ya kuwapa nafasi za ajira kupitia utaratibu maalumu wa kuwapa kipaumbele, aliyotoa alipokutana na walimu 10,000 katika Ikulu ya Nairobi Septemba 13, 2025. Katibu Mkuu wa chama cha walimu wa shule za msingi KNUT, Collins Oyuu, alimuomba Rais kuwasaidia walimu wakongwe ambao wamekosa ajira huku wanaopaswa kuwa wanafunzi wao wakiajiriwa. Mmoja wao ni James Cherop, mwenye umri wa miaka 52 kutoka Baringo, ambaye amesubiri ajira kwa miaka 24 tangu alipohitimu mafunzo mwaka 2002. Sasa anafanya vibarua katika Kaunti ya Nakuru ili kukimu familia yake ya watoto saba. "Nimepoteza hesabu ya mara ambazo nimetuma maombi. Nilikata tamaa na kuamua kufanya kazi za mikono Nakuru ili kutunza familia yangu," alisema. Kenneth Rono, mwenye umri wa miaka 47 kutoka Bomet, pia amekuwa akifanya kazi za vibarua kwa miaka 10 bila kupata ajira ya TSC. Amefanya kazi za kupalilia, kuchuma majani ya chai, kuchimba vyoo na ujenzi. Alisema shule ya kibinafsi aliyowahi kusomesha ilimlipa Sh7,000 pekee kwa mwezi, kiasi kisichotosha kutunza familia yake ya watoto wanne. Walimu katika shule za kibinafsi hulipwa kati ya Sh6,000 na Sh8,000 kwa mwezi, ikilinganishwa na mshahara wa kuanzia wa Sh26,255 kwa walimu wa TSC. Pia hawana mafao kama pensheni, bima ya matibabu na malipo ya likizo. Saddiq Hussein Mohamed, 51, kutoka Garissa, alihitimu Chuo cha Ualimu cha Garissa mwaka 1998. Alipata nafasi ya ajira lakini aliugua na kushindwa kuripoti kazini, na tangu wakati huo amekuwa akituma maombi bila mafanikio. KNUT inataka nafasi za ajira zitengwe kwa walimu wenye umri wa miaka 45 na zaidi ili wasiendelee kuachwa nyuma.

read more
T

taifaleo.nation.co.ke

@taifaleo Sun, 08 Nov 2026 04:55:32

Wabunge nao wataka usemi katika kuajiri wazee wa vijiji

Juhudi za wabunge kutaka washirikishwe katika uteuzi wa wazee wa vijiji, wanavyoajiriwa na malipo yao zimeibua vita vya kudhibiti maafisa 106,000 wanaohudumu mashinani, huku umuhimu wao ukitarajiwa kuongezeka Kenya inapoelekea uchaguzi mkuu wa Agosti mwakani. Ni miezi mitatu tu tangu wazee hao waanze kupokea posho ya Sh3,000 kila mwezi, lakini sasa wabunge wanadai kuwa watu waliokuwa wakihudumia jamii kwa muda mrefu bila malipo waliachwa nje ya orodha ya serikali. Wanasema baadhi ya machifu na maafisa wa utawala walioshiriki kuwatambua wazee hao na kukusanya taarifa zao walipendelea jamaa na marafiki zao, badala ya kuwajumuisha wale waliokuwa wakifanya kazi hiyo kwa kujitolea. Wabunge sasa wanataka Waziri wa Usalama wa Ndani Kipchumba Murkomen kuwasilisha orodha ya wazee wote 106,000 wanaolipwa na serikali ili wahakikishe kuwa waliohudumia jamii kwa muda mrefu ndio wanaonufaika. Suala hilo liliibuka Jumatano wakati wa kipindi cha maswali bungeni, ambapo mawaziri hujibu moja kwa moja maswali ya wabunge kuhusu shughuli za wizara zao. Mwakilishi wa Wanawake wa Uasin Gishu Gladys Boss alisema mwanamke mzee aliyekuwa akihudumu Langas, katika kaunti hiyo, aliachwa nje ya orodha kwa sababu hakuwa na uhusiano mzuri na Kamishna wa Kaunti. "Aliachwa nje kimakusudi kwa sababu Kamishna wa Kaunti hakumpenda. Hiki ni kisa kimoja tu; kuna visa vingi kama hivyo nchini," alisema. Alisema watu wengi walihudumu kama wazee wa vijiji kwa miaka mingi bila malipo, lakini serikali ilipoamua kuwalipa, wengine wapya walichukuliwa na kuwaondoa waliokuwa wamefanya kazi hiyo kwa uaminifu. Mbunge wa Kajiado Kusini Samuel Parashina alitaka Waziri Murkomen kueleza vigezo vilivyotumiwa katika uteuzi huo. Alisema baadhi ya machifu walichagua marafiki na jamaa zao, jambo linalozua maswali kuhusu haki na uwazi katika mchakato huo. "Je, Waziri anaweza kuwasilisha ripoti kuhusu vigezo vilivyotumiwa kuwatambua wazee hawa? Je, kulikuwa na upendeleo? Na je, wale walioachwa nje licha ya kuhudumia jamii watapewa nafasi baadaye?" aliuliza. Mbunge wa Igembe Kaskazini Julius Taitumu alisema wazee waliokuwa wakifanya kazi hiyo bila malipo ndio walioathirika zaidi baada ya serikali kutangaza posho. Alisema machifu na manaibu wao walijikita katika kuchagua marafiki na watu wa ukoo wao walipotambua kuwa kazi hiyo sasa ingekuwa na malipo. Akijibu wabunge, Bw Murkomen alisema serikali ilitarajia ushindani mkubwa wa kutaka kuwa mzee wa kijiji baada ya kuanzishwa kwa posho ya Sh3,000. "Siku hizi imekuwa fahari kuwa mzee wa kijiji. Baadhi ya watu wanajitambulisha kama wazee wa vijiji; wengine ni wa kweli na wengine si wa kweli," alisema. Aliahidi kuwa wizara itatoa rekodi za wazee wote katika ofisi za makamishna wa kaunti kote nchini ili wananchi waweze kuthibitisha wanaostahili kupokea malipo hayo. Alifichua kuwa kati ya wazee 106,000, huduma ya M-Pesa ya Safaricom ilikuwa imefanikiwa kushughulikia 96,566 na kuwalipa kupitia mfumo wa Tunza Vijiji. Taarifa za waliobaki zilirudishwa kusahihishwa kwa kuwa majina hayakulingana na nambari za vitambulisho na simu. "Usasishaji wa taarifa unaendelea na utakamilika ndani ya mwezi mmoja ili kuhakikisha wazee waliosalia wanalipwa posho zao kwa malimbikizi," alisema. Rais William Ruto alizindua sera ya usimamizi wa vijiji na utawala wa serikali ya kitaifa mwezi Agosti, hatua iliyowatambua rasmi wazee hao na kuwaingiza katika mfumo wa utawala wa kitaifa. Serikali ilikusanya taarifa zao kote nchini na kuunda sajili ya kitaifa itakayotumiwa kuwatambua na kuwawezesha kutekeleza majukumu yao. Rais alisema wazee hao ni kiungo muhimu kati ya serikali na wananchi kwa sababu wanafahamu changamoto za jamii na wako karibu na watu wanaohitaji huduma. Kwa mujibu wa takwimu za Sensa ya Kitaifa ya Watu na Makazi ya 2019, Kenya ilikuwa na kata 2,427 zinazosimamiwa na machifu na kata ndogo 6,612 chini ya manaibu wa machifu. Hata hivyo, idadi ya kata imeongezeka hadi 2,735 na kata ndogo kufikia takriban 7,000. Kwa sasa, mfumo huo una wazee wa vijiji 106,072, manaibu wa machifu 9,144 na machifu 4,008, wote wakiripoti kwa serikali ya kitaifa. Serikali inataka kuwaunganisha wazee hao katika mfumo rasmi wa utawala, kuwapa majukumu yaliyo wazi na kuwawezesha kifedha ili kurahisisha utoaji huduma mashinani

read more
T

taifaleo.nation.co.ke

@taifaleo Sun, 08 Nov 2026 03:55:37

Sababu zinazofanya wanaume wengi kukwepa ibada kanisani

Jumapili inapowadia, makanisa mengi hujaa waumini, lakini katika viti hivyo kuna pengo linalozidi kuonekana: wanaume. Ingawa baadhi yao huendelea kuhudhuria ibada, wengine wamepunguza safari za kanisani, huku wengine wakiamua kabisa kubaki nyumbani na kuacha familia zao ziende kuabudu. Sababu zinazowafanya wanaume kujitenga na kanisa ni nyingi. Kwa baadhi yao, ni shughuli za kutafuta riziki na majukumu ya familia. Wengine wamekatishwa tamaa na jinsi wanavyotendewa kanisani, tofauti za kitamaduni au lugha, huku wengine wakihisi hawapewi nafasi ya kushiriki kikamilifu katika maisha ya waumini. Peter Otieno ni mmoja wa wanaume ambao wameacha kuhudhuria ibada baada ya kuhisi kuwa kanisa lililokuwa sehemu muhimu ya maisha yake halikumjali alipohitaji msaada. Kwa miaka mingi, Otieno alikuwa kiongozi wa vijana na mhubiri katika kanisa lake. Hata hivyo, ajali ya barabarani iliyomuacha akitumia kiti cha magurudumu miaka 20 iliyopita ilibadilisha maisha yake na uhusiano wake na kanisa. Anasema alianza kuhisi kutengwa, hasa alipoona kuwa shughuli za wanaume kanisani hazikuwajumuisha watu wenye ulemavu kama yeye. Badala ya kupewa nafasi ya kushiriki, alihisi kana kwamba alichukuliwa kama mtu anayehitaji kuonewa huruma. Otieno anasema hakupata pia msaada wa kanisa kuanzisha biashara ambayo ingeweza kumwezesha kujitegemea licha ya hali yake ya kiafya. Hatimaye, aliacha kuhudhuria ibada miaka minane iliyopita. Mkewe alifariki mwaka 2018, lakini baadaye aliweza kuanzisha duka la simu na vifaa vya kielektroniki eneo la Komarock. Anasema watoto wake ndio wamempa sababu ya kuendelea kupambana na maisha. Binti yake humuombea, jambo linalomkumbusha umuhimu wa imani hata ingawa yeye mwenyewe haendi tena kanisani. Kwa Benson Buchichi, tatizo si kutokuwa na imani, bali ni kutohisi kuwa sehemu ya mazingira ya makanisa mengi anayokutana nayo jijini Nairobi. Mkewe na watoto wao huhudhuria ibada katika Kanisa la All Saints Cathedral, lakini yeye hupendelea kubaki nyumbani. Anasema tofauti za lugha na tamaduni humfanya ashindwe kujihisi huru katika baadhi ya makanisa. Licha ya kutohudhuria ibada mara kwa mara, Buchichi anasema bado huchangia kifedha shughuli za kanisa na kuunga mkono familia yake katika masuala ya imani. Hata hivyo, si wanaume wote wanaokaa nyumbani kwa sababu ya kukatishwa tamaa na kanisa. Bonface Musambai, ambaye ni daktari, anasema ratiba yake ya kazi humfanya akose muda wa kuhudhuria ibada mara kwa mara. Mkewe na watoto wao watano ni Wakatoliki, na familia hiyo huendelea kusali pamoja nyumbani. Mchungaji Solomon Kisakui anasema wanawake mara nyingi huonekana kuwa wengi kuliko wanaume katika ibada na shughuli za kanisa. Anahusisha hali hiyo na ukweli kwamba wanawake hushiriki zaidi katika vikundi vya maombi na shughuli za kueneza injili, huku wanaume wengi wakijishughulisha na biashara na kazi. Kwa upande wake, Profesa Martin Njoroge anaonya kuwa kutokuwepo kwa baba katika shughuli za kidini za familia kunaweza kuathiri jinsi watoto wanavyoshiriki katika maisha ya kanisa. Anasema makanisa yanapaswa kutafuta njia za kuwavutia wanaume badala ya kuwahukumu au kuwafanya wajihisi hawakaribishwi. Anapendekeza kuanzishwa kwa mikutano ya kiamsha kinywa kwa wanaume, vikundi vya ushauri na malezi, pamoja na vikundi vidogo vinavyowapa nafasi ya kuzungumzia changamoto zao. Kwa mujibu wa Njoroge, makanisa yanahitaji kubuni mazingira ambayo wanaume wanaweza kushiriki bila kuhisi kuwa wanapimwa au kuhukumiwa. Anasema kuwashirikisha katika shughuli za kijamii na kuwapa nafasi za uongozi kunaweza kusaidia kurejesha uhusiano wao na taasisi za kidini. Changamoto ni kwamba kwa baadhi ya wanaume, kuacha kanisa si uamuzi wa siku moja, bali ni matokeo ya miaka ya kujihisi kutengwa, kutosikilizwa au kushindwa kupata nafasi inayowafaa.

read more
T

taifaleo.nation.co.ke

@taifaleo Sun, 08 Nov 2026 02:55:23

Karata ya Gachagua kwa Kalonzo, Sifuna kuelekea 2027

Aliyekuwa Naibu Rais Rigathi Gachagua anajaribu kujenga muungano mpana wa upinzani utakaompa nafasi muhimu katika uchaguzi wa urais wa 2027. Hata hivyo, mpango wake wa kuunganisha maeneo yenye kura nyingi unakabiliwa na mvutano kuhusu nani atakayeongoza, nani atakayetoa kura na ni nani atakayekuwa na usemi mkubwa katika kugawana mamlaka. Kutoka nyumbani kwake Wamunyoro, kiongozi huyo wa Democracy for the Citizens Party (DCP) anauza ujumbe wa mashauriano, ushirikiano na umoja wa upinzani. Lakini nyuma ya ujumbe huo kuna mkakati mkali unaoitwa Operation Okoa Kenya, unaolenga kuunganisha maeneo yenye ushawishi wa kisiasa, kupunguza ushawishi wa Rais William Ruto na kuwalazimisha wapinzani kujadiliana wakiwa na nguvu za kutosha. Kiini cha mpango huo ni muungano unaopendekezwa kati ya DCP ya Gachagua, Wiper ya Kalonzo Musyoka na vuguvugu la Linda Mwananchi linaloongozwa na Edwin Sifuna. Mlima Kenya, Ukambani, Magharibi na Nyanza ndizo nguzo kuu za kisiasa zinazotarajiwa kuunda muungano huo.Gachagua aliambia Taifa Jumapili kuwa mpango utaanza kwa kuunganisha maeneo ya kijiografia, huku DCP na Wiper zikimsaidia Sifuna kupata uungwaji mkono katika maeneo yaliyokuwa ngome za marehemu Raila Odinga. "Unaanza na maeneo. Makubaliano ni kwamba DCP na Wiper zitasaidia vuguvugu la Linda Mwananchi la Edwin Sifuna kupata uungwaji mkono katika ngome za jadi za Raila Odinga, hasa Magharibi na Nyanza," alisema.Alisema baada ya Sifuna kuimarisha maeneo hayo, wataungana na Mlima Kenya na Mashariki, kisha kuimarisha Nairobi na Pwani ili kuunda muungano wenye uwezo wa kushindana na Kenya Kwanza. Kaimu Katibu Mkuu wa DCP John Methu anasema mkakati huo unalenga kujenga ukuta wa kisiasa utakaowazuia washirika wa Rais Ruto kufanya kampeni kwa urahisi katika maeneo hayo.Anasema mpango huo hautahusu tu mazungumzo ya kugawana nafasi za uongozi, bali pia kutambua na kuidhinisha mapema wagombea wenye nguvu ili kukabiliana na washirika wa serikali. "Ukuta huo utajengwa mashinani. Mpango ni kuwatangaza na kuwaidhinisha mapema wagombea wenye nguvu, hata kama hawatashinda mara moja, ili kujenga upinzani endelevu dhidi ya washirika wa Ruto," alisema Methu. Katika Magharibi, Gachagua anataka washirika wa Rais Ruto, akiwemo Farouk Kibet, Francis Atwoli, Musalia Mudavadi na Moses Wetang'ula, wakabiliwe na upinzani uliopangwa.Gavana wa Trans Nzoia George Natembeya, ambaye anaongoza kampeni za urais za Sifuna, anasema lengo ni kumzuia Ruto kurithi kura za Raila."Gachagua ana silaha kuu ambayo ni kura za Mlima Kenya zilizomfanya Dkt Ruto kuwa rais mwaka 2022. Sifuna na Musyoka ndio watakaomzuia Ruto kurithi kura za Raila. Tunataka kumzuia Ruto asipate zaidi ya asilimia 30 ya kura alizopata mwaka 2022," alisema.Hata hivyo, mkakati huo unamuweka Gachagua katika hali ngumu. Anahitaji kuonyesha kuwa anaweza kuunganisha Mlima Kenya, lakini eneo hilo limeanza kuwa uwanja wa mapambano kati ya wanasiasa wenye malengo tofauti.Mustakabali wake pia haujawa wazi baada ya Mahakama Kuu kukataa kubatilisha uamuzi wa Seneti uliomuondoa mamlakani. Ingawa anaweza kukata rufaa, changamoto hiyo inatatiza juhudi zake za kujitangaza kuwa kiongozi asiye na mpinzani katika eneo hilo.Mchambuzi wa siasa Geoffrey Mboya anasema changamoto ya Gachagua si tu kuamua iwapo atawania urais, bali pia kujua atakayeunga mkono, jinsi ya kujadiliana kwa niaba ya Mlima Kenya katika serikali ijayo na jinsi ya kuzuia wapinzani wake eneo hilo kutwaa ushawishi aliojenga. Gachagua pia anakabiliwa na upinzani kutoka kwa Muturi na aliyekuwa Waziri Peter Munya, ambao wamekataa shinikizo kwamba vyama vidogo vya Mlima Kenya kuvunjwa na kujiunga na DCP. Wanasema ushirikiano haupaswi kumaanisha kupoteza utambulisho wa vyama vyao. Munya amehoji kwa nini mazungumzo ya muungano yanafanyika nyumbani kwa Gachagua Wamunyoro badala ya jukwaa lisiloegemea upande wowote. Katika juhudi za kupanua ushawishi wake, Gachagua amefikia aliyekuwa Gavana wa Kitui Charity Ngilu, hatua inayotafsiriwa kama jaribio la kupunguza nguvu za Kalonzo katika Ukambani iwapo kiongozi huyo wa Wiper hatakubaliana na masharti yake.Mmoja wa maafisa wanaofahamu mazungumzo hayo anasema mkakati ni kutumia nguvu za kura za Mlima Kenya na Magharibi kujenga muungano wa kitaifa, huku Ngilu akisaidia kuvutia sehemu ya Ukambani iwapo Kalonzo hatakuwa tayari kufanya maelewano. Hatua hiyo imezua wasiwasi ndani ya Wiper. Seneta wa Kitui Enoch Wambua ameshutumu Ngilu kwa kudhoofisha azma ya Kalonzo ya kuwania urais.Mratibu wa wagombea wa DCP Mlima Kenya Joseph Waweru anasema Gachagua anataka mazungumzo ya mwisho ya muungano yafanyike baada ya kura za mchujo za vyama Machi 2027, ili kila chama kijue nguvu yake kupitia wagombea kitakaowapata. Lakini Mbunge wa Embakasi Mashariki Babu Owino, mshirika wa Sifuna, anataka mgombea wa urais wa upinzani atangazwe kabla ya Desemba mwaka huu. Mbunge wa Laikipia Mashariki Mwangi Kiunjuri naye amewaonya Sifuna na Kalonzo dhidi ya kuingia katika muungano ambao unaweza kutumiwa na Gachagua kutanguliza maslahi yake.

read more