T

taifaleo.nation.co.ke

@taifaleo Sat, 07 Nov 2026 05:55:10

Mapuuza ya serikali kuhusu Mackenzie yaliyochangia mauaji Shakahola

KWA miaka saba, shughuli za mhubiri Paul Mackenzie zilizohusishwa na itikadi kali na vifo vya wafuasi wake zilikuwa zikijulikana na polisi, maafisa wa mahakama, kamati za usalama na mashirika ya kulinda watoto. Hata hivyo, hatua madhubuti hazikuchukuliwa hadi makaburi ya halaiki yalipogunduliwa katika msitu wa Shakahola. Ripoti za watu kupotea, watoto kunyimwa elimu na familia kutengana zilikuwa zimewasilishwa kwa mamlaka mbalimbali. Lakini wafuasi wa Mackenzie waliendelea kuingia msituni, ambako mamia yao walikumbana na njaa, mateso na kifo. Kamati maalumu ya Seneti iliyochunguza mkasa huo ilisema katika ripoti yake ya Oktoba 19, 2023 kuwa kulikuwa na fursa nyingi za kuokoa maisha, lakini idara za serikali zilishindwa kuunganisha taarifa na kuchukua hatua. Mackenzie alikuwa akiwaagiza wafuasi wake kuacha kazi, kukataa matibabu na kupinga baadhi ya mipango ya serikali kama vile sensa, kampeni za kutoa dawa za minyoo na Huduma Namba. Kamati ya usalama ya Kaunti ya Kilifi iliwahi kumwita kueleza mafundisho yake na madai ya kuwatesa wafuasi. Maafisa walimuonya kuhusu mafundisho hayo, lakini hawakuchukua hatua zaidi. "Ushahidi uliowasilishwa kwa Kamati unaonyesha kuwa Kamati ya Usalama ya Kaunti ya Kilifi ilikuwa na taarifa za awali kuhusu shughuli za Paul Mackenzie lakini ilikosa kuchukua hatua," ripoti hiyo ilisema. Mwaka 2022, Mackenzie alidai kuwa alikuwa mkulima na alikuwa ameacha kazi ya kuhubiri. Seneti ilikosoa serikali kwa kutofuatilia madai hayo. Mackenzie alikuwa amewahi kukabiliwa na mashtaka mbalimbali. Mnamo Machi 14, 2017, alishtakiwa kwa kuendesha shule isiyosajiliwa katika kanisa lake la Good News International Ministries mjini Malindi. Alikubali makubaliano na upande wa mashtaka, akatozwa faini ya Sh20,000 na kuagizwa kuwa na tabia njema. Mnamo Oktoba mwaka huo huo, alishtakiwa tena kwa kueneza itikadi kali, kuendesha shule bila usajili, pamoja na kuwanyima watoto elimu. Hata hivyo, aliachiliwa huru Oktoba 29, 2021 kutokana na ukosefu wa ushahidi. Mwaka huo, watoto 43 wenye umri wa mwaka mmoja hadi 13, wakiwemo watatu wa Mackenzie, waliokolewa kutoka kanisa lake Mayungu. Walikuwa wakinyimwa elimu na kupewa mafundisho yake yenye itikadi kali. Mwaka 2019, Kamati ya Watumiaji wa Mahakama ya Kaunti ya Kilifi ilijadili madai ya watoto kuingizwa katika itikadi kali kupitia kanisa na kituo cha televisheni cha Mackenzie. Suala hilo lilipelekwa kwa kamati ya kitaifa na Mamlaka ya Mawasiliano. Leseni ya kituo hicho ilifutwa, lakini kamati haikufahamishwa kuhusu pendekezo la kulifuta kanisa. Ishara nyingine muhimu ilitolewa Machi 6, 2022, wakati taarifa ya kupotea kwa Sylvia Adoyo Mwende ilipotolewa katika Kituo cha Polisi cha Likoni. Inadaiwa alikuwa amepelekwa Shakahola baada ya kumtembelea Mackenzie. Konstebo Wilson Lekaken aliyekuwa akichunguza kisa hicho alisema alipata kibali cha mazishi kwa jina la Sylvia pamoja na maandishi yaliyodokeza alikuwa amefariki Shakahola na kuzikwa bila mwili kupelekwa mochari. Hata hivyo, maswali yaliibuka kuhusu iwapo kibali hicho kilithibitishwa na chifu msaidizi aliyedaiwa kukitoa na kama kaburi lilichunguzwa au mwili kufukuliwa. Mnamo Machi 2023, Francis Wanje aliyekuwa akitafuta wajukuu wake alipata amri ya mahakama ya kufukua miili ya watoto wawili waliodhaniwa kuzikwa msituni. Polisi walichukua siku tano kufika eneo hilo baada ya taarifa kutolewa kuhusu mvulana wa miaka minane na makaburi yaliyoshukiwa kuwemo Maafisa walioandamana na Wanje na Victor Kaudo wa Kituo cha Haki za Kibinadamu cha Malindi wanadaiwa kupokea simu na kuondoka, wakiwaacha raia hao wawili. Seneti haikuweza kubaini aliyepiga simu hiyo. Amri ya kufukua miili iliyotolewa Machi 21, 2023 ilitekelezwa Aprili 14, wakati ukubwa wa mkasa huo ulipoanza kufahamika

read more
T

taifaleo.nation.co.ke

@taifaleo Sat, 07 Nov 2026 04:55:40

Watengenezaji vileo nchini wapinga mswada mpya wa kuthibiti unywaji pombe

WATENGENEZAJI wa vileo nchini wamekosoa mswada mpya unaolenga kudhibiti zaidi uzalishaji na uuzaji wa pombe, wakionya kuwa mapendekezo hayo yanaweza kufuta maelfu ya ajira, kupunguza mapato ya serikali na kukuza biashara ya pombe haramu. Chama cha Watengenezaji wa Vileo nchini (ABAK) kinasema kupandisha umri wa chini wa kunywa pombe kutoka miaka 18 hadi 21 kunaweza kusababisha sekta za rejareja na ukarimu kupoteza mapato ya Sh3.3 bilioni kila mwaka. Aidha, serikali inaweza kukosa Sh1.8 bilioni za ushuru huku ajira 8,960 na maduka 1,792 yaliyo na leseni kuwa hatarini kufungwa, kwa mujibu wa makadirio ya chama hicho. Mswada wa Marekebisho ya Sheria za Vileo na Udhibiti wa Dawa za Kulevya wa 2026 uliwasilishwa kwa mara ya kwanza katika Bunge la Kitaifa Alhamisi, Novemba 5, na sasa unasubiri kujadiliwa na wabunge. Miongoni mwa mapendekezo yake ni kupandisha umri wa chini wa kununua na kunywa pombe hadi miaka 21, kuzuia uuzaji wa vileo katika maduka makubwa na maeneo mengine, kupiga marufuku mauzo kupitia mtandao na usafirishaji wa pombe hadi nyumbani, pamoja na kutoza ushuru wa Sh2 kwa kila lita ya pombe inayotengenezwa nchini au kuagizwa kutoka nje. Mwenyekiti wa ABAK, Kui Kinyanjui, alisema mapendekezo hayo yanaweza kudhoofisha kampuni halali zinazotengeneza na kusambaza pombe huku yakifungua mianya kwa wauzaji wa bidhaa haramu. "Wakati ambapo sekta yetu tayari inakabiliwa na changamoto kubwa kutoka kwa wauzaji wa pombe haramu, mswada huu unaweza kudhoofisha biashara halali na kutoa nafasi zaidi kwa pombe haramu kustawi," alisema. Aliongeza kuwa hatua hizo zitaathiri maelfu ya wafanyakazi, uwekezaji uliopangwa na mapato ya serikali, huku zikiwaweka watumiaji katika hatari kubwa zaidi. Chama hicho pia kinapinga pendekezo la kutoza Sh2 kwa kila lita ya pombe, kikisema hatua hiyo itawaongezea watengenezaji halali gharama ya takriban Sh1.3 bilioni kila mwaka.  Kwa mujibu wa ABAK, ushuru huo unaweza kuongeza bei ya pombe inayouzwa kihalali na kufanya bidhaa hizo kuwa ghali ikilinganishwa na pombe haramu inayouzwa kwa bei ya chini bila kulipa ushuru. Kinyanjui alitaka Bunge lisitishe mswada huo ili kutoa nafasi ya mashauriano na wadau kabla ya kuidhinisha mabadiliko hayo. "Tunahimiza kuwepo kwa mashauriano ya wazi yanayohusisha serikali za kaunti, wasimamizi wa sekta, wataalamu wa afya ya umma na wadau wote katika biashara ya pombe," alisema. Alisema lengo la pamoja linapaswa kuwa kulinda watumiaji, kuhifadhi ajira na kukabiliana kikamilifu na pombe haramu. Hatua hii inajiri wakati ambapo biashara ya pombe haramu imeendelea kuwa changamoto kwa kampuni halali na serikali, ambayo hupoteza ushuru kutokana na bidhaa zinazouzwa nje ya mfumo rasmi.  Utafiti wa Euromonitor wa mwaka 2025 ulioagizwa na ABAK ulikadiria kuwa pombe haramu ilichangia asilimia 60 ya pombe yote iliyotumiwa nchini kwa wingi mwaka 2024. Kiasi cha pombe hiyo kiliongezeka kwa asilimia 27 kati ya 2022 na 2024. Utafiti huo pia ulikadiria kuwa serikali ilipoteza takriban Sh120 bilioni za mapato ambayo ingeweza kukusanya mwaka 2024 kutokana na biashara ya pombe haramu, ikiwemo ya magendo, bidhaa bandia na ukwepaji wa ushuru. Mamlaka ya Kupambana na Bidhaa Bandia pia imehusishwa katika mijadala kuhusu matokeo hayo, huku watengenezaji halali wakilalamikia bidhaa haramu kuchukua sehemu kubwa ya soko. ABAK inaonya kuwa kuzuia uuzaji wa pombe katika maduka makubwa, mikahawa na mitandao kunaweza kufanya bidhaa halali kuwa ngumu kupatikana, huku wauzaji haramu wakiendelea kufanya biashara nje ya mfumo wa leseni na ushuru. Mnamo Julai 2025, serikali ilizindua sera ya kitaifa ya kuzuia, kudhibiti na kusimamia matumizi ya pombe na dawa za kulevya. Sera hiyo ilipendekeza umri wa chini wa kushughulikia, kununua, kunywa na kuuza pombe uwe miaka 21. Serikali imetetea pendekezo hilo ikisema linalenga kulinda afya ya umma na kupunguza uwezekano wa vijana kuanza kutumia pombe na dawa za kulevya wakiwa na umri mdogo. Mamlaka ya Kitaifa ya Kupambana na Matumizi ya Pombe na Dawa za Kulevya (NACADA) imeeleza wasiwasi kuhusu unywaji wa pombe miongoni mwa wanafunzi wa vyuo vikuu. Utafiti wa NACADA wa mwaka 2025 kuhusu wanafunzi wa vyuo vikuu ulionyesha kuwa asilimia 87.3 ya waliohojiwa walikuwa wakitumia pombe, na kuifanya kuwa bidhaa inayotumiwa zaidi miongoni mwa wanafunzi hao.

read more
T

taifaleo.nation.co.ke

@taifaleo Sat, 07 Nov 2026 03:55:58

Kalonzo ataka uchunguzi wa kina kuhusu ghasia za Linda Mwananchi Homa Bay

KIONGOZI wa Wiper Patriotic Front (WPF) Kalonzo Musyoka amepinga idadi rasmi ya watu waliouawa wakati wa ghasia zilizozuka katika mkutano wa Linda Mwananchi mjini Homa Bay Agosti 16, akitaka uchunguzi maalum wa umma kubaini idadi kamili ya waliofariki na waliohusika na mauaji hayo. Bw Musyoka anadai kuwa idadi ya walioangamia ni kubwa zaidi kuliko ile iliyotangazwa na polisi. Ingawa ripoti rasmi zilitaja watu wanne kufariki, kiongozi huyo wa upinzani anasema uchunguzi wao umeonyesha kuwa idadi hiyo imeongezeka na kuzidi kumi. "Tumebaini kuwa idadi imeongezeka. Tunatoa wito wa kuanzishwa kwa uchunguzi maalum ili kubaini kilichotokea na waliohusika na mauaji haya, kwa sababu nchi haiwezi kuendelea hivi," alisema. Ghasia hizo zilitokea wakati Seneta wa Nairobi Edwin Sifuna, Mbunge wa Embakasi Mashariki Babu Owino na viongozi wengine wa vuguvugu la Linda Mwananchi walipokuwa wakielekea mjini Homa Bay baada ya kufanya mikutano ya kisiasa Nyandiwa na Sindo. Vijana waliokuwa wamejihami kwa silaha, yakiwemo mapanga, waliripotiwa kuziba barabara kwa mawe na kuwatishia waliotaka kupita. Miongoni mwa waliofariki alikuwa afisa wa polisi kutoka Muhoroni aliyekuwa akiwasafirisha wenzake kutoa msaada kwa maafisa wenzao. Mfanyabiashara mwenye asili ya Uganda pia alifariki baada ya kugongwa na magari yaliyokuwa yakipita kwa kasi alipokuwa akivuka barabara. Akizungumza akiwa Homa Bay Ijumaa, baada ya msafara wake kushambuliwa Migori siku iliyotangulia, Bw Musyoka alidai tukio la Homa Bay ni mauaji ya halaiki yanayopaswa kuchunguzwa badala ya kufichwa. Alisema kaunti hiyo imekuwa ikiitwa kwa dharau "Afghanistan" na "Yemen" kutokana na visa vya mauaji, akitaka hali hiyo ikomeshwe. "Hatuwezi kufanya Homa Bay iendelee kuwa uwanja wa mauaji ya watu wasio na hatia. Kaunti hii ni sehemu ya Kenya, na hatuwezi kuendelea kuruhusu hali hii," alisema. Alikuwa ameandamana na viongozi wengine wa upinzani, akiwemo Justin Muturi, Eugene Wamalwa, Mbunge wa Nyali Mohamed Ali na Raphael Tuju. Viongozi hao walisema hawatakubali fidia ya pesa pekee kwa waathiriwa wa ghasia za kisiasa. Bw Musyoka alisema jopo la wataalamu kuhusu fidia kwa waathiriwa wa maandamano na mikutano ya umma, linaloongozwa na Profesa Makau Mutua, linakamilisha ripoti yake. Baada ya ripoti hiyo, Tume ya Haki ya Kurejesha Hali ya Kawaida waliyoanzisha, inayoongozwa na Bw Muturi, itachukua hatua zaidi za kudai haki. "Hauwezi kuwapa watu pesa tu. Hauwezi kulipia maisha ya binadamu. Lazima kuwe na haki pamoja na fidia. Bado tutawafuata kudai haki. Haki lazima itendeke kwa mashujaa wote walioangamia," alisema. Aidha, Kalonzo na kikosi chake wanapanga kutangaza Juni 25 kuwa Siku ya Kitaifa ya Uwajibikaji, itakayoadhimishwa kila mwaka kwa maandamano ya kumbukumbu. Walisema watafanya siku hiyo kuwa rasmi iwapo wataingia mamlakani mwaka ujao. Kuhusu vurugu za Migori, Bw Musyoka alidai kuwa shambulizi dhidi ya msafara wake lilikuwa limepangwa, akiwalaumu viongozi wa eneo hilo kwa kulipa vijana waliorushia magari yao mawe huku polisi wakirusha vitoa machozi. Bw Muturi alisisitiza kuwa viongozi hao wana haki ya kikatiba kutembelea maeneo yote nchini na hawatatishwa na wahuni wanaodaiwa kuajiriwa kuvuruga mikutano yao. Bw Wamalwa alisema kurushwa kwa mawe na matumizi ya vitoa machozi kwa wakati mmoja kulionyesha kuwa huenda polisi walikuwa wakishirikiana na washambuliaji. "Unapoona serikali na wahuni wakishirikiana, basi hatuna serikali tena. Tulichonacho ni serikali ya wahuni," alisema. Mbunge Mohamed Ali alitaja tukio la Migori kuwa jaribio la kuwaua viongozi wa upinzani, akisema mawe makubwa yaliyolenga magari yao yangeweza kusababisha majeraha mabaya. Bw Tuju alisema timu hiyo haitarudi nyuma kutokana na vitisho, akiwalaumu wanasiasa wa eneo hilo kwa kutumia vijana wasio na ajira kuchochea ghasia za kisiasa.

read more
T

taifaleo.nation.co.ke

@taifaleo Sat, 07 Nov 2026 02:55:09

Mackenzie kuishi jela miaka 200 kutokana na vifo Shakahola

KIONGOZI wa dhehebu la Good News International (GNI), Paul Nthenge Mackenzie, amehukumiwa kifungo cha jumla ya miaka 200 gerezani kwa mauaji ya watoto 190 na mtu mzima mmoja katika msitu wa Shakahola kati ya Januari 2021 na Septemba 2023. Jaji Diana Kavedza akiwa katika Mahakama Kuu mjini Mombasa, alimpa Mackenzie vifungo viwili tofauti vya miaka 100 kila kimoja, kutegemea jinsi waathiriwa walivyofariki. Kifungo cha kwanza kinahusu vifo vya watu 183, wakiwemo watoto 182 na mtu mzima mmoja, waliokufa kwa njaa baada ya kunyimwa chakula. Mackenzie alihukumiwa miaka 100 kwa kila shtaka kati ya mashtaka hayo 183, lakini vifungo hivyo vitaendelea kutekelezwa kwa wakati mmoja. Kifungo cha pili kinahusu watoto wanane waliouawa moja kwa moja kwa kunyongwa, kubanwa shingo, kukosa hewa au kupigwa kwa vitu butu. Mackenzie alipewa miaka 100 kwa kila shtaka kati ya hayo manane, huku vifungo hivyo pia vikitumika kwa wakati mmoja. Hata hivyo, jaji aliamuru vifungo hivyo viwili vikuu vitekelezwe kwa kufuatana, hivyo kufikisha jumla ya miaka atakayokuwa gerezani kuwa 200. Akitoa hukumu hiyo, Jaji Kavedza alisema mauaji ya Shakahola yalipangwa mapema na kuendelea kwa muda mrefu, hivyo adhabu ilipaswa kuonyesha uzito wa uhalifu huo. "Adhabu ya mahakama hii lazima ilingane na giza la matendo yao na kiwango cha juu cha adhabu kinachoruhusiwa na sheria," alisema. Jaji huyo alieleza namna watoto wadogo walivyoteseka mikononi mwa watu waliopaswa kuwalinda. Wengi wao walikuwa wakitegemea wazazi na walezi wao, lakini walinyimwa chakula, maji na ulinzi kwa makusudi.  Alisema baadhi ya waliopatikana na hatia hawakuonyesha majuto, huku wakiendelea kusisitiza kuwa watoto wao wako mbinguni na wao pia wako tayari kuwafuata. "Wahalifu wamesimama bila hata kuinamisha shingo, hawana hatia moyoni wala majuto, wakitangaza kwa imani yao potovu na kiburi kuwa watoto wao wako mbinguni na wako tayari kuwafuata. Je, watu wa aina hii wanastahili hata chembe ya huruma? Je, haki inapaswa kulegeza msimamo na kuonyesha huruma mahali ambapo huruma ilifutwa kwa utaratibu? Hapana," alisema. Jaji Kavedza alisema watoto walilemazwa na kunyimwa haki zao kwa kisingizio cha dini, huku baadhi ya manusura wakiachwa yatima na kuishi katika vituo vya watoto, ambako walezi wamekuwa wazazi wao wapya. Alisema adhabu nafuu isingeweza kurekebisha madhara ya kudumu yaliyosababishwa na mauaji hayo. Mahakama ilimtambua Mackenzie kama mpangaji mkuu wa mauaji hayo kutokana na nafasi yake kama kiongozi wa GNI na makazi ya wafuasi wake katika msitu wa Shakahola. Katika tathmini ya jukumu lake, jaji alisema Mackenzie ndiye aliyewaongoza wafuasi wake kuhamia msituni na kuendesha mikutano ambako aliwaagiza wafunge hadi wafe. Pia aliagiza watoto wawe wa kwanza kufa kwa njaa. Mahakama ilisema Mackenzie alisimamia mazishi aliyoyaita harusi, akitoa maagizo kwa wazee wa vijiji kupitia naibu wake Smart Deri Mwakalama. Pia aliamuru matumizi ya nguvu dhidi ya watoto waliokataa kufunga, waliotaka kuacha zoezi hilo au kujaribu kutoroka.  Jaji alisema adhabu haikupaswa kuzingatia tu idadi ya waliouawa, bali pia mateso waliyopitia kabla ya kufariki. "Sheria haitoi adhabu kwa nia ya kulipiza kisasi, bali kwa sababu ya kuzuia uhalifu usijirudie. Ni onyo kali kwa binadamu wote kuwa hakuna shupavu wa imani wala kiongozi katili aliye na haki ya kuua, na yeyote atakayejaribu atahisi uzito wa mkono wa mahakama," alisema. Mahakama ilipanga waathiriwa kulingana na umri na sababu zilizothibitishwa za vifo vyao, huku ikizingatia udhaifu wao na mazingira waliyokufa. Kati ya waathiriwa 191, watoto 161 walikuwa watoto wachanga wanaoanza kutembea na walio chini ya umri wa miaka tisa na nusu. Wengine 22 walikuwa na umri wa miaka 10 hadi 13, watano walikuwa na miaka 14 hadi 16 na nusu, huku umri wa watoto wawili ukishindwa kubainika. Mtu mmoja alikuwa mtu mzima. Kisa cha mtoto mchanga aliyekuwa na siku 12 pekee kilimgusa jaji, ambaye alieleza mateso aliyopitia kabla ya kufariki. "Fikiria mtoto mchanga, maisha madogo yaliyokuwa na siku 12 tu duniani, aliyenyimwa maziwa ya mama tangu kuzaliwa, kitovu chake kikiwa bado hakijapona, akaachwa akinyauka kwenye joto kali huku wale waliokuwa wakisimamia zoezi hilo wakitazama. Siku 12 za kilio dhaifu kilichopungua hadi pumzi ya mwisho," alisema. Watoto wengine 161 walikufa taratibu kutokana na njaa na kiu. Mahakama ilisema walilia wakitafuta chakula na maji, lakini badala ya kusaidiwa walikutana na ukatili kutoka kwa watu waliopaswa kuwalinda. Jaji alitaja maagizo yaliyohusishwa na Mackenzie kwamba watoto wangeingia mbinguni kupitia "mangumi na mateke." Watoto 22 wenye umri wa miaka 10 hadi 13 walikuwa na uwezo wa kuelewa usaliti wa wazazi wao, lakini hawakuwa na nguvu za kutoroka mateso hayo. Vijana watano waliokuwa na umri wa miaka 14 hadi 16 na nusu walipinga maagizo ya kufunga hadi kufa. Mahakama ilisema baadhi yao walifungwa mikono, kufungiwa ndani, kupigwa kwa vitu butu na kunyongwa. Jaji alisema wale waliojaribu kupigania maisha yao walikabiliwa kwa ukatili badala ya kulindwa.  Katika kutoa adhabu, mahakama ilizingatia haja ya kuzuia uhalifu kama huo, kutoa haki kwa waathiriwa na kulinda jamii dhidi ya watu wanaowadhuru walio dhaifu.  Hata hivyo, jaji alisisitiza kuwa kila mshtakiwa alipaswa kuhukumiwa kulingana na nafasi yake, kiwango cha ushiriki na jukumu lake katika mauaji hayo. Naibu wa Mackenzie, Smart Deri Mwakalama, alihukumiwa kifungo cha jumla ya miaka 160. Washtakiwa wengine walipata vifungo vya kati ya miaka 100 na 160 kwa makosa yanayohusiana na mauaji hayo.

read more