T

taifaleo.nation.co.ke

@taifaleo Mon, 07 Sep 2026 05:55:52

'Picha ya Bikira Maria' kwenye ukuta jikoni yaibua gumzo Kisii

KATIKA vilima vya eneobunge la Bobasi, Kaunti ya Kisii, nyumba ndogo ya udongo ambayo kwa miaka mingi imekuwa ikitumika kama jikoni sasa imegeuka kuwa kivutio cha mamia ya waumini na wadadisi. Ni katika kijiji cha Getare, Emenwa, ambako mkulima Mary Onsombi, ambaye ni Mkatoliki mcha Mungu, anasema aligundua picha inayofanana na Bikira Maria kwenye ukuta wa jikoni lake uliojaa weusi kutokana na moshi. Kilichoanza kama kivuli hafifu Ijumaa kilikuwa kimevutia maelfu ya wanakijiji kufikia Jumapili. Watu walifika kutoka maeneo mbalimbali, wakiwemo wahudumu wa bodaboda, wanafunzi na wahubiri wa madhehebu tofauti, wote wakitaka kujionea kile wanachokirejelea kama "Bikira Maria". Jirani yake, Gladys Nyandika, alisema Bi Onsombi aliona picha hiyo alipokuwa ameketi karibu na jiko lake. "Alifikiri ni moshi. Alichukua kipande cha kitambaa na kujaribu kuifuta. Kadri alivyoifuta, ndivyo ilivyozidi kudhihirika. Alisema picha hiyo ilifanana kabisa na sanamu ya 'Bikira Maria' aliye kanisani kwao," alisema. Jikoni humo hakuna jambo la kipekee. Kuna kuta za udongo zilizotiwa weusi na moshi wa kuni, jiko la mawe matatu na sufuria chache zilizoning'inizwa kwenye misumari. Lakini kwenye ukuta wa kaskazini, karibu futi tatu kutoka chini na eneo ambalo Bi Onsombi hupiga magoti anapopika, kuna umbo la kijivu-nyeupe lenye urefu wa takriban inchi 18. Kwa waumini, umbo hilo linafanana na mwanamke aliyevaa vazi refu na kufunika kichwa, huku mikono ikiwa kama yule anayeomba. Kwa wenye mashaka, huenda ni muundo uliotokana na moshi wa miaka mingi, maji kupenya ukutani na udongo kuchubuka. Jikoni hiyo sasa imegeuka kuwa mahali pa sala, huku watawa na waumini Wakatoliki wakisongamana ndani wakiwa na rozari mikononi. "Mungu akiamua kujionyesha, lazima uje uone, iwe wewe ni Mkatoliki au la," alisema mfuasi wa SDA aliyesafiri kutoka Nyamakoroto, Nyamira. Diwani wa Masige Mashariki, Michael Motume, alikuwa miongoni mwa viongozi wa kwanza kutembelea boma hilo. Alisema aliona picha isiyo ya kawaida iliyofanana na sanamu maarufu ya Bikira Maria ya Kanisa Katoliki, lakini akasema hana mamlaka ya kuthibitisha iwapo ni muujiza. Kufikia Jumapili asubuhi, njia ya kuelekea kwa Onsombi ilikuwa imejaa watu. Baadhi walipiga magoti na kusali, huku wengine wakipiga picha na video kwa TikTok. Wahudumu wa bodaboda nao walipata biashara nzuri, wakitoza Sh100 kwa safari kutoka Emenwa Centre hadi Getare. Watawa waliofika eneo hilo hawakutoa maelezo mengi, lakini walionekana kuchukua picha na kuandika kumbukumbu, huenda kwa ajili ya kuwajulisha viongozi wa Kanisa Katoliki katika Dayosisi ya Kisii. Kanisa Katoliki bado halijatoa taarifa kuhusu madai hayo ya muujiza. Vyanzo vya kanisa vilisema halikimbilii kuthibitisha madai kama hayo. Mtaalamu mmoja wa kanisa alisema ripoti kama hizo zimewahi kutokea nchini, zikiwemo picha zinazoonekana kwenye miti na miamba, na nyingi baadaye kubainika kuwa matukio ya kawaida ya kimaumbile.

read more
T

taifaleo.nation.co.ke

@taifaleo Mon, 07 Sep 2026 04:55:59

Rais Ruto asisitiza Kenya haitauza madini ghafi nje ya nchi

RAIS William Ruto amesema Serikali yake inaandaa sera itakayokomesha usafirishaji wa malighafi kutoka Kenya kwenda nje, huku kampuni zikihitajika kuwekeza nchini, kuongeza thamani ya madini na kuunda nafasi za kazi. Akizungumza akiwa Kaunti ya Samburu, wakati wa hafla ya kutoa shukrani ya Katibu wa Ugatuzi, Michael Lenasalon, Rais Ruto alisema amechukua hatua binafsi kuhakikisha usafirishaji wa madini kutoka Magadi unakomeshwa. Alisema sera hiyo itahusu rasilimali zote za nchi, zikiwemo mafuta, dhahabu na madini adimu. "Kuanzia sasa, msimamo wetu wa kisera ni kwamba iwe ni soda ya Magadi, mafuta au madini yetu yote, ikiwemo dhahabu na madini adimu, tumeamua kwamba hatutasafirisha tena malighafi," alisema. Rais alisema Serikali itahakikisha madini yanachakatwa nchini ili kuongeza thamani na kutoa ajira kwa Wakenya. Alisema pia Serikali inashirikiana na mfanyabiashara Aliko Dangote kuanzisha kiwanda cha kusafisha mafuta Lamu. Aidha, alisema Serikali inashirikiana na wawekezaji wengine kuanzisha viwanda vya kusafisha dhahabu na kuchakata madini katika maeneo mbalimbali nchini. "Itakuwa si busara kwa Serikali kusafirisha malighafi, kuunda ajira na kuongeza thamani katika nchi nyingine wakati tuna vijana wengi wanaohitaji ajira," alisema. Rais alisema alilazimika kwenda Kajiado kushughulikia mkataba wa awali wa uchimbaji, ambao alisema ulikuwa ukinufaisha zaidi kampuni kuliko Wakenya.  Alisema mkataba huo, ambapo Kenya ilipata asilimia tano pekee huku asilimia 95 ya thamani ikitengenezwa nje ya nchi, umefutwa.  "Hatuwezi kufuata malighafi zetu nje ya nchi na kununua bidhaa kwa bei ya juu huku vijana wetu wakikosa ajira," alisema. Rais alisema tenda mpya itatangazwa na kampuni zaidi zitaruhusiwa kuwekeza Kajiado. Alisema Serikali haitaki kampuni moja pekee, bali inataka zaidi ya kampuni tano na hata 10 zitumie rasilimali hizo kuunda ajira na kuongeza thamani. Jumamosi, Rais alitangaza kuwa mkataba wa uchimbaji wa Tata Chemicals, iliyojulikana zamani kama Magadi Soda, utatangazwa upya kupitia zabuni yenye ushindani. Alisema mkataba huo ulikuwa wa kunyanyasa Kenya na hauwezi kuendelea. Rais Ruto pia aliahidi kuhakikisha ushirikiano wa kisiasa kati ya UDA na ODM unaendelea hata baada ya uchaguzi wa 2027.  Alishukuru ODM kwa kusaidia kupunguza joto la kisiasa nchini.

read more