T

taifaleo.nation.co.ke

@taifaleo Sat, 05 Sep 2026 07:55:06

Tume ya IEBC yaagizwa kuangazia upya zabuni ya teknolojia ya uchaguzi

TUME Huru ya Uchaguzi na Mipaka ncini (IEBC) imeagizwa kufanya marekebisho katika zabuni yake ya ununuzi wa teknolojia itakayotumika katika Uchaguzi Mkuu wa 2027 baada ya Bodi ya Ukaguzi wa Ununuzi ya Umma (PPARB) kugundua mapungufu katika vigezo vya tathmini na mahitaji ya kiufundi yaliyowekwa kwenye nyaraka za zabuni hiyo. Bodi hiyo ilisema kuwa zabuni hiyo haikueleza kwa uwazi jinsi kutimiza mahitaji ya kiufundi yangepimwa sambamba na mfumo wa alama za tathmini, hali ambayo ingeweza kusababisha wakaguzi kutoa alama tofauti kwa mapendekezo yenye sifa zinazofanana. "Stakabadhi za zabuni zinapaswa kueleza wazi ikiwa kutimiza kila kipengele cha kiufundi ni lazima au ikiwa kuna njia mbadala za kuthibitisha utiifu huo," bodi ilisema. Bodi iliongeza kuwa pale ambapo maelezo ya kiufundi yanahusisha masharti kadhaa, stakabadhi za zabuni zinapaswa pia kufafanua iwapo masharti yote lazima yatimizwe au kama kutimiza idadi fulani ya masharti kunatosha ili zabuni ichukuliwe kuwa imekidhi vigezo. Aidha, IEBC imeagizwa kutafuta ushauri na msaada wa kiufundi kutoka kwa Mamlaka ya Udhibiti wa Ununuzi ya Umma (PPRA) kabla ya kuendelea na mchakato huo wa ununuzi. Ukaguzi huo unalenga kuhakikisha kuwa mahitaji yote yanaelezwa kwa uwazi, ushahidi unaohitajika kuthibitisha unatambuliwa bayana, na mfumo wa kutoa alama unakuwa wa haki, wa wazi na unaoweza kupimika. PPARB iliagiza IEBC kufanya marekebisho, ufafanuzi na mabadiliko yanayohitajika katika stakabadhi za zabuni, kisha ichapishe toleo jipya na kupatia wote wanaowania zabuni muda unaotakiwa kisheria, lakini usiopungua siku saba, ili kuzingatia marekebisho hayo na kuwasilisha zabuni zao. Uamuzi huo ulitokana na malalamishi yaliyowasilishwa na kampuni ya Galadirel Investment Limited, ambayo ilitaka kusitishwa kwa zabuni hiyo ikidai kuwa masharti yake yalikuwa ya kibaguzi na yalitungwa kwa njia inayonufaisha kampuni ya Miru Systems ya Korea Kusini, inayojihusisha na teknolojia za uchaguzi. Zabuni hiyo inahusu Mfumo Jumuishi wa Kusimamia Uchaguzi (IEMS) pamoja na vifaa vinavyohusiana nao, ambavyo vitasaidia vifaa vya KIEMS vinavyotumika kutambua wapigakura kwa alama za kibayometriki na kusambaza matokeo ya uchaguzi. Hii ni moja ya zabuni mbili kubwa za kimataifa zilizotangazwa na IEBC kwa maandalizi ya Uchaguzi Mkuu wa 2027. Zabuni nyingine inahusu uchapishaji wa karatasi za kura, vifaa maalum vya wapigakura wenye ulemavu wa kuona, Daftari la Wapigakura na fomu rasmi za uchaguzi. Galadirel ilidai kuwa stakabadhi za zabuni zilikuwa na masharti magumu ambayo yangeweza kuwazuia washindani wengine kushiriki. Miongoni mwa masharti yaliyopingwa ni hitaji la wanaowania zabuni kuwa na angalau miaka mitano ya uzoefu katika usambazaji wa teknolojia za uchaguzi, vifaa, mitambo na vifaa saidizi. Pia, walitakiwa kuthibitisha kuwa kati ya mwaka 2021 na 2025 walitekeleza angalau mkataba mmoja wa teknolojia ya uchaguzi na kusambaza angalau vifaa 50,000 kwa mteja mmoja katika kipindi hicho. Kampuni hiyo ilidai kuwa masharti hayo yalionekana kuakisi uzoefu na mafanikio ya Miru Systems. "Haya ni masharti yanayoonekana kufanana moja kwa moja na mafanikio ambayo Miru Systems imepata katika zabuni za hapo awali," Galadirel ilisema mahakamani. Hata hivyo, bodi ilikataa hoja kwamba kuwepo kwa mahitaji maalum pekee kunamaanisha kuwa zabuni hiyo ilibuniwa kinyume cha sheria kunufaisha kampuni fulani. Bodi ilieleza kuwa taasisi inayofanya ununuzi ina haki ya kuweka viwango vya uzoefu, uwezo wa kiufundi na umahiri wa kitaaluma vinavyohitajika kwa utekelezaji wa kandarasi husika.

read more
T

taifaleo.nation.co.ke

@taifaleo Sat, 05 Sep 2026 06:55:50

Mzozo wa fidia Mau wazuka tena familia 15,000 zikidai kuachwa nje

MPANGO wa kufidia familia zilizofurushwa kutoka Msitu wa Mau umeibua tena mzozo wa kibinadamu na kisiasa katika eneo la South Rift, huku maelfu ya waathiriwa wakidai serikali imewatelekeza. Zaidi ya familia 15,000 ambazo hazikujumuishwa katika mpango wa fidia sasa zinataka kulipwa. Zinadai baadhi ya maafisa wa serikali waliingiza majina ya jamaa na washirika wao katika orodha ya walionufaika, licha ya kutokuwa waathiriwa. Mzozo huo ulizuka baada ya Rais William Ruto kutangaza Agosti 26 katika uwanja wa Shule ya Sekondari ya Tendwet, Narok Kusini, kuwa serikali ilikuwa imelipa familia 13,000 zilizofurushwa Mau mwaka 2019. Serikali ilikuwa imesajili familia 28,000 kuwa waathiriwa wa zoezi hilo. Hata hivyo, haikutoa maelezo ya kwa nini familia 15,000 ziliachwa nje ya mpango wa fidia. Rais Ruto alisema Sh2.6 bilioni zimetolewa kwa familia 13,000, kila moja ikipokea Sh200,000 kupitia simu zao.  "Leo tunatoa Sh2.6 bilioni kwa jumla ya familia 13,000 zilizofurushwa kutoka Msitu wa Mau. Kila familia sasa itapokea Sh200,000 kama fidia," alisema. Alisema familia nyingine 2,000 zilizokuwa zinaishi katika kambi za wakimbizi wa ndani zilishapokea fidia ya Sh300,000 kila moja, hatua iliyowezesha kufungwa kwa kambi hizo baada ya zaidi ya miaka sita. Rais Ruto alisema suala la Mau lilikuwa limefikia mwisho. Hata hivyo, tangazo hilo limefufua mzozo huo badala ya kuumaliza. Familia zilizoachwa nje zimelalamika na kutishia kurejea katika Msitu wa Mau iwapo serikali haitazifidia kama wenzao waliolipwa. Katika mkutano uliofanyika Olmekenyu mnamo Alhamisi, maelfu ya waathiriwa walitaka serikali ieleze kwa nini waliondolewa kwenye orodha ya walionufaika. Walisema serikali ina siku saba kutoa suluhisho kabla yao kuchukua hatua zaidi. Diwani wa wadi ya Mara, Kipngeno Chepkwony, ambaye ndiye kiongozi pekee aliyezungumza na waathiriwa hao, aliitaka serikali kuchunguza suala hilo upya. "Tuongee na serikali na hasa Rais kuhusu suala hili ili tupate suluhisho la kudumu. Tusiruhusu suala hili kutumiwa kisiasa ili watu walioachwa nje ya mpango wa fidia waweze kuzingatiwa na kulipwa," alisema. Mmoja wa waathiriwa, Fred Mutai, alisema familia zimevumilia kwa muda mrefu.  "Familia zimeteseka kwa muda mrefu, lakini serikali imeongeza chumvi na pilipili kwenye kidonda cha zamani na kufanya hali ambayo tayari ilikuwa dhaifu kuwa mbaya zaidi," alisema.  Afisa wa DCP Leonard Cheruiyot alisema Sh200,000 hazitoshi na serikali ilipaswa kununua ardhi na kuwapa waathiriwa makazi mapya.

read more