T

taifaleo.nation.co.ke

@taifaleo Fri, 04 Sep 2026 08:55:47

TAHARIRI: Serikali iingilie kati kwa dharura kukwamua sekta ya Afya

SERIKALI inapaswa kuingilia kati kwa dharura mzozo unaoendelea kati yake na wahudumu wa afya hasa wauguzi ili kukomesha migomo na kurejesha huduma katika hospitali za umma nchini. Afya ni haki ya msingi ya kila mwananchi, hivyo haifai wagonjwa kuachwa wakiteseka kwa sababu ya mivutano kuhusu masuala ya ajira. Migomo ya wahudumu wa afya imekuwa ikisababisha usumbufu mkubwa kwa wananchi, hasa wale wanaotegemea hospitali za umma kwa matibabu. Wagonjwa wanaohitaji huduma za dharura, wajawazito, watoto, wazee na watu wenye magonjwa sugu ndio wanaobeba mzigo mkubwa zaidi wakati huduma zinapokatizwa. Ni muhimu kutambua kuwa wahudumu wa afya wana haki ya kudai mazingira bora ya kazi, mishahara na marupurupu yanayostahili pamoja na utekelezaji wa makubaliano yaliyofikiwa kati yao na serikali. Hata hivyo, serikali nayo ina wajibu wa kuhakikisha kuwa migogoro kama hiyo haitoi mwanya wa kuhatarisha maisha ya wananchi. Suluhisho la kudumu haliwezi kupatikana kupitia vitisho, lawama au mazungumzo yasiyo na mwisho. Serikali inapaswa kuwaita wadau wote wa afya mezani na kuendesha mazungumzo ya dhati yenye lengo la kufikia makubaliano yanayotekelezeka. Pale ambapo kuna ahadi ambazo hazijatekelezwa, serikali inapaswa kuweka ratiba wazi ya kuzitimiza. Aidha, ni muhimu kuwepo utaratibu wa kuhakikisha huduma muhimu zinaendelea wakati wa migomo. Huduma za dharura, uzazi, matibabu ya wagonjwa mahututi na huduma nyingine zinazookoa maisha hazipaswi kukwama kabisa. Tatizo jingine linalopaswa kushughulikiwa ni uhaba wa wahudumu katika hospitali nyingi. Serikali inapaswa kuajiri wataalamu wa kutosha, kuboresha vifaa na dawa, na kuhakikisha hospitali zina mazingira yanayowawezesha madaktari, wauguzi na wataalamu wengine kufanya kazi kwa ufanisi. Kwa upande wao, viongozi wa vyama vya wafanyakazi wanapaswa pia kutambua uzito wa jukumu walilonalo. Haki za wafanyakazi ni muhimu, lakini zinapaswa kudaiwa kwa njia inayozingatia maisha ya wagonjwa. Serikali isiisubiri hali kukithiri zaidi. Iingilie kati sasa, isuluhishe madai halali ya wahudumu wa afya na kuhakikisha hospitali zinarejelea hali ya kawaida ya kutoa huduma kikamilifu. Maisha ya wananchi hayawezi kusubiri mazungumzo yasiyo na mwisho. Kila Mkenya ana haki ya kupata huduma za afya kikatiba, nayo Serikali inayo wajibu wa kutimiza wajibu wake ifaavyo.

read more
T

taifaleo.nation.co.ke

@taifaleo Fri, 04 Sep 2026 08:00:44

Liverpool yashuka dimbani kusaka ushindi wa kwanza EPL

Liverpool watashuka dimbani kutafuta ushindi wa kwanza katika Ligi Kuu ya Uingereza (EPL) msimu huu wakiwa ugenini dhidi ya Ipswich Town hii leo katika uwanja wa Portman Road. The Reds walianza msimu kwa sare ya 2-2 dhidi ya Newcastle United kabla ya kurudia matokeo hayo hayo katika mechi yao iliyofuata dhidi ya Nottingham Forest. Hata hivyo, kikosi hicho sasa kinatumai kuondoka na alama zote tatu katika mechi ya wiki hii, huku usajili mpya wa thamani ya pauni milioni 123 (Sh21 bilioni), Bradley Barcola, akiwa sehemu ya kikosi. Kocha Andoni Iraola anatarajiwa kuendelea kumtegemea kipa Alisson Becker kati ya milingoti, huku akiwa na ulinzi wa nahodha Virgil van Dijk pamoja na beki wa kati mwenye umri wa miaka 21, Jeremy Jacquet. Baada ya juhudi za Liverpool kumsajili Malo Gusto kutoka Chelsea kushindikana dakika za mwisho, Jeremie Frimpong anatarajiwa kuanza katika nafasi ya beki wa kulia. Milos Kerkez, kwa upande wake, atakuwa akicheza upande wa kushoto wa safu ya ulinzi. Katikati ya uwanja, Ryan Gravenberch aliondolewa kwenye kikosi cha kwanza katika mchezo dhidi ya Forest na nafasi yake kuchukuliwa na Alexis Mac Allister. Nyota huyo wa Argentina anatarajiwa kuanza pamoja na Dominik Szoboszlai katika sehemu ya chini ya kiungo wa Liverpool. Katika safu ya mbele, Florian Wirtz anatarajiwa kucheza katika nafasi ya namba 10, huku akiwa na Victor Munoz na Cody Gakpo pembeni. Watatu hao watakuwa nyuma ya mvamizi Alexander Isak, ambaye anatarajiwa kuongoza safu ya mbele. Hatima ya Gakpo imekuwa gumzo baada ya uwezekano wa kuhamia Manchester City kusambaratika. Uhamisho huo ulifeli baada ya Liverpool kushindwa kupata mchezaji wa kumrithi kabla ya kumruhusu nyota huyo kuondoka. Wakati huo huo, Barcola anatarajiwa kupewa nafasi yake ya kwanza ya kuichezea Liverpool na kocha Iraola. Hata hivyo, huenda mchezaji huyo mpya akaanza mechi kwenye benchi na kuingia baadaye, badala ya kuanza moja kwa moja. Atakuwa sambamba na kinda mwenye umri wa miaka 18, Rio Ngumoha, kwenye benchi la Liverpool. The Reds wanafahamu vyema umuhimu wa kupata ushindi katika mchezo huo baada ya kuanza kampeni kwa sare mbili mfululizo. Ushindi dhidi ya Ipswich unaweza kuwapa msukumo mkubwa na kuimarisha matumaini yao ya kuwania nafasi za juu katika msimamo wa EPL. Kwa upande mwingine, Ipswich watakuwa na kazi ngumu ya kuzuia safu ya mbele ya Liverpool, ambayo inaonekana kuwa wembe.

read more
T

taifaleo.nation.co.ke

@taifaleo Fri, 04 Sep 2026 07:55:00

Kaunti zapambana kuokoa huduma za Ukimwi baada ya ufadhili wa Amerika kukatika

KUPUNGUZWA ghafla kwa ufadhili wa kimataifa wa afya kumezilazimisha kaunti zenye idadi kubwa ya watu wanaoishi na virusi vya Ukimwi kubuni njia mpya za kuhakikisha huduma haziathiriki. Homa Bay, Kisumu, Siaya, Migori na Mombasa ni miongoni mwa kaunti zinazokabili changamoto hiyo baada ya misaada kutoka kwa wafadhili wa kimataifa, hasa Mpango wa Dharura wa Rais wa Amerika wa Kukabiliana na Ukimwi (PEPFAR), kupungua. Kwa miaka mingi, fedha hizo zilisaidia kugharamia wahudumu wa afya, usambazaji wa dawa na vifaa, pamoja na huduma maalumu kuhusu Ukimwi. Tathmini iliyochapishwa Aprili 2025 na Harm Reduction International (HRI) na Kenya Legal Ethical Issues Network on HIV and AIDS (KELIN) ilionyesha ukubwa wa pengo hilo. Takriban kliniki 28 zilizokuwa zikitoa huduma za Ukimwi na tiba ya uraibu wa dawa za kulevya zililazimika kufungwa au kupunguza shughuli. Ripoti hiyo ilikadiria kuwa Serikali ya Kenya ingehitaji takriban Sh66.9 bilioni kufidia kikamilifu pengo lililoachwa na kupunguzwa kwa ufadhili wa Amerika. Hata hivyo, kaunti zimeanza kutumia mapato yao na kuunganisha huduma za Ukimwi na huduma nyingine za afya ili kuendelea kuwahudumia wagonjwa. Mwenyekiti wa Kamati ya Afya ya Baraza la Magavana na Gavana wa Mombasa Abdulswamad Shariff Nassir alisema mpito huo umekuwa wa hatua kwa hatua badala ya kusitisha huduma ghafla. "Kaunti zinatumia fedha zao za kuboresha vituo vya afya (FIF) kusaidia mahitaji yanayoendelea," alisema. Huko Migori, asilimia 30 ya fedha zinazokusanywa kila mwezi kupitia FIF hutumika kununua dawa na vifaa kulingana na mahitaji ya vituo. Afisa Mkuu wa Afya wa kaunti hiyo Caleb Opondi alisema pia wanapata msaada kutoka kwa washirika wa eneo hilo. Migori pia imeanza kuwaajiri baadhi ya wahudumu wa afya waliopoteza ajira baada ya wafadhili kusitisha ufadhili. Kisumu imeunda kamati maalumu ya mpito inayoongozwa na Naibu Gavana Matthew Ochieng ili kuandaa kaunti kukabiliana na mabadiliko hayo na kuwaajiri baadhi ya wahudumu walioathirika. Kaunti pia imeanza kupata fedha moja kwa moja kupitia makubaliano ya ushirikiano na Kituo cha Kudhibiti na Kuzuia Magonjwa cha Amerika (CDC). Homa Bay nayo imeunganisha huduma za Ukimwi na kifua kikuu (TB) katika huduma za kawaida za wagonjwa wa nje badala ya kuziendesha katika kliniki maalumu za Ukimwi. Afisa Mkuu wa Afya Grace Osewe alisema kaunti inalenga kuhakikisha huduma zinaendelea bila kuathiriwa na mabadiliko ya ufadhili. "Kuondoka kwa wafadhili hakupaswi kusababisha kukatizwa kwa huduma wala kupoteza mafanikio ambayo Homa Bay imepata katika kudhibiti Ukimwi na TB," alisema. Homa Bay pia imeongeza mafunzo kwa wahudumu wa afya na kutumia Wahudumu wa Afya ya Jamii (CHPs) kuwafikia wagonjwa katika jamii. Siaya imechukua hatua kama hiyo kwa kuunganisha huduma za Ukimwi na magonjwa mengine sugu. Hatua hiyo pia inalenga kupunguza unyanyapaa kwa kuhakikisha wagonjwa wote wanapata huduma katika sehemu moja. Nairobi imeanza kutumia mapato kutoka kwa Mamlaka ya Afya ya Jamii (SHA) kugharamia huduma. Kaunti hiyo imekusanya Sh1.8 bilioni kutoka SHA tangu Oktoba mwaka jana na sehemu ya fedha hizo inatumika kuendesha vituo vya afya. Afisa wa Afya ya Kinga Nairobi, Dkt Carol Ngunu, alisema karibu wahudumu 600 waliokuwa wakifanya kazi katika kliniki zilizokuwa zikifadhiliwa na washirika wamechukuliwa na kaunti. Hata hivyo, kupunguzwa kwa ufadhili kumeathiri zaidi huduma maalumu kwa watu wanaotumia dawa za kulevya, wakiwemo wanaopokea tiba ya methadone. HRI na KELIN zinakadiria kuwa Kenya ina takriban watu 27,056 wanaodunga dawa za kulevya, huku kiwango cha maambukizi ya HIV miongoni mwao kikiwa asilimia 11.3. Baadhi ya vituo vimefungwa kutokana na ukosefu wa fedha, huku vingine vikikabiliwa na uhaba wa dawa na huduma za ushauri nasaha. Changamoto hizo zimeongeza shinikizo kwa kaunti kuhakikisha kuwa kupungua kwa misaada ya kimataifa hakubadili huduma zinazohusiana na Ukimwi kuwa janga jipya la afya ya umma.

read more