T

taifaleo.nation.co.ke

@taifaleo Fri, 04 Sep 2026 04:55:20

Mwanamume ataka ukosefu wa nguvu za kiume utambuliwe kama ulemavu

MWANAUME mmoja Mkenya anataka matatizo kama vile ukosefu wa nguvu za kiume yatambuliwe kisheria kama ulemavu. Katika ombi alilowasilisha Bungeni, Dkt Benson Kibore amesema tatizo la nguvu za kiume na ukosefu wa hamu ya kushiriki mapenzi, hali inayojulikana kama HSDD, linahitaji kushughulikiwa kupitia sheria na sera za afya. Anasema matatizo haya, ambayo hapo awali yalihusishwa zaidi na wazee, sasa yanaonekana pia miongoni mwa vijana. Dkt Kibore anarejelea utafiti wa 2026 uliofanywa Nairobi na kuchapishwa kwenye medRxiv, ambao ulionyesha kuwa asilimia 10.4 ya vijana waliofanyiwa utafiti walikuwa na tatizo la nguvu za kiume. Wastani wa umri wao ulikuwa miaka 27. "Kwa hivyo, ukosefu wa hamu ya ngono unaohusishwa na tatizo la nguvu za kiume si tatizo la wazee pekee bali ni hali inayowakumba vijana pia," alisema katika ombi lake kwa Bunge la Kitaifa na Seneti. Dkt Kibore pia anataka HSDD itambuliwe kama suala la afya ya umma ili wanaohitaji matibabu waweze kupata huduma hiyo. Anasema matatizo ya ukosefu wa nguvu za kiume yanaweza kuathiri afya ya akili, ndoa, mahusiano na afya ya uzazi. Katika ombi hilo la Julai, anataja kutoridhika katika ndoa, kutengana kihisia, msongo wa mawazo, kuvunjika kwa mahusiano na ukosefu wa uaminifu katika ndoa kama baadhi ya madhara yanayoweza kuwapata waathiriwa. Iwapo Bunge litaidhinisha pendekezo hilo, sheria kadhaa zitalazimika kufanyiwa marekebisho, zikiwemo Sheria ya Watu Wenye Ulemavu na Sheria ya Bima ya Afya ya Jamii (SHA). Mabadiliko hayo yanaweza kuwezesha watu wenye matatizo sugu ya kingono yaliyothibitishwa kutambuliwa chini ya vigezo vya ulemavu. Pia, huduma kama uchunguzi, ushauri nasaha na matibabu zinaweza kugharamiwa kupitia Mamlaka ya Afya ya Jamii (SHA). Dkt Kibore anasema gharama ya matibabu imekuwa kikwazo kwa Wakenya wengi. Wagonjwa wengi hulipia huduma kutoka mifukoni mwao, huku ada za mashauriano katika hospitali za kibinafsi zikianzia takriban Sh5,000 na gharama ya matibabu kufikia mamia ya maelfu ya shilingi. Upasuaji wa uume, unapohitajika, unaweza kugharimu zaidi ya Sh1 milioni. Dkt Kibore pia anasema tatizo hilo linaweza kusababisha mtu kukosa kujiamini na kuathiri afya ya akili. Anarejelea pia utafiti mwingine unaoonyesha uhusiano kati ya hamu ya kushiriki ngono na afya ya moyo. Anasema kuwa kudumisha hamu nzuri ya ngono kunaweza kuwa na manufaa kwa afya ya moyo na mwili kwa ujumla. Dkt Kibore anasema unyanyapaa unaohusishwa na matatizo ya kingono huwazuia wanaume na wanawake wengi kutafuta matibabu. "Unyanyapaa unaozunguka matatizo ya kingono kwa wanaume na wanawake mara nyingi huwazuia kutafuta msaada, hivyo kuongeza muda wa mateso ndani ya familia," alisema.

read more
T

taifaleo.nation.co.ke

@taifaleo Fri, 04 Sep 2026 03:55:21

Rais kukita kambi Kajiado siku 3 kukagua miradi na kupigia debe 'rekodi yake ya maendeleo'

RAIS William Ruto ameanza ziara ya siku tatu katika Kaunti ya Kajiado, hatua inayotafsiriwa na wachambuzi kama juhudi za kuimarisha maendeleo na wakati huo huo kujiweka katika nafasi nzuri kisiasa kuelekea uchaguzi mkuu wa mwaka 2027. Rais anatarajiwa kuzuru maeneo mbalimbali ya Kajiado kati ya jana Septemba 3 na Septemba 7 kukagua na kuzindua miradi ya umeme, barabara, unyunyuzaji, masoko ya kisasa, nyumba za gharama nafuu na mabweni ya wanafunzi. Ingawa ziara hiyo imewasilishwa kama ya maendeleo, wengi wanasema ina uzito wa kisiasa kutokana na umuhimu wa kura za jamii ya Maa inayopatikana hasa katika kaunti za Kajiado, Narok na Samburu. Kaunti hizo tatu zina zaidi ya wapigakura milioni 1.09 waliosajiliwa. Ziara hiyo imejiri wiki chache baada ya Rais Ruto kufanya ziara ya siku mbili Narok, ambapo alizindua miradi kadhaa ya maendeleo na kusisitiza ushirikiano kati ya UDA na ODM. Akiwa Narok, Rais alisema kuwa hapo awali kura za eneo hilo zilikuwa zikigawanywa kati yake na aliyekuwa kiongozi wa ODM, Raila Odinga, lakini sasa ana matumaini ya kupata uungwaji mkono mkubwa kutokana na ushirikiano wa vyama hivyo viwili. Akiwa Kajiado, Rais atakagua miradi mbalimbali ikiwemo soko la kisasa la Kimana, mpango wa nyumba za bei nafuu Oloitoktok, mradi wa umeme wa Sultan Hamud-Loitoktok, masoko Namanga na Kajiado Town pamoja na miradi ya maji na barabara. Hata hivyo, Rais anakabiliwa na ushindani kutoka kwa chama cha Democracy for the Citizens Party (DCP) kinachoongozwa na aliyekuwa Naibu Rais Rigathi Gachagua. Bw Gachagua amekuwa akifanya ziara za mara kwa mara katika maeneo ya Maa akijaribu kuvutia viongozi na wapigakura wa eneo hilo. Kwa zaidi ya wapigakura nusu milioni Kajiado pekee, eneo hilo linaonekana kuwa uwanja muhimu wa mapambano ya kisiasa kuelekea uchaguzi wa 2027. Wachambuzi wanasema ziara ya Rais ni uwekezaji wa mapema wa kisiasa pamoja na juhudi za kuonyesha rekodi ya maendeleo ya serikali yake.

read more