T

taifaleo.nation.co.ke

@taifaleo Thu, 03 Sep 2026 07:55:06

Moto wateketeza msitu wa Aberdare siku nne mfululizo

MOTO umeteketeza Msitu wa Aberdare siku nne mfululizo huku hifadhi wanyamapori, miti na maeneo muhimu ya vyanzo vya maji yakiteketea. Moto huo unateketeza Msitu wa Ndaragwa, eneo la Shamata, sehemu muhimu ya vyanzo vya maji ya Ziwa Olbolosat, Ol Kalou na maeneo mengine ya Ndaragwa. Maafisa wanashuku kuwa moto huo ulianzishwa kwa bahati mbaya na waliokuwa waliokuwa wakirina asali msituni. Hata hivyo, baadhi ya wakazi wanasema kuna imani ya zamani kwamba kuchoma msitu wakati wa ukame husaidia kuvuta mvua. Wanaamini moshi mweusi unaotokana na moto huunda mawingu ambayo baadaye huleta mvua. Serikali ya Kaunti ya Nyandarua na Huduma ya Misitu Kenya (KFS), ambazo zinaongoza juhudi za kuzima moto huo, zimesema zimelemewa na zinahitaji msaada wa dharura kutoka kwa mashirika mengine ya kuhifadhi mazingira na serikali ya kitaifa. Afisa Mkuu wa uhifadhi wa misitu wa Nyandarua Daniel Mkung alisema moto huo unateketeza eneo la nyanda za juu lenye mimea mikavu, hali inayofanya iwe vigumu kuuzima. "Moto uko katika eneo la nyanda za juu ambako kuna mimea mingi mikavu. Hali hii inafanya iwe vigumu zaidi kuudhibiti. Tunahitaji msaada wote tunaoweza kupata na tunapanga jinsi ya kuwasafirisha wazima moto zaidi hadi msituni," alisema. Alisema uchunguzi wa awali unaonyesha kuwa wachunaji wa asali huenda ndio walianzisha moto huo. Hata hivyo, imani kuhusu moshi kuvuta mvua imeibua mjadala mwingine kuhusu sababu ya moto za mara kwa mara msituni wakati wa ukame. Jackson Kieru, mwenye umri wa miaka 86, alisema baadhi ya watu bado wanaamini moshi wa moto huvuta mvua. "Baadhi ya watu wanaamini moshi mweusi unaotokana na kuchoma msitu huvutia mvua. Wanaamini mawingu ya moshi hubadilika kuwa mawingu yanayoleta mvua siku chache baadaye. Ni desturi ya zamani ambayo bado inaaminiwa," alisema. Millicent Wangui, 79, alisema amesikia imani hiyo tangu akiwa mdogo. "Miaka mingi iliyopita, vijana walikuwa wakichoma moto mashambani wakiamini utaleta mvua. Huenda hiyo ndiyo sababu baadhi yao wameanza kuchoma misitu," alisema. Lakini Bw Mkung alikataa imani hiyo akisema ni hatari. "Hizo ni imani potofu. Kwa kweli zinaweza kuchelewesha mvua kutokana na gesi zinazotokana na moshi. Miti inajulikana kusaidia kuvuta mvua na hatuwezi kupata mvua zaidi kwa kuharibu misitu," alisema. Alisema wazima moto wanakabiliwa na hali ngumu kutokana na mimea mikavu na upepo mkali unaosambaza moto kwa kasi. Kamanda wa KWS katika Kaunti ya Nyandarua Paul Wambugu alisema wazima moto kutoka Hifadhi ya Kitaifa ya Aberdare wametumwa kusaidia kuzima moto huo. Afisa Mkuu wa Maji na Tabianchi wa Nyandarua Wachira Mugo alisema hali inazidi kuwa mbaya huku timu za kaunti zikishindwa kufikia baadhi ya maeneo yaliyoathiriwa kutokana na eneo kuwa na miinuko mikali. "Serikali ya kaunti haina uwezo wa kutosha kudhibiti moto huu. Vifaa vyetu vya kuzima moto haviwezi kufika katika baadhi ya maeneo yaliyoathiriwa kutokana na hali ngumu ya ardhi. Wafanyakazi wetu wamelemewa," alisema. Alisema moto huo ulikuwa ukielekea katika maeneo muhimu ya vyanzo vya maji. Aliomba msaada wa KFS, KWS na Jeshi la Ulinzi la Kenya (KDF). Moto huo umechochewa na ukame wa muda mrefu ambao umefanya mimea kuwa mikavu sana pamoja na upepo mkali unaovuma upande wa magharibi wa msitu. Gavana wa Nyandarua Kiarie Badilisha ameitaka serikali kuchukua hatua za haraka kuzuia moto huo usiharibu maeneo muhimu ya vyanzo vya maji.

read more
T

taifaleo.nation.co.ke

@taifaleo Thu, 03 Sep 2026 06:55:14

Tiketi ya Boga, Mangale kumbwaga Achani yazua tumbojoto Kwale

SIASA za ugavana katika Kaunti ya Kwale zimechukua mkondo mpya baada ya mvutano kuibuka kuhusu mpango wa kumtaka Mwenyekiti wa Bodi ya Chuo cha Ubaharia cha Bandari, Bw Lung'anzi Mangale, awe mgombea mwenza wa ugavana wa aliyekuwa Katibu wa Wizara ya Kilimo, Prof Hamadi Boga, katika Uchaguzi Mkuu wa Agosti 10, 2027. Hatua ya kuwaunganisha wanasiasa hao wawili ambao wote waliwania ugavana 2022, inalenga kutoa ushindani mkali dhidi ya Gavana Fatuma Achani, ambaye anatarajiwa kutetea kiti hicho kupitia tikiti ya Chama cha UDA. Wazee wa jamii ya Wadigo, wakiongozwa na msemaji wao Bw Chirau Makwere, ambaye pia aliwania ugavana 2022, walisema waliamua kuunga mkono Prof Boga kuwania ugavana na Bw Mangale kuwa mgombea mwenza. Wazee hao sasa wamempa aliyekuwa Prof Boga makataa ya wiki mbili kutangaza wazi mgombea mwenza wake ili kuzima sintofahamu zilizoibuka hivi majuzi baada ya kubainika kuwa, huenda Bw Mangale akaamua kuwania ugavana. "Tumeamua kwamba Prof Boga atuambie naibu wake ni nani ndani ya wiki mbili zijazo. Pia tunataka Bw Lung'azi atangaze kwa kauli yake kwamba atakuwa naibu wa Prof Boga. Hatuna msimamo mwingine isipokuwa Prof Boga kuwa mgombea wa ugavana na Bw Lungazi kuwa naibu wake," alisema Bw Makwere. Akiongea kwenye mahojiano ya redio, Bw Makwere alisema iwapo Bw Mangale hatakuwa tayari kuwa mgombea mwenza wa Prof Boga, watamruhusu apendekeze majina ya watu watatu ambao jamii itachagua mmoja wao. "Tumekuwa tukisikia sauti kutoka sehemu mbalimbali kwamba Bw Lungazi anataka kutangaza azma ya kuwa gavana. Sisi tumekataa. Tunataka awe naibu gavana. Na tutamimina kura mpaka waone," alisema Bw Makwere. Kwenye mahojiano tofauti, Bw Mangale alisema yuko kwenye kinyang'anyiro cha ugavana wa Kwale wala si kama mgombea mwenza. Alieleza kuwa, yuko kwenye chama cha ODM ingawa aliwania wadhifa huo kupitia Chama cha Pamoja African Alliance (PAA) katika uchaguzi uliopita. Haya yanajiri wiki kadhaa baada ya Prof Boga na Bw Mangale kutangaza kuwa wameamua kuweka tofauti zao kando na kuungana katika harakati za kuwania kiti hicho kwa lengo la kumbandua Gavana Achani katika uchaguzi mkuu ujao. Bi Achani amepata uungwaji mkono kutoka kwa baadhi ya viongozi wa ODM, lakini baadhi ya wanachama wamesisitiza chama hicho kina mgombea wake wa ugavana, ambaye ni Prof Boga. Katika mikutano yake ya hadhara, Bi Achani hupuuza wapinzani wake akidai wanaendeleza siasa za ukabila, na badala yake kutaka ushindani wa kisiasa uwe kwa misingi ya uwezo wa viongozi kuleta mandeleo kwa manufaa ya wananchi. "Ukabila huleta mgawanyiko katika jamii, kutokuaminiana, na hudunisha umoja wa kitaifa na kuathiri maendeleo. Kama Wakenya, tunafaa kukataa siasa za ukabila na badala yake tukumbatie umoja, uwiano na uongozi unaolenga masuala muhimu kwa manufaa ya kila mmoja," alisema hivi majuzi. Prof Boga na Bw Lungazi waliwania ugavana wa Kwale katika uchaguzi mkuu wa 2022, ambapo waliibuka wa pili na wa tatu mtawalia.

read more