T

taifaleo.nation.co.ke

@taifaleo Thu, 03 Sep 2026 03:55:28

Ruto aagiza sheria ipitishwe kuzuia wageni kufanya uchuuzi Kenya

RAIS William Ruto amesema kwamba haikubaliki kwa raia wa kigeni kuja nchini kufanya uchuuzi na biashara ndogo ndogo. Anasema wageni wana ruhusa ya kuwa wawekezaji pekee, sio kushindana na wenyeji katika biashara ndogo kama uchuuzi na maduka madogo madogo. Akizungumza baada ya kukutana na sehemu ya wafanyabiashara waliofanya maandamano wiki jana kulalamikia ushuru mpya wa KRA kuhusu shehena ya bidhaa za kutoka nje katika Ikulu ya Nairobi Jumatano, Rais aliagiza mawaziri husika kuharakisha mswada bungeni unaoharamisha aina fulani ya biashara kufanywa na raia wa kigeni. "Tuko na wafanyabiashara kutoka nchi zingine, wacha nisiseme nchi gani, wamekuja hapa na kuwa wachuuzi, wanauza duvets. Bw Mukwana na Lee Kinyanjui, tayari tuko na mswada bungeni kuhusu mambo ya biashara. Katika hiyo bill, tumesema kuna biashara mgeni hawezi kufanya hapa Kenya by law. Nataka mketi chini na hawa wafanyabiashara muangalie na tuzibe mianya yote. Isitokee kwamba mtu ametoka China na amekuja kuwa hawker au kuuza duka kidogo hapo. Ichungwa, you don't need any further instructions. Monday muamkie hiyo biashara. Hao wachuuzi wote wanafanya hii biashara kidogo kidogo wafunge na wasipofunga (ashangiliwa) tutafunga. Hatujajenga Investor Confidence ndio watu wakuje kuwa wachuuzi. Tumejenga Investor Confidence ndio watu wakuje kuwekeza," akasema Bw Ruto. Katika maandamano ya Agosti 28, 2026, waandamanaji walikusanyika katika eneo la Archives kabla ya kuelekea makao makuu ya KRA katika jengo la Times Tower katikati mwa jiji. Wafanyabiashara hao walisema mabadiliko ya kiwango kinachotumiwa kukadiria thamani ya bidhaa za uagizaji yameongeza gharama za biashara na kupunguza faida zao. Kwa mujibu wao, KRA imepandisha kiwango cha ukadiriaji kutoka 2.5m hadi 3.2m, hatua wanayodai imeongeza kwa kiasi kikubwa kodi inayolipwa kwa bidhaa zinazoagizwa kutoka nje, hususan kutoka China. Walisema mabadiliko hayo yamesababisha ongezeko la takriban asilimia 28, huku thamani ya bidhaa kwa madhumuni ya kodi ikiongezeka kutoka Sh2.5 milioni hadi Sh3.2 milioni.

read more
T

taifaleo.nation.co.ke

@taifaleo Thu, 03 Sep 2026 02:55:31

IEBC, NCIC na Polisi watoa tahadhari kuhusu dalili za hatari uchaguzi mkuu ujao

KENYA inapoelekea uchaguzi mkuu wa 2027, tayari kuna ishara za hatari zinazoweza kuzua vurugu na kuzamisha nchi katika mzozo wa kisiasa, kiuchumi na kijamii. Vurugu katika mikutano ya kisiasa, matamshi ya chuki, madai ya wizi wa kura, mizozo kuhusu zabuni za mabilioni ya fedha, taarifa za uongo na kupungua kwa imani kwa taasisi za uchaguzi ni baadhi ya changamoto zinazotajwa. Masuala hayo yalijadiliwa jana katika mkutano wa kitaifa wa usalama wa uchaguzi uliofanyika Nairobi. Tume Huru ya Uchaguzi na Mipaka (IEBC), Tume ya Kitaifa ya Uwiano na Utangamano (NCIC), Polisi, Ofisi ya Mkurugenzi wa Mashtaka ya Umma (ODPP) na Idara ya Mahakama zilitahadharisha kuhusu umuhimu wa kujifunza kutokana na machungu ya ghasia za baada ya uchaguzi wa 2007/08. Ghasia hizo zilisababisha vifo vya zaidi ya watu 1,100, 3,500 kujeruhiwa na hadi 600,000 kuhama makazi yao. Ripoti ya Kofi Annan Foundation ya Electoral Vulnerability Index ya 2026–2027 iliyotolewa Julai ilianika uwezekano wa Kenya kukumbwa na aina fulani ya ghasia zinazohusiana na uchaguzi kuwa asilimia 81.6. Ripoti hiyo ilitaja ukosefu wa imani kwa IEBC, ugumu wa maisha, ukosefu wa ajira kwa vijana, siasa za ukabila na wasiwasi kuhusu mwenendo wa polisi wakati wa maandamano. Mwenyekiti wa IEBC Erastus Ethekon alisema tume hiyo imekuwa ikielekezewa na madai mazito kutoka kwa viongozi wa kisiasa kuhusu maandalizi ya uchaguzi wa 2027. Alisema madai yasiyothibitishwa yanaweza kudhoofisha imani ya wananchi katika IEBC kabla kampeni hazijaanza kikamilifu. "Tunahitaji kuchunguza ukweli kuhusu baadhi ya madai haya ya ajabu ambayo yanalenga kuwafanya Wakenya waamini kwamba uchaguzi hautakuwa huru na wa haki," alisema. Kauli yake ilijiri baada ya aliyekuwa Naibu Rais Rigathi Gachagua kudai IEBC inapanga kuiba uchaguzi wa 2027 kupitia mfumo mpya wa usimamizi wa uchaguzi. Pia kuna mzozo kuhusu zabuni ya mabilioni ya fedha ya mfumo wa teknolojia utakaotumiwa katika uchaguzi huo. Bw Ethekon alisema IEBC italinda uhuru wake na kupinga juhudi zozote za kudhoofisha uaminifu kwa tume. Alisema hata hivyo IEBC haiwezi kufanikisha uchaguzi wa kuaminika bila ushirikiano wa polisi, mahakama na taasisi nyingine. Mkurugenzi wa Mashtaka ya Umma Renson Ingonga alionya kuwa uchunguzi dhaifu na ukosefu wa ushahidi unatatiza juhudi za kuwafungulia mashtaka wahusika wa vurugu za kisiasa na uchochezi. Aliwataka polisi na DCI kukusanya ushahidi unaohusisha washukiwa na uhalifu, wakiwemo wale wanaofadhili au kupanga makundi ya vijana wanaotumika kuvuruga mikutano. Alisema kuwakamata vijana pekee bila kuwafuatilia wanaowafadhili hakutamaliza tatizo. Mwenyekiti wa NCIC, Askofu Kepha Omae, alisema tume hiyo ina wasiwasi kuhusu kuongezeka kwa matamshi ya chuki na uchochezi kadiri shughuli za kisiasa zinavyozidi. Alisema NCIC itachukua hatua dhidi ya wanasiasa na Wakenya wengine wanaokiuka sheria kupitia kauli zao. Tume hiyo pia imekuwa ikifuatilia jumbe zinazosambazwa kwenye mitandao ya kijamii, ikiwemo WhatsApp na TikTok. Inspekta Jenerali wa Polisi Douglas Kanja alisema Polisi wameanza kutekeleza mpango wa usalama wa uchaguzi wa 2027. Jaji Daniel Musinga, aliyekuwa mgeni rasmi, alisema vitisho vipya kama matamshi ya chuki, taarifa za kupotosha, propaganda za kisiasa na matumizi ya teknolojia kuwanyanyasa wanawake kisiasa vinahitaji taasisi mbalimbali kushirikiana.

read more