T

taifaleo.nation.co.ke

@taifaleo Sun, 30 Aug 2026 05:55:49

Kalonzo avamia ngome ya Ruto Taita Taveta na kutumia mzozo wa ardhi kumshambulia

VIONGOZI wa upinzani Jumamosi walivamia Taveta, eneo linalotajwa kuwa ngome ya kisiasa ya Rais William Ruto, wakitumia mzozo wa ardhi na madai ya kufurushwa kwa wakazi kuishambulia serikali. Msafara huo uliongozwa na kiongozi wa Wiper Patriotic Front, Kalonzo Musyoka, Ulifika Mkocheni, karibu na shamba la Rais Ruto la Eldoro, ambako familia kadhaa zilizofurushwa takriban mwaka mmoja uliopita bado zinaishi katika kambi. Viongozi hao walishutumu serikali kwa madai ya kutumia maafisa wakuu kuwaondoa wananchi kwenye ardhi na kuwaacha bila makao. Katika msafara huo walikuwa kiongozi wa Democratic Party, Justin Muturi, kiongozi wa DAP-Kenya, Eugene Wamalwa, aliyekuwa Waziri wa Utumishi wa Umma, Aisha Jumwa, Mbunge wa Wundanyi ,Danson Mwashako na zaidi ya wabunge 20. Bw Musyoka aligeuza mzozo huo kuwa shambulizi kali dhidi ya Rais Ruto, akidai Rais alinunua takriban ekari 2,000 kutoka kwa mfanyabiashara Basil Criticos lakini baadaye akaongeza eneo hilo, hatua aliyosema imewaacha wenyeji bila makao. "Rais aliuziwa ekari 2,000 pekee na Basil Criticos lakini ameongeza, na kuwaacha wenyeji bila makao," alisema Bw Musyoka. Pia alikosoa matumizi ya fedha za umma kujenga barabara zinazoelekea katika shamba la Rais, akisema rasilimali za serikali zinafaa kuwanufaisha wananchi. "Leo tumeshangaa kuona Ikulu nyingine ikijengwa Taveta kwa gharama ya watu wa Taveta," alisema. Bw Muturi naye alitoa madai mazito akisema alipokuwa Mwanasheria Mkuu aliidhinisha stakabadhi za kuharakisha ujenzi wa barabara Taveta bila kujua kuwa zingemfaidi Rais moja kwa moja. "Ningejua stakabadhi nilizokuwa nikitia saini zingemfaidi Rais moja kwa moja, ningechukua hatua tofauti," alisema. Wakati huo huo, wakazi wa Jipe wamekuwa wakitaka ua unaozunguka ardhi yenye mzozo kuondolewa kufuatia uamuzi wa Mahakama ya Mazingira na Ardhi uliowaunga mkono. Wakazi hao wanadai ekari 3,000 zilitolewa kwa mpango wa Jipe-Taveta Settlement kuwawezesha maskwota kupata ardhi. Sasa wanataka serikali kutekeleza uamuzi wa mahakama, kuwarejesha waliofurushwa na kuwapa hatimiliki ili kumaliza mzozo huo wa miaka mingi. Kalonzo alimlaumu rais kwa kushindwa kukabili gharama ya maisha na kuongezeka kwa umaskini nchini. Bw Musyoka alisema serikali ya Kenya Kwanza imekuwa ikitumia vitisho, pesa na ahadi za kisiasa kuwavutia viongozi wa upinzani kwa lengo la kuimarisha nafasi ya Rais Ruto kuelekea uchaguzi ujao. Aliwashutumu viongozi wa serikali kwa kujaribu kudhoofisha upinzani kwa kuwashawishi wabunge, maseneta na magavana kujiunga na Kenya Kwanza. Bw Musyoka alimlenga Mbunge wa Taveta John Bwire, ambaye alisema alimsaidia kushinda uchaguzi wa 2022 lakini sasa anafanya kazi kwa karibu na chama tawala cha UDA. "Ninawashukuru viongozi wangu wa Wiper walioamua kutojiunga na Kenya Kwanza. Chama tawala kijue kuwa Wiper bado ni chama imara. Inasikitisha kumuona mbunge wangu wa Taveta John Bwire, ambaye nilimpigia kampeni, sasa akiwa msemaji wa UDA hapa," alisema.

read more
T

taifaleo.nation.co.ke

@taifaleo Sun, 30 Aug 2026 03:55:52

Meneja Mkuu wa KCB Bank, Rosemary azikwa usiku kinyume na amri ya mahakama

MZOZO kuhusu kifo cha Rosemary Chemutai Koech, meneja mkuu wa Benki ya KCB, na 'umiliki' wa mwili wake umechukua mkondo mpya baada ya familia yake kumzika usiku wa kuamkia Jumamosi licha ya amri ya mahakama iliyositisha mazishi hayo kwa muda. Rosemary, aliyekuwa mkuu wa kitengo cha ulinzi wa data KCB, alifariki Agosti 21 akiwa na umri wa miaka 40 katika nyumba yake ya Ngong, Kaunti ya Kajiado. Kifo chake kilitokea alipokuwa amejitenga na mumewe, Kevin Migwe Kimwatu, kufuatia matatizo ya ndoa. Mapema Ijumaa, Mahakama ya Milimani jijini Nairobi iliamuru kwa muda mazishi yake kufanyika na ikazuia Lee Funeral Home kutoa mwili huo hadi kesi iliyowasilishwa na mumewe isikizwe na kuamuliwa. Hakimu Mkuu Mwandamizi Agnes Mwangi alitoa amri ya kuzuia wanafamilia, Lee Funeral Home na KCB kuhamisha mwili wa marehemu. Pia alisema mazishi yasifanyike bila idhini ya mume wa marehemu. Hata hivyo, mazishi yalifanyika saa saba na nusu usiku katika kijiji cha Chepseon, eneo la Kipkelion Mashariki, Kaunti ya Kericho. Akizungumza na waombolezaji Jumamosi, mwenyekiti wa ukoo Samwel Keter alisema familia iliamua kufanya hivyo kwa kuzingatia mila za Kalenjin. "Yanayosambazwa mitandaoni si ya kweli. Binti yetu alifariki na kwa mujibu wa utamaduni wetu, mtu wa aina hiyo hapaswi kukaa bila kuzikwa kwa zaidi ya siku tatu au nne. Pia, baada ya uchunguzi wa maiti kufanyika, mazishi yanapaswa kufanyika ndani ya siku mbili. Tulifanya tulichofanya kwa kuzingatia mila zetu ili tukio kama hilo lisijirudie," alisema Keter. Mwanachama wa Shirika la Koo za Jamii ya Kipsigis, Joseph Towett Kalyasoi, alisema si jambo la ajabu kwa jamii hiyo kufanya mazishi baada ya jua kutua. "Zamani, miili ilikuwa ikizikwa usiku miongoni mwa jamii ya Kipsigis, ndiyo maana hadi leo baadhi ya shughuli za mwisho za mazishi hufanyika jioni sana. Hii ni mila ya muda mrefu," alisema. Towett aliongeza kuwa wazazi wa mwanamke aliyeolewa wakiamua kumzika kutokana na tofauti kati yake na mumewe, basi wanapaswa kurejesha mahari iliyolipwa wakati wa ndoa. Wakati huo huo, imebainika kuwa mwili wa Rosemary ulihamishwa kutoka Nairobi kwenda Kericho siku tatu kabla ya mazishi huku mvutano ukiendelea kati ya wazazi wake na mumewe. Chanzo cha familia kilichozungumza kwa siri kilisema hata baadhi ya wanachama wa kamati ya mazishi hawakujua mahali mwili ulikokuwa hadi ulipoondolewa mochari. Ulinzi mkali wa polisi katika makazi ya familia ulivutia hisia za majirani huku ndugu wa karibu wakisimamia taratibu za mazishi. Kwa upande wake, Kimwatu alikuwa ameenda mahakamani kuomba wazazi wa marehemu, Paul Kipkorir Koech na Beatrice Koech, pamoja na dadake Judy Koech-Oyamo na KCB, wazuiwe kuendelea na mipango ya mazishi. Alidai kuwa alikuwa ametengwa katika maandalizi ya mazishi licha ya kuwa mume halali wa Rosemary. Stakabadhi za mahakama zinaonyesha kuwa wawili hao walifunga ndoa katika Kanisa Katoliki la St Austin mjini Nairobi mnamo Agosti 24, 2013 na walibarikiwa kupata watoto wanne. Kimwatu alikiri kuwa ndoa yao ilikuwa na changamoto lakini akasema walikuwa katika juhudi za kumaliza tofauti zao na waliendelea kuwasiliana mara kwa mara hadi siku ya kifo chake. "Ndoa yetu kwa ujumla ilikuwa ya upendo, furaha na ushirikiano. Kama ndoa nyingine zote, ilikuwa na changamoto zake, lakini hazikuwahi kufikia kiwango cha kuondoa upendo na furaha iliyokuwepo kati yetu," alisema katika stakabadhi za mahakama. Aliongeza kuwa walikuwa wameachana kwa muda wa miezi minne pekee na kwamba kabla ya kifo chake, Rosemary alikuwa amekubali kurejea nyumbani kwa familia yao. Kimwatu alisema kuwa kama mume wa kisheria alikuwa na haki ya kupanga mazishi ya mkewe na alikusudia kumzika katika makazi ya familia yao huko Matasia, Ngong, Kaunti ya Kajiado. Kesi hiyo imepangwa kutajwa tena mahakamani Agosti 31 huku maswali yakisalia kuhusu utekelezaji wa amri ya mahakama na uhalali wa mazishi yaliyofanyika Kericho.

read more
T

taifaleo.nation.co.ke

@taifaleo Sun, 30 Aug 2026 04:55:07

Azma ya Raila Jnr Kibra yachemsha Orero, Imran

KUJITOSA kwa Raila Junior katika kinyang'anyiro cha ubunge wa Kibra, Nairobi, kumeanza kuzua pingamizi miongoni mwa baadhi ya wawaniaji wa ODM, huku mwana huyo mdogo wa aliyekuwa Waziri Mkuu Raila Odinga akisaka kiti hicho 2027. Kibra kwa miongo imekuwa ngome ya kisiasa ya familia ya Odinga. Marehemu Raila aliwakilisha eneo hilo bungeni kuanzia 1992 hadi 2013, wakati Kibra ilikuwa sehemu ya Lang'ata. Kila mara nchi ilipokabiliwa na maamuzi magumu ya kisiasa, Raila alirejea Kibra kutoa mwelekeo ambao baadaye ulikumbatiwa na maeneo mengine nchini. Mnamo Novemba 30, 2009 wakati wa mvutano kuhusu uamuzi wa kufurusha watu kutoka msitu wa Mau, Raila alitangaza hadharani kwamba alikuwa tayari kurejea Kibra akapike mandazi iwapo suala hilo lingemgharimu kisiasa. Kuingia kwa Raila Junior katika kivumbi hicho kumezua ushindani mkali wa kisiasa kati yake, mbunge wa sasa wa Kibra Peter Orero na aliyekuwa mbunge wa hapo Imran Okoth. Junior amekuwa akishiriki miradi ya kijamii na kukutana na makundi mbalimbali huku akiweka misingi ya kampeni zake kuelekea 2027.  "Kibra ilikuwa ngome ya kisiasa ya babangu, na kama familia tumekuwa na safari ndefu pamoja na watu wa eneo hili. Nikichaguliwa, nitamakinikia sana elimu kwa kuhakikisha kuwa basari zinapatikana ili hakuna mtoto anayekosa fursa ya kupata elimu," Raila Junior alisema katika mahojiano na Taifa Leo. "Najua baadhi ya sekta, kama afya na maji, zimekabidhiwa serikali za kaunti, lakini nitafanya kila niwezalo kuhakikisha huduma hizi zinawafikia watu wa Kibra. Tutazingatia sana kuboresha maisha ya wakazi wa eneo hili kwa kila njia iwezekanavyo," akaongeza. Junior pia alifichua kwamba kwa miaka mingi alikuwa mmoja wa waliompangia babake mikakati ya kisiasa Kibra. Wiki hii, mama yake, Ida Odinga, alipokuwa akisherehekea siku yake ya kuzaliwa, alitangaza kwamba amempa Raila Junior baraka za kutimiza ndoto zake za kisiasa, ikiwemo azma yake ya kuwania ubunge wa Kibra. "Nyinyi watu wa Kibra mmeamua, na sina chaguo jingine. Namkabidhi mwanangu mikononi mwenu. Viongozi mlio hapa, mtunze, mfundishe na mpe mwongozo. Wengi wenu mlianza siasa pamoja na Baba. Mwonyesheni njia," akasema Mama Ida. Alisisitiza kwamba siasa za Junior zinapaswa kuwa safi na zisizo na matusi wala vurugu, akisema Kibra, ilikuwa msingi wa safari ya kisiasa ya familia ya Odinga. "Washawishi watu kwa maneno yako na uwaambie kile unachoweza kuwafanyia," akasema. Hata hivyo, Bw Orero anadai kwamba Junior anasukumwa na baadhi ya wawakilishi wa wadi wateule ambao hawana ushawishi wa kisiasa Kibra. Alisisitiza kuwa yuko tayari kukutana naye kwenye uchaguzi.  "Baadhi ya wawakilishi wadi maalum wanaomsukuma wamepoteza uchaguzi mara nne na wanalenga maslahi yao binafsi. Hata hivyo, kazi yangu kwa watu wa Kibra iko wazi kwa kila mtu kuiona. Kwa sasa sina mpinzani. Aje tushindane, nami nitamshinda," akasema Bw Orero. Mbunge huyo alishangaa kwa nini Raila Junior ameingia kwenye kinyang'anyiro hicho ilhali dada yake, Winnie Odinga, aliwahi kukinyemelea kabla ya kujiondoa na kuelekeza nguvu zake katika kinyang'anyiro cha useneta wa Nairobi.  "Winnie alikuja kwangu mwenyewe na kuniambia kwamba anataka kuwania useneta wa Nairobi na kwamba hana nia tena ya kugombea Kibra. Sasa Raila Junior anasukumwa, lakini niko tayari. Ninaiheshimu familia ya Odinga na nina imani nitashinda uteuzi wa ODM," akaongeza. Bw Orero alisema licha ya kuwa karibu na familia ya Odinga, hajazungumza na Mama Ida kuhusu azma ya Junior. "Kuna nini cha kuzungumza? Junior ana haki yake ya kidemokrasia na sitaki kuwadharau au kuonekana niko kwenye vita nao. Waache watu waamue," akasema. Bw Orero alisema wakati wa uongozi wake ameboresha elimu kuimarisha michezo pamoja na kujenga na kukarabati barabara kadhaa Kibra. "Nilichofanya kinazidi kazi ya watangulizi wangu tangu 2013. Nimesambaza zaidi ya Sh65 milioni za bursari na, mbali na CDF, kuna miradi mingi tumekamilisha kupitia Benki ya Dunia. Mimi ni mbunge mwenye bidii, kwa hivyo atanishinda aje ?" akauliza. Kwa upande wake, aliyekuwa mbunge Imran Okoth ametishia kuondoka ODM na kuwania kiti hicho kama mgombea huru iwapo chama hakitaendesha uteuzi wa haki na huru. "Uteuzi wa 2022 haukuwa wa haki na huru. Mara hii, watu wanastahili kupata nafasi ya kumchagua kiongozi wanayemtaka badala ya kulazimishiwa mtu. Nimekuwa nikifanya kampeni na ninaamini mimi ndiye mtu anayefaa kuwa mbunge," akasema Imran.  Bw Imran alichukua kiti hicho kutoka kwa marehemu kaka yake, Ken Okoth kupitia uchaguzi mdogo mnamo 2019 na anasema miaka yake miwili madarakani iliacha rekodi inayoonekana ya maendeleo. "Mbunge wa sasa hajafanya chochote, na Kibra inaanza kurejea ilivyokuwa awali. Nataka kurejea na kuendeleza kazi niliyoianza.  "Junior yuko huru kuja kuwania, lakini anapaswa pia kujua kwamba sisi ni wanachama wa ODM na tunasisitiza kusiwe na mapendeleo yoyote. Orero, Junior na mimi tushindane kwa haki, na atakayeshinda apewe tiketi ya ODM," akaongeza.

read more