T

taifaleo.nation.co.ke

@taifaleo Tue, 07 Jul 2026 08:58:12

MAONI: Dalili ziko wazi Muungano wa Upinzani hauna mshikamano

MUUNGANO wa upinzani umeangukiwa na mizimwi ya dhiki chungu nzima za kisiasa. Muungano huo umeendelea kubanwa katika kuandaa mikutano huru kwa kushambuliwa na wahuni mara kwa mara, viongozi katika upinzani nao wanajikanganya kwa kukosa kusema kwa kauli moja. Kila mmoja wao anahema kwa kishindo akitaka kuwa mgombea urais. Ingawa viongozi hao wanatangaza umoja katika kampeni zao wakati wa mchana, baadhi yao kama Caleb Amisi wamekosa imani na mrengo wa Linda Mwananchi na kujiunga na Chama cha PRM. Huenda Amisi ametabiri kusambaratishwa kwa mrengo huo na chamchela ya tamaa za viongozi wa upinzani. Kuna migogoro ya ndani kwa ndani katika upinzani na huenda hivi karibuni nyufa katika muungano huo zikaongezeka na upinzani kulemazwa zaidi kisiasa. Viongozi katika muungano huo hawana msimamo mmoja. Rigathi Gachagua anahisi kuwa mwaniaji wa urais wa muungano huo anafaa kutajwa uchaguzi unapokaribia huku Justin Muturi akitaka uteuzi ufanyike mapema. Ni nani wa kuaminika? Sifuna amepata nguvu mpya kutoka kwa viongozi wa Magharibi kuwania urais huku Kalonzo Musyoka akionekana bora zaidi kuchukua nafasi hiyo. Kenya Kwanza nayo imenoa makali yake na kujaribu kufuta nyayo za upinzani katika maeneo yaliyoonekana kushabikia upinzani. Kwanza, wapo viongozi wa Kenya Kwanza wanaoendelea kujitolea kushabikia serikali ukanda wa mlima Kenya uliodhaniwa kuwa ngome ya chama cha DCP. Moses Kuria, Kimani Ichungwa, Anne Waiguru na wengine wamebaki kupigia upatu awamu ya pili ya serikali ya UDA. Hii inasambaratisha kufaulu kwa upinzani kwani eneo hilo halina ari kubwa ya kuwa na mgombea wa urais. Siasa za kuwa uwepo wa Mlima Kenya Mashariki na Magharibi zimetokota. Kundi la Mashariki likishinikizwa kujiona tofauti na lile la Magharibi ili uzuia wananchi hao kushirikiana katika kufanya uamuzi wa kupiga kura. Hali hii itauzuia upinzani kunyakua kura nyingi hivyo kupiga jeki kapu la kura la UDA. Kufikia sasa, upinzani haujaweza kushirikiana kubuni sera za kuuongoza ili kuonyesha mshikamano wao. Kutia chumvi kwenye kidonda ni kuwa kuna kundi la Linda Mwananchi lililoonekana kushika kasi kisiasa na kutaka kujisimamia kisiasa. Hili litakuwa pigo kubwa katika muungano wa upinzani. Kuondoka kwa Caleb Amisi kutoka Linda Mwananchi huenda ukawa mwanzo wa kuyumba kwa upinzani. Viongozi na vyama vingine katika Linda Mwananchi bado wanasoma dalili na pengine watajiunga na Kenya kwanza kwa kuogopa kupigwa na baridi ya kisiasa kwani nguvu za upinzani huenda zikazidi kuwa hafifu na kufanya wakose kuchaguliwa katika maeneo yao. Ushabiki uliokuwepo wa vijana katika upinzani pia umepoa hivyo vijana huenda wanasubiri mwamko mpya wa kuwapa hamasa za kupiga kura. Kangai ni mwalimu na mchanganuzi wa masuala ya kisiasa.

read more
T

taifaleo.nation.co.ke

@taifaleo Tue, 07 Jul 2026 08:17:11

Viongozi vijana wapanga msafara wa amani Gusii baada ya shambulio la Linda Mwananchi

SIKU chache tu baada ya mtu mmoja kuuawa wakati wa shambulio dhidi ya msafara wa Linda Mwananchi huko Keumbu, viongozi vijana kutoka eneo la Gusii wametangaza msafara wa amani ili kuhubiri umoja na kulaani vurugu za kisiasa. Msafara huo wa Gusii uliopewa jina "Omorembe," neno la Ekegusii linalomaanisha amani, utaanza Alhamisi, Julai 9, 2026, kuanzia saa tatu asubuhi huko Keroka. Msafara huo utapita Keumbu, eneo la machafuko mabaya ya Ijumaa, kabla ya kuelekea Mjini Kisii na kuishia soko la Daraja Mbili. Waandaaji wanasema harakati hiyo haina upendeleo wowote na inalenga kuwaleta pamoja viongozi wa makanisa, viongozi wa jamii, Baraza la Wazee kutoka Jamii ya Abagusii, wasanii, wasamaria wema na vikundi vyote vya kisiasa. Mabango yaliyotolewa na waandaaji  na yaliyotiwa alama nyekundu, nyeusi na kijani kibichi yenye alama za mikono yenye damu, yana ujumbe mzito: "Acha umwagaji damu na vurugu." Haya yanajiri huku washukiwa saba waliokamatwa kuhusu shambulio hilo la Keumbu wakizuiliwa na mahakama ya Kisii Jumatatu. Hakimu Mkazi Mkuu Caroline Jeruto alitoa amri hiyo baada ya afisa aliyewakamata na mwendesha mashtaka kukosa kufika mahakamani na faili za kuwashtaki kwao. Mbunge wa Nyaribari Chache Zaheer Jhanda, pia bado hajatimiza wito wa kufika makao makuu ya Idara ya Uchunguzi wa Makosa ya Jinai (DCI) ya Kisii ili kuandikisha taarifa baada ya kuhusishwa na vurugu hizo. Shambulio dhidi ya msafara wa vuguvugu la Linda Mwananchi lilisababisha mtu mmoja kufariki na magari kadhaa kuharibiwa, likiwemo moja la Jaji Mkuu wa zamani David Maraga. "Lazima tuurudishe mji wa Keumbu sifa zake kama mahali pa amani, si vurugu. Hatuwezi kuruhusu siasa kuwageuza majirani kuwa maadui," alisema Gilbert Nyangaresi, kiongozi wa vijana kutoka Wadi ya Bobarcho, eneobunge la Nyaribari Chache. Ratiba ya msafara huo itakuwa na vituo vifupi katika kila mji kwa ajili ya hotuba za amani, sala zinazoongozwa na viongozi wa makanisa wa eneo hilo, na maonyesho ya wasanii wa Gusii. Huko Keroka, timu hiyo itawahutubia wakazi katika jukwaa kuu kabla ya kuondoka. Huko Keumbu, wanapanga kuweka shada la maua ili kumuenzi mtu aliyeuawa wiki iliyopita. Mji wa Kisii utaandaa mkutano mkubwa zaidi katika Mzunguko wa capital, huku Daraja Mbili ikiwa kituo cha mwisho. Shambulio la Keumbu limekosolewa kitaifa na kufufua hofu ya kuongezeka kwa kutovumiliana katika eneo hilo kabla ya Uchaguzi Mkuu wa 2027. Viongozi kutoka pande zote za kisiasa wametaka uchunguzi wa haraka kufanywa na wahusika kuchukuliwa hatua. Baraza la Wazee la Abagusii pia limewaonya vijana dhidi ya kutumiwa na wanasiasa kusababisha machafuko. Wafanyabiashara huko Keumbu wamekaribisha msafara huo. "Tangu Ijumaa, mauzo yamekuwa chini. Watu wanaogopa. Ikiwa msafara huu utasaidia kurejesha utulivu, tunauunga mkono," alisema Phylis Mokono, ambaye anaendesha hoteli karibu na stani ya magari ya Keumbu.

read more