T

taifaleo.nation.co.ke

@taifaleo Tue, 07 Jul 2026 02:55:46

IEBC yafufua mpango wa kupimia wanasiasa pesa za kampeni

TUME Huru ya Uchaguzi na Mipaka (IEBC) imefufua mpango wake wa kudhibiti matumizi ya fedha katika kampeni za uchaguzi kwa kuchapisha rasimu ya kanuni mpya zinazolenga kuweka kiasi cha matumizi ya wagombea na vyama vya kisiasa katika Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2027. Katika rasimu hiyo iliyochapishwa Jumatatu, Julai 6, 2026, IEBC imependekeza kuwa mgombea urais asitumie zaidi ya Sh4.44 bilioni katika kampeni zake, huku matumizi ya chama cha kisiasa yakipangwa kutozidi Sh17.7 bilioni. Kwa mujibu wa mapendekezo hayo, wagombea wa ugavana, useneta na uwakilishi wa wanawake wataruhusiwa kutumia kati ya Sh12.3 milioni na Sh123 milioni, kutegemea ukubwa wa kaunti na idadi ya wakazi. Wanaowania ubunge watatumia kati ya Sh17.5 milioni na Sh123 milioni, huku wanaowania uwakilishi wa wadi katika mabunge ya kaunti wakiruhusiwa kutumia kati ya Sh2.5 milioni na Sh20 milioni kulingana na ukubwa na idadi ya wakazi wa wadi husika. Hii ni mara ya pili kwa IEBC kujaribu kudhibiti matumizi ya fedha za kampeni baada ya juhudi za mwaka 2016 kugonga mwamba. Wakati huo, Bunge lilisitisha utekelezaji wa kanuni hizo kwa kurekebisha Sheria ya Ufadhili wa Kampeni za Uchaguzi na kuahirisha utekelezaji wake hadi baada ya uchaguzi wa mwaka 2017. Uwajibikaji Mwenyekiti wa IEBC Erastus Ethekon amesema kanuni hizo zinalenga kuimarisha uwajibikaji na uwazi katika usimamizi wa fedha za kampeni. "Kanuni hizi zinakusudia kuimarisha uwajibikaji katika usimamizi wa fedha za kampeni za wagombeaji na vyama vya kisiasa," alisema Bw Ethekon. Alisema Sheria ya Ufadhili wa Kampeni za Uchaguzi ya mwaka 2013 inapatia IEBC mamlaka ya kuweka viwango vya michango, matumizi na kusimamia uwajibikaji wa fedha za kampeni. IEBC pia imewapa Wakenya hadi Julai 15, 2026 kuwasilisha maoni yao kuhusu rasimu hiyo kabla ya kanuni hizo kuidhinishwa. Wakati huo huo, tume hiyo imekumbusha wadau kuhusu ratiba ya maandalizi ya uchaguzi wa mwaka 2027. Kwa mujibu wa ratiba hiyo, maafisa wa umma wanaonuia kugombea viti watalazimika kujiuzulu ifikapo Februari 9, 2027, miezi sita kabla ya uchaguzi. Vyama vya kisiasa vitapaswa kuwasilisha orodha ya wanachama na majina ya wanaotaka kushiriki kura za mchujo ifikapo Machi 16, 2027, huku mchujo wa vyama ukitarajiwa kukamilika ifikapo Mei 9, 2027. Uteuzi rasmi wa wagombea wa vyama na wawaniaji huru utafanyika kati ya Mei 29 na Juni 11, 2027, huku malalamishi yote yanayohusu uteuzi yakitakiwa kuwasilishwa kwa IEBC kabla ya Juni 12, 2027. Hatua ya IEBC ya kupendekeza kiwango cha pesa za matumizi ya kampeni inajiri wakati ambapo wanasiasa wengi wamekuwa wakitumia mabilioni ya fedha katika shughuli za uwezeshaji wa wananchi, ambazo zimekuwa zikitafsiriwa kama kampeni za mapema kuelekea uchaguzi mkuu wa mwaka ujao.

read more
T

taifaleo.nation.co.ke

@taifaleo Tue, 07 Jul 2026 01:55:13

Kampeni zachacha Ol Kalou zikibaki siku 10 kura zipigwe

HUKU zikisalia siku kumi pekee kabla ya uchaguzi mdogo wa ubunge wa Ol Kalou, ushindani huo umegeuka kuwa kipimo cha nguvu za kisiasa katika eneo la Mlima Kenya kuelekea Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2027. Mirengo inayoshindana imetaja uchaguzi huo kama kura ya maamuzi kuhusu mwelekeo wa kisiasa wa eneo hilo, huku kila upande ukitaka kuthibitisha kuwa unaungwa mkono na wapigakura wengi. Wagombeaji wanaopigiwa upatu ni Douglas Waweru wa chama cha Democracy for Citizens Party (DCP), Muchina Nyaga wa chama tawala cha United Democratic Alliance (UDA) na Wilson Kigwa wa Jubilee. [caption id="attachment_189827" align="alignnone" width="2000"] Mgombeaji kiti cha Ol Kalou kwa tikiti ya UDA Samuel Muchina Nyagah akipokezwa cheti cha uteuzi na Katibu Mkuu Hassan Omar mnamo Mei. Picha|Boniface Bogita[/caption] Wengine sita pia wanawania kiti hicho. Kiti hicho kilibaki wazi baada ya kifo cha Njuguna Kiaraho wa chama cha Jubilee mnamo Machi 29, 2026. Mgombeaji wa Jubilee, Bw Kigwa, anakabiliwa na changamoto baada ya kiongozi wa chama hicho, rais mstaafu Uhuru Kenyatta, na mgombea wake wa urais Dkt Fred Matiang'i, kutoshiriki kampeni zake. Aidha, Mbunge Mteule wa Jubilee Sabina Chege ameasi chama chake na sasa anamuunga mkono mgombeaji wa UDA. Uchaguzi huo umegeuka kuwa pambano kati ya serikali ya Rais William Ruto na upinzani unaoongozwa na aliyekuwa Naibu Rais Rigathi Gachagua. Bw Gachagua ametangaza kuwa atafanya kampeni Ol Kalou kwa siku tatu kuanzia Julai 10 kabla ya kampeni kufungwa Julai 13. Nyumba ya Seneta wa Nyandarua John Methu katika kijiji cha Mugumo imekuwa kituo cha mikutano ya kisiasa ya wafuasi wa Bw Gachagua, huku viongozi wa serikali wakifanya ziara mbalimbali za maendeleo wakiahidi miradi ili kuvutia wapigakura. Kati ya wagombeaji tisa, ni Bw Nyaga pekee anayemuunga mkono waziwazi Rais Ruto na serikali ya UDA, huku wengine wakiwa upande wa upinzani. Katika mdahalo uliopeperushwa na Inooro TV Julai 5, Bw Nyaga alikabiliwa na mashambulizi kutoka kwa wagombeaji wengine lakini alitetea sera zake. Bw Gachagua amesema idadi kubwa ya wagombea ni ishara ya demokrasia na kwamba hakuna anayepaswa kuzuiwa kugombea. Hata hivyo, wachambuzi wa siasa wanaonya kuwa Bw Gachagua ndiye anayehatarisha zaidi kisiasa iwapo mgombea anayemuunga mkono atashindwa, kwani hali hiyo itadhoofisha madai yake ya kuwa kinara wa kisiasa wa Mlima Kenya na kuathiri azma yake ya kuwania urais mwaka 2027. Kwa upande mwingine, Naibu Rais Kithure Kindiki amesema ushindi wa UDA katika uchaguzi huo utathibitisha kuwa siasa za ubaguzi na kujitenga hazina nafasi katika eneo la Mlima Kenya. Shinikizo pia linaongezeka kwa Prof Kindiki kushiriki moja kwa moja katika kampeni hizo, huku matokeo yakitarajiwa kuathiri nafasi yake ya kuendelea kuwa mgombea mwenza wa Rais Ruto mwaka 2027. Mbunge wa Laikipia Mashariki Mwangi Kiunjuri, ambaye ni mmoja wa viongozi wanaompigia debe mgombea wa UDA, alisema chama hicho kina uhakika wa kushinda. "Tunaendelea vizuri na takwimu zetu zinaonyesha tutashinda. mgombea wetu ndiye bora," alisema. Lakini Mbunge wa Kipipiri Wanjiku Muhia, anayemuunga mkono Bw Gachagua, alisema mgombea wa DCP ndiye anayeongoza. Alisema uchaguzi huo unalenga kuthibitisha kuwa eneo la Mlima Kenya linaweza kufanya maamuzi yake ya kisiasa bila kushinikizwa. Mchambuzi wa siasa Malila Munywoki amesema uchaguzi huo utakuwa mtihani muhimu kwa Tume Huru ya Uchaguzi na Mipaka (IEBC) na Idara za usalama kuonyesha vinaweza kusimamia uchaguzi huru, wa haki na wa amani kabla ya uchaguzi mkuu wa mwaka 2027. Naye Gavana wa Nyandarua Kiarie Badilisha hajaweka wazi mgombeaji anayemuunga mkono, lakini amekuwa akiwaambia wakazi kuwa kisiasa yuko upande ambao wananchi wengi wa kaunti hiyo wanaunga mkono, kauli ambayo imezua uvumi kuwa huenda akahama chama kabla ya uchaguzi mkuu wa mwaka 2027.

read more
T

taifaleo.nation.co.ke

@taifaleo Tue, 07 Jul 2026 00:55:25

Msajili Mkuu wa Ardhi hatarini kukamatwa katika kesi ya ardhi ya Mama Ngina, Criticos

MSAJILI Mkuu wa Ardhi yuko hatarini kukamatwa baada ya Mahakama ya Mazingira na Ardhi kumpata na hatia ya kuidharau kwa kukosa kutekeleza amri iliyotolewa katika mzozo wa ardhi unaowahusisha aliyekuwa Mama wa Taifa Mama Ngina Kenyatta na mfanyabiashara Basil Criticos. Katika uamuzi mkali unaosisitiza kuwa mahakama haitavumilia ukaidi wa kutotekeleza maagizo yake, Jaji C.G. Mbogo amemwamuru Msajili Mkuu wa Ardhi afike binafsi mahakamani Julai 28, 2026, kueleza ni kwa nini asichukuliwe hatua kwa kukaidi hukumu iliyotolewa zaidi ya miezi sita iliyopita. Jaji alionya kuwa ikiwa msajili huyo hatajitokeza mahakamani, kibali cha kukamatwa kwake kitatolewa. Uamuzi huo unatokana na mzozo wa muda mrefu kuhusu umiliki wa ardhi, ambapo mahakama ilibaini kuwa Ofisi ya Usajili wa Ardhi ilishindwa kutekeleza hukumu iliyotolewa Desemba 11, 2025, licha ya kukumbushwa mara kadhaa na mwenye amri hiyo ya mahakama. Ombi hilo liliwasilishwa na mfanyabiashara Basil Criticos aliyedai kuwa Msajili Mkuu wa Ardhi amekuwa akikwamisha utekelezaji wa hukumu kwa kukataa kutoa cheti cha muda cha umiliki wa ardhi hiyo yenye utata. Kwa mujibu wa stakabadhi za mahakama, msajili alikumbushwa kupitia barua mnamo Desemba 17, 2025 na Januari 13, 2026, huku hukumu hiyo ikisajiliwa rasmi dhidi ya hati ya ardhi Januari 22, 2026. Hata hivyo, hakuna hatua iliyochukuliwa. Akiwa amechoshwa na kucheleweshwa huko, Bw Criticos alirejea mahakamani akiomba msajili alazimishwe kueleza sababu za kutotekeleza amri ya mahakama na pia achapishe katika Gazeti Rasmi la Serikali taarifa ya kufutwa kwa hati zote za ardhi zilizotolewa kinyume cha sheria kutokana na ardhi hiyo. Kwa upande wake, Msajili Mkuu wa Ardhi alijitetea kupitia hati iliyowasilishwa na afisa wa usajili wa ardhi Nyandoro David Nyambaso. Alieleza kuwa cheti cha muda cha umiliki tayari kilikuwa kimeandaliwa lakini hakikuweza kutolewa baada ya kugundua hitilafu katika stakabadhi za kuhamisha ardhi. Kwa mujibu wa kiapo hicho, hati ya kuhamisha ardhi ilishuhudiwa na D.A. Gama Ross ambaye sasa ni marehemu, jambo ambalo lilihitaji ufafanuzi kabla ya usajili kuendelea. Msajili huyo pia alidai kuwa ardhi hiyo tayari ilikuwa imepimwa, kupangwa na kugawiwa wavamizi waliokuwa wakisubiri kupewa hati miliki, akisema kuwa kufuta hati hizo kupitia Gazeti Rasmi bila kufuata utaratibu wa kisheria kungekuwa kinyume cha sheria. Hata hivyo, Jaji Mbogo alitupilia mbali hoja hizo akisema ztayari zilijadiliwa kabla ya hukumu kutolewa, hivyo haziwezi kutumiwa kuhalalisha kutotekelezwa kwa amri za mahakama. Jaji alikubaliana na Bw Criticos kwamba msajili alikuwa akijaribu kufufua hoja ambazo tayari zilikuwa zimeamuliwa na mahakama na akabaini kuwa hakuna shaka kuwa Msajili Mkuu wa Ardhi anafahamu amri ya mahakama lakini alichagua kutotii.

read more