T

taifaleo.nation.co.ke

@taifaleo Mon, 06 Jul 2026 23:25:21

Akili-Unde ndiyo mada kuu katika sherehe ya SIKIDU jijini Bujumbura

AKILI-UNDE au Akili-Mnemba (AI) itakuwa kiungo muhimu katika maadhimisho ya tano ya Siku ya Kiswahili Duniani (SIKIDU) mwaka huu huku viongozi wa Afrika Mashariki, wataalamu wa lugha, wabunaji wa sera na wajuzi wa teknolojia wakihimiza kuimarishwa kwa matumizi ya Kiswahili katika enzi hii ya kidijitali. Maadhimisho hayo ya siku tatu, yaliyoandaliwa na Tume ya Afrika Mashariki ya Kiswahili (EAKC), yalianza jijini Bujumbura, Burundi, mnamo Julai 5 na yatafikia kilele chake leo Julai 7 sambamba na Kongamano la Tatu la Kimataifa la Kiswahili la EAKC. Kaulimbiu ya hafla hiyo ni 'Kiswahili, Wingi Lugha na Akili-Unde". Akizungumza kabla ya ufunguzi rasmi wa kongamano hilo, Katibu Mtendaji wa EAKC, Dkt Caroline Asiimwe, alisema kongamano hilo litajadili namna Kiswahili kinavyoweza kuwa lugha kuu ya Afrika katika matumizi ya Akili-Unde, ubunifu na mageuzi ya kidijitali. Alisema kaulimbiu ya kikanda inajaliza kaulimbiu ya kimataifa ya UNESCO ya Siku ya Kiswahili Duniani mwaka huu isemayo: "Kiswahili kwa Amani, Mshikamano na Diplomasia ya Uchumi wa Kimataifa". Kwa mujibu wa Dkt Asiimwe, Kiswahili kinachozungumzwa na zaidi ya watu milioni 250 duniani kinaendelea kukua kwa kasi na sasa kinatumika zaidi katika diplomasia, elimu, vyombo vya habari na majukwaa ya kidijitali. Alibainisha kuwa licha ya Akili-Unde kubadilisha mawasiliano duniani, lugha nyingi za Afrika bado hazijawakilishwa ipasavyo katika teknolojia zinazoibuka. Hivyo basi, kuna haja ya kuunda mifumo ya Akili-Unde inayotambua na kuunga mkono matumizi ya Kiswahili. "Lazima tuhakikishe Kiswahili hakibadilishwi tu na mapinduzi ya kidijitali, bali kinakuwa sehemu ya kuyaongoza," alisema. Kongamano hilo pia linaadhimisha miaka 10 tangu kuanzishwa kwa Tume ya EAKC, ambayo ilianzishwa ili kuratibu juhudi za kukuza na kuendeleza Kiswahili katika Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC). Dkt Asiimwe alizitaka serikali, kampuni za teknolojia, watafiti na washirika wa maendeleo kuwekeza katika kanzi-data huria za Kiswahili, mifumo mikubwa ya lugha (Large Language Models) na zana za Akili-Unde zinazoakisi uanuwai wa lugha na tamaduni za Afrika. Pia alihimiza kuongezwa kwa msaada kwa vijana wabunifu ili waweze kubuni suluhu za kidijitali, maudhui ya mtandaoni na biashara zinazotegemea teknolojia kwa kutumia Kiswahili. Aidha, tume hiyo ilizihimiza nchi wanachama wa EAC kupitisha sera zinazotambua Kiswahili kuwa nguzo muhimu ya uunganifu wa kikanda, ushiriki wa wananchi na maendeleo endelevu. Kongamano hilo litajumuisha mijadala ya sera, uwasilishaji wa tafiti, maonesho ya teknolojia na shughuli za kuwashirikisha vijana, kwa lengo la kutoa mapendekezo ya vitendo yatakayoharakisha ukuzaji wa nafasi ya Kiswahili katika ubunifu wa kidijitali. Alisema matokeo ya kongamano hili yanatarajiwa kuimarisha mshikamano wa kikanda, kuboresha mawasiliano Afrika Mashariki na kukiweka Kiswahili katika nafasi ya kushindana kimataifa kama lugha ya teknolojia, amani, mshikamano na diplomasia ya uchumi. "Tukiwa katika kipindi ambacho utamaduni unatagusana na teknolojia ya kisasa, mustakabali wetu unapaswa kuandikwa kwa lugha zetu wenyewe. Kwa kukumbatia Akili-Unde, tunaweza kuikuza nafasi ya Afrika duniani, kupunguza pengo la kidijitali na kukifanya Kiswahili kuwa mojawapo ya lugha zinazoongoza katika ubunifu na ushawishi wa kimataifa," alisema. Siku ya Kiswahili Duniani ilitangazwa rasmi katika Mkutano Mkuu wa UNESCO mwaka wa 2021 ili kutambua umuhimu wa Kiswahili kama mojawapo ya lugha zinazozungumzwa na watu wengi duniani na kama chombo muhimu cha kuimarisha mazungumzo kati ya tamaduni mbalimbali. Kiswahili ndicho lugha ya kwanza ya Kiafrika kutambuliwa kwa hadhi hiyo na Umoja wa Mataifa (UN). Maadhimisho ya mwaka huu yanatarajiwa kudhihirisha kwa kina mchango wa Kiswahili katika ukuzaji wa amani, maendeleo endelevu na diplomasia ya uchumi, hasa katika muktadha wa kuimarika kwa ushirikiano wa kikanda barani Afrika na kuongezeka kwa ushawishi wa bara hili duniani. UNESCO pia itaendelea kuunga mkono matukio, mijadala na ushirikiano kati ya nchi za Afrika Mashariki na wadau wa utamaduni huu ili kukisawiri Kiswahili kama daraja linalowaunganisha watu wa mataifa mbalimbali.

read more
T

taifaleo.nation.co.ke

@taifaleo Mon, 06 Jul 2026 22:55:51

Mapadri hawawezi kujificha katika 'useja' kuhepa watoto wanaozaa, korti yaambia kanisa

MAHAKAMA Kuu imeamuru Dayosisi ya Eldoret ya Kanisa Katoliki kumjumuisha mwanamume anayedaiwa kuzaliwa na Padri aliyefariki katika ugavi wa mali yake, ikisema watoto wote wana haki ya kurithi wazazi wao bila kujali mazingira ya kuzaliwa kwao. Jaji Reuben Nyakundi aliamua kuwa ushahidi uliowasilishwa mahakamani ulithibitisha kuwa DK, aliyezaliwa Julai 4, 2003, ni mtoto wa kibaolojia wa marehemu padri JKN, aliyefariki Julai 2015. Kabla ya kifo chake, kasisi huyo alikuwa amemteua Askofu Cornelius Korir kuwa msimamizi wa wosia wake. Hata hivyo, Askofu Korir alifariki mwaka 2017 kabla ya kukamilisha usimamizi wa mali hiyo, na nafasi yake ikachukuliwa na Askofu Dominic Kimengich. Mchakato wa ugavi wa mali ulichukua mkondo mpya baada ya mama wa DK, NJR, kupinga kuondolewa kwa mwanawe kwenye orodha ya warithi. Wasimamizi wa mali hiyo walipinga ombi hilo wakidai kuwa Padri JKN alikuwa kasisi aliyekuwa ameweka nadhiri ya useja, hivyo asingeweza kupata mtoto. Lakini Jaji Nyakundi alisema cheti cha kuzaliwa cha DK, kinachomtaja marehemu kuwa babake, pamoja na ushahidi wa mama yake, vilitosha kuthibitisha kwa kiwango kinachohitajika katika kesi ya aina hiyo. "Ni wazi kuwa mali ya marehemu haiwezi kumfanya DK kuwa mtoto asiye na haki kwa kukosa kumtengea sehemu ya urithi wa marehemu," alisema jaji. Mahakama pia ilitangaza kuwa cheti cha kuzaliwa kilichotolewa Machi 12, 2008 kinamtambua marehemu kuwa baba wa mtoto huyo. Katika uamuzi wake, Jaji Nyakundi alisema watoto waliozaliwa nje ya ndoa ni warithi halali wa mali ya wazazi wao na kwamba wosia hauwezi kutumiwa kunyima watoto hao haki zao za kikatiba. "Watoto waliozaliwa kutokana na mahusiano kama hayo wana haki ya kurithi mali ya wazazi wao, iwe ni mali inayohamishika au isiyohamishika, na hakuna wosia unaoweza kutumika kuwanyima haki hizo," alisema. Mahakama iliwapa wasimamizi wa mali siku 60 kumgawia DK sehemu yake ya urithi, ikionya kuwa wakishindwa kufanya hivyo, hati ya usimamizi wa mali itafutwa na mchakato mpya wa urithi utaanzishwa. Jaji pia alikataa ombi la kufukua mwili wa kasisi huyo kwa uchunguzi wa vinasaba (DNA), akisema hatua hiyo ingeingilia haki za faragha za watu wengine bila sababu ya msingi. Katika ushahidi wake, NJR alisema alikutana na Padri JKN mwaka 1993 alipokuwa mhadhiri katika Chuo Kikuu cha Moi. Alidai uhusiano wao ulianza kama wa ushauri kabla ya kuwa wa kimapenzi, na kwamba kasisi huyo alimsaidia kielimu, kumpatia kazi na kugharamia mahitaji ya mtoto wao, ikiwemo karo, kodi ya nyumba na matumizi mengine. Jaji alisema upande uliopinga madai hayo haukuwasilisha ushahidi wa moja kwa moja wa kupinga uhusiano huo.

read more
T

taifaleo.nation.co.ke

@taifaleo Mon, 06 Jul 2026 21:55:10

Sifuna ajipanga, atia guu moja nje ya ODM akianza kuwazia urais

SENETA wa Nairobi Edwin Sifuna anatarajiwa kuongoza wimbi la viongozi kujiondoa katika chama cha ODM baada ya viongozi wa jamii ya Waluhya wanaohusishwa na mrengo wa Linda Mwananchi kukubaliana kumpigia debe kuwania urais mwaka wa 2027 kupitia chama kipya cha kisiasa. Uamuzi huo ulifikiwa Jumapili katika mkutano ulioandaliwa na Gavana wa Trans Nzoia George Natembeya, ukiwaleta pamoja Bw Sifuna, Seneta wa Vihiga Godfrey Osotsi, Mbunge wa Kabuchai Majimbo Kalasinga, Mbunge wa Bumula Wamboka Wanami pamoja na viongozi wengine. Viongozi hao walitangaza kuwa wako katika hatua za mwisho za kuunda chama kipya watakachotumia katika uchaguzi mkuu wa mwaka wa 2027. Hatua hiyo pia inaonekana kufungua ukurasa mpya kwa Bw Sifuna ambaye kwa sasa anakabiliwa na mzozo wa kisheria kuhusu wadhifa wake kama Katibu Mkuu wa ODM. Akizungumza baada ya mkutano huo, Seneta Osotsi alisema bado wanazingatia uwezekano wa kutumia jina Linda Mwananchi licha ya Msajili wa Vyama vya Kisiasa kukataa ombi lao la usajili mwezi Machi mwaka huu kwa msingi kuwa jina hilo linafanana na kauli-mbiu iliyopo tayari na hivyo kukiuka Sheria ya Vyama vya Kisiasa. Alisema iwapo wataamua kuendelea na jina hilo, hawatakuwa na budi ila kupinga uamuzi wa Msajili wa Vyama vya Kisiasa mahakamani wakisisitiza kuwa haukujikita katika msingi wa kisheria. Bw Osotsi alieleza kuwa chama hicho hakitakuwa cha viongozi wa Magharibi pekee bali kitawaleta pamoja viongozi wote wanaohusishwa na mrengo wa Linda Mwananchi kutoka maeneo mbalimbali nchini. Viongozi hao wamepanga kufanya mikutano miwili mikubwa ya kisiasa katika kaunti za Trans Nzoia na Bungoma mnamo Julai 25 na 26, mtawalia. Mikutano hiyo itatumika kuzindua rasmi mkakati wao wa kisiasa kuelekea uchaguzi mkuu wa mwaka 2027 pamoja na kuanza kampeni za mashinani katika maeneo yote 38 ya uchaguzi ya eneo la Magharibi. Katika mkutano wa Bungoma, Bw Sifuna anatarajiwa kutawazwa rasmi kuwa kinara wa kisiasa wa eneo la Magharibi na kupewa baraka za wazee kuwania urais. "Azimio letu ni kwamba Bw Sifuna atagombea urais mwaka wa 2027. Hivi karibuni tutatangaza chama tutakachotumia kuwania urais," alisema Bw Natembeya. Aliongeza kuwa viongozi hao wataanzisha kampeni kali za kuwahamasisha wananchi kujisajili kama wapigakura na kuunga mkono ajenda yao ya kisiasa. Kwa upande wake, Bw Osotsi alisema eneo la Magharibi limeendelea kugawanyika kisiasa kwa manufaa ya viongozi kutoka maeneo mengine, akisisitiza kuwa wakati umefika kwa wakazi wa eneo hilo kupigania kiti cha juu zaidi ya uongozi nchini. Mrengo wa Linda Mwananchi pia unajumuisha viongozi wengine mashuhuri akiwemo Gavana wa Siaya James Orengo, Mbunge wa Embakasi Mashariki Babu Owino, Mbunge wa Suba Kusini Caroli Omondi, Mbunge wa Kitutu Chache Kusini Anthony Kibagendi, Mbunge wa Kitutu Masaba Clive Gisairo, Seneta wa Kisii Richard Onyonka, Mbunge wa Kaiti Joshua Kimilu na Gavana wa Murang'a Irungu Kang'ata. Bw Natembeya alisema kwa sasa anaendelea kuwa mratibu wa kisiasa wa mrengo wa Linda Mwananchi na pia muungano wa upinzani unaoongozwa na aliyekuwa Naibu Rais Rigathi Gachagua pamoja na kiongozi wa Wiper Kalonzo Musyoka katika eneo la Magharibi. Hata hivyo, Bw Osotsi alisema Bw Natembeya anatarajiwa kutangaza rasmi kujiunga na mrengo wa Linda Mwananchi wakati wa mkutano wa Julai 25. Mbunge wa Funyula Wilberforce Oundo alisema iwapo hawatafaulu kusajili chama kipya kwa muda uliosalia kabla ya uchaguzi mkuu, watanunua chama ambacho tayari kimesajiliwa ili kitumike kama chombo chao cha kisiasa. Alisema uamuzi wao wa kujiondoa ODM umetokana na tofauti za kisiasa na kundi linaloongozwa na Oburu Oginga, ambalo limejitokeza kumuunga Rais William Ruto kuwania muhula wa pili. Wakati huo huo, Seneta wa Kakamega Boni Khalwale amethibitisha kuwa ana uhusiano na chama kipya cha United Patriotic Movement (UPM), ambacho tayari kimekidhi masharti ya usajili na kinasubiri usajili kamili. Alisema UPM ni chama cha kitaifa kitakachowaleta pamoja viongozi wanaotaka kuona Rais Ruto akihudumu kwa muhula mmoja pekee, akiongeza kuwa taarifa rasmi kuhusu iwapo kitakuwa chombo kipya cha viongozi wa Linda Mwananchi itatolewa katika wiki zijazo. Hatua hizi zinaashiria kuanza kwa mabadiliko makubwa ya kisiasa kuelekea uchaguzi mkuu wa mwaka 2027, huku vyama vikuu vikitarajiwa kupoteza baadhi ya viongozi wao wanaotafuta vyama vipya vya kisiasa vya kuwania nyadhifa mbalimbali.

read more
T

taifaleo.nation.co.ke

@taifaleo Mon, 06 Jul 2026 22:25:11

SIKIDU: Sababu ya Kiswahili kuwa rasilimali kuu inayofaa kubidhaishwa

HII leo, dunia nzima inaadhimisha makala ya tano ya Siku ya Kiswahili Duniani (SIKIDU), tangu Shirika la Umoja wa Mataifa la Elimu, Sayansi na Utamaduni (UNESCO) litoe tangazo mnamo mwaka wa 2021, kutambua na kuthibitisha Kiswahili kuwa lugha yenye umuhimu mkubwa duniani katika mazingira ya wingi-lugha. Kiswahili na lugha nyingine ni amali, rasilimali na nyenzo zinazohitaji kutunzwa na kukuzwa kwa ajili ya maendeleo. Kwa sababu hiyo, wataalamu wanaelekea kukubaliana kwamba mojawapo ya mikabala ya kuziangalia lugha ni ule wa kutoziona kama nyenzo za mawasiliano tu, bali pia kama bidhaa au rasilimali. Je, Afrika Mashariki imejinufaisha vipi kutokana na ubidhaishaji wa Kiswahili? Dunia inapokisherehekea Kiswahili, Afrika ya Mashariki inapaswa kuwa kwenye mstari wa mbele katika utetezi wa lugha hii, na utamaduni wake kwa minajili ya kujinufaisha kiuchumi. Tunapochunguza masuala ya siasa za kijiografia za lugha (geopolitics of languages), inabainika bayana kwamba mataifa mengine ulimwenguni yamebidhaaisha lugha zao kwa njia na namna mbalimbali. Kwanza, mataifa hayo yametumia lugha zao kufaidi kwenye masuala ya kidiplomasia na ushawishi (soft power influence). Je, tumewahi kujiuliza ni kwa nini Wachina wameanzisha taasisi kama vile Confucius Institute katika Vyuo Vikuu vya Nairobi na Kenyatta? Ni kwa nini Wafaransa wana Alliance Francais jijini Nairobi? Je, ni kwa nini Wajerumani wamestawisha Goethe Institute jijini Nairobi? Je, ni kwa nini Waingereza wamestawisha na kuimarisha shirika la Uchapishaji la Oxford University Press kote duniani? Je, maswali haya yanafungamana vipi na jinsi Afrika Mashariki (kitovu cha Kiswahili) inavyokishughulikia na kukiahangaikia Kiswahili? Si jambo la mjadala tena kwamba Kiswahili ndiyo lugha ya kutazamwa sana barani Afrika, kuliko lugha nyingine kuu za bara hili. Afrika ya Mashariki ina bahati kubwa kuwa na Kiswahili, ambacho ni mojawapo ya rasilimali muhimu ya eneo hili. Si lazima rasilimali ziwe mafuta, almasi, na misitu pekee. Idadi ya wazungumzaji wa Kiswahili kote ulimwenguni inakisiwa kuwa baina ya watu milioni 150 na 250. Wengi wa wazungumzaji hawa ni wenyeji wa Afrika ya Mashariki na Kati na Maeneo ya Maziwa Makuu. Ingawa Kiswahili ni lingua franca ya Afrika Mashariki, wasemaji asilia (watu wanaozungumza Kiswahili kama lugha yao ya 'mama' ni kati ya milioni 5 na 15. Fasihi simulizi inadokeza kwamba Waswahili walitoka sehemu za kaskazini ya pwani ya Kenya – mahali panapoitwa Shungwaya karibu na mji wa Lamu. Kutoka mahali hapa, walihamia sehemu nyingine za pwani ya Afrika Mashariki kwa sababu ya vita, njaa, magonjwa n.k. Waswahili asilia (kindakindaki), chambacho mtaalamu Ireri Mbaabu waliitwa Wangozi na walizungumza Kingozi. Hili ni jina la lakabu lililotokana na vitendo vyao vya kupima ardhi kwa kutumia kanda za ngozi. Jina 'Waswahili' ama lilitokana na 'Wa- ziwa –hili' (watu wa ziwa hili) au asili ya Kiarabu 'Sahil' (umoja) na 'Sawahil' (wingi) kwa maana ya watu wa pwani. Mbaabu anadai kuwa neno 'Kiswahili' lilianza kutumika sehemu ya kaskazini mwa pwani karibu na mji wa Lamu kati ya mwaka wa 700 – 800 Baada ya Yesu Kristo. Hii leo, Kiswahili si lugha ya pwani tu. Imekwisha kupasua kingo zake na kuenea katika sehemu mbalimbali ulimwenguni – na kupanua mawanda na maana 'Mswahili', jinsi inavyofahamika. Kuna takriban makundi manne ya 'Waswahili'. Kwanza, ni Waswahili wenye asili ya Kibantu. Pili, tuna Waswahili waliozaliwa kutokana na ndoa kati ya Waarabu na Waswahili asili (kindakindaki). Tatu, ni 'Waswahili' wanaotoka katika makabila mengine ya Kiafrika ambao wanashabikia na kuuenzi utamaduni wa Mswahili. Mwisho, kuna kundi la watu wanaoenzi na kuishughulikia lugha ya Kiswahili katika ulingo wa taaluma. Nilivyokwisha kutaja, Kiswahili ndiyo lugha ya kutazamwa barani Afrika karne hii. Ramani ya lugha inaonesha kwamba Kiswahili ni mojawapo ya lugha kumi na moja zenye wazungumzaji wengi zaidi barani Afrika. Kiswahili ndicho kinashikilia nafasi ya kwanza kwa kuwa na takribani zaidi ya wazungumzaji milioni 150 barani Afrika (wengi wao wakiwa wenyeji wa Afrika Mashariki). Lugha nyingine Afrika zenye wasemaji wengi ni Amharic, Kioromo , pamoja na Kiarabu (Afrika kaskazini). Katika Afrika ya Magharibi, tuna Kiyoruba na Igbo. Katika eneo la Afrika ya Kusini tuna Kizulu na Kishona. Kati ya lugha hizi zote, Kiswahili kimeungwa mkono na wataalamu wengi kuwa lingua franca ya Afrika. Kutokana na umaarufu wa Kiswahili, mataifa ya Afrika Mashariki yanapaswa kuimarisha uundaji na utekelezaji wa sera murua zitakazofanikisha michakato ya ubidhaishaji wake kwa minajili ya kujitajirisha kiuchumi – yanavyofanya mataifa mengine kuhusu lugha zao. Bitugi Matundura ni mhadhiri wa Kiswahili katika Chuo Kikuu cha Chuka

read more