T

taifaleo.nation.co.ke

@taifaleo Wed, 19 Aug 2026 17:24:07

El Nino: Shirika latoa tahadhari kwa serikali za Afrika Mashariki

Serikali za Afrika Mashariki zimehimizwa kuwekeza mapema katika kukabiliana na athari za mabadiliko ya tabianchi badala ya kusubiri mafuriko na ukame kutokea ndipo zianze kutoa fedha za dharura. Shirika la Vi Agroforestry limesema maandalizi hayo ni muhimu huku utabiri ukionyesha uwezekano wa mvua nyingi na mafuriko katika maeneo ya Afrika Mashariki kati ya Oktoba na Desemba mwaka huu. Shirika hilo limesema El Niño haifai kuonekana kama tishio la msimu mmoja pekee, bali ni ishara ya haja ya kuimarisha uwezo wa jamii kukabiliana na majanga ya hali ya hewa. Kwa mujibu wa shirika hilo, uharibifu wa ardhi, maeneo ya vyanzo vya maji na maisha ya wakulima umeongeza madhara yanayosababishwa na mvua kubwa, mafuriko na ukame. Utabiri wa hivi karibuni unaonyesha kuwa baadhi ya maeneo ya Afrika Mashariki yanaweza kupokea mvua nyingi kuliko kawaida katika msimu wa Oktoba hadi Desemba, jambo linaloweza kusababisha mafuriko, maporomoko ya ardhi, uharibifu wa mazao na kuhama kwa familia. Vi Agroforestry imesema serikali zinapaswa kuelekeza fedha zaidi kwa wakulima wadogo, wanawake, vijana na wafugaji ambao wako mstari wa mbele katika kusimamia ardhi na maji. Shirika hilo limependekeza kupanuliwa kwa kilimo-misitu, ambapo miti hupandwa pamoja na mazao na mifugo, kama njia mojawapo ya kupunguza madhara ya mabadiliko ya tabianchi. Limesema miti na udongo wenye afya husaidia kupunguza kasi ya maji yanayotiririka, kuzuia mmomonyoko wa udongo na kuongeza uwezo wa ardhi kuhifadhi maji. Kwa wakulima, miti pia inaweza kuwa chanzo cha matunda, chakula cha mifugo, kuni na kipato wakati mazao yanapoharibiwa na hali mbaya ya hewa. Vi Agroforestry pia imetaka serikali kuwekeza katika uvunaji wa maji, uhifadhi wa udongo, urejeshaji wa maeneo ya mito na vyanzo vya maji, vitalu vya miti na mifumo ya kilimo inayostahimili mabadiliko ya hali ya hewa. Shirika hilo limesema mifumo ya kutoa tahadhari mapema inapaswa kuimarishwa ili wakulima wapate taarifa kwa wakati na kuchukua hatua kabla ya mvua kubwa kuanza. Aidha, limewataka wafadhili, taasisi za kifedha na kampuni binafsi kuongeza fedha kwa miradi inayoongozwa na jamii. Limesema wanawake, vijana, wakulima wadogo na wafugaji hawapaswi kuonekana kama wapokeaji wa msaada pekee, bali washirikishwe katika kupanga na kutekeleza miradi ya kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi. Vi Agroforestry imesema ingawa maandalizi ya dharura kama kusafisha mitaro na kuimarisha huduma za uokoaji ni muhimu, hatua hizo hazitoshi bila uwekezaji wa muda mrefu. "El Niño itapita, lakini hali ya hewa isiyotabirika itaendelea," shirika hilo limesema. Limesema hatua zinazochukuliwa sasa ndizo zitakazoamua iwapo majanga yajayo yataendelea kusababisha hasara kubwa au jamii zitakuwa na uwezo wa kukabiliana nayo.

read more
T

taifaleo.nation.co.ke

@taifaleo Wed, 19 Aug 2026 16:55:30

Walikwepa madhila ya ndoa na kuingilia kilimo

KATIKA eneo kame la Kinna, Kaunti ya Isiolo, ambako ukame na mabadiliko ya tabianchi yamefanya kilimo na ufugaji kuwa changamoto kubwa, kundi la wakulima limegundua kuwa kilimo endelevu kinaweza kuwa njia ya kujikomboa kutoka kwa umaskini na kutegemea chakula cha msaada. Kupitia kilimo cha mvungulio (greenhouse) na mfumo wa umwagiliaji mimea na mashamba maji kwa njia ya matone chini ya Nasole SACCO, manusura wa ukatili wa kijinsia kwenye ndoa sasa wanajipatia kipato, kulea familia zao na kuandika ukurasa mpya wa maisha. Miongoni mwao ni Najma Ado, ambaye alitoka kwenye ndoa kufuatia madhila na vita vya kijinsia, na mkazi wa Kinna, ambaye leo hii analima mboga na viungo kwenye greenhouse. Anasema hakuwahi kufikiria kwamba siku moja angejitegemea kupitia kilimo. "Nilipitia changamoto kibao kwenye ndoa, ikiwemo kupigwa na aliyekuwa mume wangu," anasimulia. Maisha yalibadilika baada ya kujiunga na Nasole SACCO, chama cha ushirika Isiolo, ambako alipata mkopo wa Sh40, 000 na mafunzo ya kilimo kinachohimili mabadiliko ya tabianchi. "Leo hii mimi ni mkulima. Mapato ninayopata yananisaidia kulisha watoto wangu, kuwalipia karo, na kusaidia kukidhi mahitaji yao na hata kusaidia wazazi wangu," anasema. Safari yake haikuwa rahisi. Najma aliolewa akiwa na umri wa miaka 14 na akawa mama akiwa bado mchanga. Badala ya kuendelea na masomo, aliingia kwenye ndoa iliyogeuka kuwa ngome ya mateso na ukatili wa kijinsia. [caption id="attachment_191341" align="aligncenter" width="300"] Najma Ado Mohamed, mama asiye na mume na manusura wa ukatili wa kijinsia (GBV) kutoka Kinna, Kaunti ya Isiolo, akisimulia safari yake katika kilimo kinachozingatia mabadiliko ya tabianchi. Picha|Sammy Waweru[/caption] "Baada ya kupata mtoto wangu wa kwanza, mume wangu alianza kunipiga. Nilivumilia kwa miaka kadhaa kabla ya kuamua kuondoka," akaambia Akilimali wakati wa mahojiano katika Kijiji cha Kinna. Baada ya kurejea nyumbani akiwa na watoto wawili na bila chanzo cha mapato, alikabiliwa na maisha magumu katika eneo ambalo ukame wa mara kwa mara umeathiri maisha ya wakazi wengi. Kupitia Nasole SACCO, alipata fursa ya kujifunza kuhusu kilimo cha kisasa, usimamizi wa fedha na ujasiriamali. Pia, alifunzwa jinsi ya kuweka akiba ambayo imemuwezesha kupanga maisha yake ya baadaye. "Sitaki kurudi tena katika maisha ya mateso. Watoto wangu sasa wanaishi kwa amani na wanaendelea na masomo yao," akasema. Alidokeza kwamba mafunzo kuhusu haki za wanawake yamewapa wanawake wengi ujasiri wa kupinga ukatili wa kijinsia, dhuluma na kutafuta msaada wanapodhulumiwa. Mbali na Najma, Mariam Mohamed naye amepata matumaini kupitia kilimo. Kwenye kivungulio, analima nyanya, pilipili mboga (maarufu kama hoho) na mchicha kwa kutumia mfumo wa umwagiliaji mimea na mashamba maji kwa kutumia mifereji kudondoa matone. Mariam anasema wazazi wake walitalikiana alipokuwa na umri wa miaka saba. Baadaye aliolewa akiwa bado mdogo kimiaka, lakini ndoa hiyo pia ilivunjika na kumlazimu kuanza maisha upya akiwa na watoto wake. "Nilitegemea msaada kutoka kwa watu wengine ili kuishi. Maisha yalikuwa magumu sana," anakumbuka. Alijiunga na kikundi cha wanawake mwaka 2012 na baadaye akawa mwanachama wa Nasole SACCO. "Nilianza kuweka akiba ya Sh100 kwa wiki na baada ya miezi sita niwekeza fedha hizo kwenye kilimo," anafichua. [caption id="attachment_191342" align="aligncenter" width="300"] Mariam Mohamed akionyesha nyanya zilizovunwa kutoka kwenye kivungulio eneo la Kinna, Kaunti ya Isiolo. Yeye ni mama asiye na mume, manusura wa ukatili wa kijinsia (GBV) na mwanachama wa Nasole SACCO. Picha|Sammy Waweru[/caption] Leo hii Mariam huuza mboga na hupata wastani wa Sh500 kwa siku, fedha zinazomwezesha kulipia watoto karo, kununua chakula na kugharamia mahitaji ya familia. "Kupitia Nasole SACCO, nimeweza kusomesha watoto wangu. Zamani nilitegemea watu, lakini sasa ninaweza kuitunza familia yangu," anasema. Anasema kutokana na mabadiliko ya tabianchi, kilimo cha kisasa; kikiwemo teknolojia ya mvungulio na mfumo wa umwagiliaji mimea na mashamba maji kwa kutumia mifereji kudondoa matone, kimekuwa suluhisho muhimu kwa wakazi wa Isiolo. Kulingana na Makai Mamo, Naibu Mwenyekiti wa Nasole SACCO, chama hicho cha ushirika kilichosajiliwa rasmi mwaka 2019, sasa kina wanachama wapatao 310, wakiwemo wanawake 230. Anasema pamoja na kutoa mikopo na huduma za kifedha, SACCO hiyo inalenga kusaidia manusura wa ukatili wa kijinsia kujitegemea kimaendeleo. "Tunawaunganisha wanawake na taasisi za kifedha, mipango ya serikali inayowapiga jeki na mashirika mbalimbali ili wapate fursa za kujijenga upya kimaisha," anasema. Kutokana na ukame wa mara kwa mara, wanachama wamekumbatia kilimo cha mvungulio, mfumo wa umwagiliaji mimea na mashamba maji kwa kutumia mifereji kudondoa matone, ufugaji wa samaki na nyuki ili kuongeza uzalishaji na mapato. Kwa ushirikiano na Heifer International, World Food Programme, Catholic Relief Services na We World Kenya Foundation, wanachama hupatiwa mafunzo kuhusu usimamizi wa fedha, ujasiriamali, mahusiano bora ya kifamilia na kilimo kinachokabiliana na mabadiliko ya tabianchi.

read more