T

taifaleo.nation.co.ke

@taifaleo Sun, 18 Oct 2026 10:31:21

Umuhimu wa lishebora kwa wanawake wajawazito, utafiti

UJAUZITO NA UZAZI  WANAWAKE wenye mimba wanashauriwa kuzingatia lishe bora na salama kiafya ikiwemo kula aina tofauti za samaki (seafood) mara kwa mara ili kuzuia baadhi ya matatizo sugu yanayowaathiri watoto wachanga.  Utafiti mpya umehusisha chango (colic) na eczema, matatizo yanayoathiri watoto wachanga, na chakula anachokula mwanamke mjamzito kabla ya kujifungua.  Watoto wachanga waliozaliwa na kina mama waliozingatia lishe bora kiafya, wana kiwango cha chini cha tishio la kuugua chango na eczema, kulingana na wataalam.  Aidha, utafiti huo uliashiria ulaji wa seafood mara kwa mara kwa wanawake wajawazito husaidia kupunguza tishio la watoto wachanga la kuathiriwa na matatizo haya.  Tafiti za awali zimeonyesha kuwa watoto wanaoathiriwa na chango wana uwezekano mkubwa wa kuugua matatizo sugu kiafya baadaye maishani ikiwemo mzio wa chakula, mzio wa pua na ugonjwa wa pumu.  Katika utafiti mpya ambao ni wa kwanza kuchunguza uhusiano huu, wanasayansi walitathmini jjinsi lishe wakati wa ujauzito inavyoweza kuchangia chango, na hususan mseto wa chango na eczema.  Professor wa Matibabu ya Watoto katika Chuo cha Harvard Medical School, Jenifer Lightdale, anafafanua kuwa watoto wachanga wanaoathiriwa na mchanganyiko wa chango na eczema wana tishio la juu zaidi la kukumbwa na maradhi ya mzio wanapokua.  Wanawake wajawazito zaidi ya 1,300 walishirikishwa katika utafiti huu ambapo lishebora kiafya ilijumuisha ulaji kwa wingi wa matunda, mboga, nafaka isiyosafishwa, maharage, viwango vya chini vya mafuta, protini na maziwa.  Vyakula vya nyama nyekundu au iliyopakiwa, vinywaji vilivyoongezwa sukari, chumvi na nafaka iliyosafishwa vilijumuisha lishe duni kiafya.  Washiriki pia waliripoti kuhusu ulaji wa vyakula vinavyofahamika kuchochea mzio ikiwemo njugu karanga, samli ya njugu karanga, mayai, maziwa, samaki wenye mapezi na wasio nayo.  "Matokeo yetu yanatoa sababu nyingine ya kusaidia wanawake wenye mimba kufanikisha lishe bora inayowiana kiafya, hasa kusisitiza ulaji wa seafood," alisema kiongozi wa utafiti Emily Oken.  Alifafanua kuwa, ingawa kina mama hutamani kufanya kila wawezalo kwa manufaa ya watoto wao wachanga, aghalabu hukumbana na vizingiti kifedha na vinginevyo katika juhudi za kupata lishebora kiafya.

read more
T

taifaleo.nation.co.ke

@taifaleo Sun, 18 Oct 2026 10:06:05

Ni fumbo jinsi penzi hugeuka shubiri, wengine wakiishia kuangamizana!

FATAKI  MPAKA kati ya mapenzi na chuki ni finyu sana. Mtu anayempenda mwingine sana na kuwa radhi kumfanyia lolote hata 'kumpa maisha yake,' ndiye yuleyule anayeweza kumchukia mwenzake kwa ari na hamasa sawia kiasi cha kumfanyia maovu yasiyoelezeka.  Matukio yanayoshuhudiwa katika miaka ya karibuni kuhusu wanandoa na wapenzi waliopendana na kuendana kama pacha wa toke nitoke kabla ya kuchukiana, kutendeana uhayawani zaidi ya wanyama wenyewe, ni ithbati tosha.  Uhalisia huu unasisitiza haja ya kuhakikisha kuwa, iwapo ni lazima uwe na mpenzi au kufunga ndoa, unafanya hivyo na mtu mkarimu, mwenye maadili na utu!  Iwe ni mwanamke au mwanamme, umuhimu wa kuwa na uhusiano wa kimapenzi au kufunga ndoa na mtu anayekuthamini kwanza kama binadamu mwenye fikra zake razini na hisia, mwenye moyo wa huruma na msingi wa kimaadili au imani inayojikita kwenye kumwogopa Rabuka, hauwezi ukasisitizwa vya kutosha.  Sifa hizi zitakufaa mno wewe binafsi pamoja na mwenzako baadaye wakati kwa bahati mbaya, au nzuri, msisimko wa mapenzi utadidimia, ashiki kufifia na macho kufunguka na kukabiliana ana kwa ana na uhalisia wa mtu unayeishi au kuchumbiana naye.  Hakuna anayeingia kwenye mahusiano ya kimapenzi au kwenye ndoa akiwa na matumaini kwamba haitadumu. Wengi huwa na taswira ya jinsi watakavyoishi pamoja kwa furaha hadi uzeeni wao bila kutarajia kwamba mahusiano yao yatasambaratika.  Si ajabu kuwa ndoa huitwa kufunga pingu za maisha baada ya kulishana kiapo cha kuwa pamoja hadi wote au mmoja wao atakapomuaga mwenzake buriani.  Hata hivyo, mambo ni kangaja huenda yakaja na wakati mwingine, uchumba au ndoa husambaratika na wapenzi au wanandoa walioshibana wakakinaiana na kuchukiana vibaya.  Hapo ndipo baadhi ya wahasiriwa, katika juhudi za kulipiza kisasi au kuponza machungu kwa usaliti, kutemwa, huanza kumwaga mtama kuhusu mambo yao ya siri huku umma ukilazimishwa kutazama kwa mshangao sinema wasiofahamu ndewe wala sikio.  Ni katika kipindi hiki ambapo sifa za utu, huruma, na maadili huchangia pakubwa kumwezesha mtu binafsi kujizuia kumdhalilisha mwenzake baada ya mahusiano kuvunjika. 

read more