taifaleo.nation.co.ke
@taifaleo Sun, 16 Aug 2026 04:55:31
Ripoti yaonyesha KTDA ilikopa kuwafurahisha wakulima na bonasi
KWA miaka mingi, bonasi ya chai imekuwa ikichukuliwa na wakulima wadogo kama kipimo cha mafanikio yao shambani. Malipo makubwa ya mwisho wa mwaka yamekuwa yakitafsiriwa kuwa ushahidi wa uzalishaji mzuri, bei nzuri za chai na usimamizi bora wa viwanda. Hata hivyo, ukaguzi uliofanywa na Bodi ya Chai Kenya umefichua ukweli tofauti. Ripoti hiyo inaonyesha kuwa katika baadhi ya viwanda, sehemu ya bonasi iliyolipwa wakulima haikutokana na mapato ya mauzo ya chai bali ilitokana na mikopo kutoka benki za kibiashara. Kwa maneno mengine, baadhi ya wakulima walilipwa kile kilichoonekana kuwa bonasi ilhali fedha hizo zilikuwa mikopo ambayo baadaye ilibaki kama deni la kiwanda. Madeni hayo sasa yanapaswa kulipwa kutoka kwa mapato ya baadaye ya wakulima hao hao. Ripoti ya Machi 2026 iliyoandaliwa baada ya agizo la Wizara ya Kilimo inaonyesha kuwa kufikia Desemba 31, 2025, viwanda 69 vya chai vilikuwa na madeni ya jumla ya Sh34.05 bilioni. Kati ya fedha hizo, Sh30.36 bilioni zilikuwa mikopo iliyochukuliwa kwa jina la kufadhili shughuli za chai na bonasi za wakulima. Sekta ya chai ni muhimu sana nchini Kenya. Viwanda 71 vya wakulima wadogo vinamilikiwa na zaidi ya wakulima 650,000 na huzalisha zaidi ya nusu ya chai yote nchini. Mwaka 2025, sekta hiyo ilileta zaidi ya Sh215 bilioni. Lakini sasa baadhi ya viwanda vinakabiliwa na mzigo mkubwa wa madeni. Ripoti ya ukaguzi imeonya kuwa uwezo wa baadhi ya viwanda kuendelea kufanya kazi uko mashakani kutokana na kiwango kikubwa cha madeni. Kiwanda cha Kapkoros kiliongoza kwa kuwa na deni la Sh2.77 bilioni, kikifuatiwa na Litein na deni la Sh1.88 bilioni, Mogogosiek Sh1.60 bilioni na Kapset Sh1.48 bilioni. Wakaguzi walibaini kuwa katika kipindi cha miezi sita hadi Desemba 2025, kampuni ya KTDA Management Services iliratibu mikopo ya mabilioni ya fedha kupitia benki mbalimbali kwa viwanda 55 ili kufadhili malipo ya pili ya wakulima. Jumla ya Sh30.47 bilioni zilichukuliwa kutoka benki mbalimbali. Hata hivyo, mahitaji halisi ya viwanda kwa ajili ya bonasi na malipo mengine yalikuwa Sh25.29 bilioni pekee. Hivyo, wakaguzi hawakuweza kueleza sababu ya kukopa Sh5 bilioni zaidi. Ripoti hiyo pia imeibua maswali kuhusu jinsi fedha hizo zilivyotumiwa. Imebainika kwamba sehemu ya mikopo iliyochukuliwa kwa jina la bonasi ilitumika pia kulipa madeni ya zamani gharama za uendeshaji wa viwanda na mikopo mingine iliyokuwepo awali. Matokeo yake ni kwamba baadhi ya wakulima waliamini walikuwa wanapokea faida kutokana na mauzo ya chai ilhali fedha walizopokea zilikuwa sehemu ya mikopo. Ukaguzi huo pia umebaini udhaifu mkubwa katika usimamizi wa mikopo. Katika baadhi ya viwanda, bodi za wakurugenzi ziliidhinisha mikopo bila kutaja kiwango kinachopaswa kukopwa. Katika visa vingine, viwanda vilikopa zaidi ya kiwango kilichoidhinishwa. Tatizo jingine lilihusisha tathmini ya thamani ya chai iliyokuwa bado haijauzwa. Wakaguzi waligundua kuwa baadhi ya viwanda viliongeza thamani ya chai hiyo kwa kiwango kikubwa kuliko bei halisi ya soko. Hatua hiyo iliviwezesha kukopa fedha nyingi zaidi na kutangaza bonasi kubwa kuliko uwezo wao wa kifedha. Bodi ya Chai sasa inapendekeza kuwa malipo ya bonasi yajayo yawe yanategemea mapato halisi na fedha zilizopo, badala ya mikopo na makadirio yaliyopandishwa ya thamani ya chai. Kwa wakulima, funzo kuu kutoka kwa ripoti hiyo ni kwamba bonasi kubwa si lazima iwe ishara ya mwaka mzuri wa biashara. Wakati mwingine inaweza kuwa fedha za mkopo ambazo baadaye hulipwa kupitia mapato yao ya siku zijazo.
read moretaifaleo.nation.co.ke
@taifaleo Sun, 16 Aug 2026 03:55:36
Siasa: Kindiki sasa akimbilia wazee kutafuta nyota
NAIBU Rais Kithure Kindiki anaendelea kutumia wazee kuunganisha eneo la Mlima Kenya ili kuwa na umoja wa kisiasa kuelekea Uchaguzi Mkuu wa 2027. Wiki jana, alikutana na wazee wa jamii ya Ameru Njuri Ncheke waliompa baraka zao. Jana, Profesa Kindiki alikutana na maelfu ya wazee kutoka Mlima Kenya Mashariki na kuwaomba wazungumze na wenzao wa Mlima Kenya Magharibi kuhusu jinsi eneo hilo lenye wapigakura wengi linavyoweza kuwa na msimamo mmoja. Akizungumza katika Uwanja wa Nembure, Embu, Profesa Kindiki alisema maeneo hayo mawili yanapaswa kubaki pamoja kwa ajili ya maendeleo. Hata hivyo, alimshmbulia vikali na mtangulizi wake, Rigathi Gachagua, akimtuhumu kumdhalilisha na kumshambulia kisiasa. "Nilijaribu kumwambia Gachagua awe na tabia nzuri na apunguze kasi ili Mlima Kenya Mashariki na Magharibi ziishi kwa amani, lakini alikataa. Badala yake aliendelea kunidharau. Hana heshima. Akiendelea kuchafua jina langu, nitamuanika na kushughulika naye," Kindiki alisema. Profesa Kindiki pia alimkejeli Gachagua akisema hana hadhi ya kumfundisha siasa. Profesa Kindiki alisema umoja wa Mlima Kenya Mashariki na Magharibi ni muhimu ikiwa eneo hilo litaendelea kuwa na nafasi katika uongozi wa kitaifa na kunufaika kimaendeleo. Aliahidi kuhakikisha maeneo hayo yanaungana na kuzungumza kwa sauti moja kuhusu siasa na maendeleo. Pia alisema maeneo hayo yanapaswa kushirikiana kuhakikisha Rais William Ruto anachaguliwa tena mwaka ujao. Alimtuhumu Gachagua kwa kugawanya Mlima Kenya kwa maslahi yake ya kisiasa. "Gachagua anataka Mlima Kenya ugawanyike ili usinufaike na rasilimali za kitaifa. Gachagua ni mtu mbaya na wananchi hawapaswi kumsikiliza," alisema. Mkutano huo uliwakutanisha viongozi na wanachama wa mabaraza ya wazee ya Njuri Ncheke kutoka Meru, Nyaangi Ndiriri kutoka Mbeere, Kiama Kia Muembu kutoka Embu na Mwea Council of Elders. Wazee hao, zaidi ya 30,000 walitaka Profesa Kindiki aheshimiwe kama Naibu Rais na kiongozi wa juu kutoka Mlima Kenya Mashariki. Walisema wakati umefika kwa Mlima Kenya Magharibi kulipa fadhila kwa kuunga mkono Kindiki bila masharti katika wadhifa wake wa Naibu Rais na katika matarajio yake ya baadaye ya kuwa rais wa kwanza wa Kenya kutoka Mlima Kenya Mashariki. Wazee hao pia walitangaza Kindiki kuwa msemaji wa kisiasa wa Mlima Kenya, wakisema yeyote anayetaka kuzungumza na wakazi wa eneo hilo kuhusu siasa anapaswa kufanya hivyo kupitia Naibu Rais. Walitaja miaka ambayo Mlima Kenya Mashariki uliunga mkono viongozi kutoka Magharibi, akiwemo Jomo Kenyatta, Mwai Kibaki na Uhuru Kenyatta, pamoja na manaibu wa rais Joseph Karanja na George Saitoti. Profesa Kindiki alisema watu wa Mlima Kenya Mashariki wamekuwa wakiunga mkono viongozi kutoka Magharibi bila malalamiko. Alisema ni jambo la kusikitisha kuona baadhi ya viongozi wakimlipa kwa matusi na kumshambulia kwa maneno, licha ya kuwa yeye ndiye mtu wa kwanza kutoka Mlima Kenya Mashariki kushikilia wadhifa wa pili kwa ukubwa nchini. Alisema alimpa heshima Gachagua alipokuwa Naibu Rais na hakuwahi kumtukana alipokuwa Waziri wa Usalama wa Ndani. Kindiki pia aliunga mkono ombi la wazee la mazungumzo rasmi na wenzao kutoka Mlima Kenya Magharibi ili kuunda msimamo mmoja kuhusu mustakabali wa kisiasa, kiuchumi, kitamaduni na kimaendeleo wa eneo hilo. "Tunaunga mkono ombi la wazee wa Mlima Kenya Mashariki kuzungumza na wazee wa Mlima Kenya Magharibi kuhusu jinsi ya kuunganisha jamii zetu. Tutaheshimu watakachokubaliana," alisema. Wazee pia waliomba miradi ya maendeleo ikamilishwe haraka, ikiwemo ujenzi wa barabara ya njia mbili kutoka Makutano kupitia Embu, Chuka, Meru hadi Maua na Daraja la Nithi.
read moreRight Column Content