T

taifaleo.nation.co.ke

@taifaleo Tue, 06 Oct 2026 16:13:45

Hesabu za siasa za 2027 zinamla kichwa Sifuna

AZMA ya Edwin Sifuna ya kuwania urais inaonekana kuingia katika kipindi chake kigumu zaidi. Kilichoanza kama harakati yenye nguvu na umoja chini ya Linda Mwananchi sasa kimeanza kugeuka mgawanyiko na kuibua misafara tofauti ya kisiasa. Kila kikosi kikuu kilichoonekana kuwa tayari kuunga mkono mradi wa urais wa vuguvugu hilo sasa kinaonekana kujenga utambulisho wake wa kisiasa. Swali si tena ikiwa Linda Mwananchi ina nyufa, bali ikiwa Sifuna atastahimili kuziziba nyufa hizo kabla ya uchaguzi wa 2027. Kuibuka na kuimarika kwa vyama vinavyohusishwa na wanasiasa kama Babu Owino, James Orengo, Caleb Hamisi, Boni Khalwale, George Natembeya, Eugene Wamalwa na Rigathi Gachagua kunazua maswali mazito. Je, wanajiandaa kwa mazungumzo ya kisiasa, wanajilinda dhidi ya kusalitiwa, au ni ishara ya kutokuaminiana ndani ya upinzani? Uamuzi wa Sifuna kukumbatia The Equitable Party (TEP) dakika za mwisho unaibua maswali chungu nzima. Je, ulikuwa mkakati uliopangwa kwa makini au anajaribu kupakata kivuli baada ya kushindwa kuifanya Linda Mwananchi kuwa chombo chake cha urais? Muda sasa unakuwa silaha ya kisiasa. Muda wa usajili, uteuzi wa wagombea na mipango ya miungano unakaribia, je, Sifuna ataweza kumudu suitafahamu ya kisiasa na kiuchaguzi kwa muda mrefu? Ikiwa TEP itakuwa chombo chake, je, jina, utambulisho na maana ya kisiasa ya TEP vinaweza kubadilishwa kuwa Linda Mwananchi kwa haraka? Zaidi ya hayo,Sifuna yuko tayari kubeba gharama kubwa ya kifedha na kiutawala ya kuipa TEP msukumo wa kitaifa uliokuwa umeanza kuhusishwa na Linda Mwananchi? Umaarufu wa mikutano na mitandao ya kijamii hauwezi moja kwa moja kugeuka kuwa kura, mawakala, ofisi, vifaa vya kampeni na mtandao wa vituo vya kupigia kura. Sifuna kuwauliza wenzake na wafuasi wake ikiwa wako tayari kwenda naye hadi "mwisho wa safari" au kumwacha kunaonyesha shinikizo la kisiasa linalomkabili. Anapaswa kuponya migawanyiko ya Linda Mwananchi, kujenga msingi wa kitaifa, kukijenga chama chake, kuwaunganisha viongozi wa upinzani na kuwashawishi Wakenya kuwa anaweza kumpa Rais William Ruto ushindani wa kweli. Ingawa baadhi ya wafuasi wake wanahisi kuwa jina Sifuna pekee linatosha kusisimua wananchi na kupata kura, anacho kibarua kutafuta fedha za kampeni na kujadiliana na viongozi wakuu ambao huenda nao wana matarajio ya urais au nafasi kubwa za kisiasa. Zaidi ya yote, lazima awajengee imani kwamba kumuunga mkono hakutakuwa kujitoa mhanga kisiasa. Je, Sifuna alielewa kikamilifu mzigo uliomsubiri kabla ya kutangaza azma yake ya urais? Mihemko ya kisiasa inaweza kuleta taswira ya umoja, hasa wakati wa mikutano mikubwa, kauli mbiu na umaarufu mitandaoni vinapotafsiriwa kama vidokezo vya kupata ushindi. Ndoto ya Sifuna bado haijafa, lakini njia imekuwa ngumu zaidi. Adui wake mkubwa kisiasa huenda sirais Ruto, bali mgawanyiko ndani ya upinzani wenyewe. Takribani ionozi wote wa upinzani wanakariri umuhimu wa kuungana na kumteua mwaniaji mmoja kuwania urais. Je, watakapofanya hivyo watampa Sifuna nafasi hiyo? Iwapo hawezi kubadilisha kutokuaminiana kuwa mazungumzo, vyama pinzani kuwa muungano na shauku ya kisiasa kuwa hamasa ya kitaifa, ndoto ya Linda Mwananchi inaweza kukumbana na anguko la mapema. Je, Sifuna ataweza kuwaunganisha vigogo waliokuwa wameahidi kutembea naye, kabla hawajaamua kutembea kivyao?

read more
T

taifaleo.nation.co.ke

@taifaleo Tue, 06 Oct 2026 03:22:00

Shule za kutwa za sekondari zimejaa ada haramu, yasema ripoti

WANAFUNZI wa shule za kutwa ndio wanaobeba mzigo mkubwa wa ada haramu, huku karibu theluthi mbili wakitumwa nyumbani au kuzuiwa kuingia darasani wazazi wanaposhindwa kulipa, utafiti mpya umebaini. Utafiti wa Elimu Bora Working Group (EBWG) ulionyesha kuwa asilimia 64.9 ya wanafunzi wa shule za kutwa wamewahi kufukuzwa au kuzuiwa kuingia darasani kwa sababu ya ada hizo, ikilinganishwa na asilimia 40.5 katika shule za bweni. Bw Chris Owalla wa EBWG alisema sera ya serikali ya elimu ya sekondari bila malipo imeshindwa kuwasaidia watoto wanaohitaji msaada zaidi. "Sera ya elimu ya sekondari bila malipo haifanyi kazi kwa sababu watoto wa shule za kutwa ndio wanaoteseka zaidi," alisema. Utafiti huo uliowahusisha wazazi, walezi 388 katika kaunti 11 ulibaini kuwa shule za umma zinatoza ada haramu za kati ya Sh15,000 na Sh20,000 kwa shule za kutwa, huku za bweni zikitoza hadi Sh60,000. Baadhi ya ada hizo hutajwa kuwa za chakula cha mchana, masomo ya ziada, maendeleo ya shule, ICT, shughuli za chama cha wazazi na walimu(PTA) na masomo ya likizo. Utafiti huo ulionyesha kuwa mzigo huo huwa mkubwa zaidi kwa familia maskini. Asilimia 61.3 ya familia zinazopata chini ya Sh10,000 kwa mwezi zilisema watoto wao wamewahi kufukuzwa shule, ikilinganishwa na asilimia 23.1 ya familia zinazopata kati ya Sh30,001 na Sh60,000. Bw Cornelius Oduor wa EBWG alisema asilimia 61.6 ya waliohojiwa walisema ada hizo ni ngumu au wasizoweza kumudu huku karibu asilimia 37 wakisema wamewahi kukopa au kuuza mali ili kuzilipia. Utafiti pia ulionyesha kuwa asilimia 87.4 ya wazazi hawajawahi kulalamika kuhusu ada hizo kwa kuhofia watoto wao kuadhibiwa. EBWG sasa inataka Wizara ya Elimu kufanya ukaguzi wa kitaifa wa ada katika shule zote za umma, kuwaadhibu wanaotoza zisizoidhinishwa na kuwarejeshea wazazi fedha walizolipa kinyume cha sheria.  

read more
T

taifaleo.nation.co.ke

@taifaleo Tue, 06 Oct 2026 14:52:44

Kutawazwa kwa Kindiki kwagawanya wazee

KUTAWAZWA kwa Naibu Rais Kithure Kindiki kuwa msemaji wa Mlima Kenya kumeibua mgawanyiko katika Baraza la Wazee la Kiama Kia Ma, huku makundi mawili yakidai kuwa ndiyo yenye mamlaka halali. Mkutano wa siri wa wazee 63 ulioitishwa Septemba 28 na mlezi wa baraza hilo, Kung'u Muigai, ulihitimisha kuwa Kiama Kia Ma, lililoanzishwa mwaka 2010, limegawanyika na kwa sasa halina mamlaka halali ya kumtawaza kiongozi yeyote hadi mzozo huo utatuliwe. Bw Muigai alisema mkutano huo ulianza saa mbili usiku na kumalizika karibu saa nane alfajiri. "Ilikuwa wazi kuwa Kiama Kia Ma lililoanzishwa mwaka 2010 na lililopaswa kufanya uchaguzi kila baada ya miaka minne sasa limegawanyika," alisema. Mzozo huo unahusishwa pia na madai ya kughushi hati za usajili wa baraza hilo. Cheti kilichodaiwa kutolewa Agosti 20, 2019 kilikataliwa na Ofisi ya Msajili wa Mashirika, iliyosema saini iliyokuwa kwenye cheti hicho haikuwa ya afisa aliyedaiwa kuitia. Mwaka 2022, Ofisi ya Mkurugenzi wa Mashtaka ya Umma (ODPP) iliagiza Inspekta Jenerali wa Polisi kuchunguza madai ya kughushi cheti hicho na kuwasilisha ripoti. Mzozo huo pia umehusishwa na siasa za kuelekea uchaguzi wa 2027, huku madai yakitolewa kuhusu aliyekuwa Naibu Rais Rigathi Gachagua. Hata hivyo, Gachagua amekanusha kuhusika na akawataja wazee waliomtawaza Kindiki kuwa "bandia". Kindiki naye amejitenga na mzozo huo, akisema sherehe hiyo ilikuwa mpango wa wazee. "Nilikuwa mgeni wao. Wao ndio wanapaswa kujibu maswali hayo," alisema. Sherehe ya kumtawaza Kindiki ilifanyika katika Uwanja wa Kirigiti, Kaunti ya Kiambu, Septemba 19.

read more