T

taifaleo.nation.co.ke

@taifaleo Mon, 05 Oct 2026 09:55:26

Mafundi wanaounda boti za 'fiberglass' wanavyojihatarisha kiafya, wataalam

WATAALAMU wa afya Pwani wamewaonya mafundi wanaojihusisha na kutengeneza boti na mashua, hasa zile za 'fiberglass', dhidi ya kutovalia vifaa vya kujikinga (PPE) wakiwa kazini. Matabibu hao wanasema kutovalia vifaa vya kujikinga kama vile magwanda ya mwili, glavu, barakoa na miwani mwishowe humwacha fundi anyejishughulisha na kazi ya kutengeneza vyombo hivyo vya baharini akiugua maradhi mbalimbali, ikiwemo yale ya kupumua, ya ngozi, upofu na kadhalika. Daktari na Mtaalamu Spesheli wa Ngozi mjini Mombasa, Said Mzee anasema utengenezaji wa mashua au boti za fiberglass (nyuzi za kioo) sanasana unahusisha kemikali hatari na vumbi laini inayoweza kuharibu mwili. Dkt Mzee alishikilia kuwa wafanyakazi wasiovaa barakoa maalum na vifaa vya kinga (PPE) wanakabiliwa na hatari kubwa za kiafya. "Kazi hii inahusisha kemikali hatari na chembechembe ndogo zinazoweza kusababisha madhara makubwa ya muda mrefu mwilini. Ikumbukwe kuwa kukata, kusugua na kulainisha vifaa vya mashua huzalisha vumbi laini. Vumbi hili likivutwa puani linaweza kusababisha majeraha kwenye mapafu, pumu, na magonjwa sugu ya mfumo wa upumuaji," akasema Dkt Mzee. Alifafanua kwamba kemikali zinazotokana na fiberglass pia zikigusa ngozi au macho moja kwa moja zinasababisha mwasho mkali na hata kuharibifu macho yenyewe. "Nyuzi ndogo za kioo huchoma ngozi na kusababisha mwasho mkali, uwekundu, na vidonda, pamoja na kuwasha kwa macho. Isitoshe, kemikali zinazotumika hutoa harufu kali inayoweza kusababisha kizunguzungu, maumivu ya kichwa, na kichefuchefu," akaeleza Dkt Mzee. Naye Mtaalamu wa Afya kwenye kituo cha matibabu cha Blue Nile Mkoroshoni, kaunti ya Kilifi, Dkt Duncan Chai, alitaja utumiaji wa gundi maalum, kemikali na rangi za kupulizia kutoa gesi na mvuke wa kemikali sumu. Kulingana na Dkt Chai, kemikali hizo zinaweza kudhuru mfumo wa neva, ini, figo, na hata kusababisha saratani baada ya muda mrefu au miaka mingi ya wahusika kudumu kwenye kazi zao. Dkt Chai aliwashauri mafundi kuhakikisha wanavalia mavazi au vifaa vya kujikinga au kujilinda kikamilifu kila wanapokuwa kazini. "Ushauri wangu ni kwamba mafundi na wasaidizi wao lazima wavalie kinga dhabiti wanapokuwa kwenye mazingira yao ya utendakazi. Wavalie barakoa zifaazo ili wasivute hewa ya kemikali. Pia wavae glavu imara kulinda mikono yao wakati wa kuchanganya kemikali na kushika vifaa vyenye ncha kali. Miwani maalum ya kulinda macho yao dhidi ya vumbi la fiber na kemikali zinazoruka pia ni muhimu wawe nayo," akasema Dkt Chai. Wataalamu hao wa afya pia waliwashauri mafundi kuhakikisha wanafanya kazi kwenye maeneo wazi ambayo yana mfumo mzuri wa hewa kuzuia mrundikano wa hewa chafu na sumu. Uchunguzi uliofanywa na Taifa Leo kwenye miji ya Pwani, ikiwemo Lamu, Malindi, Kilifi, Mtwapa, Kwale, Shomoni na Diani ulibaini kuwa mara nyingi mafundi wanaofanya kazi za kutengeneza mashua hupuuzilia mbali matumizi ya vifaa vya kujikinga (PPE) wanapokuwa kazini. Mwanamazingira na Mtaalamu wa Mabadiliko ya tabianchi, Bw Mohamed Dirie Rashid alihoji kuwa mabaki na taka za mashua za fiberglass zinazotengenezwa au kutupwa karibu na fukwe za bahari ni tishio kubwa kwa mazingira na viumbe vya baharini. Bw Dirie anasema fiberglass inapoachwa juani na kupigwa na mawimbi, huanza kumomonyoka na kuvunjika vipande vidogo sana. Chembechembe hizo mwishowe huishia kumezwa na samaki, kamba, na viumbe wengine na hatimaye kuingia kwenye miili ya binadamu wanapokula vyakula vya baharini. Bw Mohamed Khuzema Salim, mmoja wa mafundi wanaojishughulisha na utengenezaji na ukarabati wa mashua na boti, hasa zile za fiberglass waliiomba serikali kuu, ile ya kaunti na wahisani kuwasaidia kutenga na kuwajengea maskani maalum za kutekelezea shughuli zao bila ya waokujidhuru na kudhuru wengine. "Pia tunaomba hayo magwanda na vifaa vingine vya kujikinga (PPE) tufadhiliwe navyo ili kufanya kazi tukiwa salama," akasema Bw Khuzema.

read more
T

taifaleo.nation.co.ke

@taifaleo Mon, 05 Oct 2026 08:55:50

Nairobi, Nakuru zadaiwa Sh75.7 bilioni

KAUNTI za Nairobi na Nakuru zinadaiwa Sh75.7 bilioni za mapato ambayo hayajalipwa, kiasi kinachozidi madeni yanayodaiwa na kaunti 45 zilizosalia kwa pamoja. Kiasi hicho ni zaidi ya theluthi mbili ya Sh113.3 bilioni ambazo kaunti zote 47 zinadaiwa kufikia Juni 30, 2026. Kwa mujibu wa ripoti ya utekelezaji wa serikali za kaunti ya mwaka wa kifedha wa 2025/2026 iliyoandaliwa na Mdhibiti wa Bajeti (COB) Margaret Nyakang'o, Nairobi inaongoza kwa deni la mapato la Sh59.09 bilioni, ikifuatiwa na Nakuru yenye Sh16.64 bilioni. Madeni ya Nairobi yanawakilisha asilimia 52.15 ya jumla ya mapato ambayo hayajalipwa kwa kaunti zote, huku Nakuru ikiwa na asilimia 14.69. "Mnamo Juni 30, 2026, Kaunti ya Nairobi ilikuwa na madeni ya juu zaidi ya Sh59.09 bilioni, ambayo ni asilimia 52.15 ya jumla ya mapato ambayo hayajalipwa. Kaunti ya Nakuru ilikuwa na Sh16.64 bilioni (asilimia 14.69) ya jumla ya madeni ya mapato," inasema ripoti hiyo. Sehemu kubwa ya madeni hayo inatokana na ushuru wa ardhi, kodi za nyumba na ada nyingine, huku baadhi ya madeni yakiwa yametokana na zaidi ya miaka 10 iliyopita. Ripoti hiyo inasema hali hii inaonyesha changamoto katika ukusanyaji wa mapato, utekelezaji wa sheria na usimamizi wa fedha, jambo linalopunguza uwezo wa kaunti kutoa huduma na kugharamia maendeleo. Mtaalamu wa utawala David Ngugi alisema kurejeshwa kwa Sh113.3 bilioni kungeongeza uwezo wa kaunti kugharamia huduma muhimu na kupunguza utegemezi wao kwa serikali kuu. "Sh113.3 bilioni zinaweza kubadilisha kwa kiasi kikubwa huduma za afya katika kaunti kadhaa. Zinaweza kugharamia na kuweka vifaa katika hospitali za kisasa katika kaunti kadhaa," akasema Bw Ngugi. "Kiasi hicho ni karibu asilimia 35 ya mgao wa fedha kwa kaunti. Pia kinaweza kugharamia miradi kadhaa mikubwa ya maji," akaongeza Bw Ngugi. Ripoti ilisema kaunti nyingi hazijafanya juhudi za kutosha kurejesha madeni hayo, hali ambayo imezifanya kutegemea zaidi fedha kutoka serikali kuu ambazo wakati mwingine huchelewa. Nairobi, ushuru wa ardhi ndio unaochangia sehemu kubwa ya deni, huku wamiliki wa mali wakidaiwa Sh51.34 bilioni. Kaunti hiyo pia inadaiwa Sh5.64 bilioni za ada za matumizi ya maeneo ya umma, Sh440.6 milioni za kodi za nyumba na ada za vibanda vya biashara, pamoja na Sh283.7 milioni kutokana na matangazo ya nje na mabango. Kampuni ya Umeme inatajwa kama mmoja wa wanaodaiwa wakubwa, ikiwa inadaiwa Sh5.6 bilioni za ada za matumizi ya maeneo ya umma. Nakuru, deni la mapato ni zaidi ya mara tatu ya Sh5.4 bilioni ambazo kaunti hiyo ilikusanya katika mwaka wa kifedha wa 2025/2026. Ushuru wa ardhi ulikuwa Sh11.8 bilioni ya deni hilo, huku kodi za nyumba ikiwa Sh782 milioni. SHA inadaiwa Sh456.9 milioni na NHIF iliyovunjwa Sh432.9 milioni. Mombasa ilikuwa na deni la tatu kwa ukubwa la Sh13.68 bilioni, ikifuatiwa na Kiambu yenye Sh5.63 bilioni. Kaunti nyingine zenye madeni makubwa ni Kitui (Sh2.2 bilioni), Busia na Kakamega (Sh1.7 bilioni kila moja), Laikipia (Sh1.4bilioni), Kisii (Sh1.3 bilioni), na Nyeri na Bomet (Sh1.2 bilioni kila moja). Kwa mujibu wa Tume ya Ugavi wa Mapato, kaunti zina uwezo wa kukusanya angalau Sh260 bilioni kila mwaka lakini zinaendelea kukusanya chini ya Sh100 bilioni. Katika mwaka wa kifedha wa 2025/2026, kaunti zote 47 zilikusanya Sh96 bilioni kutoka Sh60 bilioni mwaka uliotangulia. Bi Nyakang'o amezishauri kaunti kuimarisha mifumo ya ukusanyaji wa mapato, kutumia teknolojia na kuchukua hatua kali dhidi ya kampuni zinadaiwa ili kuongeza mapato na kupunguza utegemezi wa serikali kuu.

read more