T

taifaleo.nation.co.ke

@taifaleo Tue, 17 Nov 2026 17:22:56

Kakaye Saitoti aunga mkono anayedai kuwa mwana wa marehemu makamu huyo wa rais wa zamani

KAKA ya aliyekuwa makamu wa rais marehemu George Saitoti, ameunga mkono madai ya James Njage anayetaka kutambuliwa kama mwana wa mwanasiasa huyo aliyehudumu kama mbunge wa Kajiado kaskazini na kupewa sehemu ya urithi wake. Bw Ronald Musengi, aliyekuwa kamishna wa Tume ya Huduma za Polisi, alisema vipimo vya DNA alivyofanyiwa pamoja na Bw Njage vimethibitisha kuwa ni mpwa wake wa damu. Katika ripoti iliyowasilishwa mahakamani, uwezekano wa wawili hao kuwa na uhusiano wa damu ulionyeshwa kuwa asilimia 99.9999. Bw Musengi alisema aliamua kufanyiwa vipimo hivyo baada ya kukutana na Bw Njage na kusikiliza simulizi yake kuhusu maisha yake ya utotoni na uhusiano wake na marehemu Saitoti. Alisema maelezo ya Bw Njage kuhusu siku aliyofariki baba yake yalimfanya atake kuthibitisha uhusiano wao. Bw Njage anataka mahakama kufungua upya kesi ya urithi wa Saitoti, akisema aliachwa nje wakati mali ya marehemu ilipogawanywa kati ya mjane wake Margaret Wanjiku Saitoti na mwanawe Zachary Musengi. Anasema wakati mali hiyo ilipogawanywa alikuwa mtoto mdogo akiishi nje ya Kenya, hivyo hakufahamishwa kuhusu kesi wala kupewa nafasi ya kudai haki yake. Pia anataka wasimamizi wa mirathi kutoa hesabu kamili ya mali, mapato ya nyumba za kukodisha, uwekezaji, miamala ya benki na madeni. Bw Njage pia ameiomba mahakama kuruhusu mwili wa Saitoti kufukuliwa ili vipimo vingine vya DNA vifanywe na wataalamu wa serikali na maabara binafsi. Hata hivyo, mjane wa Saitoti amepinga ombi hilo, akisema hamfahamu Bw Njage wala hana ushahidi wa kumhusisha na marehemu. Anasema Saitoti hakuwahi kumtambua, kumtunza au kumsaidia Njage alipokuwa hai. Pia anadai kuwa madai hayo yamewasilishwa baada ya miaka 14, muda mrefu ambao Bw Njage angeweza kudai haki yake. Mjane huyo pia anapinga kufukuliwa kwa mwili, akisema kutasababisha maumivu kwa familia, huku mabaki ya Saitoti yakiwa yaliungua katika ajali ya helikopta iliyomuua Juni 10, 2012, eneo la Kibiku kwenye msitu wa Ngong. Mahakama sasa italazimika kuamua iwapo kuna sababu za kutosha kufungua upya kesi hiyo na kuchunguza madai ya Bw Njage.

read more
T

taifaleo.nation.co.ke

@taifaleo Tue, 17 Nov 2026 14:45:38

MAONI: Huenda Babu Owino akabaki yatima wa kisiasa kwa kujipambania kivyake

UCHAGUZI wa ugavana wa Nairobi wa mwaka ujao unazidi kuwa mtihani mgumu wa kisiasa kwa Mbunge wa Embakasi Mashariki, Babu Owino. Awali alichukuliwa kama mmoja wa wagombea wenye nafasi kubwa ya kutwaa usukani wa Jiji la Nairobi ila Babu sasa amejikuta katika mazingira magumu ya kisiasa yanayotawaliwa na ushindani wa madaraka, mazungumzo ya miungano na kutokuwa na uhakika kuhusu nani anayedhibiti mwelekeo wa upinzani. Kiini cha dhoruba hii ni ushindani unaochipuka kati ya azma ya Babu ya kuwania ugavana na hesabu pana za kisiasa za Muungano wa Upinzani. Chama cha DCP, chini ya uongozi wa Rigathi Gachagua, kimeonekana kumpa James Gakuya nafasi ya kuwa mgombea wake wa ugavana wa Nairobi. Hali hii inamweka Babu katika mazingira magumu, hasa iwapo upinzani utaamua kuwa na mgombea mmoja wa pamoja. Hali inazidi kuwa tata kutokana na kuingia kwa kundi la Linda Mwananchi linalohusishwa na Seneta Edwin Sifuna. Babu ni miongoni mwa watu waliokuwa na mchango mkubwa katika kuanzishwa kwa vuguvugu la Linda Mwananchi kabla ya kusajili chama cha The Mwananchi Party (TMP) kama chombo chake cha kisiasa. Suala hili linampaka tope machoni pa wenzake kuwa mwanasiasa mnafiki anayetanguliza malengo yake bila kuwahusisha wenzake. Ikiwa Sifuna alikuwa na imani na chama kipya chake Babu Owino - TMP, asingeendelea na mpango wa kukisajili chama cha Linda Mwananchi Movement. Huenda hapa ndipo hukumu za dhambi zake zilianzia. Tofauti kuhusu chombo cha kisiasa katika uchaguzi zinaibua dalili za kutokuelewana katika upinzani. Baadhi ya viongozi wa Linda Mwananchi wamekipendelea chombo cha kisiasa cha Linda Mwananchi Movement, zaidi ya chama chake Babu -TMP. Je, Babu anasukumwa pembeni kisiasa au anaandaliwa kuwa kafara katika makubaliano makubwa ya upinzani ili kumwadhibu? Umbali unaoonekana kati ya Babu na baadhi ya viongozi wenye ushawishi katika upinzani si jambo la kufumbiwa macho. Mikutano ya Gachagua na Kalonzo Musyoka, Sifuna pamoja na viongozi wengine wa upinzani inaashiria kuwa mazungumzo ya mwaka wa 2027 yanaendeshwa na vigogo wa upinzani bila uwepo wake Babu Owino. Hatari iliyopo ni kwamba Nairobi inaweza kugeuzwa kuwa sehemu ya majadiliano ya kisiasa yanayolengwa zaidi katika kugawana nafasi za uongozi katika vyama tanzu vya upinzani. Jambo la kisiasa la eneo la Mlima Kenya haliwezi pia kupuuzwa. Gachagua anapotafuta kuimarisha ushawishi wake wa kisiasa, kuachia chama kingine ugavana wa Nairobi kunaweza kuwa jambo gumu, hasa ikizingatiwa kuwa mji mkuu ni tuzo muhimu ya kisiasa na kiuchumi. Kwa hivyo, azma ya Gakuya inawakilisha zaidi ya matarajio ya mtu binafsi; inaonyesha nia ya DCP kujenga ngome yake ya kisiasa Nairobi. Vilevile, uhusiano wa ODM na Gavana Johnson Sakaja unazidisha changamoto kwa Babu. Viongozi wa ODM wameonyesha utayari wa kuzingatia kumuunga mkono Sakaja kwa muhula wa pili baada ya kujiunga na ODM. Hatimaye, changamoto kubwa ya Babu huenda isiwe kumshinda Sakaja au Gakuya. Ni kuhimili siasa za washirika hasimu wa karibu. Huenda Babu Owino akabaki yatima wa kisiasa na kujipambania baada ya upinzani kuonyesha dalili za kutomkumbatia katika safari ya ugavana wa Nairobi.

read more