T

taifaleo.nation.co.ke

@taifaleo Tue, 29 Sep 2026 08:30:36

HELB iondolewe riba kupunguzia wanafunzi mzigo wa madeni, wadau wasema

WADAU wa elimu wanataka riba inayotozwa kwenye mikopo ya wanafunzi ifutiliwe mbali ili kupunguza mzigo wa madeni na kuwarahisishia njia ya kurejesha hela walizokopeshwa. Baraza la Elimu la Waislamu limependekeza kuondolewa kwa kipengele kinachotoza riba katika Mswada wa Ufadhili wa Elimu ya Juu na Vyuo vya Kadri, 2026, unaojadiliwa na Kamati ya Elimu katika Bunge la Kitaifa. Baraza hilo limeitaka Kamati hiyo kufuta Kifungu kinachoweka riba kwenye mikopo, pamoja na kile kinachogusia muda wa kurejesha mikopo. "Aliyekopeshwa arudishe kiasi alichokopa na ikiwa kuna ada ya usimamizi ya kutozwa basi kuwe na mjadala kuhusu kiasi hicho," akasema Said Abdalla, mwanachama wa baraza hilo. Alikuwa akiongea mbele ya kamati hiyo wakati wa kikao cha kupokea maoni ya umma kilichoongozwa na mbunge wa Mandera Kusini Abdul Haro. Kwa sasa, mikopo ya wanafunzi wa vyuo vikuu na vyuo vya kiufundi inatozwa riba ya asilimia nne kwa mwaka kwa deni linalodaiwa, pamoja na ada ya Sh1,000 ya kila mwaka ya kusimamia akaunti ya mikopo. Wanafunzi wengi wanaoomba mikopo kupitia Bodi ya Mikopo ya Elimu ya Juu (HELB) hutoka familia maskini na hutegemea fedha hizo kugharimia karo, malazi na matumizi ya kila siku. Hadi Juni 2025, idadi ya waliokiuka masharti ya kulipa mikopo ilikuwa 256,000, kabla ya kuongezeka kwa karibu asilimia 50 hadi 380,530 kwa kipindi cha miezi mitano. Wadau wanasema kuondolewa kwa riba kunaweza kuwapa walionufaika nafasi nzuri zaidi ya kurejesha mikopo yao bila mzigo wa madeni kuendelea kuongezeka. Muungano wa Shule za Upili na Vyuo Anuwai (KUPPET) pia umeeleza wasiwasi kuhusu mfumo unaopendekezwa wa ufadhili, ukisema hazina hiyo haijitegemei. Katibu Mkuu wa KUPPET Akello Misori alisema hali hiyo inaweza kufanya mgao wa kila mwaka usiwe wa uhakika na kuwaacha wanafunzi wanaoendelea na masomo bila fedha za kukamilisha kozi . "Hakuna hakikisho kwamba wanafunzi wanaoendelea na masomo watapata ufadhili hadi watakapokamilisha masomo yao," akasema Bw Misori. Vuguvugu la Elimu Bora (EBWG) nalo limeitaka serikali kutoa ufadhili kamili kwa wanafunzi wa vyuo vikuu na taasisi za elimu ya juu, ikijumuisha karo, malazi, chakula, vifaa vya mafunzona usafiri. Kundi hilo pia limependekeza ufadhili utolewe kupitia ruzuku, ufadhili wa masomo na mikopo, kutegemea mahitaji ya mwanafunzi na aina ya gharama inayohusika. Mwakilishi wa EBWG Mohamed Farah alisema kila mwanafunzi anayekubaliwa katika taasisi ya umma iliyoidhinishwa, anapaswa kupata msaada wa kutosha kugharamia masomo kwa muda wote yuko chuoni. "Ufadhili kamili unamaanisha kugharamia karo, malazi, masomo, usafiri, afya, mafunzo ya kazi, utafiti na gharama nyingine muhimu," akasema. Mshauri wa sera na mikakati katika EBWG, Boaz Waruku naye alisema Helb inafaa kutoa ruzuku, ufadhili wa masomo au mikopo kulingana na mahitaji ya mwanafunzi.

read more
T

taifaleo.nation.co.ke

@taifaleo Tue, 29 Sep 2026 08:00:45

IEBC kusajili wapigakura wapya kutoka mataifa 26 Ughaibuni

TUME Huru ya Uchaguzi na Mipaka (IEBC) imepanua usajili wa Wakenya wanaoishi ughaibuni kutoka nchi 12 hadi 26, hatua inayolenga kuwapa Wakenya wengi zaidi nafasi ya kushiriki uchaguzi mkuu wa Agosti 2027. Wakati huo huo, tume hiyo imekanusha madai kwamba inasajili raia wa nchi jirani kuwa wapigakura nchini Kenya. Mwenyekiti wa IEBC Erastus Ethekon amesema Wakenya wanaoishi ughaibuni wana haki ya kushiriki uchaguzi kama sehemu ya wajibu wao wa kikatiba. "Tume imeidhinisha mchakato wa kutambua nchi zaidi ili kuongeza idadi ya Wakenya wanaoshiriki uchaguzi kutoka nchi za nje. Usajili utaanza baada ya kuzinduliwa kwa awamu ya pili ya Usajili Endelevu wa Wapigakura," akasema Bw Ethekon. Usajili wa Wakenya walio nje ya nchi ulianza katika nchi chache wakati wa uchaguzi wa 2013 na kuongezwa katika chaguzi zilizofuata, hadi kufikia nchi 12 katika uchaguzi wa 2022. Bw Ethekon alisema hatua hiyo inazingatia Kifungu cha cha Katiba kinachotaka usajili wa Wakenya wanaoishi nje ya nchi uendelee ili watimize haki yao ya kushiriki uchaguzi. Alisema usajili wa wapigakura walioko nje ya nchi si mchakato wa siri au usio rasmi, bali ni jukumu la IEBC lililotambuliwa na Katiba na linalotekelezwa kupitia mifumo maalumu chini ya usimamizi wa tume. Alikanusha pia madai kwamba IEBC inawasajili raia wa Uganda kuwa wapigakura, akisema madai hayo yanaweza kudhoofisha imani ya umma katika uadilifu na usalama wa uchaguzi. Bw Ethekon alisema hadi sasa hakuna mtu, shirika au kikundi kilichowasilisha ushahidi wa kuaminika kuhusu madai ya ukiukaji wa sheria au ubadhirifu. Alisema iwapo ushahidi wa kuaminika utawasilishwa, tume itachukua hatua zinazofaa, ikiwemo uchunguzi wa makosa ya jinai na kuwafikisha wahusika mahakamani.

read more