T

taifaleo.nation.co.ke

@taifaleo Fri, 25 Sep 2026 07:55:37

Shughuli zakwama Mombasa mihadarati ya thamani ya Sh8.2 bilioni ikiteketezwa

SHUGHULI za kawaida zilisitishwa kwa muda Mombasa Alhamisi asubuhi wakati msafara wenye ulinzi mkali ulipokuwa ukielekea katika kiwanda cha simiti cha Bamburi kutoka kambi ya jeshi la wanamaji iliyo Mtongwe. Msafara huo uliojumuisha walinzi wa usalama wenye silaha ulikuwa ukienda kwa shughuli ya kuteketeza dawa za kulevya aina ya methamphetamine zilizokadiriwa kuwa za Sh8.2 bilioni. Operesheni hiyo ilihusisha maafisa kutoka Jeshi la Wanamaji, Idara ya Kuchunguza Uhalifu (DCI), Idara ya Huduma ya Polisi, Polisi wa Kimataifa (Interpol) na Afisi ya Mkurugenzi wa Mashtaka ya Umma (ODPP). Tanuri za Bamburi Cement zimeidhinishwa na Mamlaka ya Kitaifa ya Usimamizi wa Mazingira (NEMA) kwa ajili ya uharibifu salama na uchakataji wa taka hatari na zisizo hatari. Kupitia Geocycle Kenya, kiwanda hicho pia hutumia taka zinazochomwa kama chanzo mbadala cha nishati ya joto katika uzalishaji wa simiti. Dawa hizo haramu kwanza zilipimwa uzani na kuthibitishwa kuwa zile halisi zilizokamatwa, kabla ya mahakama kutoa amri ya mwisho kuruhusu mchakato uliofuata.  Hakimu Mkuu Anthony Mwicigi alisimamia shughuli hiyo na kuamrisha kwamba dawa hizo ziharibiwe, baada ya mahakama kuridhika kwamba zilikuwa zile zile ambazo zilipatikana kwa washukiwa. Washukiwa hao ambao ni raia wa Iran ni Jaseem Darzadeh Nia, Nadeem Jadgal, Hassan Baloch, Raheem Baksh, Imran Baloch na Imtiyaz Daryay. Wanadaiwa kusafirisha kilo 1,036.044 za methamphetamine zenye thamani ya takriban Sh8.2 bilioni, na kesi yao bado inaendelea katika Mahakama ya Shanzu. Upande wa mashtaka unadai kuwa dawa hizo zilisafirishwa ndani ya meli MV Mashaallah, ambayo inadaiwa haikusajiliwa na haikuwa na uraia wa nchi yoyote. Meli hiyo ilikamatwa katika bahari kuu, huku kosa linalodaiwa kutendeka kati ya Oktoba 17 na 20, 2025. Washukiwa hao sasa wataanza kuwasilisha utetezi wao mmoja baada ya mwingine huku kesi hiyo ikiendelea. Tanuri ya Bamburi Cement imewahi kutumiwa kwa shughuli kama hiyo awali. Katika mwaka wa 2025, mihadarati aina ya heroin na kokeni za Sh400 milioni ziliharibiwa hapo baada ya washukiwa kupatikana na hatia au kupoteza maisha kwa njia zisizoeleweka. Waziri wa Usalama wa Ndani, Bw Kipchumba Murkomen, alisema shughuli hiyo ya Alhamisi ilithibitisha nia ya serikali kukatiza mitandao ya ulanguzi wa dawa za kulevya kimataifa.  "Leo tunatuma ujumbe sio tu kwa watumizi bali pia walanguzi wakubwa wa mihadarati. Tumeweka wazi kwamba serikali itatwaa mali za walanguzi wote na kuzitumia kurekebisha tabia za waraibu na shughuli nyingine za kukabiliana na biashara hiyo haramu," akasema. Shughuli nzima ilifanywa kwa utaratibu na kushirikisha pande zote husika za kesi, ili kuepusha changamoto kama zile zilizoibuka baada ya serikali kulipua meli iliyodaiwa kuwa na mihadarati baharini mwaka wa 2014 chini ya aliyekuwa rais Uhuru Kenyatta. Hatua hiyo ilizua utata na kutatiza kesi iliyokua ikiendelea, hadi baadhi ya washukiwa wakaachiliwa huru mwaka wa 2025 wakati mahakama ilipoamua kulikuwa na udhaifu wa kisheria, ikiwemo uharibifu wa meli husika kabla ushahidi muhimu kukusanywa.

read more
T

taifaleo.nation.co.ke

@taifaleo Fri, 25 Sep 2026 06:55:30

Kauli ya Uhuru yafufua kidonda cha uchaguzi wa 2022

KAULI ya aliyekuwa Rais Uhuru Kenyatta kwamba bado anaamini marehemu Raila Odinga ndiye aliyeshinda uchaguzi mkuu wa urais wa mwaka 2022 imezua mjadala mkali wa kisiasa, huku ikifungua upya majeraha ya uchaguzi huo na kuibua maswali mapya kuhusu yaliyojiri baada ya kura za Agosti 9, 2022. Akizungumza katika makao makuu ya chama cha Jubilee jijini Nairobi, Bw Kenyatta alisema hana shaka kuwa Raila Odinga alipata kura za kutosha kushinda urais, lakini mambo yalienda kwa njia ambayo hakutaka yajirudie tena. "Tulifanya kila kitu kuhakikisha Baba anakuwa Rais wa Jamhuri ya Kenya. Alipata kura na hadi leo ninaamini ndiye aliyeshinda kura hizo. Tunajua yaliyotokea na hatutaki yatokee tena kwa njia hiyo," alisema. Kauli hiyo imezua mvutano mpya kati ya viongozi wa chama tawala cha UDA, viongozi wa ODM na hata baadhi ya wanafamilia wa marehemu Raila Odinga. Mjadala huo umefufua kumbukumbu za uchaguzi wa 2022 wakati Tume Huru ya Uchaguzi na Mipaka (IEBC) ilimtangaza William Ruto mshindi kwa kura 7,176,141 sawa na asilimia 50.49 dhidi ya kura 6,942,930 za Raila Odinga zilizokuwa asilimia 48.85. Baadaye Mahakama ya Juu ilitupilia mbali kesi zote zilizopinga ushindi wa Dkt Ruto na kuthibitisha matokeo hayo mnamo Septemba 5, 2022.  Kiongozi wa ODM, Dkt Oburu Oginga, alisema kauli ya Uhuru inathibitisha kile ambacho chama chake kiliamini wakati huo, lakini imezua maswali mapya. "Ikiwa alikuwa na hakika Raila alishinda, kwa nini serikali yake ilikabidhi madaraka kwa mtu ambaye aliamini hakushinda uchaguzi?" alihoji. Dkt Oginga alisema ODM ilitumia njia zote za kikatiba kupinga matokeo ya uchaguzi lakini baada ya kushindwa mahakamani iliamua kuacha suala hilo na kuendelea mbele kwa manufaa ya taifa. "Baada ya kutumia njia zote za kikatiba zilizokuwapo, tuliamua kulimaliza suala hilo na kusonga mbele kama nchi," alisema. Aidha alionya dhidi ya kutumia uchaguzi wa 2022 na mchango wa Raila Odinga kama silaha ya kampeni za kisiasa kuelekea uchaguzi wa 2027. Kwa upande wake, Bw Kenyatta alitetea nafasi yake katika kampeni za Raila mwaka 2022 na kupinga madai kwamba hakufanya vya kutosha kumuunga mkono. "Wanaposema walinishinda, je ni mimi niliyekuwa kwenye kura au alikuwa Raila Odinga? Niliwezaje kushindwa ilhali nilikuwa nasaidia Raila?" aliuliza. Rais William Ruto naye aliwahi kumjibu Bw Kenyatta katika mkutano huko Siaya, akisema ikiwa hakumshinda alipokuwa rais, itakuwa vigumu zaidi kumshinda sasa akiwa amestaafu.  "Uhuru Kenyatta hakunishinda alipokuwa Rais, sasa mimi ndiye Rais na yeye amestaafu. Atawezaje kunishinda?" alihoji Dkt Ruto.   Katibu Mkuu wa UDA, Hassan Omar alikataa madai ya Bw Kenyatta na kusisitiza kuwa Dkt Ruto alishinda uchaguzi huo kwa njia halali. "Rais William Ruto alishinda uchaguzi wa mwaka 2022 kwa uwazi na kwa uhalali kamili," alisema Omar. Naye kiongozi wa Wiper Kalonzo Musyoka ameongeza uzito wa mjadala huo kwa kudai kuwa upande wa Raila Odinga uliibiwa ushindi sio tu mwaka 2022 bali pia katika uchaguzi wa 2013 na 2017. Akizungumza Kitui, Kalonzo alisema anaamini muungano wao ulishinda mara zote tatu lakini haukutangazwa mshindi. Kauli za Bw Kenyatta pia zimegawanya maoni ndani ya familia ya Odinga. Ndugu yake Raila, Omondi Oginga, alimkosoa kwa kufufua suala hilo miaka kadhaa baada ya uchaguzi na baada ya kifo cha kiongozi huyo wa ODM. "Uhuru hapaswi kucheza mchezo huu nasi. Raila ameondoka na hatufurahii suala hili kufufuliwa tena. Alikuwa madarakani na alikuwa na uwezo wote, kwa nini hakuchukua hatua wakati huo?" alihoji. Seneta wa Narok Ledama Ole Kina naye alihoji kwa nini Bw Kenyatta anatoa madai hayo sasa ilhali alikuwa Rais, Amiri Jeshi Mkuu na ndiye aliyekabidhi mamlaka kwa Dkt Ruto. Mjadala huo umefufua historia ya uchaguzi tata nchini Kenya, hasa uchaguzi wa 2007 uliosababisha machafuko makubwa ya baada ya uchaguzi, pamoja na ule wa 2017 ambao Mahakama ya Juu ilibatilisha na kuagiza urudiwe. Sasa, huku maandalizi ya uchaguzi wa 2027 yakianza kushika kasi, kauli ya Uhuru imefanya uchaguzi wa 2022 kurejea tena katikati ya siasa za taifa.

read more