T

taifaleo.nation.co.ke

@taifaleo Thu, 17 Sep 2026 05:55:54

Kupinga matokeo ya urais kunahitaji ushahidi mzito zaidi, asema Jaji Ouko

WANAOPINGA matokeo ya uchaguzi wa urais lazima wathibitishe zaidi ya kuwepo kwa ukiukaji wa sheria au kasoro katika upigaji kura ili matokeo yaliyotangazwa yabatilishwe, Jaji wa Mahakama ya Juu William Ouko amesema. Jaji Ouko alisema lazima wanaopinga matokeo hayo waonyeshe kuwa ukiukaji unaodaiwa uliathiri matokeo au uliharibu kwa kiwango kikubwa uadilifu wa uchaguzi kiasi kwamba mahakama haiwezi kwa njia yoyote ile kuunga mkono matokeo hayo. Alisema hayo Jumanne wakati wa mhadhara wa umma katika Chuo Kikuu cha Kikatoliki cha Afrika Mashariki. "Ni jukumu la mlalamishi kuthibitisha kuwa uchaguzi uliendeshwa vibaya sana na ukakumbwa na kasoro na ukiukaji wa sheria kiasi kwamba haijalishi nani alitangazwa mshindi. Yaani, uchaguzi ulikumbwa na kasoro nyingi ambazo kwa jumla ziliharibu kwa kiasi kikubwa uadilifu wa uchaguzi," alisema. Aliongeza: "Si kila ukiukaji wa sheria unaosababisha uchaguzi kutangazwa batili." Jaji Ouko alikumbusha kuwa kabla ya Katiba ya 2010, changamoto za matokeo ya urais zilikabiliwa na vikwazo vya kisheria na kiutaratibu. Katika kesi ya mwaka wa 1997, kesi ya aliyekuwa mgombea wa urais Mwai Kibaki kupinga ushindi wa Rais Daniel arap Moi lilitupiliwa mbali kwa sababu Kibaki hakumfikishia Moi stakabadhi za kesi binafsi. Kwa mujibu wa Jaji Ouko, uamuzi huo ulionyesha udhaifu wa mfumo uliokuwepo ambao haukuwezesha mzozo kuhusu uhalali wa mamlaka ya urais kushughulikiwa kikamilifu kwa misingi ya ushahidi. Hali hiyo ilizidi kuwa mbaya baada ya uchaguzi wenye utata wa mwaka 2007 na ghasia zilizofuata. Tume ya Kriegler ilieleza wasiwasi kuhusu imani ya wananchi katika taasisi za uchaguzi na mahakama. Jaji Ouko alisema mgogoro huo ulionyesha kuwa mizozo ya uchaguzi isipotatuliwa kupitia taasisi za kikatiba inaweza kuhamia uwanja wa kisiasa. Katiba ya 2010 ilijibu changamoto hizo kwa kupatia Mahakama ya Juu mamlaka ya kipekee ya kushughulikia kesi zinazopinga uchaguzi wa urais. Jaji Ouko alisema hatua hiyo ililenga kuhakikisha kuwa mzozo kuhusu kiti cha juu zaidi nchini unapata uamuzi wenye mamlaka na wa mwisho. Kisheria, kesi ya kupinga matokeo ya urais lazima liwasilishwe ndani ya siku saba baada ya kutangazwa kwa matokeo. Mahakama inapaswa kutoa uamuzi ndani ya siku 14, huku uchaguzi mpya ukifanyika ndani ya siku 60 endapo uchaguzi utabatilishwa. "Hata hivyo, kufanya mambo kwa haraka hakufai kuchanganywa na pupa," alisema Jaji Ouko, akisisitiza umuhimu wa kusawazisha kasi na haki ya kila upande kusikilizwa. Alisema mzigo wa kisheria wa kuthibitisha madai hubaki kwa mlalamishi, ingawa mzigo wa kutoa ushahidi unaweza kuhamia upande mwingine pale mlalamishi anapowasilisha ushahidi wa kutosha unaohitaji majibu.

read more
T

taifaleo.nation.co.ke

@taifaleo Thu, 17 Sep 2026 06:55:30

Wanaopinga kuongezewa muhula kwa Rais Tshisekedi wa DRC wanyakwa

KINSHASA, DR Congo: POLISI nchini Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC) Jumanne waliwatia nguvuni waandamanaji katika miji kadhaa waliokuwa wakipinga mabadiliko yanayopendekezwa ya Katiba. Wakosoaji wanahofia mabadiliko hayo yanaweza kumruhusu Rais Felix Tshisekedi kuwania muhula wa tatu. Katika jiji kuu la Kinshasa, polisi walitumia vitoza machozi na kufyatua risasi hewani wakati ambapo maandamano yalikuwa yamechacha. Maandamano hayo yaliitishwa na Muungano wa upinzani wa C64, unaohusishwa na waliokuwa wagombea urais Martin Fayulu, Moise Katumbi na Delly Sesanga. Mamia ya watu walishiriki maandamano hayo Kinshasa, kulingana na yaliyonakiliwa na vyombo vya habari vya ndani na nje ya nchi. Maandamano hayo yalikuwa yameidhinishwa na yalianza kwa amani, lakini vurugu ziliibuka kati ya waandamanaji na wafuasi wa serikali. Pande zote zilitupiana mawe na baadhi ya waandamanaji wakaonekana wakiwa na mapanga, hali iliyosababisha polisi kuingilia kati. Katika miji ya Lubumbashi na Uvira, maandamano yalipigwa marufuku na serikali za mitaa, lakini waandamanaji walijibwaga barabarani kabla ya polisi kuwatawanya. Hii ni mara ya pili ndani ya miezi michache kwa C64 kuandaa maandamano dhidi ya mabadiliko ya Katiba. Maandamano ya awali yaliyofanyika Kinshasa mwezi Juni yalivunjwa kwa nguvu na vikosi vya usalama. Mvutano huo unatokea wiki tatu baada ya Rais Tshisekedi kutangaza mpango wa kuandaa mazungumzo ya kitaifa yatakayoleta pamoja vyama vya upinzani, mashirika ya kiraia na viongozi wa dini. Hata hivyo, waasi wanaodhibiti maeneo ya mashariki mwa nchi hawakujumuishwa. Tshisekedi amesema mazungumzo hayo yanalenga kushughulikia changamoto za kisiasa nchini humo. Hata hivyo, vyama vya upinzani na Kanisa Katoliki wamepinga mabadiliko yanayopendekezwa ya Katiba. Katiba ya DRC inasema mihula ya kuhudumu kwa rais huwa ni miwili ya miaka mitano kila mmoja. Hata hivyo, Bunge lilipitisha mswada mnamo Juni unaoruhusu mabadiliko ya Katiba kupigiwa kura ya maoni. Baadhi ya viongozi wa muungano unaounga mkono Tshisekedi wameunga mkono marekebisho ambayo yanaweza kumruhusu kuendelea kugombea urais. Hatua hiyo imezua wasiwasi miongoni mwa wapinzani na taasisi za kidini kuhusu mustakabali wa demokrasia na utulivu wa kisiasa nchini humo.

read more
T

taifaleo.nation.co.ke

@taifaleo Thu, 17 Sep 2026 08:55:47

MAONI: Linda Mwananchi isitanue misuli ya maslahi, ijali wapendavyo raia

MKUTANO wa Linda Mwananchi ulioandaliwa katika uwanja wa Jacaranda, Nairobi ni kati ya mikutano mikubwa ambayo imetia wasiwasi serikali ya Rais William Ruto na Muungano wa upinzani unaojumuisha Kalonzo Musyoka, Rigathi Gachagua, Eugene Wamalwa, Dkt Fred Matiangi, Justin Muturi na Bi Martha Karua. Kundi la Seneta wa Nairobi Edwin Watenya Sifuna liliteka Nairobi kwa kishindo kikubwa. Magazeti yakapata masoko, redio zikawataja vinara bila ukomo na vijana wa mitandao ya kijamii wakachapisha matukio muhimu ya maeneo walikofika wanasiasa hao wakijumuisha Mbunge wa Embakasi Mashariki Babu Owino, Gavana wa Siaya James Orengo, mwenzake wa Trans Nzoia George Natembeya kati ya wengine. Hata hivyo, katika chereko zote hizo, kuna vita vya chini kwa chini kuhusu ni nani anayestahili kuwa kiongozi wa Linda Mwananchi na pia mgombea Urais. Tofauti hizi kati ya Sifuna, Babu Owino na James Orengo huenda zikaliwacha vuguvugu hilo na majeraha makubwa kwa sababu jeshi kubwa la vijana lilikuwa nyuma yake. Nyufa katika ukuta huo pia zitagawanya hamu ya vijana kwa mapande tofauti na kumpa Rais Ruto nafasi rahisi kutwaa Urais kwa mara nyingine. Vivyo hivyo, kukiwa na mgawanyiko hapo katika Linda Mwananchi muungano wa United Opposition utaanza kujigamba kuwa huo ndio uliokuwa upinzani halisi wa kukabiliana na Rais Ruto. Ikumbukwe kuwa kundi hilo la vijana lina msukumo kiasi kwamba mabalozi wa nchi tofauti wanakutana na Sifuna kwa misingi kuwa athari zake zimekuwa kubwa katika jicho la diplomasia na uwezekano wa yeye kuwa Rais wa sita wa Jamhuri ya Kenya upo. Hoja nyingine inayojitokeza katika vurugumechi hii kati ya Sifuna, Orengo na Babu Owino ni kuwa walijitenga na chama cha ODM kwa kile walichodai kuwa ukosefu wa demokrasia. Je, vitendo vyao kwa sasa vinaakisi uzingativu wa demokrasia ama ni misuli ya masilahi? Waliosalia katika chama cha ODM kama mwenyekiti wake Gladys Wanga na kiongozi wa chama Oburu Oginga kwa sasa wanapiga sherehe kutokana na msukosuko huu ndani ya Linda Mwananchi. Kabla uchaguzi mkuu wa 2002, mizozo kama hii ilikuwa katika muungano wa NAK kwanza kati ya Mwai Kibaki, Wamalwa Kijana na Charity Ngilu. Kila mmoja alikuwa anataka kuwa Rais lakini wadau wakakubalia kuwa Kibaki apeperushe bendera, Wamalwa awe naibu wake. Hii iliwafanya kuaminika na hata Raila Odinga akajiunga nao bila masharti. Kundi la Sifuna litashawishi muungano wa upinzani kuliunga mkono tu endapo litakuwa na msimamo, vinginevyo safari ya kumpeleka Ruto Sugoi hatakuwa rahisi. Paul Nabiswa ni mhariri, NTV

read more