T

taifaleo.nation.co.ke

@taifaleo Thu, 17 Sep 2026 04:55:33

Alitusaidia kifedha, msamehe, wazazi wa Sharon warai korti kuhusu Obado

WAZAZI wa mwanafunzi wa Chuo Kikuu cha Rongo aliyeuawa kinyama, Sharon Otieno, wameomba Mahakama Kuu imsamehe aliyekuwa Gavana wa Migori Okoth Obado na kumpa adhabu isiyohusisha kifungo gerezani. Douglas Zacharia Otieno na Melida Auma waliwasilisha ombi hilo mbele ya Jaji Cecilia Githua wakati wa hatua ya kumpa Obado adhabu baada ya kupatikana na hatia ya kumuua binti yao. Wazazi hao waliomba mahakama izingatie mazingira yote ya kesi hiyo, ikiwemo mambo yanayoweza kupunguza au kuongeza uzito wa adhabu, kabla ya kutoa uamuzi. Walisema licha ya maumivu makubwa yaliyosababishwa na kifo cha Sharon, wamechagua kumsamehe Obado na wanataka mahakama izingatie msamaha wao. "Familia inamshukuru sana Mheshimiwa Jaji kwa kuhakikisha haki imetendeka kupitia hukumu ya kumpata na hatia. Hata hivyo, katika hatua hii muhimu ya kutoa adhabu, familia inaomba mahakama itumie busara yake kusawazisha haki na ombi la familia ya mwathiriwa," walisema. Sharon, aliyekuwa na umri wa miaka 26, alikuwa mwanafunzi wa mwaka wa pili katika Chuo Kikuu cha Rongo. Alikuwa na ujauzito wa wiki 28 alipouawa kati ya Septemba 3 na 4, 2018, katika eneo la Owade, Homa Bay. Alikuwa ametekwa nyara pamoja na mwanahabari ambaye alifanikiwa kutoroka. Obado, aliyekuwa msaidizi wake wa kibinafsi Michael Oyamo na Caspal Obiero walipatikana na hatia ya kumuua Sharon mwezi Julai. Mahakama ilisema watatu hao walishirikiana na watu wengine ambao hawakufikishwa mahakamani kutekeleza mauaji hayo. Katika ombi lao, wazazi walisema Sharon alikuwa tegemeo muhimu la familia na kifo chake kiliwaacha wakiwa wamevunjika moyo na pia katika hali ngumu kifedha. Hata hivyo, walisema Obado alijitokeza baadaye kuwasaidia kifedha. "Baada ya msiba huu, mshtakiwa wa kwanza (Obado) alifanya jambo la kipekee; alijitokeza na kusaidia familia na nyumba yetu kifedha. Hakufanya hivyo kwa amri ya mahakama, bali kwa hiari yake, akiongozwa na huruma na nia ya kuboresha hali ya maisha ya familia," walisema. Wazazi hao walisema msaada huo unafaa kuzingatiwa katika hatua ya kumwadhibu. Walieleza kuwa wanataka haki ya kurekebisha madhara yaliyosababishwa na uhalifu huo izingatiwe, badala ya adhabu pekee. "Tunaomba mahakama ikomeshe mzunguko wa maumivu. Tunaomba adhabu inayolenga kumrekebisha badala ya kulipiza kisasi pekee, na kumpa mshtakiwa wa kwanza nafasi ya kujirekebisha," walisema. Pia waliomba mahakama itumie Kifungu cha 23 cha Sheria ya Kulinda Waathiriwa na kuamuru fidia kwa familia pamoja na adhabu isiyohusisha kifungo. Hata hivyo, waliomba uamuzi huo uzingatie maslahi ya umma, haja ya kuzuia uhalifu kama huo na miongozo ya kutoa adhabu. Wazazi hao walisema wameishi na maumivu makubwa tangu Sharon alipouawa, wakieleza miaka iliyojaa machozi, kukosa usingizi na ndoto mbaya. Walisema wanataka kufunga ukurasa wa tukio hilo na kuendelea na maisha baada ya miaka ya kupitia kile walichokiita kipindi kigumu zaidi katika maisha yao. Ingawa walikiri uzito wa kosa lililotendwa, wazazi hao walisema hakuna anayeelewa ukubwa wa hasara yao kuliko wao wenyewe.

read more
T

taifaleo.nation.co.ke

@taifaleo Thu, 17 Sep 2026 03:55:54

Hali si shwari ndani ya Linda Mwananchi

MIVUTANO kuhusu madaraka na azma zinazokinzana za kisiasa miongoni mwa viongozi wakuu wa Linda Mwananchi imejitokeza hadharani, huku makundi tofauti yakionekana kuvutana kuhusu mwelekeo wa vuguvugu hilo kuelekea uchaguzi mkuu wa 2027. Kiini cha mzozo huo ni kutoaminiana na mvutano kuhusu chama kitakachotumiwa na viongozi hao waliotoka ODM. Uhasama huo mkali unashirikisha Seneta wa Nairobi, Edwin Sifuna na Mbunge wa Embakasi Mashariki Babu Owino na wanasiasa ambao wapo katika kambi yao. Kambi moja inayomuunga mkono Bw Owino inataka Bw Sifuna agombee urais kupitia chama kipya cha Mwananchi Party, ambacho bado hakijazinduliwa rasmi. Kwa upande mwingine, Gavana wa Trans Nzoia George Natembeya anataka Seneta huyo atumie Ukombozi People's Party (UPP). Bw Owino anadaiwa kupata Muungano Party, chama cha aliyekuwa Gavana wa Kitui Kivutha Kibwana, kwa ajili ya kukibadilisha kuwa Mwananchi Party. Naye Gavana Natembeya anafanya mabadiliko katika United Democratic Party (UDP), iliyowahi kuhusishwa na marehemu Cyrus Jirongo, ili iwe UPP. Mvutano huo umechangiwa zaidi na maslahi ya kieneo kati ya viongozi wa Nyanza na Magharibi, pamoja na tangazo la Gavana wa Siaya James Orengo kwamba anataka kuwania tiketi ya urais ya Linda Mwananchi. Aidha, kuna swali kuhusu nani atakuwa kiongozi mkuu wa kisiasa wa vuguvugu hilo. Kuibuka kwa Bw Sifuna kama kiongozi maarufu zaidi kumeripotiwa kuwakwaza baadhi ya viongozi wakuu wanaohisi wanapaswa kuwa na nafasi na ushawishi sawa. Bw Owino alisema Jumanne kuwa mzozo huo unahusu zaidi chama cha kisiasa kitakachotumiwa katika uchaguzi wa 2027. Alisema alipata chama mapema mwaka huu na alikuwa akipanga kukitumia kuwania ugavana wa Nairobi kabla ya Linda Mwananchi kuanzishwa. Alisema awali yeye na wanachama wengine watatu walipewa jukumu la kutafuta chama. Mbunge wa Saboti Caleb Amisi alikuwa tayari ana chama, lakini baadaye alijiondoa baada ya kutofautiana na baadhi ya viongozi. Bw Owino alisema alipomweleza Bw Sifuna kuhusu vyama hivyo viwili, Seneta huyo alimwambia hakukuwa na tatizo mradi kuwe na muungano, huku kila mmoja akiwa kiongozi wa chama chake. Hata hivyo, alisema mvutano kuhusu chama cha kutumia bado unaendelea kuwatikisa. "Baada ya hapo kumekuwa na kuvutana kuhusu chama atakachotumia. Nimeamua kwamba tuwe na chama kimoja, lakini ikiwa hilo haliwezekani, basi tuwe na muungano kwa sababu ni miungano ambayo imeshinda chaguzi nchini," alisema. Seneta wa Vihiga, Godfrey Osotsi, ambaye ni mshirika wa Bw Sifuna, alikutana na Bw Owino Jumatano katika juhudi za kusuluhisha tofauti hizo. Hata hivyo, Bw Osotsi alipuuza ripoti za tofauti kubwa, akidai kuwa kuna juhudi za Serikali kuigawanya vuguvugu hilo kupitia propaganda. Mbunge wa Funyula Oundo Midenyo alisema kuwa hakukuwa na makubaliano yoyote kuwa Bw Sifuna angetumia chama cha Owino. "Bado tunaendelea kuafikiana lakini hakukuwa na muafaka wowote kwamba Sifuna atumie chama cha Owino," akasema Bw Oundo. Naye Mbunge wa Kabuchai Majimbo Kalasinga alihoji kwa nini Bw Owino hataki kumruhusu Bw Sifuna kuwa kiongozi wa chama chake ikiwa kweli anamuunga mkono katika azma ya urais. Mvutano huo pia umeonekana katika mikutano ya Linda Mwananchi ambao vinara hao walikwepo wikendi. Katika mkutano wa Jacaranda jijini Nairobi, maswali yaliibuka kuhusu itifaki baada ya Bw Owino kumwalika Bw Sifuna kuzungumza kwanza, badala ya kupewa nafasi ya mwisho kama kiongozi mkuu wa mkutano. Mvutano mwingine ulionekana katika mkutano wa Kitale mwezi mmoja uliopita, ambapo Mbunge wa Bumula Wanami Wamboka alichukua kipaza sauti kutoka kwa Bw Owino akiwa bado anazungumza. Aidha, kambi za Bw Orengo na Bw Sifuna zimeanza kutofautiana baada ya Gavana wa Siaya kutangaza azma yake ya kuwania urais, hatua ambayo iliwakasirisha baadhi ya wandani wa Bw Sifuna.

read more
T

taifaleo.nation.co.ke

@taifaleo Thu, 17 Sep 2026 02:55:51

Kujiondoa kwa Uhuru kwafungua vita vya ubabe Jubilee kati ya Matiang'i na Kioni

CHAMA cha Jubilee kimetumbukia katika vita vipya vya uongozi huku aliyekuwa Rais Uhuru Kenyatta akijiandaa kuacha rasmi uongozi wa chama hicho baada ya Mahakama Kuu kuamua kuwa marais wastaafu hawawezi kuendelea kushikilia nyadhifa za uongozi wa vyama zaidi ya miezi sita baada ya kuondoka Ikulu. Uamuzi huo umefungua mapambano mapya ya kumrithi Bw Kenyatta, huku Naibu Viongozi wa Jubilee Jeremiah Kioni na Fred Matiang'i wakiwa miongoni mwa wanachama muhimu katika mchuano huo. Kiini cha mzozo huo si kiti cha kiongozi pekee, bali pia udhibiti wa mtandao wa chama, mali, fedha na ushawishi wa kisiasa kuelekea Uchaguzi Mkuu wa 2027. Bw Kioni Jumanne alitangaza nia yake ya kuwania wadhifa wa Kiongozi wa Jubilee, siku moja tu baada ya Bw Kenyatta kutangaza atasalimisha uongozi wa chama. Katika taarifa yake, Bw Kenyatta alisema yuko tayari kukabidhi uongozi wa Jubilee kupitia mchakato unaozingatia katiba ya chama. Bw Kenyatta alikuwa amebaki katika uongozi wa Jubilee licha ya mzozo wa ndani uliochelewesha mabadiliko. Mnamo Machi 2025, alirejea kudhibiti chama hicho baada ya mapambano ya muda mrefu kati ya makundi hasimu. Hata hivyo, uamuzi wa Jaji Lawrence Mugambi sasa umefanya kuondoka kwake kuwa suala la kisheria badala ya uamuzi wa kisiasa. Jaji Mugambi alifafanua kuwa marais wastaafu hawazuiwi kuwa wanachama wa vyama au kushiriki shughuli za kisiasa. Kilichozuiwa ni kushikilia rasmi uongozi wa chama baada ya muda uliowekwa. Uamuzi huo umeacha Jubilee katika mchakato nyeti wa kutafuta atakayechukua nafasi ya Bw Kenyatta na kuamua mwelekeo wa chama kabla ya uchaguzi ujao. Bw Kioni sasa anataka uongozi huo upatikane kupitia Kongamano la Kitaifa la Wajumbe (NDC), akipinga uwezekano wa kiongozi mpya kupitia makubaliano ya ndani. "Jubilee ni chama cha kitaifa na kilikuwa chama tawala. Kwa hivyo, viongozi wetu hawateuliwi, wanachaguliwa na wajumbe katika Kongamano la Kitaifa la Wajumbe," alisema. Kauli hiyo imeleta mtazamo tofauti kuhusu urithi wa chama, hasa ikizingatiwa kuwa Bw Matiang'i tayari ndiye mgombea urais wa Jubilee wa 2027. Baadhi ya wafuasi wa Bw Matiang'i walitarajia kuwa hadhi yake ya kisiasa pamoja na uteuzi wake kuwa mgombea urais ungemweka katika nafasi nzuri ya kurithi uongozi wa chama baada ya Bw Kenyatta. Lakini kuibuka kwa Bw Kioni kumefanya swali hilo kuwa tata zaidi. Mmoja wa watu wa karibu na chama alisema nafasi ya kiongozi wa chama na mgombea urais ni tofauti, na kwamba mmoja hawezi kumpisha mwingine moja kwa moja. "Uzuri wa Jubilee ni kwamba, kiongozi wa chama anapoondoka, manaibu wawili wana haki, nafasi na uwezo sawa wa kuwania nafasi hiyo. Hiyo ndiyo demokrasia," alisema. Bw Kioni na Bw Matiang'i wote ni manaibu wa kiongozi wa Jubilee, jambo linaloweka msingi wa ushindani wa moja kwa moja kati ya makundi yanayowaunga mkono. Jubilee ni miongoni mwa vyama vilivyotawala siasa za Kenya wakati wa utawala wa Bw Kenyatta, ikiwa na wabunge na viongozi wengi wa kaunti. Nguvu zake zimepungua tangu Bw Kenyatta alipoondoka madarakani, lakini chama bado ni sehemu muhimu ya siasa za upinzani na mipango ya miungano kuelekea 2027. Pia kuna suala la fedha. Jubilee imewahi kuwa miongoni mwa wanufaika wakubwa wa Hazina ya Vyama vya Kisiasa, ikipokea takriban Sh240.4 milioni katika mwaka wa 2017/18, Sh434.6 milioni mwaka uliofuata, Sh564.2 milioni mwaka wa 2019/20, Sh515 milioni mwaka wa 2020/21 na Sh1.02 bilioni mwaka wa 2021/22. Kwa jumla, chama kilipokea zaidi ya Sh2.77 bilioni katika miaka hiyo mitano. Hata hivyo, mgao huo umepungua kutokana na kuporomoka kwa nguvu zake za kisiasa. Katika mwaka wa kifedha wa 2026/27, Jubilee imetengewa Sh128.86 milioni kutoka kwa Hazina ya Vyama vya Kisiasa. Mchanganuzi wa siasa Geoffrey Mboya alisema fedha ni sehemu tu ya mvuto wa chama hicho. Alisema udhibiti wa Jubilee pia unamaanisha kushikilia miundo ya wanachama, mtandao wa kitaifa, chapa ya chama na mamlaka ya kujadiliana kuhusu nafasi yake katika miungano ya kisiasa. Wakati huo huo, chama hicho kinakabiliwa na shinikizo la kurekebisha miundo yake kabla ya uchaguzi wa 2027.

read more