T

taifaleo.nation.co.ke

@taifaleo Sat, 12 Sep 2026 05:55:11

Omar aunga Shahbal kupinga mpango wa kukinga gavana Nassir

KATIBU Mkuu wa chama cha United Democratic Alliance (UDA), Hassan Omar, ameungana na mfanyabiashara Suleiman Shahbal kupinga juhudi zozote za kisiasa zinazolenga kuwazuia wagombeaji wengine kuwania ugavana kaunti ya Mombasa na kumpa Gavana Abdulswamad Nassir njia rahisi ya kutetea kiti chake mwaka wa 2027. Omar alisema uamuzi wa nani anapaswa kuongoza Mombasa unapaswa kuachwa mikononi mwa wapigakura na si kufanywa kupitia makubaliano ya viongozi wa kisiasa. Alisisitiza kuwa kila mwanasiasa anapaswa kurejea kwa wananchi na kujieleza kuhusu rekodi yake ya uongozi badala ya kutegemea mipango ya kutangaza wagombeaji. "Kusiwe na makubaliano ya kisiasa wala mtu kulazimishwa kujiondoa. Wananchi ndio waamue wanayetaka kuwa kiongozi wao," alisema Omar. Kiongozi huyo wa UDA, ambaye pia anawania ugavana Mombasa, alikosoa vikali utawala wa sasa wa kaunti hiyo akidai kuwa umeshindwa kutimiza matarajio ya wakazi. Alisema wakazi wa Mombasa wana haki ya kuchagua kiongozi mpya na kwamba kiti cha ugavana hakipaswi kuamuliwa kwenye meza za mazungumzo. Kauli za Omar zinaoana na msimamo wa Shahbal ambaye amekuwa akipinga kile anachodai ni njama ya kisiasa ya kumzuia kuwania ugavana. Shahbal amesisitiza kuwa atawania kiti hicho licha ya Rais William Ruto kumshauri aendelee kuwekeza katika sekta ya biashara badala ya kuingia tena katika siasa za uchaguzi. Akizungumza katika hafla ya uwekezaji Ikulu Nairobi hivi majuzi, Rais Ruto alisema mchango mkubwa wa Shahbal kwa taifa ni kupitia uwekezaji unaozalisha ajira na kukuza uchumi. Hata hivyo, Shahbal alikataa ushauri huo na kutangaza kuwa jina lake litakuwa kwenye kura mwaka wa 2027. Mfanyabiashara huyo pia alidai kuwa baadhi ya viongozi wa kisiasa wanatumia miundo ya vyama na hoja ya kutengewa maeneo ya kisiasa ili kuamua nani anapaswa kugombea viti mbalimbali vya uongozi. Wakati huo huo, baadhi ya madiwani kaunti ya Mombasa wamemtetea Gavana Nassir na kumtaka Shahbal kutii ushauri wa Rais. Wamesisitiza kuwa gavana huyo ana rekodi nzuri katika sekta za afya, elimu na maendeleo mengine ya kijamii. Mvutano huo umeweka Omar na Shahbal katika muungano usio wa kawaida. Ingawa wote wawili wanapania kugombea ugavana wa Mombasa na huenda wakawa wapinzani wakubwa baadaye, kwa sasa wanashirikiana kupinga juhudi zozote za kumhakikishia Nassir muhula wa pili kupitia makubaliano ya kisiasa. Huku Shahbal akisisitiza kuwa hatajiondoa kwenye kinyang'anyiro, Omar akiendelea kufanya kampeni zake na Nassir akitetea utawala wake, ushindani wa ugavana Mombasa unaonekana kuwa miongoni mwa vita vya kisiasa vitakavyovutia macho ya wengi kuelekea uchaguzi mkuu wa mwaka 2027.

read more
T

taifaleo.nation.co.ke

@taifaleo Sat, 12 Sep 2026 04:55:00

Mahangaiko tele raia wa kigeni wakihofia kuendelea kukaa nchini

HOFU, sintofahamu na wasiwasi zimetanda miongoni mwa raia wa kigeni wanaofanya biashara ndogo ndogo nchini kufuatia agizo la serikali linalowataka warekebishe hati zao za uhamiaji na vibali vya kufanya kazi ndani ya siku 90. Kwa Archade Nshimirimana, raia wa Burundi mwenye umri wa miaka 34 anayeishi Kitengela, maisha aliyojenga kwa zaidi ya miaka 11 yanaonekana kutikiswa na mwelekeo mpya wa serikali. Nshimirimana aliwasili Kenya kama mkimbizi mwaka 2015 akitoroka ghasia za kisiasa nchini Burundi. Alianza maisha kama kinyozi kabla ya kusomea huduma za urembo na hatimaye kufungua saluni yake. "Nimejenga maisha yangu hapa. Nimeoa Mkenya na nimekuwa nikisaidia wazazi wangu walioko Burundi. Wiki iliyopita imejaa hofu na mkanganyiko," alisema. Kitengela, ambayo imekuwa makazi ya maelfu ya wageni kutoka Burundi, Congo, Rwanda na Uganda, ilishuhudia biashara nyingi zinazomilikiwa na wageni zikifungwa kwa muda baada ya tangazo hilo. Wageni wengi hushughulika na biashara za vyakula, saluni, ushonaji na huduma za bodaboda. Hali kama hiyo imeshuhudiwa Nakuru ambako wafanyabiashara wengi wa kigeni wanakiri kuwa wameathiriwa kiuchumi. Iradukunda Samson, mwenye umri wa miaka 21 kutoka Burundi, amekuwa akiuza vibanzi mitaani kwa miaka mitatu. Mapato yake humwezesha kulipa kodi ya nyumba, kujikimu na kusaidia familia yake nyumbani. Alisema hofu ya kushambuliwa imewafanya baadhi ya wageni kuacha kazi huku wengine wakirejea nchini mwao. "Tuko tayari kupata vibali vinavyohitajika, lakini tunaogopa kutoka nje kwenda kufanya biashara," alisema. Katika mtaa wa Bondeni, Nakuru, Uragiwenimama Jeondodieu anayefahamika kama John, huendesha kibanda pamoja na mke wake Mkenya. Alisema wageni wengi wameishi kwa amani na wenyeji kwa miaka mingi na wanapaswa kupewa nafasi ya kurekebisha stakabadhi zao badala ya kuonekana kama wahalifu. Wakati huo huo, serikali ya Burundi imeitaka Kenya kuhakikisha usalama wa raia wak na maafisa wa serikali ya Kenya wamewahakikishia wageni usalama wao huku wakiwataka kutumia muda wa siku 90 kutafuta vibali na hati zinazohitajika. Mkuu wa Mawaziri Musalia Mudavadi alifafanua kuwa muda huo haukusudiwi kuwafukuza wageni bali kuwapa nafasi ya kutii sheria. Licha ya hakikisho hilo, wengi bado wanaishi kwa taharuki, wakisubiri kuona kitakachotokea baada ya muda wa siku 90 kukamilika. Baadhi yao wana matumaini kuwa wataendelea kuishi na kufanya kazi Kenya, nchi ambayo wameiita nyumbani kwa miaka mingi.

read more