taifaleo.nation.co.ke
@taifaleo Tue, 01 Sep 2026 15:35:53
Bei ya maziwa yapanda Nyanza na South Rift kufuatia uhaba mkubwa
BEI ya maziwa imepanda katika baadhi ya maeneo ya Nyanza na Kusini mwa Bonde Ufa, hali inayoathiri familia na wafanyabiashara wa bidhaa mbalimbali hasa vyakula. Katika Kaunti ya Homa Bay, pakiti ya maziwa ya mililita 500 sasa inauzwa kwa Sh70, kutoka Sh55 hadi Sh60. Wanaopika na kuuza chai wamelazimika kupunguza kiwango cha maziwa wanachotumia ili kudumisha bei na kulinda faida yao. Pamela Otieno, anayeendesha kibanda cha chakula Homa Bay, alisema bado anauza kikombe cha chai kwa Sh20 lakini amepunguza maziwa anayoweka kwenye chai. "Nilikuwa naweka pakiti tano za maziwa katika lita 20 za chai, lakini sasa nimepunguza hadi nne," akasema. Kutokana na kuadimika kwa maziwa, baadhi ya wateja wameanza kulalamika kuwa chai imepoteza ladha yake ya awali. Kisumu, Migori na Kisii pia zimekumbwa na mabadiliko ya bei na uhaba wa maziwa. Kule Kisumu, pakiti ya mililita 500 inauzwa kwa Sh80.
read moretaifaleo.nation.co.ke
@taifaleo Wed, 02 Sep 2026 02:55:37
Orengo: Mimi ndio nimeiva kuwa rais na nitashindana na Sifuna kwa tiketi 2027
GAVANA wa Siaya James Orengo amemtaka Seneta wa Nairobi Edwin Sifuna na wagombeaji wengine ndani ya Linda Mwananchi kukubali uteuzi wa wazi wanaposaka mwaniaji wao wa urais kuelekea uchaguzi mkuu wa 2027. Katika mahojiano na Taifa Leo Jumanne, Bw Orengo alisema hana tatizo kushindana na Bw Sifuna au mgombea mwingine yeyote wa upinzani. Alisisitiza jambo muhimu ni kuhakikisha vuguvugu hilo linapata mgombea mmoja wa kukabiliana na Rais William Ruto katika uchaguzi wa 2027. "Hakuna ubaya kwa wagombea mbalimbali kuwa na azma ya urais ndani ya Linda Mwananchi au upinzani. Muhimu ni kuwapa wote fursa ya kupitia mchakato wa uteuzi wa wazi na wa kuaminika, ili hatimaye tupate mgombea mmoja wa kukabiliana na Ruto. Huo ndio msingi wa umoja wa upinzani," akasema Bw Orengo. Gavana huyo mkongwe alisisitiza kuwa uteuzi haupaswi kuamuliwa katika vikao vya siri, akitaja uchaguzi wa urais wa ODM wa 2007 ambapo Raila Odinga, William Ruto, Musalia Mudavadi, Najib Balala na Joe Nyaga walishindana kabla ya chama kumpata mgombea wake. Alitaja pia uchaguzi wa 2002, ambapo vyama vya upinzani vilifanya mashauriano kabla ya Bw Odinga, aliyekuwa akiongoza LDP, kumuunga mkono Mwai Kibaki kupitia kauli ya "Kibaki Tosha". Bw Orengo alisema mifano hiyo inaonyesha kuwa umoja wa upinzani hauhitaji kuondoa mapema azma za wagombea mbalimbali wenye nia ya kusaka urais. Ingawa hivyo, msimamo wake umemweka pabaya na washirika wa Bw Sifuna, ambao wamekuwa wakisema wafuasi wa Linda Mwananchi tayari wameamua kumuunga mkono seneta huyo wa Nairobi. Gavana wa Trans Nzoia George Natembeya ni miongoni mwa viongozi wa Magharibi waliomuunga mkono Bw Sifuna na kusema wananchi wamekuwa wakisema "Sisi Ndio Sifuna" katika mikutano ya vuguvugu hilo. Mbunge wa Kabuchai Majimbo Kalasinga alisema hakuna haja ya kuchanganya wafuasi kwa kujitokeza kwa wagombea wengine. "Hatupaswi kuchanganyikiwa. Wakenya wamejitokeza katika kila mkutano wa Linda Mwananchi na kusema wanamtaka Edwin Sifuna kuwa mgombea wa urais," akasema Bw Kalasinga. Seneta wa Vihiga Godfrey Osotsi, hata hivyo, alisema vuguvugu hilo linamheshimu Bw Orengo kutokana na uzoefu wake wa kisiasa na mchango wake katika masuala ya mageuzi. "Vuguvugu linamheshimu sana Gavana Orengo kutokana na hadhi na uzoefu wake mkubwa katika masuala ya mageuzi," akasema Bw Osotsi, akiongeza kuwa kutakuwa na utaratibu wa kutatua suala hilo wakati ufaao. Mwanasiasa wa Jubilee Pauline Njoroge pia akiongea katika Kaunti ya Meru wakati wa mkutano wao wa kisiasa alisema suala la mgombeaji wao wa urais lishaamuliwa. "Wafuasi wetu wameweka wazi kuwa wanayemtaka ni Sifuna. Hilo limethibitishwa kupitia mikutano yetu maeneo mbalimbali nchini," akasema Bi Njoroge. Bw Orengo pia alisema jamii mbalimbali zina haki ya kufanya mashauriano kuhusu maslahi yao ya kisiasa, akitaja mijadala inayoendelea Mlima Kenya na Ukambani. Kando na kambi ya Bw Sifuna, azma ya Bw Orengo pia imewachemsha viongozi kutoka Nyanza wanaounga mkono kuchaguliwa tena kwa Rais Ruto. Waziri wa Kawi Opiyo Wandayi amemshutumu Bw Orengo kwa kutumiwa kugawanya kura za Waluo, akilinganisha hali hiyo na uchaguzi wa 2002. "Jinsi alivyotumiwa na Daniel arap Moi kugawanya kura zetu 2002, sasa anatumika tena na Uhuru kugawanya kura zetu, lakini hilo halitatokea," akasema Bw Wandayi. Waziri huyo pia alisema viongozi wa Siaya wamekubaliana kumuunga mkono Rais Ruto na sasa wanamakinikia usajili wa wapiga kura. Mwenyekiti wa ODM Gladys Wanga, pia amepuuzilia mbali uwezekano wa Bw Orengo kushinda urais, akisema hana umaarufu wowote wa maana nchini. Huku mjadala ukiendelea, Linda Mwananchi pia inajaribu kujigeuza kutoka jukwaa la kisiasa hadi chama kitakachoshiriki uchaguzi wa 2027. Hata hivyo, ombi lake la kuhifadhi jina Linda Mwananchi Party lilikataliwa na Afisi ya Msajili wa Vyama vya Siasa, hatua ambayo imeongeza changamoto kwa vuguvugu hilo. Bw Orengo pia alitetea uamuzi wake wa kukosa mkutano wa Linda Mwananchi Meru mnamo Jumapili akisema haikuhusiana na ubabe kati yake na Bw Sifuna. "Nilikuwa na shughuli nyingine nzito na Babu aliwasilisha salamu na udhuru wangu. Bado namakinikia wazo la kuwa na mgombeaji mmoja wa upinzani," akasema. Mchanganuzi wa masuala ya kisiasa Chris Omore naye anasema ukosefu wa chama thabiti huenda ukalemeza azma ya Mabw Orengo na Sifuna kumpa Rais Ruto upinzani mkali 2027.
read moretaifaleo.nation.co.ke
@taifaleo Wed, 02 Sep 2026 03:55:32
Vigogo wa 'Broadbased' waahidi Ruto kura milioni 7 Nyanza, Magharibi uchaguzi mkuu
WANASIASA wanaounga mkono serikali kutoka Nyanza na Magharibi wametangaza mipango ya kuendesha kampeni za pamoja kwa lengo la kumwezesha Rais William Ruto kupata kura milioni 7 maeneo hayo 2027. Mpango huo unalenga kuvutia kura katika ngome za kisiasa za marehemu Waziri Mkuu Raila Odinga chini ya Waziri wa Kawi Opiyo Wandayi. Sehemu ya mikakati hiyo pia ni kushinikiza watengewe nafasi ya Naibu Rais. ODM imependekeza Waziri wa Vyama vya Ushirika Wycliffe Oparanya kama mmoja wa wanaoweza kuchukua nafasi ya Profesa Kithure Kindiki. Luo Nyanza, inayojumuisha kaunti za Kisumu, Migori, Siaya na Homa Bay, ina wapiga kura milioni 2.41 kwa mujibu wa sajili ya sasa ya Tume Huru ya Uchaguzi na Mipaka Nchini (IEBC). IEBC inakadiria idadi hiyo kufikia milioni 2.78 katika uchaguzi wa Agosti 10, 2027. Magharibi nayo ina kaunti za Kakamega, Busia, Bungoma, Vihiga na Trans Nzoia zina wapiga kura milioni 2.9 kwa sasa, huku idadi hiyo ikitarajiwa kufikia milioni 3.4 ifikapo uchaguzi ujao. Hata hivyo, mpango huo unakabiliwa na upinzani kutoka kwa vuguvugu la Linda Mwananchi, ambalo limekuwa likipata umaarufu katika maeneo hayo. Baadhi ya viongozi wa Magharibi, akiwemo Gavana wa Trans Nzoia George Natembeya, Seneta wa Vihiga Godfrey Osotsi na Seneta wa Kakamega Boni Khakwale, wamejipanga kumuunga mkono Seneta wa Nairobi Edwin Sifuna kwa urais. Nyanza pia inapitia mabadiliko makubwa ya kisiasa tangu kifo cha Bw Odinga. Gavana wa Siaya James Orengo na Mbunge wa Suba Kusini Caroli Omondi wameungana na Bw Sifuna kupinga ushawishi wa uongozi wa sasa wa ODM. Hata hivyo, washirika wa Rais Ruto wanasema wataunganisha jamii za Luo na Luhya ili kumuunga mkono katika uchaguzi wa 2027. Jamii hizo kwa kiasi kikubwa zilimuunga mkono Bw Odinga katika uchaguzi wa 2022.
read moreRight Column Content