T

taifaleo.nation.co.ke

@taifaleo Sat, 29 Aug 2026 05:55:45

Idadi ya walioangamia nchini Nepal yafika 470

WITO umetolewa kwa mataifa mbalimbali kuingilia kati ili kuisaidia nchi ya Nepal baada ya idadi ya waliofariki kutokana na mafuriko makubwa yaliyokumba maeneo ya milimani ikiwa zaidi ya 470 huku zaidi ya watu 1,000 wakiendelea kutafutwa. Waokoaji wanaendelea kukagua mabonde na vijiji vilivyofunikwa na matope, mawe na vifusi baada ya mafuriko makubwa yaliyotokea Jumatano. Janga hilo lilitokea baada ya sehemu ya barafu katika Milima ya Himalaya kuyeyuka na kusababisha mkondo mkubwa wa maji, matope na mawe kuingia kwenye mito ya milimani. Awali kulikuwa na dhana kwamba tetemeko la ardhi ndilo lililosababisha maafa hayo, lakini uchunguzi wa baadaye ulionyesha kuwa kuyeyuka kwa barafu na miamba ndiko kulikosababisha mafuriko hayo. Mafuriko hayo yameathiri vibaya eneo la Rasuwa na maeneo mengine kaskazini mwa Nepal, karibu na mpaka wa China. Vijiji, barabara, madaraja na miundombinu mingine vimeharibiwa, hali inayofanya shughuli za uokoaji kuwa ngumu. Taarifa za mamlaka ya utalii Nepal zinaonyesha kuwa watalii 667 hawajulikani waliko, wakiwemo raia wa nchi 31. Takribani wageni 540 kati yao ni raia wa kigeni. India imeorodhesha raia wake 288 waliopotea, huku Amerika ikiwa na angalau 65, Malaysia 55, Ukraine 53, Uingereza 33, Australia 25 na Canada 25. Mafuriko pia yameathiri upande wa Tibet unaodhibitiwa na China. Katika jimbo la Gyirong, watu 558, wakiwemo raia 260 wa kigeni, wameripotiwa kupotea, huku China ikithibitisha vifo vitatu. Serikali za Nepal na China zimepeleka helikopta na vikosi vya uokoaji katika maeneo yaliyoathirika. Hata hivyo, barabara zilizokatika na mawasiliano kuvurugika vimeathiri juhudi za kuwafikia manusura. Wakati huo huo, mamlaka zimeonya kuhusu hatari nyingine ya mafuriko baada ya maji kuziba sehemu ya Mto Bhotekoshi na kuunda ziwa linaloweza kuvunja kingo na kusababisha mafuriko zaidi. Wakazi katika maeneo yaliyo hatarini wameonywa kuwa tayari kwa uokoaji. Nepal hupokea mvua nyingi wakati wa msimu wa monsoon, lakini wataalamu wameonya kuwa mabadiliko ya hali ya hewa yanaongeza hatari ya kuyeyuka kwa barafu na kutokea kwa mafuriko makubwa. Shughuli za uokoaji zinaendelea huku familia zikisubiri taarifa kuhusu ndugu zao waliopotea.

read more
T

taifaleo.nation.co.ke

@taifaleo Sat, 29 Aug 2026 06:55:30

Wafanyakazi wa KPA wahofia kupoteza kazi serikali ikitafuta wawekezaji wa kibinafsi

WAFANYAKAZI wa Mamlaka ya Bandari nchini (KPA) wameingiwa na wasiwasi kuhusu mustakabali wa ajira zao huku serikali ikijiandaa kuwapa wawekezaji binafsi nafasi ya kuendesha baadhi ya shughuli katika bandari za Mombasa na Lamu. Wasiwasi huo umeibuka baada ya Kamati ya Ushirikiano kati ya Sekta ya Umma na Binafsi (PPP) kuidhinisha tafiti za uwezekano wa kuhusisha sekta binafsi katika vituo muhimu vya bandari. Mkurugenzi Mkuu wa tume ya mipango ya uwekezaji kati ya umma na kampuni za kibinafi (PPP) Kefa Seda alisema Alhamisi kuwa uamuzi huo umefungua njia ya kuanza mchakato wa zabuni mwezi Septemba. Mali zitakazohusika katika awamu ya kwanza ni Gati 11 hadi 14 za Bandari ya Mombasa, Mombasa Container Terminal 1, Lamu Container Terminal na Eneo Maalum la Kiuchumi la Lamu (SEZ). "Uidhinishaji huu unahamisha mali hizi muhimu za bandari kutoka hatua ya utafiti hadi hatua ya ununuzi chini ya mfumo wa PPP," Bw Seda alisema. Mpango huo ni sehemu ya mabadiliko ya bandari za Mombasa na Lamu kuwa mfumo wa 'landlord port', ambapo serikali itaendelea kumiliki mali hizo huku sekta binafsi ikisimamia shughuli za kila siku. Hata hivyo, wafanyakazi wana hofu kuwa mpango huo unaweza kusababisha kupunguzwa kwa nafasi za ajira au kubadilishwa kwa mikataba yao. Wasiwasi huo umeongezwa na zabuni ya KPA ya kukodisha vifaa na huduma za uendeshaji, inayotaja kuajiri takriban wafanyakazi 4,700 wenye ujuzi maalum. "Kufikia sasa hatujui hatima yetu baada ya zabuni hii kuchapishwa. Wasiwasi wetu mkubwa ni aina ya wafanyakazi wanaohitajika bandarini," alisema mfanyakazi mmoja wa KPA. Nyaraka za mpango huo zinawapa wafanyakazi chaguo la kubaki KPA, kuhamishiwa taasisi nyingine za serikali au kutumwa kwa kampuni binafsi kwa hiari. Mkurugenzi Mkuu wa KPA, Kapteni William Ruto, amekanusha madai kwamba bandari inauzwa, akisema serikali itaendelea kuwa mmiliki wa miundombinu. Alisema sekta binafsi italeta mtaji na utaalamu ili kuboresha ufanisi wa bandari. Bandari ya Mombasa ilihudumia tani milioni 45.45 za mizigo mwaka jana, kutoka tani milioni 40.99 mwaka 2024, huku trafiki ya makontena ikizidi TEU milioni 2.11. Kwa sasa, wafanyakazi wanataka serikali iwape hakikisho kuhusu ajira zao kabla ya mchakato wa zabuni kuanza mwezi ujao.

read more