T

taifaleo.nation.co.ke

@taifaleo Wed, 12 Aug 2026 11:45:45

ODM katika hatari ya kupoteza Nairobi

CHAMA cha Orange Democratic Movement (ODM) kinakabiliwa na kazi ngumu kudumisha ubabe wake jijini Nairobi katika uchaguzi wa 2027 baada ya kifo cha kigogo Raila Odinga. Tangu 2005 chama hicho cha chungwa kilipoanzishwa, Raila alihakikisha ODM inalemea vyama vingine huku akiwa mwaniaji wa urais aliyeshabikiwa sana na wakazi jiji kuu. Katika kura ya 2017 ODM ilishinda kiti cha useneta, mbunge mwakilishi wa kike, viti 38 vya udiwani na viti vinane kati ya 17 vya ubunge. Wabunge wa ODM Nairobi kwa sasa ni TJ Kajwang (Ruaraka), Phelix Odiwuor 'Jalang'o' (Langata), Peter Orero (Kibra), Anthony Oluoch (Mathare), Tim Wanyonyi (Westlands), Beatrice Elachi (Embakasi Kaskazini), George Aladwa (Makadara) na Babu Owino (Embakasi Mashariki). Pia ni kupitia ODM ambapo Esther Passaris na Edwin Sifuna walishinda viti vya mbunge mwakilishi wa kike na seneta mtawalia. Hata hivyo, baada ya kifo cha Raila chungwa inakabiliwa na kibarua moto hasa kufuatia mpasuko chamani ambapo sasa kuna mirengo miwili. Mrengo wa kinara wa chama Dkt Oburu Oginga unatifuana na ule wa Linda Mwananchi unaoongozwa na Seneta Sifuna. Hali kwamba ODM inaonekana kupata ugumu kudumisha umaarufu wake ilidhihirika wiki mbili zilizopita baada ya Wanyonyi kukutana na Dkt Oginga, ambapo aliombwa arejee jiji kuu ili kuwania kiti cha ugavana 2027. Hata hivyo, Wanyonyi alikataa akisema ashakita siasa zake Bungoma huku duru zikiarifu kwamba pia ana makovu ya kupokonywa tikiti ya chama kuwania ugavana mnamo 2022. Licha ya Wanyonyi kuonekana kuwa kifua mbele wakati huo, marehemu Raila alimshawishi atetee kiti chake cha ubunge huku Muungano wa Azimio ukimwasilisha Polycarp Igathe. "Ni kweli Tim Wanyonyi alikutana na akina Dkt Oginga ambapo walijaribu kumshawishi arejee Nairobi kuwania ugavana, lakini akakataa. Aliwaambia kuwa ashaamua kupigania ugavana wa Bungoma na hata ashaanza kampeni," alisema Mbunge wa Sirisia, John Waluke, ambaye ni mwandani wa Wanyonyi na anayeunga mkono azma yake ya 2027. "Tim ameshaanza kampeni zake na ndiye kifua mbele katika kiny'ang'anyiro cha ugavana Bungoma. Hatuwezi kukubali arejee tena kuwania ugavana Nairobi," akaongeza Waluke. Mbunge huyo wa Westlands tayari amejitokeza hadharani na kutangaza kwamba anaegemea mrengo wa Linda Mwanachi wake Seneta Sifuna. Ingawa hakuhudhuria mikutano ya Linda Mwananchi mjini Trans Nzoia na Bungoma majuma mawili yaliyopita, alituma wawakilishi wake na hata akatoa mabasi ya kusafirisha raia. Mbunge wa Makadara George Aladwa ndiye sasa amejitokeza kusema analenga ugavana kupitia ODM, huku Babu Owino wa Linda Mwananchi akiwa tayari kasema hadharani awali kwamba hatatumia ODM kusaka kiti hicho. Kumekuwa na wito gavana wa sasa Johnson Sakaja ajiunge na ODM ili kuwania ugavana kwa chama hicho, lakini Aladwa amesisitiza lazima kuwe na mchujo wa chama kupata mgombea halisi atakayetwaa tikiti hiyo. Huku Passaris akiweka wazi kuwa hatatetea kiti chake cha mwakilishi wa kike, ODM haina mgombeaji mkakamavu katika nafasi hiyo. Aliyekuwa Mwenyekiti wa Chama cha Mawakili Nchini (LSK) Faith Odhiambo ametangaza kusaka kiti hicho. Anaegemea Linda Mwananchi. ODM pia inakabiliwa na migawanyiko ya ndani hasa katika mrengo wa Dkt Oginga. Imebainika kuwa wasioridhika wataamua kuwania kama wagombeaji huru, na huenda wakabwagwa na wawaniaji wa vyama pinzani. Kulingana na mchanganuzi wa masuala ya kisiasa Martin Andati, ODM kwa sasa imesalia kigae na isipobadili mikakati ushawishi wake katika jiji kuu utaisha. "Raila alikuwa mjanja na mwenye mikakati, na hilo lilimsaidia kutawala siasa za jiji kwa miaka mingi. Jambo ambalo kwa sasa ni vigumu. Oburu hana ushawishi wowote kisiasa Nairobi. Wasipobadili mikakati chama kitapoteza sana 2027," akasema mchanganuzi wa masuala ya siasa Martin Andati. Anaonya kuwa ODM kwa sasa imesalia kigae na isipobadili mikakati uhai wake wa kisiasa jijini utaisha. "Oburu hana ushawishi wowote kisiasa Nairobi. Unaona hata hana wagombeaji maarufu wa ugavana, mbunge mwakilishi wa kike na useneta. Viongozi wengi maarufu wako mrengo wa Linda Mwananchi. Kwa hivyo wasipobadili mikakati chama kitapoteza sana uwakilishi 2027," akaeleza.

read more
T

taifaleo.nation.co.ke

@taifaleo Wed, 12 Aug 2026 10:55:49

WALIOBOBEA: Andrew Omanga alitikisa sana siasa za eneo la Gusii miaka ya themanini

ANDREW John Omanga alijijengea jina kama mmoja wa wanasiasa waliokuwa na ushawishi mkubwa katika eneo la Gusii licha ya kuepuka umaarufu wa kisiasa uliokuwa na viongozi wenzake. Alikuwa mbunge wa Nyaribari, waziri katika serikali za marais Jomo Kenyatta na Daniel arap Moi, na mmoja wa watumishi wa umma waliobobea kabla ya kuingia rasmi katika siasa. Safari yake ya kisiasa ilianza mwaka 1979 alipochaguliwa kuwa Mbunge wa eneo kubwa la Nyaribari baada ya kumshinda Lawrence Sagini katika uchaguzi mkuu. Ushindi huo ulimfungulia mlango kuingia katika Baraza la Mawaziri la kwanza la Rais Daniel arap Moi, aliyekuwa amechukua mamlaka baada ya kifo cha Mzee Jomo Kenyatta mwaka 1978. Omanga aliingia serikalini kwa ushawishi wa aliyekuwa Katibu Mkuu wa Utumishi wa Umma, Simeon Nyachae, ambaye wakati huo alikuwa mmoja wa maafisa wenye nguvu zaidi serikalini. Katika baraza hilo jipya pia walikuwamo Nicholas Biwott, Moses Mudavadi, Joseph Kamotho, Charles Rubia, John Okwanyo, G.G. Kariuki, Arthur Magugu, Jonathan Ng'eno na Kabeere M'Mbijjewe. Rais Moi alisema serikali yake mpya ingeweka mkazo katika kujenga taifa na kuboresha utendaji wa serikali. Omanga aliteuliwa kuwa Waziri wa Mazingira na Maliasili kabla ya baadaye kuhamishiwa Wizara ya Viwanda. Aliyekuwa Makamu Mkuu wa Chuo Kikuu cha Jomo Kenyatta cha Kilimo na Teknolojia, Profesa Ratemo Michieka, alikumbuka Omanga kama kiongozi aliyependa elimu na hakupoteza muda. Katika kitabu chake Trails in Academic and Administrative Leadership, Michieka anaeleza kuwa Omanga alimpongeza kwa kazi nzuri aliyokuwa akifanya chuoni na papo hapo akampa barua ya kumteua kuwa mjumbe wa Bodi ya Bahari na Uvuvi ya Kenya ili kusaidia juhudi za kulinda mazingira ya pwani. Mnamo Mei 1980, Omanga aliandika historia baada ya kuchukua likizo rasmi, hali iliyomlazimu Rais Moi kutumia mamlaka yake kuhamishia kwa muda majukumu yake kwa Waziri wa Maendeleo ya Maji Jonathan Ng'eno. Mojawapo wa mambo yaliyotikisa kipindi chake serikalini lilihusu ufadhili wa Kituo cha Kimataifa cha Mikutano cha Kenyatta (KICC). Mwaka 1985, chama tawala cha KANU kiliamua kuwa KICC iwe sehemu ya mali yake pamoja na Kenya Times Media Trust na Press Trust Printing Company. Hata hivyo, serikali iliendelea kufadhili shughuli za KICC kupitia Wizara ya Utalii. Akizungumza bungeni Oktoba 9, 1986, Omanga alitetea hatua hiyo akisema kituo hicho kilikuwa muhimu kwa maendeleo ya utalii wa mikutano. Alikumbusha wabunge kuwa KICC ilikuwa imeandaa mikutano mikubwa ya kimataifa kama ule wa Benki ya Dunia na Kongamano la Umoja wa Mataifa kuhusu Wanawake, ambalo lilitangaza Kenya duniani. Alisema serikali ilinuia kuboresha KICC ili iweze kushindana na vituo vya kisasa vya mataifa kama Singapore. Licha ya hayo, mwaka 1989 KANU ilichukua rasmi umiliki wa jengo hilo baada ya ardhi iliyokuwa imejengwa kuhamishiwa chama hicho. Hatua hiyo ilifutwa mwaka 2003 kupitia amri ya Rais Mwai Kibaki. Katika siasa za Gusii, Omanga pia alijikuta akipingana na aliyekuwa mlezi wake kisiasa, Simeon Nyachae. Mwaka 1988 aliongoza kundi la wabunge wa eneo hilo kupinga azma ya Nyachae kugombea ubunge wa Nyaribari Chache. Kupitia tamko lililojulikana kama Azimio la Kebirigo, walidai Nyachae alikuwa akinuia kutumia utajiri wake kufadhili wagombea dhidi yao. Hatua hiyo ilichangia Nyachae kuzuiwa kushiriki uchaguzi mkuu wa mwaka huo. Hata hivyo, baada ya kurejeshwa kwa mfumo wa vyama vingi mwaka 1992, Omanga alijiondoa kwenye kinyang'anyiro ili kumpisha Nyachae. Mwaka 1993 aliteuliwa kuwa Mwenyekiti Mtendaji wa Shirika la Kenya National Assurance Corporation. Omanga alifariki dunia mwaka 2004 akiwa na umri wa miaka 72. Aliacha wake wawili, Clare na Grace, pamoja na watoto 10. Baada ya kifo chake, Clare Omanga aliendelea na shughuli za maendeleo alizoanzisha mumewe na pia aliwahi kuwa diwani wa kuteuliwa. Mwaka 1995 alikuwa sehemu ya ujumbe wa Kenya uliohudhuria Kongamano la Nne la Umoja wa Mataifa kuhusu Wanawake mjini Beijing, China. Tofauti na wanasiasa wengine wa Gusii kama Nyachae, Zachary Onyonka na Lawrence Sagini, Omanga hakupenda kujitafutia umaarufu kupitia vyombo vya habari. Badala yake alijikita katika miradi ya maendeleo mashinani. Anakumbukwa kwa kujenga madarasa, majengo ya shule na miradi mingine ya kijamii katika eneo la Nyaribari kabla halijagawanywa. Kabla ya kuingia katika siasa, Omanga alikuwa msomi aliyebobea. Alisomea Shule ya Amasago na baadaye St Mary's Nyabururu kabla ya kujiunga na Shule ya Upili ya Yala mwaka 1947. Mwaka 1950 alihamia Shule ya Upili ya Mang'u. Baadaye alisomea Shahada ya Sanaa katika Chuo Kikuu cha Makerere nchini Uganda, akibobea katika Kiingereza, Jiografia na Uchumi. Mwaka 1956 alijiunga alienda mjini Bombay, India, alikopata Shahada ya Uzamili katika Sayansi ya Siasa. Aliporejea Kenya aliajiriwa kama Meneja katika Kampuni ya East African Tobacco, ambayo sasa ni BAT. Aliingia katika utumishi wa umma mwaka 1961 kama Katibu Msaidizi na mwaka 1966 Rais Jomo Kenyatta akamteua kuwa Katibu Mkuu katika Ofisi ya Makamu wa Rais na Wizara ya Masuala ya Ndani, hatua iliyofungua njia ya safari yake ndefu katika siasa za Kenya.

read more
T

taifaleo.nation.co.ke

@taifaleo Wed, 12 Aug 2026 10:14:13

KINAYA: Kaa rada usitumie akili zako kama kofia 2027

HIVI ungali na akili zako au umeziangusha njiani? Adabu nazo umedumisha au umeziangika mahali ili kwanza uingie mjini kupambana na wanaume? Siku tukimpenda Kasongo na UDA yake kama biriani, wapinzani wake walitubeza kwamba fuvu zetu zilikuwa ombwe. Vibonzo vilichorwa kuonyesha vichwa vyetu vikiwa na mashimo makubwa yasiyokuwa na kitu. Vingine vilionyesha watu wa Azimio wakiokota bongo zetu chini, kutuletea na kutwambia: "Shika, ubongo wako huu, nimeuokota chini." Nasi tukikataa na kusema: "Usiwe na hofu, sihitaji ubongo kamwe." Siasa zinaweza kukuvuruga kichwa ukabaki kujiuliza kama kweli unahitaji kufikiria, au uwaachie wanasiasa watumie akili zao, angalau weye zako zipumzike kidogo. Ukizipumzisha tu, unachezwa shere na kubaki ukilia kwa miaka mitano ijayo au zaidi. Baadhi ya wanoko wa Azimio walipitiliza unoko wao na kujifanya wanatusomea mistari fulani ya Biblia: "Waraka wa Mtume Paulo kwa watoto wa UDA… Hebu sikilizeni nyie watoto wa shetani…!" Siasa zina vituko vyake, na lazima uwe mvumilivu wa kusikiliza maoni tofauti na yako, hata ikiwa yanasikika kama kelele za mwendawazimu sokoni. Labda katika kelele hizo kuna cha kujifunza. Nimekuuliza iwapo ungali na adabu kwa kuwa wakati mwingine mja hukataa kabisa kuwa mwema. Nakumbuka enzi za makeke ya ujana tukitaniana kwamba sisi tuliotokea Mlima Kenya tuliangika adabu kwenye mti fulani mjini Ruiru kabla kuingia jiji kuu Nairobi. Kisa na maana? Nairobi ni shamba la mawe, hakuna mama wa mtu, hivyo usitarajie kuhurumiwa au kusaidiwa na yeyote. Maisha yakikushinda unarejea kwenu kijijini kula mahindi na maharagwe. Leo sijui nikuandikie waraka, nikukumbushe kuwa na adabu kila wakati, au nikuhimize kutoangusha akili zao njiani. Kuanzia leo, una mwaka mzima wa kuhitaji vitu hivyo vyote. Naam, kuvihitaji hasa kwa kuwa wanasiasa wameanza kutembeza janja zao, kukukoroga akili na kukusihi uache kufikiria ili mtumie akili zao. Eti zako si muhimu wakati huu wa kampeni za uchaguzi ujao. Hofu yangu si janja za wanasiasa bali uwezo wako kutambua unapodanganywa na wajanja hao, na kutumia akili inavyostahili wala si kama kofia ya kukingia jua. Sina shaka akili unazo nyingi. Nahofia tu kwamba unaweza kuamua kuzipumzisha utumie za wanasiasa. Nahofia pia kuwa huenda ukakosa adabu na kufanya mambo ya kutia aibu ili uwafurahishe wanasiasa. Kosa kubwa unaloweza kufanya ni kula hongo ili uchague mwizi, mshirikina, mcheza-kamari na watu wengine waovu kama hao. Ol Kalou imetuonyesha kwamba tunaweza kula pesa za wezi na tukawanyima kura zetu. - Douglas Mutua ni mwanahabari Mkenya anayeishi Amerika (mutua_muema@yahoo.com)

read more