T

taifaleo.nation.co.ke

@taifaleo Sat, 19 Sep 2026 16:45:14

Wito Kenya iweke mikakati kukuza mastaa chipukizi

Kocha wa Rising Stars Gilbert Selebwa ameitaka Kenya kuwa mikakati ya muda mrefu ya kukuza chipukizi,  utakaowezesha taifa kuwa na wachezaji wanaopanda kutoka timu za wadogo hadi wakubwa. Selebwa alitoa ombi hilo baada ya matumaini ya Kenya kufuzu kwa fainali za mwakani za Kombe la Mataifa ya Afrika (AFCON) kwa wachezaji wasiozidi miaka za 20, kufifia kufuatia sare ya 1-1 dhidi ya Sudan Kusini katika mechi yao ya mwisho ya kufuzu Kundi 'C' Jumamosi jijini Dar es Salaam. "Watu wanapaswa kuelewa kwamba kujenga timu ina utaratibu wake. Hii ilikuwa mara yangu ya kwanza kunoa timu ya taifa na asilimia 70 ya wachezaji walikuwa wakicheza katika kiwango hiki kwa mara ya kwanza. Matarajio yalikuwa makubwa kutoka kwetu," alisema Selebwa. Alisema pia muundo wa kikosi hicho ulidhihirisha pengo lililopo katika mfumo wa Kenya wa kukuza vipaji vya vijana. "Ukiangalia jinsi tulivyounda kikosi, asilimia 90 ya wachezaji hawakuwa wamecheza katika AFCON ya mwaka jana, huku wengi wao wakiwa wamepandishwa hadi timu za U20 na U23," alisema. Selebwa anaamini Kenya inahitaji kuwa na kundi thabiti la wachezaji wanaopitia hatua timu za chipukizi za timu za taifa za vijana badala ya kuunda vikosi wakati mashindano yanapokaribia. "Tunapaswa kuwa na kundi maalum la wachezaji wanaopanda kutoka U15 hadi U17 na kisha U20 kwa sababu hilo ndilo tunalokosa," alisema kocha huyo wa zamani wa AFC Leopards, Shabana FC na Muhoroni Youth. Pia aliitaka Shirikisho la Soka Kenya (FKF) kuhakikisha makocha waliohitimu na wenye uwezo wanawekwa katika ngazi za chini ili kutambua na kukuza vipaji. "FKF inahitaji kuwa na makocha sahihi wanaoshuka chini kuwanoa wachezaji. Hii itasaidia kuimarisha timu zetu za vijana," aliongeza Selebwa. Kenya ilimaliza kampeni yake ya kufuzu kwa AFCON bila ushindi baada ya kupoteza 2-0 dhidi ya Burundi katika mechi yake ya kwanza kabla ya kutoka sare ya 1-1 na Sudan Kusini. Brighton Nancheri aliokoa pointi moja kwa Rising Stars kwa kusawazisha dakika ya 93 baada ya Sudan Kusini kupata bao kupitia Jonathan Ajoung dakika ya 26. Matokeo hayo yaliiacha Kenya katika nafasi ya pili Kundi C ikiwa na pointi moja, sawa na Sudan Kusini lakini ikiwa mbele kwa tofauti ya mabao. Burundi iliongoza kundi hilo kwa pointi sita na kufuzu kwa nusu-fainali. Kufuatia kutolewa huko, Kenya itakosa AFCON za mwaka ujao nchini Ghana.

read more
T

taifaleo.nation.co.ke

@taifaleo Sun, 20 Sep 2026 16:14:13

Wanafunzi wafunzwa namna ya kuzoa na kuchakata upya taka kiuchumi

KARATASI zilizotumika, chupa za plastiki, makopo na vifungashio vingine vinavyotupwa kwa pamoja mara nyingi huonekana kama taka zisizo na thamani. Lakini yamkini usilojua ni kwamba iwapo taka hizo zitatenganishwa kwa usahihi, zinaweza kubadilika zikawa vifaa vipya kabisa kwa mwanadamu huku vikitoa fursa za kipato kwa maelfu ya watu wanaoshiriki katika sekta ya uchakataji upya wa vifaa vilivyotumika (recycling). Ni kwa msingi huo ambapo mpango mpya unaolenga kuwafundisha wanafunzi kutenganisha taka kisha kuiunda taka hiyo kuwa vifaa muhimu, ulibuniwa, ukiwalenga watoto kama washiriki muhimu katika kubadilisha namna taka zinavyokusanywa na kushughulikiwa nchini. Mpango huo unalenga kuifanya shule kuwa mahali ambapo tabia ya kutenganisha taka, kutambua vifaa vinavyoweza kuchakataliwa upya/kurejelewa na kuelewa thamani ya rasilimali zilizotumika inaanza mapema. Kupitia mpango huo, unaojulikana kama Tuwezeshe, kampuni ya PAKPRO (Packaging Producer Responsibility Organisation) na Kenya Scouts Association (KSA) zinalenga kuwapa wanafunzi maarifa na ujuzi wa vitendo kuhusu usimamiaji wa taka za vifaa vya kufungia bidhaa, kama vile plastiki, karatasi, makopo na vifaa vingine vinavyoweza kuchakatwa tena. Ushirikiano huo ulizinduliwa katika Kambi ya Maskauti ya Rowallan, Nairobi, ukiwalenga watoto wenye umri wa kati ya miaka sita na 24. Sehemu muhimu ya mpango huo ni usambazaji wa mapipa 600 katika shule 150, ambapo wanafunzi watafundishwa kutenganisha taka badala ya kuzichanganya zote katika pipa moja. Lengo ni kuhakikisha kuwa vifaa vinavyoweza kurejelewa vinakusanywa kwa njia inayowezesha kupelekwa kwa wakusanyaji, vituo vya ununuzi wa taka na wachakataji walio katika sekta rasmi ya urejeleaji. Akizungumza wakati wa uzinduzi huo, Afisa Mkuu Mtendaji wa PAKPRO, Joyce Gachugi-Waweru, alisema mabadiliko ya kweli katika usimamizi wa taka yanahitaji kuanza na elimu na tabia zinazojengwa mapema. Alisema watoto wa leo ndio watakaokuwa viongozi na wafanyaji wa maamuzi katika kipindi cha miaka 20 ijayo, hivyo ni muhimu kuwafunza namna taka zinavyoweza kuwa rasilimali badala ya mzigo. "Tunataka kizazi kitakachoelewa kuwa taka si kitu cha kutupwa tu. Kuna vifaa vinavyoweza kurejelewa na kuendelea kuwa na thamani katika uchumi, ikiwa vitatenganishwa na kushughulikiwa ipasavyo," alisema. Kwa mujibu wa PAKPRO, uchanganyaji wa taka bado ni changamoto kubwa inayopunguza ufanisi wa urejeleaji. Vifaa vinavyoweza kuchakatwa vinapochanganywa na mabaki ya chakula na taka nyingine, huwa vigumu zaidi kutenganishwa na mara nyingi hupoteza thamani yake. Mpango wa Tuwezeshe unalenga kushughulikia changamoto hiyo kuanzia katika chanzo cha taka - shuleni- kwa kuwapa wanafunzi uwezo wa kutambua, kutenganisha na kuhifadhi vifaa vinavyoweza kurejelewa. Kamishna Mkuu wa KSA, Victor Radido, alisema ushirikiano huo utawezesha maskauti kutumia mtandao wao wa shule na vikundi vya vijana kueneza maarifa kuhusu usimamizi bora wa taka. Alisema elimu hiyo haitakiwi kubaki darasani pekee, bali inapaswa kuwafikia wazazi na jamii kupitia tabia ambazo wanafunzi wataendelea nazo wakiwa nyumbani. "Tunataka watoto wetu waelewe kwamba usimamiaji taka unaanza na hatua rahisi kama kuweka karatasi, plastiki na taka nyingine katika mapipa yanayofaa. Hii ni tabia watakayoweza kuendeleza shuleni, nyumbani na katika jamii," alisema. Washirika hao wanasema mpango huo hautahusu kuweka mapipa pekee, bali pia kuwasaidia wanafunzi kuelewa kinachotokea baada ya taka kuwekwa kwenye pipa. Hii ni pamoja na kufahamu safari ya chupa ya plastiki, karatasi au makopo kutoka shuleni hadi kwa mkusanyaji na hatimaye kwa mchakataji anayezigeuza kuwa malighafi au bidhaa mpya. Walimu pia watapewa nafasi ya kuongoza shughuli za vitendo, ikiwemo mashindano ya usafi, mafunzo ya ubunifu wa kutumia tena vifaa na ufuatiliaji wa kiasi cha taka kinachokusanywa. Hatua hizi zitasaidia shule kupima maendeleo na kudumisha mpango kwa muda mrefu zaidi. PAKPRO imekuwa ikishirikiana na wadau mbalimbali kuimarisha mifumo ya ukusanyaji na urejeleaji wa taka za vifungashio. Shirika hilo linasema zaidi ya chupa bilioni moja za plastiki zimekusanywa kupitia mifumo ya urejeleaji inayohusishwa na juhudi zake, huku zaidi ya Sh100 milioni zikiwa zimeelekezwa katika kukuza shughuli za urejeleaji na kuwawezesha wahusika katika sekta hiyo. Sekta ya urejeleaji inahusisha maelfu ya watu, wakiwemo wakusanyaji taka, waendeshaji wa vituo vya ununuzi wa taka, wasafirishaji, waunganishaji na wachakataji. Kwao, taka zilizotenganishwa vizuri ni malighafi yenye thamani. Kwa kuwafundisha wanafunzi kutenganisha taka, mpango huo unalenga pia kuwaonyesha uhusiano kati ya tabia za kila siku na fursa za kiuchumi zinazotokana na urejeleaji. Wanafunzi watakapojifunza kutenganisha taka shuleni, wanatarajiwa kupeleka maarifa hayo nyumbani na kuwahamasisha familia zao kufuata utaratibu huo. Ushirikiano huo unatekelezwa wakati Kenya ikiendelea kuimarisha mifumo ya usimamizi endelevu wa taka chini ya sheria na kanuni zinazosisitiza kupunguza taka, kutumia tena na kurejeleza vifaa vinavyoweza kurejeshwa. PAKPRO na KSA zinasema mpango wa Tuwezeshe ni hatua ya kujenga kizazi kitakachotambua kuwa thamani ya taka haimaliziki zinapotumiwa mara ya kwanza. Badala yake, kupitia utenganishaji sahihi, vifaa hivyo vinaweza kurejea katika uzalishaji, kusaidia biashara za urejeleaji na kupunguza kiasi cha taka kinachoishia kwenye jalala kama Dandora, Kayole na vingenevyo.

read more