T

taifaleo.nation.co.ke

@taifaleo Mon, 13 Jul 2026 06:54:54

Upinzani unahitaji umoja thabiti kabla ya 2027 au ikulu isalie ndoto ya mchana

VIONGOZI wa upinzani wanapaswa kusuluhisha mizozo yao na kuendesha mijadala kwa faragha, ili kusitiri mapungufu yanayoweza kudhoofisha taswira yao mbele ya umma. Kwa sasa, misimamo yao imekosa uthabiti katika juhudi za kushughulikia umoja, jambo linalohatarisha mageuzi ya uongozi wa taifa. Takribani kila kiongozi wa upinzani ameonyesha nia ya kugombea urais mnamo 2027. Hali hii inadhihirisha wazi kuwa umoja miongoni mwao bado ni changamoto kubwa katika mikakati ya kukabiliana na Rais William Ruto kwenye kinyang'anyiro cha urais. Iwapo mbinu yao ni kumtangaza mmoja wao baadaye kuwa mgombea wa urais, basi ni vyema waendelee kwa umakini. Lakini iwapo hawana mkakati huo, wanakosea pakubwa, kwani Rais Ruto na kikosi chake wako tayari kutumia udhaifu wao kama daraja la kujipatia ushindi. Upinzani wenye nia ya mageuzi haupaswi kuwa na sauti mbili. Mgawanyiko ndani ya umoja ni hatari. Badala ya mizozo ya vyama, viongozi wanapaswa kutoa suluhu kupitia meza moja ya mazungumzo faraghani. Licha ya vyama vyao kuwa tofauti, viongozi kutoka pembe zote za Kenya wanapaswa kuungana na kuunda muungano mmoja, utakaomteua kiongozi mwenye ushawishi mkubwa zaidi kupambana na Rais Ruto. Hatua ya kila mmoja kuona kuwa anatosha bila kumpa nafasi aliye na nguvu zaidi ni unafiki na ubinafsi unaoweza kusambaratisha upinzani na kumpa Rais Ruto kibarua chepesi. Mfano mzuri ni Jaji Mkuu mstaafu David Maraga, aliyeshirikiana na vuguvugu la Linda Mwananchi katika hafla ya kundi hilo kule Gusii. Sio lazima upinzani ujenge makao yake ndani ya Linda Mwananchi, lakini ni muhimu kutafuta jukwaa linaloweza kuwasetiri ilimradi wawe wamoja. Hatua zinazofaa ni mbili pekee: Muungano wa Upinzani Ulio Ungana au Linda Mwananchi. WAMBULWA ni mwanafunzi wa chuo Kikuu Cha Maseno

read more
T

taifaleo.nation.co.ke

@taifaleo Mon, 13 Jul 2026 07:18:24

Wizara ya Fedha yatakiwa kuondoa VAT kwenye mitambo na mashine za uchakataji mazao

WIZARA ya Kilimo na Maendeleo ya Mifugo inaendelea na mazungumzo na Wizara ya Fedha na Hazina ya Kitaifa ili kuondoa ushuru (VAT) kwenye mitambo ya uchakataji na uongezaji thamani wa mazao ya kilimo, hatua inayolenga kusaidia ukumbatiaji matumizi ya teknolojia, kuongeza uzalishaji na kuboresha ushindani wa bidhaa za Kenya katika soko la kimataifa. [caption id="attachment_190047" align="aligncenter" width="300"] Waziri wa Kilimo Mutahi Kagwe akiendesha trekta aina ya Sonalika wakati wa uzinduzi wake KICC, Nairobi na Elgon Kenya. Picha|Sammy Waweru[/caption] , anasema pendekezo hilo linahusu mitambo inayotumika kuchakata maziwa, chai na mazao mengine ya kilimo. Anasema kupunguza gharama ya kununua vifaa hivyo kutaboresha uwekezaji katika mtandao mzima wa thamani wa sekta ya kilimo. Akizungumza jijini Nairobi majuzi katika hafla ya kampuni ya Elgon Kenya kuzindua usambazaji wa trekta za Sonalika, ukumbi wa KICC, Kagwe alisema matumizi ya teknolojia ya kisasa ni nguzo muhimu katika mpango wa serikali wa kubadilisha kilimo kuwa biashara ya kisasa, yenye faida na inayovutia vijana. "Mbali na matrekta, tunataka pia vifaa vya uchakataji na uongezaji thamani wa mazao viondolewe VAT. Hatua hii itaimarisha biashara ya kilimo, kuongeza ushindani wa bidhaa zetu na kukuza mauzo ya mazao nje ya nchi," alisema. Waziri alibainisha kuwa matrekta tayari hayatozwi ushuru, jambo lililosaidia kupunguza gharama za kuyapata. Kuondoa VAT kwenye mitambo ya uchakataji kutachochea uwekezaji na ukuaji wa viwanda vijijini. Kagwe alisema changamoto kubwa zinazokwamisha matumizi ya teknolojia ni gharama kubwa za mitambo na baadhi ya wakulima kung'ang'ania mbinu za zamani za uzalishaji. "Ndio maana ushiriki wa vijana ni muhimu. Wako tayari kukumbatia teknolojia mpya na mbinu za kisasa za kilimo," alisema. [caption id="attachment_190048" align="aligncenter" width="300"] Dkt Bimal Kantaria, Mkurugenzi Mkuu Elgon Kenya akitazama trekta la Sonalika. Picha|Sammy Waweru[/caption] Kagwe aliongeza kuwa matumizi ya teknolojia na mifumo ya kidijitali yatavutia vijana wanaotazama kilimo kama biashara badala ya shughuli ya kujikimu. Kwa miaka mingi, matrekta mengi yamekuwa yakiuzwa kwa zaidi ya Sh4 milioni, hali inayofanya wakulima wengi kushindwa kuyamudu. Hata hivyo, Kagwe alisema matrekta ya Sonalika yanayouzwa kwa bei ya kuanzia karibu Sh1.4 milioni yataongeza upatikanaji wa teknolojia hiyo kwa wakulima, vyama vya ushirika na biashara za vijijini. Mkurugenzi Mkuu wa Elgon Kenya na Mwenyekiti wa Agriculture Sector Network (ASNET), Dkt Bimal Kantaria, alisema kampuni hiyo inalenga kuwapa wakulima wadogo matrekta bora kwa gharama nafuu. "Sonalika ina zaidi ya matrekta milioni moja yanayotumika duniani, huku India ikizalisha karibu milioni moja kila mwaka," Dkt Kantaria alielezea. Alisema Elgon Kenya imeshirikiana na benki za Equity, Stanbic na Prime kutoa mikopo ya hadi asilimia 90 kununua trekta, hivyo mkulima anaweza kulinunua akiwa na kima cha Sh200,000 huku pesa zilizosalia akilipa mashirika hayo ya kifedha polepole. Aidha, Elgon Kenya inapanga kuanzisha matumizi ya droni na suluhu za kilimo zinazotumia akili bandia (AI), ili wakulima waweze kupata huduma za kisasa kupitia simu za mkononi.

read more
T

taifaleo.nation.co.ke

@taifaleo Mon, 13 Jul 2026 06:16:57

TAHARIRI: Serikali inalala kazini wakati ambapo uhuni unakita mizizi nchini

SERIKALI haiwezi kuruhusiwa kukaa kimya huku visa vya uhuni wa kisiasa vikiongezeka. Kwa muda mrefu serikali imekuwa ikitoa vitisho vikali visivyotekelezwa. Kila mara viongozi wa Wizara ya Usalama wa Ndani, Idara ya Polisi na Tume ya Uchaguzi (IEBC) huahidi kuwachukulia hatua wanaovuruga mikutano ya kisiasa na kuhatarisha maisha ya wananchi. Kumbe ni maneno matupu tu! Jana, nusura dereva wa Gavana wa Murang'a Irungu Kang'ata apoteze maisha baada ya kushambuliwa wakati wa kampeni za uchaguzi mdogo wa ubunge wa Ol Kalou, Kaunti ya Nyandarua. Wakati huohuo, viongozi wa mrengo wa Linda Mwananchi wakiongozwa na Seneta wa Nairobi Edwin Sifuna na Gavana wa Siaya James Orengo walikumbana na vurugu katika mkutano wao jijini Kisumu. Matukio hayo yanajiri siku moja tu baada ya wafuasi wa chama cha DCP kushambuliwa walipokuwa wakifanya kampeni Ol Kalou, huku wiki moja tu ikiwa imepita tangu mtu mmoja auawe katika ghasia za Keumbu, Kaunti ya Kisii. Msururu huu wa matukio unaonyesha kuwa usalama katika mikutano ya kisiasa unaendelea kuzorota kwa kasi ya kutisha. Kinachotia wasiwasi zaidi ni kwamba matukio haya yanatokea mwaka mmoja kabla ya uchaguzi mkuu wa 2027, kipindi ambacho kawaida huwa na joto la kisiasa. Ikiwa hatua hazitachukuliwa sasa, nchi hii inaweza kujikuta ikirejea katika machafuko ya kisiasa sawia na yanayotokea kila mara uchaguzi unapokaribia. Waziri wa Usalama wa Ndani, Kipchumba Murkomen amekuwa akitoa onyo kwa wanaojihusisha na ghasia hizi. Je, Idara ya Polisi na IEBC nazo zimechukua hatua gani? Ahadi hizo zitakuwa na maana gani ikiwa kila siku wananchi wanaendelea kushuhudia mashambulizi mapya bila wahusika kuwajibishwa? Kilicho muhimu si kutoa matamko ya kulaani baada ya vurugu kutokea, bali kuzuia vurugu hizo kabla hazijaanza. Serikali ina vyombo vya ujasusi, polisi na mamlaka yote ya kutosha kubaini wanaopanga na kufadhili magenge ya kisiasa. Kushindwa kufanya hivyo kunazua maswali kuhusu dhamira ya kweli ya kukomesha jinamizi hili. Sheria lazima itekelezwe bila upendeleo wa kisiasa. Mtu yeyote anayepanga, kufadhili au kushiriki katika mashambulizi ya kisiasa anapaswa kukamatwa na kufikishwa mahakamani, bila kujali cheo, chama au ushawishi wake. Huo ndio utakuwa mwanzo wa kurejesha imani ya wananchi katika vyombo vya dola. Demokrasia haiwezi kustawi pale ambapo vurugu imekithiri. Serikali ina wajibu wa kuhakikisha kila mwanasiasa na kila Mkenya ana uhuru wa kushiriki shughuli za kisiasa bila hofu ya kushambuliwa. Wakati wa ahadi umepita; kilichosalia sasa ni hatua madhubuti.

read more