T

taifaleo.nation.co.ke

@taifaleo Mon, 13 Jul 2026 09:05:10

Bei ya mafuta yaanza kupanda tena baada ya Amerika kurejelea vita na Iran

TEHRAN, Iran: MASHAMBULIZI baina ya wanajeshi wa Amerika na Iran yaliyoendelea tokea wikendi yamechangia kupanda tena kwa bei ya mafuta ulimwenguni. Iran ililenga vituo vya kijeshi vya Amerika katika eneo la Ghuba na kutangaza kuwa imefunga tena Mlango-bahari wa Hormuz. Wanajeshi wa Iran Jumatatu walisema walilenga kambi za jeshi la Amerika nchini Bahrain na Kuwait na kuharibu vifaa vya kijeshi nchini Oman. Pia Iran ilishambulia ghala la silaha katika kambi ya jeshi la Anga la Prince Hassan nchini Jordan huku ikilipiza kisasi shambulizi lolote linalotekelezwa na Amerika. Amerika nayo ilishambulia mifumo ya ulinzi wa anga ya Iran, kambi ya jeshi pwani na boti za kijeshi. Ilitumia ndege za kivita, meli za kijeshi na ndege zisizo na rubani (droni). Mapigano hayo yanaonyesha kuwa muafaka wa kusitisha vita kati ya nchi hizo mbili sasa umekiukwa. Muafaka huo uliafikiwa mnamo Juni na ulilenga kufungua Mlango-bahari wa Hormuz na kusitisha vita kabisa kwa siku 60. Katika mahojiano mafupi na Reuters Jumapili, Rais wa Amerika Donald Trump alitabiri kuwa mara hii watalemea Iran katika vita hivyo. "Tunawashinda vibaya," akasema Trump. Kiongozi huyo tayari ameweka wazi kuwa hatilii manani muafaka uliotiwa saini ambao anasema umekufa japo akasema iwapo Iran inataka kunusurika bado kutakuwa na mazungumzo. Mwakilishi wa Iran kwenye mazungumzo na Amerika, Mohammad Baqer Qalibaf amesema kuwa wapo tayari kwa vita na hawatakubali kuhadaiwa tena. "Enzi za makubaliano yanayoegemea upande mmoja zimekwisha. Tuliwaambia watimize ahadi zeo au walipe gharama na sasa ukweli unaonekana," akasema. Vita vilivyoanzishwa na Amerika-Israel dhidi ya Iran mnamo Februari 28 vimevuruga usalama katika eneo la Ghuba na kuenea katika Mashariki ya Kati. Iran imeonyesha uwezo mkubwa wa kijeshi na umekuwa ukishambulia kambi za wanajeshi wa Amerika Mashariki ya Kati. Vita hivyo vimesababisha maelfu ya watu kuuawa, wengi wao wakiwa Iran na Lebanon. Iran imezima shughuli katika Strait of Hormuz na sasa kando na bei ya mafuta kupanda kuna mfumuko wa bei ya bidhaa kote ulimwenguni. Aidha Iran inasisitiza kuwa itafungua mkondo huo na kuruhusu meli za kupitisha mafuta iwapo Amerika itazima shughuli za kijeshi katika Pwani yake.

read more
T

taifaleo.nation.co.ke

@taifaleo Mon, 13 Jul 2026 08:39:52

Kampuni inavyotumia ubunifu kuvutia wateja wa maua

WAKATI mamia ya wageni wa humu nchini na kutoka mataifa mbalimbali walipofurika katika Maonyesho ya Kimataifa ya Kibiashara ya Maua (IFTEX) jijini Nairobi, kampuni moja ya Kenya ilivutia wengi kwa ubunifu wa kipekee uliosimamisha shughuli katika Ukumbi wa Visa Oshwal. Banda la Ole Engai Growers lilikuwa miongoni mwa yaliyopigwa picha zaidi katika maonyesho hayo ya mwaka huu, 2026 baada ya kuwasilisha sanamu ya farasi mwenye ukubwa wa wastani wa mnyama huyo, iliyotengenezwa kwa maua mabichi yaliyolimwa kwenye mashamba ya kampuni hiyo. Farasi huyo wa maua, aliyebuniwa kuadhimisha Mwaka wa Farasi katika kalenda ya Mwaka Mpya wa Kichina, aliunganisha sanaa na kilimo kwa njia iliyovutia wageni katika maonyesho yaliyofanyika kati ya Juni 2 na 4. Sanamu hiyo ilionekana kana kwamba ilikuwa hai kutokana na umbo lake lililoundwa kwa ustadi mkubwa, likiwa na kichwa, manyoya shingoni, mwili na miguu iliyopambwa kwa maua meupe, ya kijani na ya krimu. Ua aina ya gypsophila ndilo lililotumika zaidi kuunda mwili wa farasi huyo, likimpa mwonekano mweupe na laini kama wingu. Muundo huo uliashiria nguvu, kasi na ustahimilivu—sifa zinazohusishwa na farasi katika utamaduni wa Kichina, na pia ukuaji wa kampuni hiyo katika sekta ya maua. "Mwaka huu, 2026, ni Mwaka wa Farasi kulingana na kalenda ya Kichina. Tulitaka kuonyesha nguvu, ukuaji na uvumilivu kama kampuni kupitia maua tunayozalisha wenyewe," alisema Mkurugenzi Mwenza kampuni hiyo, Anjili Shah. Anjili alieleza kuwa wazo hilo lilibuniwa na timu ya kiufundi ya kampuni ikiongozwa na mbunifu mkuu ambaye amekuwa akiandaa mabanda yaliyoshinda tuzo katika maonyesho ya IFTEX kwa miaka kadhaa. Ubunifu huo uliiwezesha Ole Engai Growers kutwaa Tuzo ya Fedha ya Ubora wa Ubunifu (Silver Award for Design Excellence), baada ya mwaka uliopita kushinda tuzo ya banda bora zaidi. [caption id="attachment_190053" align="aligncenter" width="300"] Tuzo ya Ole Engai Growers baada ya kutumia muundo wa farasi wenye mvuto wakati wa Maonyesho ya IFTEX 2026. Picha|Sammy Waweru[/caption] Mwanzilishi mwenza na mkurugenzi wa kampuni hiyo, Sanir Shah, alisema maonyesho hayo yalionyesha uwezo wa kampuni hiyo kuzalisha maua ya kiwango cha juu na kubuni kazi za kipekee bila kutegemea maua kutoka kwa wazalishaji wengine. "Ole Engai Growers huzalisha maua katika shamba lenye ukubwa wa karibu hekta 29 eneo la Kaptagat, Eldoret, Kaunti ya Uasin Gishu," Sanir alifichua. Mbali na gypsophila, kampuni hiyo pia hulima maua aina ya delphinium ya rangi mbalimbali, asters, kangaroo paws, dianthus na kiwi mellow kulingana na mahitaji ya soko. Kulingana na Sanir, kampuni hiyo huuza nje takribani tani 1,200 za maua kila mwaka, masoko makubwa yakiwa Ulaya huku Mashariki ya Kati ikiandikisha ukuaji wa oda. Hata hivyo, alisema sekta hiyo inakabiliwa na changamoto kubwa kutokana na kupanda kwa gharama za usafirishaji wa mizigo kwa njia ya ndege. "Miaka mitano iliyopita tulikuwa tukilipa karibu Dola 1.4 za Amerika kwa kilo moja ya maua kusafirishwa. Sasa gharama imevuka Dola 4 kwa kilo. Hii imeathiri faida yetu," alisema. Baraza la Maua Kenya (KFC), pia, limeeleza kuwa gharama hizo zimeongezeka kutokana na kupanda kwa bei ya mafuta, jambo linaloongeza gharama za usafirishaji wa bidhaa zinazoharibika haraka kama maua. [caption id="attachment_190054" align="aligncenter" width="300"] Ole Engai Growers huzalisha maua katika shamba lenye ukubwa wa karibu hekta 29 eneo la Kaptagat, Eldoret, Kaunti ya Uasin Gishu. Picha|Sammy Waweru[/caption] "Kwa sasa, usafirishaji pekee unachangia zaidi ya asilimia 40 ya gharama zote za kuuza maua nje wakati wa msimu wa mauzo bora," anasema Clement Tulezi, Afisa Mkuu Mtendaji KFC. Aidha, bei ya mbolea imeongezeka kwa karibu asilimia 25 huku gharama za uzalishaji zikiongezeka kwa kati ya asilimia 20 na 30. Changamoto nyingine ni mabadiliko ya tabianchi ambayo yamevuruga ratiba za uzalishaji kutokana na mvua zisizotabirika. Anjili alisema hali hiyo imefanya upangaji wa shughuli za shambani kuwa mgumu zaidi. Licha ya changamoto hizo, Ole Engai Growers inaendelea kupanua uzalishaji na kutafuta masoko mapya, hasa Mashariki ya Kati ya nchi za Uarabuni. Kwa ujumla, sekta ya maua nchini Kenya inaendelea kuwa mhimili muhimu wa uchumi. Mwaka 2025 iliiingizia nchi karibu Dola milioni 845 za Amerika (zaidi ya Sh110 bilioni), huku Kenya ikiendelea kuuza maua katika zaidi ya nchi 60 duniani, asilimia 70 ya mauzo hayo yakielekezwa katika soko la Umoja wa Ulaya (EU).

read more