T

taifaleo.nation.co.ke

@taifaleo Sun, 12 Jul 2026 12:33:10

Kitengo kipya cha matibabu ya figo chafunguliwa Hospitali ya Mama Lucy

Gavana wa Nairobi Johnson Sakaja ametangaza kufunguliwa kwa Kitengo kipya kilichopanuliwa cha huduma za figo (Renal Unit) katika Hospitali ya Mama Lucy Kibaki. Ufunguzi huo unalenga kuboresha upatikanaji wa huduma za kuokoa maisha za usafishaji damu (dialysis) na kuimarisha huduma maalumu za afya katika kaunti hiyo. Kitengo hicho cha kisasa, kilichoko katika Hospitali ya Level 5 ya Mama Lucy Kibaki, Umoja II, Embakasi Magharibi, kimewekewa mashine za kisasa na kina wahudumu wenye uzoefu katika matibabu ya magonjwa ya figo ili kutoa huduma kamili kwa wagonjwa. Akizungumza wakati wa uzinduzi huo, Gavana Sakaja alisema kitengo hicho kitatoa matibabu ya kina ya magonjwa ya figo, mipango ya matibabu inayolingana na mahitaji ya kila mgonjwa, ushauri wa lishe na mtindo wa maisha, pamoja na huduma za ushauri nasaha na msaada kwa wagonjwa. "Upanuzi wa huduma zetu za figo unaonyesha dhamira yetu ya kuhakikisha wakazi wa Nairobi wanapata huduma bora na nafuu bila kulazimika kusafiri umbali mrefu. Kituo hiki kitaboresha matokeo ya matibabu kwa wagonjwa wanaoishi na magonjwa ya figo," akasema Gavana Sakaja. Gavana huyo alibainisha kuwa kitengo kipya ni sehemu ya uwekezaji unaoendelea wa Serikali ya Kaunti ya Nairobi katika huduma maalumu za afya, unaolenga kupunguza hali ambapo wagonjwa wanaenda hospitali nyingine na pia kuleta huduma bora za matibabu karibu na wananchi. Hospitali hiyo imewahimiza wagonjwa wanaohitaji huduma za  matibabu maalumu ya figo kupanga miadi kupitia Kitengo cha Figo kilichotengwa kwa huduma hizo. Uzinduzi huo ni sehemu ya maboresho yanayoendelea katika Hospitali ya Mama Lucy Kibaki, yakiwemo upanuzi wa huduma za wagonjwa mahututi, kumbi za kisasa za upasuaji, idara ya dharura iliyoboreshwa na uwezo ulioimarishwa wa uchunguzi wa magonjwa. Maboresho hayo yanadhihirisha dhamira ya Serikali ya Kaunti ya Nairobi ya kuimarisha miundombinu ya huduma za afya ya umma. Gavana Sakaja pia aliwahimiza wakazi wanaohitaji huduma za matibabu ya figo kutembelea Kitengo kipya cha Figo katika Hospitali ya Mama Lucy Kibaki, iliyoko Kangundo Road, Umoja II. Alisema huduma hizo zinapatikana chini ya mpango wa Mamlaka ya Afya ya Jamii (SHA), hatua itakayorahisisha upatikanaji wa huduma nafuu na bora za dialysis pamoja na matibabu maalumu ya magonjwa ya figo kwa wakazi wa Nairobi.

read more
T

taifaleo.nation.co.ke

@taifaleo Sun, 12 Jul 2026 11:57:04

Junior Starlets yafuzu kombe la dunia

Timu ya Kenya ya vichuna chini ya miaka 17, Junior Starlets, imefuzu Kombe la Dunia la Mwaka huu,  baada ya kuichabanga Afrika Kusini 3-1 katika mechi ya marudiano ya hatua ya mwisho jana ugani Nyayo.  Kenya ilifuzu kwa jumla ya mabao 5-1 baada ya pia kushinda mechi ya kwanza 2-0 mjini Pretoria wiki iliyopita. Ushindi huo umeihakikishia Kenya tiketi ya kushiriki fainali zitakazoandaliwa nchini Morocco kuanzia Oktoba 17 hadi Novemba 8, 2026. Hii ni mara ya pili kwa Junior Starlets kufuzu kwa fainali za Kombe la Dunia baada ya kushiriki kwa mara ya kwanza katika makala ya 2024 yaliyofanyika nchini Jamhuri ya Dominika chini ya ukufunzi wa Mildred Cheche. [caption id="attachment_190028" align="alignnone" width="1296"] Wachezaji wa Junior Starlets wakisherehekea baada ya kufunga bao dhidi ya Afrika Kusini na kufuzu Kombe la Dunia la wachezaji chini ya miaka 17 katika uga wa Nyayo jijini Nairobi jana. PICHA |HISANI[/caption] Mechi hiyo ilianza kwa dakika moja ya ukimya kumuenzi mchezaji wa zamani wa timu ya taifa  ya Afrika Kusini, Jayden Adams, aliyefariki dunia Ijumaa akiwa na umri wa miaka 25. Kocha Cheche alianzisha kikosi kilekile kilichoibuka na ushindi wa mabao 2-0 mjini Pretoria. Mishel Ng'ono alianza langoni huku safu ya ulinzi ikiongozwa na Brendah Awuor, Fleviah Khatenje, Sylvia Namisi na Berveline Awuor. Kiungo kilikuwa na Noelina Akuku, Mwanakombo Bakari na Gaudencia Maloba huku Lindey Weey Atieno na Faith Boke wakimsaidia mshambuliaji Brenda Achieng. Afrika Kusini ilianza kwa kasi na kupata bao la mapema katika dakika ya tano kupitia kwa nahodha Katleho Malebana baada ya safu ya ulinzi ya Kenya kufanya makosa. Dakika tatu baadaye, Kenya ilikaribia kusawazisha baada ya Faith Boke kumpasia Brenda Achieng aliyebaki ana kwa ana na kipa, lakini shuti lake halikulenga lango. Kenya iliendelea kushinikiza na kupata mpira wa adhabu katika dakika ya 15 baada ya Achieng kuchezewa visivyo nje ya eneo la hatari, lakini mpira wa Lindey Weey ulipaa nje. [caption id="attachment_190027" align="alignnone" width="2560"] Kiungo wa Junior Starlets Gaudencia Maloba akisherehekea baada ya kufunga bao dhidi ya Afrika Kusini katika uga wa Nyayo jijini Nairobi jana. PICHA |HISANI[/caption] Afrika Kusini ilipoteza nafasi nzuri ya kuongeza bao katika dakika ya 18 wakati Pilate Moloi alipompita kipa Ng'ono na mabeki wawili kabla ya shuti lake kupita nje kidogo ya lango. Licha ya Kenya kutawala mchezo katika dakika za mwisho za kipindi cha kwanza, ilishindwa kutumia vyema nafasi ilizopata na kwenda mapumzikoni ikiwa nyuma 1-0. Mwanzoni mwa kipindi cha pili, Cheche alimleta Emily Adhiambo kuchukua nafasi ya Lindey Weey, mabadiliko yaliyoongeza nguvu katika safu ya ushambuliaji ya Kenya. Starlets waliendelea kulisakama lango la wageni huku Achieng akikaribia kusawazisha katika dakika ya 54, lakini shuti lake liligonga wavu. Shinikizo la Kenya lilizaa matunda dakika ya 70 wakati Gaudencia Maloba aliposawazisha. Kenya iliongeza bao la pili kupitia kwa Awuor aliyefunga kwa mkwaju wa penalti baada ya wenyeji kutunukiwa adhabu hiyo. Mshambuliaji wa akiba Elizabeth Alizeba Achieng alihitimisha ushindi huo katika dakika za nyongeza kwa kufunga bao la tatu na kuiwezesha Kenya kuibuka na ushindi wa mabao 3-1 na kufuzu kwa jumla ya mabao 5-1. Sasa Junior Starlets wataelekeza macho yao nchini Morocco wakilenga kufanya vizuri zaidi kuliko walivyofanya katika ushiriki wao wa kwanza wa Kombe la Dunia mwaka 2024

read more
T

taifaleo.nation.co.ke

@taifaleo Sun, 12 Jul 2026 08:52:51

Mwalimu Marube, 'tabibu' wa Hisabati na Fizikia: 'Si uchawi, siri ni nidhamu na mazoezi'

KWA wanafunzi wengi, kutajwa kwa masomo ya Hisabati na Fizikia pekee hutosha kuzua wasiwasi ndani yao. Wengine huamini kuwa ni masomo magumu yanayohitaji kipaji cha pekee cha kuzaliwa nacho. Hata hivyo, mwalimu Moses Marube ana mtazamo tofauti kabisa. Kwake, mafanikio katika masomo haya hayategemei kipaji pekee bali hujengwa kupitia bidii, nidhamu na mwongozo sahihi. Marube, ambaye kwa sasa anafundisha Hisabati na Fizikia katika Shule ya Upili ya Nduru Girls, Kaunti ya Kisii, anasema kuwa wanafunzi wanaofanya vyema katika masomo hayo huwa na tabia moja muhimu – hawatishwi na changamoto. "Mwanafunzi anapokutana na swali gumu hafai kuliona kama kikwazo. Kila swali gumu ni fursa ya kujifunza jambo jipya. Mafanikio huanza pale mwanafunzi anapoamua kutafuta suluhisho badala ya kukata tamaa," anasema. Kwa mtazamo wake, wanafunzi bora hujifunza kutokana na makosa yao na huwa tayari kuuliza maswali wanapokwama. Aidha, hawasubiri kipindi cha mitihani ndipo washike vitabu, bali hujenga utamaduni wa kujifunza kila siku. "Hisabati na Fizikia ni kama kujenga nyumba. Huwezi kuanza na paa kabla ya msingi. Ukielewa dhana za msingi na kufanya mazoezi mara kwa mara, mada ngumu huwa rahisi kueleweka," anaeleza. Safari ya Marube mwenyewe ni ushahidi wa thamani ya juhudi na kujituma. Alizaliwa katika eneo la Tabaka, Kisii, na kuanza masomo yake katika Shule ya Msingi ya Tabaka Hillcrest kabla ya kujiunga na Shule ya Upili ya Moi Gesusu Boys. Matokeo yake mazuri yalimfungulia mlango wa kujiunga na Chuo Kikuu cha Egerton kusomea shahada ya ualimu (Hisabati/Fizikia). Akiwa mwanambee katika familia ya watoto wanne, Marube anawapongeza wazazi wake, Bw Peter Marube na Bi Gladys Kerubo, kwa mchango wao mkubwa katika safari yake ya elimu. Akiwa katika shule ya upili, alikuwa mpenzi wa kandanda na mpira wa vikapu na miongoni mwa wanafunzi bora darasani. "Nilichagua taaluma ya ualimu kwa sababu nilitaka kuwasaidia wanafunzi kuondoa hofu waliyo nayo kuhusu Hisabati na Fizikia. Lengo langu ni kuwaonyesha kwamba kila mwanafunzi ana uwezo wa kufaulu iwapo atapata mwongozo sahihi na kuwa tayari kufanya kazi kwa bidii," anasema. Kabla ya kujiunga na Nduru Girls mapema mwaka huu, Marube aliwahi kufundisha katika Lampros Education Centre jijini Nairobi na baadaye Shule ya Tuamini jijini Nakuru. Mbali na kufundisha, Marube pia hushiriki shughuli za kuwanoa wanafunzi katika mchezo wa mpira wa vikapu kwa ushirikiano na Bw Agola anayesimamia Idara ya Michezo shuleni Nduru Girls. Juhudi zao zimezaa matunda baada ya timu hiyo kutuzwa katika mashindano ya kiwango cha Kaunti ya Kisii muhula huu. Kwa wanafunzi wanaotamani kufanya vyema katika masomo ya sayansi, Marube ana ushauri wa wazi. "Usiogope makosa kwa sababu ndiyo daraja la kukuelekeza penye mafanikio. Fanya mazoezi kila siku, sikiliza mwalimu wako, uliza unapokwama na uwe na subira. Hakuna uchawi katika Hisabati wala Fizikia. Siri yake ni nidhamu, mazoezi ya mara kwa mara na mtazamo chanya." Anaongeza: "Mafanikio makubwa huanza na hatua ndogo zinazorudiwa kila siku. Mwanafunzi anayejifunza kwa uthabiti leo ndiye mtaalamu wa kesho. Ukiamini unaweza kuelewa Hisabati na Fizikia, tayari umeanza safari ya kufaulu."

read more