T

taifaleo.nation.co.ke

@taifaleo Wed, 02 Sep 2026 02:55:37

Orengo: Mimi ndio nimeiva kuwa rais na nitashindana na Sifuna kwa tiketi 2027

GAVANA wa Siaya James Orengo amemtaka Seneta wa Nairobi Edwin Sifuna na wagombeaji wengine ndani ya Linda Mwananchi kukubali uteuzi wa wazi wanaposaka mwaniaji wao wa urais kuelekea uchaguzi mkuu wa 2027. Katika mahojiano na Taifa Leo Jumanne, Bw Orengo alisema hana tatizo kushindana na Bw Sifuna au mgombea mwingine yeyote wa upinzani. Alisisitiza jambo muhimu ni kuhakikisha vuguvugu hilo linapata mgombea mmoja wa kukabiliana na Rais William Ruto katika uchaguzi wa 2027. "Hakuna ubaya kwa wagombea mbalimbali kuwa na azma ya urais ndani ya Linda Mwananchi au upinzani. Muhimu ni kuwapa wote fursa ya kupitia mchakato wa uteuzi wa wazi na wa kuaminika, ili hatimaye tupate mgombea mmoja wa kukabiliana na Ruto. Huo ndio msingi wa umoja wa upinzani," akasema Bw Orengo. Gavana huyo mkongwe alisisitiza kuwa uteuzi haupaswi kuamuliwa katika vikao vya siri, akitaja uchaguzi wa urais wa ODM wa 2007 ambapo Raila Odinga, William Ruto, Musalia Mudavadi, Najib Balala na Joe Nyaga walishindana kabla ya chama kumpata mgombea wake. Alitaja pia uchaguzi wa 2002, ambapo vyama vya upinzani vilifanya mashauriano kabla ya Bw Odinga, aliyekuwa akiongoza LDP, kumuunga mkono Mwai Kibaki kupitia kauli ya "Kibaki Tosha". Bw Orengo alisema mifano hiyo inaonyesha kuwa umoja wa upinzani hauhitaji kuondoa mapema azma za wagombea mbalimbali wenye nia ya kusaka urais. Ingawa hivyo, msimamo wake umemweka pabaya na washirika wa Bw Sifuna, ambao wamekuwa wakisema wafuasi wa Linda Mwananchi tayari wameamua kumuunga mkono seneta huyo wa Nairobi. Gavana wa Trans Nzoia George Natembeya ni miongoni mwa viongozi wa Magharibi waliomuunga mkono Bw Sifuna na kusema wananchi wamekuwa wakisema "Sisi Ndio Sifuna" katika mikutano ya vuguvugu hilo. Mbunge wa Kabuchai Majimbo Kalasinga alisema hakuna haja ya kuchanganya wafuasi kwa kujitokeza kwa wagombea wengine. "Hatupaswi kuchanganyikiwa. Wakenya wamejitokeza katika kila mkutano wa Linda Mwananchi na kusema wanamtaka Edwin Sifuna kuwa mgombea wa urais," akasema Bw Kalasinga. Seneta wa Vihiga Godfrey Osotsi, hata hivyo, alisema vuguvugu hilo linamheshimu Bw Orengo kutokana na uzoefu wake wa kisiasa na mchango wake katika masuala ya mageuzi. "Vuguvugu linamheshimu sana Gavana Orengo kutokana na hadhi na uzoefu wake mkubwa katika masuala ya mageuzi," akasema Bw Osotsi, akiongeza kuwa kutakuwa na utaratibu wa kutatua suala hilo wakati ufaao. Mwanasiasa wa Jubilee Pauline Njoroge pia akiongea katika Kaunti ya Meru wakati wa mkutano wao wa kisiasa alisema suala la mgombeaji wao wa urais lishaamuliwa. "Wafuasi wetu wameweka wazi kuwa wanayemtaka ni Sifuna. Hilo limethibitishwa kupitia mikutano yetu maeneo mbalimbali nchini," akasema Bi Njoroge. Bw Orengo pia alisema jamii mbalimbali zina haki ya kufanya mashauriano kuhusu maslahi yao ya kisiasa, akitaja mijadala inayoendelea Mlima Kenya na Ukambani. Kando na kambi ya Bw Sifuna, azma ya Bw Orengo pia imewachemsha viongozi kutoka Nyanza wanaounga mkono kuchaguliwa tena kwa Rais Ruto. Waziri wa Kawi Opiyo Wandayi amemshutumu Bw Orengo kwa kutumiwa kugawanya kura za Waluo, akilinganisha hali hiyo na uchaguzi wa 2002. "Jinsi alivyotumiwa na Daniel arap Moi kugawanya kura zetu 2002, sasa anatumika tena na Uhuru kugawanya kura zetu, lakini hilo halitatokea," akasema Bw Wandayi. Waziri huyo pia alisema viongozi wa Siaya wamekubaliana kumuunga mkono Rais Ruto na sasa wanamakinikia usajili wa wapiga kura. Mwenyekiti wa ODM Gladys Wanga, pia amepuuzilia mbali uwezekano wa Bw Orengo kushinda urais, akisema hana umaarufu wowote wa maana nchini. Huku mjadala ukiendelea, Linda Mwananchi pia inajaribu kujigeuza kutoka jukwaa la kisiasa hadi chama kitakachoshiriki uchaguzi wa 2027. Hata hivyo, ombi lake la kuhifadhi jina Linda Mwananchi Party lilikataliwa na Afisi ya Msajili wa Vyama vya Siasa, hatua ambayo imeongeza changamoto kwa vuguvugu hilo. Bw Orengo pia alitetea uamuzi wake wa kukosa mkutano wa Linda Mwananchi Meru mnamo Jumapili akisema haikuhusiana na ubabe kati yake na Bw Sifuna. "Nilikuwa na shughuli nyingine nzito na Babu aliwasilisha salamu na udhuru wangu. Bado namakinikia wazo la kuwa na mgombeaji mmoja wa upinzani," akasema. Mchanganuzi wa masuala ya kisiasa Chris Omore naye anasema ukosefu wa chama thabiti huenda ukalemeza azma ya Mabw Orengo na Sifuna kumpa Rais Ruto upinzani mkali 2027.

read more
T

taifaleo.nation.co.ke

@taifaleo Wed, 02 Sep 2026 03:55:32

Vigogo wa 'Broadbased' waahidi Ruto kura milioni 7 Nyanza, Magharibi uchaguzi mkuu

WANASIASA wanaounga mkono serikali kutoka Nyanza na Magharibi wametangaza mipango ya kuendesha kampeni za pamoja kwa lengo la kumwezesha Rais William Ruto kupata kura milioni 7 maeneo hayo 2027. Mpango huo unalenga kuvutia kura katika ngome za kisiasa za marehemu Waziri Mkuu Raila Odinga chini ya Waziri wa Kawi Opiyo Wandayi. Sehemu ya mikakati hiyo pia ni kushinikiza watengewe nafasi ya Naibu Rais. ODM imependekeza Waziri wa Vyama vya Ushirika Wycliffe Oparanya kama mmoja wa wanaoweza kuchukua nafasi ya Profesa Kithure Kindiki. Luo Nyanza, inayojumuisha kaunti za Kisumu, Migori, Siaya na Homa Bay, ina wapiga kura milioni 2.41 kwa mujibu wa sajili ya sasa ya Tume Huru ya Uchaguzi na Mipaka Nchini (IEBC). IEBC inakadiria idadi hiyo kufikia milioni 2.78 katika uchaguzi wa Agosti 10, 2027. Magharibi nayo ina kaunti za Kakamega, Busia, Bungoma, Vihiga na Trans Nzoia zina wapiga kura milioni 2.9 kwa sasa, huku idadi hiyo ikitarajiwa kufikia milioni 3.4 ifikapo uchaguzi ujao. Hata hivyo, mpango huo unakabiliwa na upinzani kutoka kwa vuguvugu la Linda Mwananchi, ambalo limekuwa likipata umaarufu katika maeneo hayo. Baadhi ya viongozi wa Magharibi, akiwemo Gavana wa Trans Nzoia George Natembeya, Seneta wa Vihiga Godfrey Osotsi na Seneta wa Kakamega Boni Khakwale, wamejipanga kumuunga mkono Seneta wa Nairobi Edwin Sifuna kwa urais. Nyanza pia inapitia mabadiliko makubwa ya kisiasa tangu kifo cha Bw Odinga. Gavana wa Siaya James Orengo na Mbunge wa Suba Kusini Caroli Omondi wameungana na Bw Sifuna kupinga ushawishi wa uongozi wa sasa wa ODM. Hata hivyo, washirika wa Rais Ruto wanasema wataunganisha jamii za Luo na Luhya ili kumuunga mkono katika uchaguzi wa 2027. Jamii hizo kwa kiasi kikubwa zilimuunga mkono Bw Odinga katika uchaguzi wa 2022.

read more
T

taifaleo.nation.co.ke

@taifaleo Wed, 02 Sep 2026 04:55:21

Wauguzi wavamiwa na wahuni Kisii wakijiandaa kuwasilisha malalamishi kwa serikali

WAUGUZI wanaoendelea na mgomo katika Kaunti ya Kisii, jana walishambuliwa na watu wanaodaiwa kuwa wahuni walipokuwa wakijiandaa kushiriki mgomo wa amani na kuwasilisha malalamishi yao kwa serikali ya kaunti hiyo. Walishambuliwa katika uwanja wa Hospitali ya Rufaa ya Kisii, tukio ambalo viongozi wa muungano wao walilikemea na kulitaja kuwa la kuhofisha mno. Wauguzi ambao hawakutaka kutajwa, walisema wanaume wapatao 40 waliojihami kwa mipini ya majembe walivamia walipokuwa wakijiandaa kuandamana. Katibu Mkuu wa Muungano wa Wauguzi (KNUN), Seth Panyako, alitaja shambulizi hilo kuwa la kipuzi, akilalamika kuwa polisi waliofahamishwa awali kuhusu mipango ya maandamano hayo walifeli kuwalinda wauguzi. "Polisi Kisii wameingiliwa. Tulitoa notisi bayana kwa polisi kuwa tutafanya maandamano ya amani. Maafisa wa polisi walikuja lakini badala ya kutoa ulinzi, waliagiza wauguzi kuondoka, wakisema ikiwa watakaidi, wahuni hao wa kulipwa wataachiliwa kwao," akasema Bw Panyako akihutubia vyombo vya habari. "Tunalaani vikali tukio hili. Tunauliza polisi mjini Kisii kwa nini waliruhusu wahuni kushambulia wauguzi wasio na fujo, kana kwamba hawaugui. Hatutakuwa na huruma kwa wasio na huruma nasi. Sisi ni wauguzi; wanaweza kuwa na bunduki na silaha, lakini tunaweza pia kuwa hatari." Homabay, wauguzi wameapa kukaidi wito wa Baraza la Magavana (CoG) kurejea kazini huku majadiliano yakiendelea. Mwenyekiti wa Baraza, Bw Ahmed Abdullahi, aliwahimiza wauguzi nchini kote kurejelea majukumu yao huku magavana wakishughulikia malalamishi yao. Gavana huyo wa Wajir, alisema baraza limejadili Mkataba wa Makubaliano kuhusu Malipo (CBA) lakini baadhi ya kaunti zimeshindwa kuutekeleza, huku wauguzi wakisema hawatasikiza ombi hilo. Mkurugenzi wa Muungano Kitaifa wa Wauguzi na Wakunga (KNUNM) tawi la Homa Bay, Emmadick Okeyo, alisema kususia kazi ndiyo hatua yao. "Hatutarejea kazini hadi malalamishi yetu yatakaposhughulikiwa," akasema Bw Okeyo. Mwenyekiti wa tawi hilo, Bw Enock Ocharo aliitaka CoG kukoma kuwatishia wauguzi. "CoG ijishughulishe na kuangazia malalamishi yetu. Vitisho wanavyotoa havina athari yoyote," akasema Bw Ocharo. Kisumu, baadhi ya wagonjwa wanageukia maduka ya kuuza dawa huku mgomo unaoendelea wa wauguzi ukitatiza huduma katika hospitali ya rufaa Kisumu. Wauguzi wanataka mkataba wao wa CBA utiwe saini ili uthibitishwe kisheria. Mkataba huo unatoa mwongozo kuhusu maendeleo kitaaluma, marupurupu na malipo mengineyo. Aidha, wanataka wenzao walioajiriwa chini ya mpango wa Afya kwa Wote (UHC) wakati wa hatamu ya Rais mstaafu Uhuru Kenyatta kuajiriwa kwa kandarasi za kudumu. Wauguzi wa UHC kwa sasa wameajiriwa kwa kandarasi za muda. Wanaitisha vilevile utekelezaji kamili wa Muafaka wa Kurejea Kazini 2017 uliotiwa saini kati ya muungano wao na CoG.

read more
T

taifaleo.nation.co.ke

@taifaleo Wed, 02 Sep 2026 05:55:06

Wanasema utahitaji kuwa imara kisaikolojia kufaulu katika biashara ya majeneza: Tambua kivipi

WATENGENEZAJI na wauzaji majeneza Pwani wanakiri kuvuna pakubwa na kujijenga kimaisha licha biashara hiyo kuwa na changamoto tele, hasa kimtazamo wa jamii. Mafundi na wauzaji wa majeneza waliohojiwa na Akili Mali katika kaunti za Kilifi, Mombasa, Kwale, Taita Taveta na Mpeketoni (Lamu) walisisitiza kuwa biashara hiyo ina malipo ya kuridhisha ila inahitaji ustahimilivu mkubwa wa kisaikolojia kutokana na mtazamo uliopo wa jamii na mazingira yenyewe ya kikazi. George Kirao Nzaro, 26, ambaye ni fundi na muuzaji majeneza mjini Malindi, Kaunti ya Kilifi, amedumu kwenye biashara hiyo kwa karibu miaka minane sasa. Alijitosa katika kazi hiyo 2018 mwaka mmoja baada ya kuacha masomo yake ya kidato cha kwanza kutokana na ukosefu wa karo. Alipokea ujuzi kupitia duka moja la mbao lililomwajiri na ambalo pia lilishughulikia masuala ya majeneza mjini Kilifi. Ni kutokana na ujuzi na ustadi aliopokea uliomfanya kubadilisha makazi yake ya kazi, hivyo kuhama kutoka kijiji chao cha Misufini, viungani mwa mji wa Kilifi na kufungua eneo lake binafsi la Heri Directors lililoko mtaa wa Seabreeze mjini Malindi. Kwenye duka hilo, Kirao huchonga mbao, kuzipiga msasa, kugonga na kuunda majeneza kabla ya kuyatia nakshi na rangi tayari kwa wateja. Anasema yeye hakosi angalau Sh90,000 kila mwezi kupitia uundaji na uuzaji wa majeneza na wakati mwingine huunda hadi Sh250,000. "Kuna nyakati ambapo unajipata umekaa tu ukisubiri hadi wiki mbili au mwezi mzima bila kuuza jeneza lolote. Ni biashara inayohitaji uvumilivu kwani huwezi kuombea mtu afe. Ila kuna msimu utapata biashara ikinawiri kwa kuuza majeneza mengi, hivyo kupata hela ya juu," anasema Kirao. Kariuki Kimani, mfanyibiashara na mmiliki wa duka la majeneza na huduma nyingine za mazishi, ikiwemo usafirishaji maiti la Eureka Supreme Services lililoko katikati mwa mji wa Mpeketoni, Kaunti ya Lamu, anaitaja biashara hiyo kuwa muhimu kwa jamii, akiwasihi vijana kutoibagua. Amedumu kwenye biashara hiyo karibu miaka kumi. Yeye huuza jeneza moja kwa kati ya Sh10,000 hadi Sh50,000, ukadiriaji wa bei kwake ukitegemea ukubwa wa jeneza, muundo, aina, urembo, hadhi au tabaka ambalo mteja atataka. "Tuko na hadi hadhi au tabaka la VIP kwa wanaotafuta huduma zetu, iwe ni jeneza, usafirishaji marehemu, mahema hadi maziko," anaeleza. "Jamii ifahamu kuwa kazi ya majeneza ina kipato. Kipato hicho kisingekuwepo basi duka langu halingedumu miaka yote kumi"Abdallah Mainge, mfanyibiashara wa majeneza, usafirishaji wa maiti na mazishi anayemiliki duka la Malindi Funeral Services and Coffin Centre lililoko mkabala na Hospitali Kuu ya Kaunti Ndogo ya Malindi, anaisifu biashara hiyo kwa kumsaidia kuyakimu maisha yake na ya familia pia. Alianza kazi hiyo 2017. "Mwaka 2017 kulikuwa na sintofahamu za kisiasa kidogo nchini, hali iliyopelekea biashara ya utalii kusambaratika. Nikalazimika kugeuza gari langu kuwa la kusafirishia maiti. Huduma ya kusafirisha maiti kutoka mji wa Malindi hadi Gede au Gongoni ilikuwa kati ya Sh10,000 hadi Sh25,000 kwa wakati huo. Hapo ndipo nikatambua kuwa nyanja hii ya matanga pia ina kipato," anaeleza. Baadaye alipanua huduma zake, ambapo mbali na kusafirisha maiti kwa maziko, pia aliafikia kufungua duka lake la Malindi Funeral Services and Coffin Centre ili kuuza jeneza, nguo za kuvalisha maiti, mahema, mapambo ya matangani nakadhalika. Yeye huuza jeneza moja kati ya Sh15,000 hadi zaidi ya Sh100,000 akishikilia kuwa bei pia inakadiriwa kulingana na matakwa ya mteja mwenyewe. Kwa mwezi yeye hakosi kati ya Sh100,000 hadi Sh200,000 japo anashikilia kuwa mapato hayo hubadilikabadilika kulingana na misimu. "Ninapeana huduma mbalimbali. Hapa utapata majeneza ya bei tofauti. Kuna yale ya kawaida hadi ya kifahari yanayouzwa kwa maelfu ya fedha kulingana na uwezo wa mteja," akasema Bw Mainge. Anakiri kuwa biashara ya kuuza jeneza ina changamoto tele kwani miongoni mwa mambo magumu zaidi maishani mwake ni kujaribu kujadiliana bei na mteja ambaye tayari amefiliwa akiwa maombolezoni. "Sisi wenye biashara hizi lazima tuwe na mioyo migumu na pia kuelewa wateja wetu ambao tayari wamepatwa na msiba tunapojadiliana bei. Watu wengi awali waliogopa biashara ya majeneza na kusafirisha maiti wakidhani sisi hushangilia kifo ili tupate pesa. La hasha. Hii ni mojawapo ya mbinu ya kusaidia jamii zetu manake tusipokuwepo itamaanisha kutakuwa na tatizo la watu kuzikwa," akasema Bw Mainge. Anaililia serikali ya Kaunti ya Kilifi na ile ya kitaifa kupunguza makato ya kodi wanayolumbikiziwa kila mara bila kujali jinsi biashara zao zinavyohudumu, iwe ni katika hali nzuri au misimu ya chini. "Awali tulikuwa tukikatwa kodi ya mwaka ya Sh6,000 na kaunti yetu ya Kilifi. Kwa sasa makato yamepandishwa hadi karibu Sh14,000 ambayo ni karibu mara mbili ya makato ya awali. Wafanye jambo. Tunaumia," akasema Bw Mainge. Kahindi Mdzomba, mmiliki na muuzaji majeneza eneo la Makadara katika jiji kuu la Mombasa, pia anaitaja biashara ya majeneza kuwa ya kutegemeeka kimapato. "Biashara hii ya majeneza siyo rahisi vile. Tunakubali kwamba inatatiza kisaikolojia. Waonaje wewe hii hali ya kufanya kazi huku ukizungukwa na ishara za maombolezo na simanzi kila siku? Ni biashara inayohitaji uwe na akili dhabiti na ujasiri. Imetujenga kimaisha," akasema Bw Mdzomba. Anasema kila mwezi hakosi angalau Sh60,000 ambayo ni faida hasa baada ya kuwalipa wasaidizi wake anaofanya kazi nao dukani kwake. Naye Stephen Mwabili, muuzaji majeneza mjini Voi, Taita Taveta, alisema changamoto kuu wanayokumbana nayo kila siku kazini ni kushughulikia wateja walio katika majonzi makubwa, jambo linalohitaji uvumilivu na busara ya hali ya juu. Kwa upande wake, Solomon Ndegwa, fundi wa majeneza katika duka lililoko mkabala na hospitali ya rufaa ya Msambweni, Kaunti ya Kwale, anasema kazi ni kazi.

read more
T

taifaleo.nation.co.ke

@taifaleo Wed, 02 Sep 2026 06:55:12

Wavinya akataa marekebisho ya madiwani kupunguza bajeti ya kaunti

MZOZO wa bajeti kati ya Gavana wa Machakos Wavinya Ndeti na baadhi ya madiwani wa Bunge la Kaunti umechacha baada ya gavana huyo kukataa marekebisho yaliyofanywa kwenye bajeti ya Sh17.8 bilioni ya mwaka wa kifedha wa 2026/2027. Hatua hiyo imeibua makabiliano mapya katika Bunge la Kaunti, huku madiwani wakiwa na chini ya wiki mbili za kutathmini upya uamuzi wa kupunguza Sh853 milioni kutoka kwa bajeti hiyo. Bi Ndeti aliwasilisha barua ya kupinga marekebisho hayo alipofika katika Bunge la Kaunti Jumatatu akiwa ameandamana na Katibu wa Kaunti Muya Ndambuki, Waziri wa Fedha Catherine Mutanu na maafisa wengine wakuu. Alimkabili Karani wa Bunge la Kaunti Peter Mbatha, akimshtumu kwa kushirikiana na Spika Anne Kiusya kumzuia kuwasilisha mapendekezo yake. "Kwa nini usipokee tu barua hiyo kama sheria inavyohitaji na uniachie nikabiliane na madiwani?" akamuuliza Bw Mbatha. Baada ya barua hizo kupokewa, Bi Ndeti alisema hawezi kuidhinisha bajeti iliyorekebishwa kwa sababu inatishia huduma muhimu kwa wakazi. "Siwezi kutia saini bajeti inayokiuka wazi mipaka iliyowekwa kisheria, kubomoa huduma muhimu za umma na kuhatarisha moja kwa moja maisha ya watu wetu," akasema. Marekebisho hayo yameathiri zaidi fedha za miradi ya barabara na baadhi ya mipango muhimu ya gavana, ikiwemo Huduma ya Vijana ya Machakos, mpango wa maziwa kwa watoto wa shule za chekechea na mpango wa mikopo nafuu uliotengewa Sh100 milioni. Bi Ndeti anasema kupunguzwa kwa fedha kutalemaza utoaji wa huduma, huku madiwani wanaomuunga mkono wakisisitiza kuwa walifanya marekebisho hayo baada ya kuchunguza matumizi yenye utata. "Gavana anaita mabadiliko haya kupunguzwa kwa bajeti. Sisi tunaita uchunguzi wa bajeti, kuweka kipaumbele upya na kugawa fedha upya. Tunapinga ubadhirifu na kurudiwa kwa miradi. Tunataka thamani ya fedha," akasema Diwani wa Kalama, Bw Boniface Maeke. Mzozo huo unaendeleza mvutano wa kisiasa kati ya Bi Ndeti na baadhi ya madiwani. Waziri wa Fedha, Bi Mutanu amekuwa katikati ya mzozo huo baada ya kufutwa kazi na gavana Julai, siku ambayo Bi Ndeti alikabiliwa na hoja ya kumtimua. Bi Mutanu alirejeshwa kazini wiki moja baadaye baada ya Mahakama Kuu kuingilia kati. Mzozo wa sasa ulianza baada ya Bunge la Kaunti kuruhusu gavana kutumia asilimia 50 ya bajeti ya 2026/2027 kusubiri kupitishwa kwa Mswada wa Matumizi.

read more
T

taifaleo.nation.co.ke

@taifaleo Wed, 02 Sep 2026 07:55:10

TSC yatangaza nafasi 1,631 kwa walimu wanaotaka kupanda ngazi

TUME ya kuajiri walimu (TSC) imetangaza upya nyadhifa 1,631 za kuwapandisha cheo wasimamizi wa shule, na kuwapa fursa nyingine walimu wanaomezea mate nyadhifa za uongozi huku kukiwa na uhaba wa wasimamizi waliothibitishwa katika shule za umma. Nyadhifa hizo zinajumuisha nafasi 1,470 za Naibu Mwalimu mkuu, 132 Naibu Mwalimu Mkuu III na 29 za Mwalimu Mkuu II katika shule za msingi na sekondari. Tume imealika maombi kutoka kwa walimu wanaohudumu waliofuzu kujaza nafasi hizi za kupandishwa cheo kuambatana na Mwongozo wa Maendeleo Kitaaluma kwa Walimu. Maombi ni sharti yapokewe kufikia usiku wa manane Jumatatu Septemba 14, 2026, ilisema TSC katika notisi. Tangazo hilo jipya limejiri wiki chache tu baada ya Tume kuzindua mchakato wa kupandisha cheo uliojumuisha walimu 34,016 katika daraja zote, katika kile kilichotajwa kuwa moja kati ya shughuli kubwa zaidi za maendeleo kitaaluma katika miaka ya majuzi. Shughuli hiyo iliyotangazwa Julai, iliangazia nyadhifa kuanzia Mwalimu wa Ngazi ya Juu II hadi Mwalimu Mkuu na ilijumuisha nyadhifa za kufundisha, usimamizi wa shule, kuboresha mtaala na vyuo vya mafunzo ya walimu. Nyadhifa mpya zilizotangazwa ni muhimu, kwa sababu zinalenga nafasi za usimamizi wa shule wakati ambapo maelfu ya shule za umma zinaendeshwa bila wasimamizi waliothibitishwa. Mchakato huo wa kupandisha vyeo umejiri kukiwa na malalamishi kuhusu kukwama kitaaluma katika huduma ya kufundisha. TSC ilieleza Bunge kwamba walimu 178,871 wa shule za msingi na sekondari wamesalia katika daraja lile lile la kazi kutokana na upungufu kwenye bajeti, huku tume ikisema inahitaji mabilioni kushughulikia suala hilo. Tume ilisema sehemu kubwa ya walimu waliokwama kitaaluma ni kutoka gredi C3 kwa walimu wa sekondari na gredi C1 kwa walimu wa shule ya msingi ambapo waelimishaji wengi wamesalia kwa miaka mingi licha ya kutimiza viwango vya kufuzu kupandishwa cheo. "Tunaitaka TSC kutangaza mara moja nyadhifa za kuwapandisha vyeo walimu 135,000 ambao wamekwama katika daraja zao za kazi," alisema Katibu Mkuu wa Kuppet, Bw Akello Misori.

read more
T

taifaleo.nation.co.ke

@taifaleo Wed, 02 Sep 2026 12:00:43

Hichilema aapishwa kwa muhula wa pili mpinzani wake mkuu akifungiwa jela

LUSAKA, Zambia: RAIS wa Zambia Hakainde Hichilema Jumanne aliapishwa rasmi kwa muhula wake wa pili huku mpinzani wake mkuu akiwa gerezani akikabiliwa na mashtaka ya uhaini. Kuapishwa kwake kumekamilisha mchakato wa uchaguzi wa Agosti 13 ambao waangalizi walisema ulikumbwa na dosari kubwa na ukiukaji wa haki. Hichilema aliingia madarakani mnamo 2021 akiahidi kurejesha demokrasia baada ya kuishutumu serikali iliyotangulia kwa kuiba uchaguzi na kuwafunga wapinzani. Hata hivyo, waangalizi wa uchaguzi wa ndani na kimataifa wameripoti dosari kadhaa katika uchaguzi huo, zikiwemo madai ya udanganyifu katika hesabu za kura, kukamatwa kwa wabunge wa upinzani, wanajeshi kuwekwa katika vituo vya kupigia kura na kufungwa kwa mahakama. Mpinzani wake Brian Mundubile na mgombea mwenza wake Makebi Zulu pia walishtakiwa kwa uhaini mwishoni mwa wiki. Zambia, inazalisha shaba kwa wingi, imekuwa kitovu cha ushindani kati ya China na Amerika kutokana na utajiri wake wa madini. Nchi hizo mbili zilimpongeza Hichilema kwa ushindi wake na kutuma wawakilishi kwenye hafla ya kuapishwa kwake. Zambia imekuwa ikifanya uchaguzi tangu miaka ya 1990 ilipokumbatia mfumo wa vyama vingi, ingawa baadhi yake imekuwa na dosari. Wachanganuzi wanaonya kuwa uchaguzi huu unaweza kuweka mfano utakaowawezesha viongozi wa baadaye kujilazimisha madarakani badala ya kuimarisha demokrasia. "Hadhi ya Zambia ya kidemokrasia iko hatarini. Hatujawahi kushuhudia mkanganyiko wa aina hii," akasema mwanahistoria Euston Chiputa. Alikuwa akirejelea kusimamishwa kwa kuhesabiwa kura, kuwekwa kwa wanajeshi katika vituo vya kuhesabia kura na kukamatwa kwa viongozi wa upinzani. Waangalizi wa uchaguzi walisema kulikuwa na dalili za kuongezwa kwa kura katika hesabu ya Hichilema, ingawa walikubaliana kuwa angeshinda hata bila kura hizo zinazodaiwa kuongezwa. Tume ya Uchaguzi ya Zambia ilisema madai yoyote ya udanganyifu yanapaswa kuwasilishwa mahakamani. Kinaya ni kwamba mahakama ilifungwa siku ya mwisho ya kuwasilisha kesi ya kupinga matokeo. Baadaye zilisema hakuna malalamishi yaliyowasilishwa. Serikali pia haijatoa maelezo ya kutosha kuhusu mashtaka dhidi ya Mundubile na viongozi wengine 12 wa upinzani waliotiwa gerezani. Licha ya machafuko ya kisiasa, wawekezaji bado wanaendelea kuonyesha imani kwa uchumi wa Zambia. Hichilema aliongoza mchakato wa kupunguza deni na kuimarisha uchumi katika muhula wake wa kwanza, hatua iliyomfanya kuwa chaguo linalopendelewa na wawekezaji wanaotaka mwendelezo wa sera. Hata hivyo, mtafiti wa Chatham House Christopher Vandome alisema mafanikio ya kiuchumi ya muda mfupi hayawezi kuficha madhara ya muda mrefu ya kuangamiza taasisi za kidemokrasia.

read more
T

taifaleo.nation.co.ke

@taifaleo Wed, 02 Sep 2026 14:31:54

MAONI: Caroli Omondi ni mwanamikakati stadi ambaye hucheza chini ya maji

MMOJA wa wanasiasa ambaye anategemewa kwa mustakabali wa umoja wa upinzani ni Mbunge wa Suba Kusini Caroli Omondi. Zipo sababu kadhaa zinazomkweza Caroli katika siasa Kenya inapojiandaa katika uchaguzi mkuu ujao wa Agosti 10, 2027. Kwanza, yeye ndiye msemaji wa kundi la Linda Mwananchi linaloongozwa na seneta wa Nairobi Edwin Sifuna na washirika wake. Pili ni katibu mkuu wa muungano wa Azimio, vyama ambavyo viliunga mkono Raila Odinga katika uchaguzi mkuu wa Agosti 8, 2022. Moja ya sifa kubwa ya Caroli ni kuwa msemaji bora wa lugha zote mbili ila Kingereza chake kinashuka taratibu na kwa ufundi mkubwa. Inawezekana Linda Mwananchi ilimteua bila kufahamu usuli wake vizuri. Caroli ana tajiriba kubwa ya upatanishi na alikuwa kiungo muhimu kwa upande wa aliyekuwa kiongozi wa ODM Raila wakati wa mazungumzo baada ya ghasia za uchaguzi za 2007/2008. Katika mahojiano yangu awali kidogo, aliniambia zile wanazoita mitaani "za ndani" yaani habari ambazo ni siri. Ila sasa Caroli ana jukumu kubwa mno kupita Edwin Sifuna, Babu Owino, James Orengo na kundi lile jingine la Kalonzo Musyoka. Anatakiwa kuhakikisha makundi haya yanapatana na mgombea mmoja kukabiliana na Rais William Ruto ambaye anataka ridhaa nyingine ya Wakenya. Awali nyufa zimeanza kujitokeza katika kundi la Linda Mwananchi kuhusu anayestahili kuwa kiongozi wa chama na hata mgombea Urais. Pili, Kalonzo, Gachagua na washirika kila mtu anapaza sauti kuwa anatosha kuongoza Kenya. Tatu anatoka eneo la Nyanza ambalo linadai kuwa Raila Odinga aliwaacha kwa serikali jumuishi. Caroli alionyesha makali yake kwa kufanikisha ziara ya Linda Mwananchi katika kaunti ya Homa Bay. Pamoja na kuwa kulikuwa na vurugu kubwa na kusababisha maafa, kikosi cha Caroli kilifanikiwa kuuza sera kwa wakazi wa Homa Bay licha ya kuwepo kwa vitisho kutoka kwa wafuasi wa Gavana Gladys Wanga ambaye ndiye mwenyekiti wa chama cha ODM. Moja ya dhima muhimu inayomsubiri ni kufifisha nguvu za ODM ambazo wahafidhina kutoka eneo lake hawadhanii kuwa ni jambo linalowezekana kwa wepesi. Ruto alipo anajua uwezo wa ungaunga za Caroli. Upinzani nao una mtihani mkubwa kumpa dhamana ya kusimamia mchakato wa kuupatanisha na kusalia kama gundi endapo watataka kuwa wenyeji wa ikulu. Wafuasi wa Sifuna wanamtaka debeni, Matiang'i anasema ataikomboa nchi, Kalonzo ana huu wakati pekee huku Gachagua akijigamba kuwa nyota yake inaangaza. Kazi kwa Caroli. Je, ataonyesha njia ya upinzani ya 2002? Paul Nabiswa ni mhariri, NTV

read more