T

taifaleo.nation.co.ke

@taifaleo Wed, 02 Sep 2026 15:42:09

Hasira kuhusu kutekwa kwa mhariri wa Standand Group Alex Kiprotich

MASHIRIKA ya habari nchini yameitaka Serikali kufanya uchunguzi huru na wa haraka kuhusu madai ya kutekwa kwa Mhariri Mwandamizi wa Standard Group, Alex Kiprotich. Wameonya kuwa mashambulizi dhidi ya wanahabari yanazua hofu nchini kuelekea uchaguzi mkuu wa 2027. Bw Kiprotich alitekwa na wanaume waliokuwa na silaha katika barabara ya Gilgil-Nakuru Jumanne usiku, muda mfupi kabla ya saa tatu na dakika 20 usiku. Video ya tukio hilo inaonyesha gari aina ya Subaru lenye nambari ya usajili KDC 125E likimpita kisha kumzuia. Wanaume waliokuwa na silaha walimwamuru atoke kwenye gari lake kabla ya kumwingiza kwa lazima katika gari lao. Alipatikana ametupwa karibu na Bwawa la Masinga, Machakos Jumatano asubuhi, zaidi ya saa tisa baada ya kutekwa; umbali wa zaidi ya kilomita 200 kutoka eneo la tukio. Bw Kiprotich alipewa hifadhi na familia moja ya eneo hilo kabla ya kikosi cha Standard Group kilichoongozwa na Afisa Mkuu Mtendaji wa kampuni hiyo, Chaacha Mwita, kumchukua karibu saa kumi na mbili na nusu asubuhi. Alikuwa salama kimwili lakini alishtuka sana kiasi cha kutoweza kuzungumza na wanahabari. Tukio hilo limeibua hasira miongoni mwa mashirika ya habari na ya kutetea haki za binadamu, huku yakitaka waliohusika kutambuliwa na kufikishwa mahakamani. Chama cha Wahariri Kenya, Chama cha Wanahabari Kenya (KUJ) na Chama cha Wanawake katika Habari Kenya (AMWIK), chini ya Kenya Media Sector Working Group, vilisema tukio hilo ni sehemu ya mfululizo wa vitisho dhidi ya wanahabari. Katibu Mkuu wa KUJ, Eric Oduor, alisema shambulio dhidi ya mwanahabari yeyote ni shambulio dhidi ya uhuru wa vyombo vya habari. Alisema uchunguzi wa awali umebaini baadhi ya watu waliohusika na tukio hilo na kwamba mashirika hayo yatawasilisha malalamishi kwa Mamlaka Huru ya Kusimamia Utendakazi wa Polisi (IPOA) na Ofisi ya Mkurugenzi wa Mashtaka ya Umma (ODPP). "Tutaandikia ODPP ichukue hatua na iwapo haitafanya hivyo, tutawafungulia mashtaka maafisa waliohusika," alisema Bw Oduor. Hofu zaidi imezuka kutokana na madai kwamba mwezi Juni 27 pia kulikuwa na jaribio jingine la kumteka Bw Kiprotich. Uchunguzi wa ndani wa Standard Group kuhusu tukio hilo umedaiwa kubaini gari lililotumiwa na watekaji ni la kitengo cha Crime Research and Intelligence Bureau (CRIB) cha Polisi, lakini hakuna afisa aliyewajibishwa. Rais wa Chama cha Wahariri Kenya, Zubeida Kananu, alisema kushindwa kuwachukulia hatua wahusika wa mashambulizi ya awali kumewapa ujasiri wanaowalenga wanahabari. Viongozi hao pia walielezea wasiwasi kuhusu kushuka kwa Kenya katika orodha ya uhuru wa vyombo vya habari duniani ya Reporters Without Borders (RSF). Kenya imeshuka kutoka nafasi ya 69 mwaka 2022 hadi ya 106 kati ya nchi 180. Chama cha Wamiliki wa Vyombo vya Habari (MOA) pia kimetaka kufanywe uchunguzi huru, wa haraka na wa wazi. Mwenyekiti wake Agnes Kalekye alisema chama hicho kimehuzunishwa na tukio hilo lakini kimefarijika kwamba Bw Kiprotich alipatikana akiwa hai. Alisisitiza kuwa wanahabari wanapaswa kuruhusiwa kutekeleza majukumu yao bila vitisho au kuingiliwa. Rebecca Mutiso, meneja wa Uhuru wa Vyombo vya Habari na Utetezi katika Baraza la Vyombo vya Habari Kenya, aliwataka watu walio na malalamishi kutumia njia halali za kuyatatua badala ya kuwalenga wanahabari. "Leo unataka kumnyamazisha mwanahabari, lakini itakuwaje haki zako zitakapokiukwa na uhitaji mwanahabari huyo huyo kuripoti kisa chako?" akauliza. Amnesty International Kenya pia imetaka uchunguzi huru na wa uwazi, ikisema tukio hilo ni tishio kubwa kwa uhuru wa kujieleza na vyombo vya habari.

read more
T

taifaleo.nation.co.ke

@taifaleo Mon, 31 Aug 2026 06:55:34

Mgomo JKIA wazua hasara, safari zikichelewa

ABIRIAkatika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Jomo Kenyatta (JKIA) waliingiwa na wasiwasi na sintofahamu kuhusu safari zao baada ya wafanyakazi wa sekta ya anga kuanza tena mgomo. Hali hiyo ilisababisha safari kadhaa za ndege ndani na nje ya nchi kucheleweshwa. Wasafiri walisema hawakupewa taarifa ya kutosha kuhusu mgomo huo, huku baadhi yao wakifika uwanjani na kugundua kuwa safari zao zilikuwa zimecheleweshwa. Muungano wa Wafanyakazi wa Usafiri wa Anga nchini (KAWU) ulianza tena mgomo Jumamosi usiku kutokana na malalamishi mbalimbali, yakiwemo yale yaliyosababisha kusimamishwa kwa mgomo wa awali mwezi uliopita. Mwenyekiti wa KAWU Walter Ongeri aliambia Taifa Leo kuwa wafanyakazi waliamua kurejea kwenye mgomo baada ya serikali kushindwa kutekeleza masharti ya mkataba wa maelewano (MoU) uliotiwa saini na muungano huo. "Tulitia saini makubaliano ya kurejea kazini lakini, kwa bahati mbaya, KAA na KCAA zimeshindwa kushughulikia malalamishi yetu. Asasi hizo mbili hazijajitolea kikamilifu katika mazungumzo na zimeshindwa kushirikiana nasi katika kutafuta suluhu ya malalamishi yetu," akasema Katibu Mkuu wa KAWU Moss Ndiema.  Glen Omindu, aliyekuwa anatarajia kusafiri Dubai kwa ndege ya saa saba mchana, alisema abiria hawakuwa wameambiwa wangetoka saa ngapi. "Hakukuwa na onyo lolote na hilo ndilo tatizo. Ndege ilikuwa iondoke saa saba lakini bado hatujaambiwa tutasafiri lini. Tutalazimika kutafuta cha kufanya kwa sasa na ninatumai mambo yatakuwa sawa au niahirishe safari," akasema Bw Omindu. Faith Mbugua, aliyefika uwanjani saa nne asubuhi kwa safari yake ya saa saba, alisema abiria walikuwa wakihangaika kupata taarifa kuhusu safari yao. "Tumechanganyikiwa sana. Tulikuwa hapa saa nne na tukaambiwa kuna mgomo. Safari yetu sasa imepangwa kuondoka saa 2:50 usiku," akasema. Stephen Maguro, aliyekuwa akisafiri Rwanda kuhudhuria mkutano, pia alisema safari yake ilikuwa imecheleweshwa. Mamlaka ya Viwanja vya Ndege nchini (KAA) ilisema viwanja vya ndege kote nchini vilikuwa vikikumbwa na abiria kucheleweshewa safari. "KAA inashirikiana kwa karibu na mashirika husika ya anga, kampuni za ndege na wadau wengine kudhibiti hali hiyo, kupunguza usumbufu na kuhakikisha shughuli za viwanja vya ndege zinaendelea kwa utaratibu," akasema.  KAA iliwashauri abiria kuwasiliana na kampuni zao za ndege kupata taarifa kuhusu safari zao. Wakati huo huo, maafisa wa KAWU, Wizara ya Uchukuzi na mashirika ya anga walikuwa katika kikao cha dharura Jumapili kutafuta suluhu kuhusu mgomo.

read more
T

taifaleo.nation.co.ke

@taifaleo Mon, 31 Aug 2026 04:55:53

Wabunge wa 'Broabased' wakosolewa kwa uzembe kamatini

WABUNGE wanaounga mkono serikali ambao wanaongoza kamati muhimu za Bunge wamekosolewa kwa kushindwa kuwawajibisha mawaziri kuhusu masuala yanayowahusu wananchi. Ripoti iliyowasilishwa na Naibu Kiongozi wa Wengi katika Bunge, Owen Baiya, ilifichua kuwa kamati 19 za Bunge zilikuwa zimeshindwa kutoa majibu kwa maswali yaliyoulizwa na wabunge kwa niaba ya wananchi kufikia wakati Bunge lilipoenda likizo ya mwezi mmoja Alhamisi. Kamati ya Utawala na Usalama wa Ndani iliongoza kwa kuwa na maombi 26 ambayo hayakuwa yamejibiwa. Kamati hiyo inaongozwa na Mbunge wa Narok West, Gabriel Tongoyo. Kamati ya Uchukuzi na Miundombinu, inayoongozwa na Mbunge wa Ndia George Kariuki, ilikuwa ya pili kwa kuwa na maswali 21 ambayo hayajajibiwa kuhusu kuimarishwa kwa miundombinu. Kamati ya Elimu inayoongozwa na Mbunge wa Tinderet Julius Melly ilikuwa na maswali 18 ambayo hayajajibiwa kuhusu sekta ya elimu.  Bw Tongoyo, Bw Kariuki na Bw Melly walichaguliwa kwa tiketi ya UDA, chama tawala katika serikali ya Kenya Kwanza. Ripoti hiyo iliandaliwa kwa maagizo ya Spika wa Bunge Moses Wetang'ula baada ya wabunge kutaka kujua hatua zilizochukuliwa kuhusu maombi yao ya taarifa.  "Wabunge wanahitaji kujua jinsi maombi yao ya taarifa yalivyoshughulikiwa na kamati mbalimbali," alisema Bw Baiya alipowasilisha ripoti hiyo.  Bw Baiya aliwataka wenyeviti wa kamati kuhakikisha majibu kutoka kwa mawaziri na mashirika ya serikali yanawasilishwa kwa wakati.  "Wanafanya hivyo kwa niaba ya wapigakura wao. Hilo linatulazimu sisi kama wenyeviti wa kamati kuhakikisha yanajibiwa kwa ufupi, kwa usahihi na kwa wakati. Hii itahakikisha Bunge halifanyi kazi bure," akasema. Kamati za Afya na Fedha na Mipango ya Kitaifa, zinazoongozwa na James Nyikal (Seme) na Kuria Kimani (Molo), kila moja ilikuwa na maombi manane ambayo hayajajibiwa. Kamati ya Ardhi, inayoongozwa na Joash Nyamoko (Mugirango Kaskazini), ilikuwa na maswali saba, huku Kamati ya Ulinzi, Ujasusi na Uhusiano wa Kimataifa ikiwa na sita. Kamati za Kilimo na Mifugo, Nishati na Leba kila moja zilikuwa na maswali matano ambayo hayajajibiwa. Kamati ya Mazingira, Misitu na Madini ilikuwa na manne, huku kamati za Utalii na Wanyamapori na Nyumba, Mipango Miji na Kazi za Umma kila moja ikiwa na matatu. Kamati nyingine zilizokuwa na maswali ambayo hayajajibiwa ni Mawasiliano, Habari na Ubunifu (mawili), Sheria na Haki (moja), Ulinzi wa Jamii (moja), Biashara, Viwanda na Vyama vya Ushirika (moja) na Bajeti na Matumizi (moja). Wabunge hupokea posho za vikao vya kamati pamoja na mshahara na marupurupu mengine. Mwenyekiti wa kamati hupokea Sh15,000 kwa kila kikao, hadi kiwango cha juu cha Sh240,000 kwa mwezi.

read more
T

taifaleo.nation.co.ke

@taifaleo Mon, 31 Aug 2026 03:55:51

Wantam: Sifuna atua Meru kwa kishindo!

SIKU chache baada ya kukumbwa na ghasia zilizosababisha vifo katika Kaunti ya Homa Bay, viongozi wa vuguvugu la Linda Mwananchi jana walijipigia debe katika Kaunti ya Meru wakisema hakuna kiwango cha ghasia kitakachozima kiu chao cha mabadiliko. Vuguvugu hilo linaloongozwa na Seneta wa Nairobi Edwin Sifuna, lilifika Meru kwa mapokezi makubwa mwenyeji wao akiwa aliyekuwa Gavana wa Meru Kawira Mwangaza, ambaye pia ni kiongozi wa Umoja na Maendeleo Party (UMP). Viongozi hao walihutubia wananchi katika maeneo ya Kiirua, Githongo, Nkubu, Meru mjini na Kianjai. "Tunawashukuru watu wa Meru kwa kudumisha amani na kuonyesha jinsi demokrasia inavyopaswa kufanya kazi," akasema Bw Sifuna. Katika mikutano hiyo, Bw Sifuna aliishambulia serikali ya Rais William Ruto, akiilaumu kwa kupuuza Katiba, sheria na ahadi ilizotoa wakati wa kampeni za uchaguzi. Alisema lengo la Linda Mwananchi ni kurejesha utawala wa sheria, kuheshimu haki za binadamu na kuimarisha demokrasia. "Rais Ruto alikuwa ameahidi kuheshimu Katiba, siku moja tu baada ya maadhimisho ya miaka 16 ya Katiba, wafanyabiashara walitandikwa na kurushiwa vitoza machozi Nairobi walipokuwa wakipinga ushuru wa juu," akasema Bw Sifuna. Katibu huyo wa zamani wa ODM pia alimshambulia Waziri wa Usalama wa Ndani Kipchumba Murkomen, akisema ameshindwa kukabiliana na uhuni na makundi ya vijana wanaovuruga mikutano ya upinzani. Alisema iwapo Linda Mwananchi itaunda serikali ijayo, Bw Murkomen atakuwa miongoni mwa mawaziri wa kwanza kuondolewa. Viongozi hao walisisitiza umuhimu wa vyama vya upinzani kuungana ili kumenyana na Rais Ruto katika uchaguzi mkuu wa 2027. Mbunge wa Embakasi Mashariki Babu Owino alisema upinzani unapaswa kuwasilisha mgombea mmoja wa urais ili kuongeza nafasi ya kuwahi ushindi. Vilevile, viongozi hao waliishutumu serikali kwa kushindwa kushughulikia ukosefu wa ajira na gharama ya juu ya maisha. Bw Owino aliikosoa serikali kuhusu zabuni ya Sh2.5 bilioni ya sare za polisi, akisema fedha hizo zingetumika vyema kuanzisha viwanda na kuunda nafasi za ajira kwa vijana. Gavana wa Trans Nzoia George Natembeya aliitaka Tume Huru ya Uchaguzi na Mipaka (IEBC) kuimarisha mifumo yake na kuhakikisha uchaguzi wa 2027 utakuwa huru na wa kuaminika. "Serikali inatoa vitambulisho kwa vijana ambao hawajafikisha umri wa miaka 18 katika baadhi ya sehem za nchi. IEBC inafaa kuwa chonjo na kuzima juhudi zozote za udanganyifu," akasema Bw Natembeya. Viongozi hao pia walimtetea Bi Mwangaza, wakidai aliondolewa madarakani kwa njia isiyo ya haki na wanasiasa wanaounga mkono serikali.

read more