T

taifaleo.nation.co.ke

@taifaleo Sun, 30 Aug 2026 16:03:03

Wataalamu 12 waanza kuandaa manifesto ya UDA-ODM kuelekea 2027

KAMATI ya wataalamu walioteuliwa kuandaa mwongozo wa kisiasa na manifesto ya pamoja ya vyama vya UDA na ODM kuelekea Uchaguzi Mkuu wa 2027 imeanza kazi rasmi huku ikipanga kufanya mashauriano kitaifa yatakayohusisha wananchi kutoka maeneo mbalimbali nchini. Mkurugenzi Mkuu wa UDA, Nicodemus Bore, ambaye ni mwanachama wa kamati hiyo alisema wataalamu hao tayari wamefanya mkutano wao wa kwanza na sasa wanajipanga katika makundi ya kiufundi ili kuanza kazi ya kuandaa msingi wa ushirikiano wa kisiasa kati ya Rais William Ruto na kiongozi wa ODM, Dkt Oburu Oginga. "Tayari tumekutana na kufanya kikao chetu cha kwanza. Sasa tunaandaa mikutano mingine na kupanga jinsi ya kufanya kazi kupitia makundi ya kiufundi. Kazi imeanza rasmi," alisema Bore. Alisema wananchi wanapaswa kutarajia mashauriano makubwa kote nchini ili kuhakikisha maoni ya makundi mbalimbali yanazingatiwa kabla ya mapendekezo ya mwisho kuandaliwa. Kwa mujibu wa Bore, hatua ya kwanza itakuwa kupitia upya manifesto za UDA na ODM za 2022, kutathmini utekelezaji wa ahadi zilizotolewa na kubaini maeneo yaliyofanikiwa na yale yanayohitaji kuboreshwa. "Tunataka kuhakikisha ahadi tulizotoa 2022 zinatimizwa kikamilifu," alisema. Kamati hiyo ina wanachama 12, ambapo kila chama kimetoa wataalamu watano huku Bore na Mkurugenzi Mkuu wa ODM Oduor Ong'wen wakihudumu kama wanachama wa moja kwa moja. Kwa upande wa ODM, wanachama ni Isaac Wanuge, Maryam Abdullahi Mbaruk, Profesa Leonida Kerubo Omosa, Carey Orege na Profesa Bernard Muok. UDA imewakilishwa na Dkt Emmanuel Nzai, Dkt Daniel Mwai, Bramwel Simiyu, Mohammed Hassan na Dkt Cecilia Ng'etich. Orege, ambaye ni mwenyekiti wa muda wa kamati hiyo, alisema wamemaliza mkutano wa utangulizi na sasa wanasubiri mwongozo rasmi wa majukumu yao kabla ya kuandaa ratiba kamili ya kazi. Muundo wa kamati hiyo unaonyesha kuwa UDA na ODM zimeweka mkazo katika badala ya umaarufu wa kisiasa. Wanachama wake wanatoka katika sekta za uchumi, afya, miundombinu, elimu, sayansi, maendeleo, utawala wa umma na uongozi wa vyama vya siasa. Changamoto kubwa inayowakabili wataalamu hao ni kuoanisha sera za vyama viwili ambavyo vilikuwa katika pande tofauti za kisiasa katika uchaguzi uliopita na kuandaa ajenda moja itakayowavutia wapigakura. Bore alisema kamati hiyo itachunguza mafanikio yaliyopatikana, changamoto zilizobaki na maeneo ambayo serikali ingeweza kufanya vizuri zaidi. "Hatutaki kuonekana tunaishi katika ulimwengu wa njozi. Tunataka matarajio ya wananchi kutoka maeneo yote ya nchi yawe sehemu ya manifesto," alisema. Rais Ruto alitangaza kuundwa kwa kamati hiyo baada ya mkutano wa viongozi wa UDA na ODM, akisema kazi yao haitakuwa tu kuandika manifesto ya kampeni bali pia kuweka msingi wa maono ya maendeleo ya taifa.

read more
T

taifaleo.nation.co.ke

@taifaleo Sun, 30 Aug 2026 16:43:34

Nimepunguza kasi ya madeni, asema Ruto

RAIS William Ruto ametetea vikali rekodi ya serikali yake kuhusu deni la taifa, akisema Kenya imefanikiwa kupunguza kasi ya kukopa ikilinganishwa na tawala mbili zilizotangulia. Kwa mujibu wa Rais, kipimo muhimu si iwapo nchi imeacha kukopa kabisa, bali ni kiwango ambacho deni la umma limekuwa likiongezeka. Alisema deni la taifa lilikuwa takriban Sh10.3 trilioni alipoingia madarakani mnamo 2022 na linatarajiwa kufikia karibu Sh13 trilioni kufikia mwisho wa mwaka huu, ongezeko analodai ni la asilimia 27 pekee katika kipindi cha miaka mitano. "Moi alipoondoka madarakani, deni la taifa lilikuwa Sh630 bilioni. Kibaki alilirithi na kuliongeza hadi Sh1.8 trilioni ndani ya miaka 10. Hilo ni ongezeko la karibu mara tatu," alisema Rais Ruto. Aliongeza kuwa Rais Uhuru Kenyatta alipomaliza muhula wake 2022 aliacha deni la Sh10.3 trilioni, kiwango ambacho kilikuwa kimeongezeka mara tano kutoka alichokuta Kibaki. "Katika miaka yangu mitano, deni limeongezeka kutoka Sh10.3 trilioni hadi Sh13 trilioni. Hilo si ongezeko la mara kadhaa bali ni asilimia 27 pekee," alisema. Kauli hiyo ndiyo msingi wa hoja yake kwamba, alitimiza moja ya ahadi zake kuu za kampeni za mwaka 2022 za kudhibiti tabia ya kukopa kupita kiasi. "Nilisema ukiwa ndani ya shimo, jambo la kwanza ni kuacha kuchimba. Hivyo ndivyo tulivyokuta nchi ikiwa," alisema. Rais alisema alinuia kupunguza kutegemea mikopo, ushuru na madeni kwa kubadilisha jinsi miradi ya maendeleo inavyofadhiliwa. Anasema serikali yake imeendelea kuwekeza katika miundombinu na miradi ya kijamii bila kuongeza deni la kawaida la serikali kwa kasi iliyoshuhudiwa miaka ya nyuma. Miongoni mwa miradi mikubwa aliyotaja ni barabara ya Rironi-Nakuru-Mau Summit, Mradi wa Northern Kenya Gateway, upanuzi wa reli ya kisasa (SGR) kuelekea Kisumu na Malaba, pamoja na miradi ya maji na nishati. Pia alitaja Mpango wa Nyumba Nafuu, ambao una zaidi ya nyumba 300,000 katika hatua tofauti za ujenzi, mabweni ya wanafunzi na masoko ya kisasa. Kwa mujibu wa Rais, uwekezaji katika nyumba, masoko na mabweni pekee umefikia takriban Sh1.2 trilioni. Hata hivyo, wakosoaji wake wanaonya kuwa kuangalia tu kiwango rasmi cha deni hakutoshi. Wanasema kuna majukumu mengine ya kifedha yanayoibuliwa kupitia mbinu mbadala za ufadhili ambayo huenda hayajaonekana moja kwa moja katika deni rasmi la taifa. Mojawapo ya hoja hizo ni kutumia mapato ya baadaye ya ushuru wa matengenezo ya barabara kama dhamana ya kufadhili miradi au kulipa wakandarasi. Shirika la Fedha la Kimataifa (IMF) pia limekuwa likihimiza kutambuliwa kwa aina mbalimbali za madeni na wajibu wa kifedha yanayotokana na ushirikiano kati ya sekta ya umma na binafsi. Rais Ruto anasema suluhisho lake ni kuanzisha Hazina ya Kitaifa ya Miundombinu, inayolenga kuvutia uwekezaji kutoka kwa sekta binafsi, hazina ya pensheni na taasisi za maendeleo badala ya kutegemea mikopo ya serikali pekee. Lakini mafanikio ya mpango huo yatategemea uwazi, usimamizi na uwezo wa miradi hiyo kuzalisha mapato bila kuwaachia walipakodi mzigo wa siri wa kifedha.

read more
T

taifaleo.nation.co.ke

@taifaleo Sun, 30 Aug 2026 14:52:24

Kuria 'atabiri' kuhusu atakayeapishwa kuwa rais 2027

ALIYEKUWA Waziri Moses Kuria ameibua mjadala kuhusu uchaguzi wa urais wa 2027 baada ya kutoa kauli tata kuhusu atakayeapishwa kuwa rais baada ya uchaguzi huo. Kuria, ambaye ni kiongozi wa Chama Cha Kazi (CCK), aliandika kwenye mitandao ya kijamii Jumatano usiku, Agosti 26, 2026, akionekana kudokeza kuwa tayari anajua kitakachotokea katika uchaguzi huo. "2027: Sijui nani atashinda. Lakini najua nani ataapishwa," Kuria aliandika. Katika kauli hiyo fupi hakutaja jina la mtu anayetarajia ataapishwa kuwa rais, hali iliyowaacha wafuasi wake wakikisia maana aliyokusudia. Kuria ameendelea kumuunga mkono Rais William Ruto hata baada ya kuondoka serikalini. Tangu ajiuzulu kama mshauri wa Rais Ruto, Kuria amerejea kikamilifu katika siasa akitoa maoni kuhusu masuala ya kisiasa. Alitoa kauli hiyo siku ambayo aliyekuwa Naibu Rais Rigathi Gachagua alitoa madai kuhusu maandalizi ya uchaguzi wa 2027. Gachagua, ambaye sasa anaongoza chama cha upinzani cha DCP, alishutumu utawala wa Rais Ruto na IEBC kwa kuweka mazingira ya kuvuruga uchaguzi wa 2027. Gachagua alielekeza wasiwasi wake hasa kwenye ununuzi wa teknolojia ya uchaguzi, akidai mchakato huo unaweza kutumiwa kuathiri matokeo ya uchaguzi. Pia alimuonya Mwenyekiti wa IEBC Erastus Ethekon kusimama na Wakenya, akisema jaribio lolote la kuvuruga uchaguzi litakuwa na madhara makubwa. Aidha, alidai kushindwa kwa Ruto 2027 kutakuwa kwa kishindo kiasi kwamba hakutaweza kufichwa kupitia kuvuruga mchakato wa uchaguzi. Hata hivyo, madai hayo yamepuuzwa na maafisa wakuu wa serikali. Katika hali hiyo, kauli tata ya Kuria imeongeza mwelekeo mpya katika mjadala wa kisiasa unaozidi kushika kasi kuelekea uchaguzi mkuu wa 2027.

read more