T

taifaleo.nation.co.ke

@taifaleo Sun, 30 Aug 2026 08:55:56

Zaidi ya watu 3,000 bado hawajulikani walipo Nepal

JUHUDI za kuwaokoa waathiriwa wa mafuriko makubwa katika mpaka wa Nepal na Tibet nchini China zilirejelewa jana, baada ya kusitishwa kwa muda kutokana na hofu ya kutokea kwa mafuriko tena kutokana na kuyeyuka kwa barafu mlimani. Idadi ya waliofariki katika mkasa huo imefikia 633, huku karibu watu 3,000 wakiripotiwa kutoweka. Polisi nchini Nepal ilisema jana kuwa watu 626 wamefariki kutokana na mafuriko hayo, huku Mamlaka ya Kudhibiti Majanga ikiripoti kuwa watu 2,426 bado hawajulikani waliko.  Kati ya waliotoweka nchini Nepal, 517 ni raia wa kigeni, ambao huenda ni watalii au wafanyakazi kutoka mataifa mengine. Nchini China, mamlaka ilisema watu wasiopungua saba wamefariki katika eneo la Tibet, huku wengine 554 wakiripotiwa kutoweka. Kutokana na ukubwa wa janga hilo, serikali ya Nepal iliomba msaada maalumu kutoka India na China ili kuongeza uwezo wa operesheni za uokoaji. Timu kutoka mataifa hayo, zikiwemo wataalamu wa uokoaji zilitarajiwa kuwasili jana. Msemaji wa Wizara ya Mashauri ya Kigeni ya Nepal, Lok Bahadur Poudel Chhetri, alisema uamuzi huo ulifanywa kwa dharura kutokana na maisha ya watu kuwa hatarini. "Maisha yako hatarini na hali ni ya dharura sana. Hapo awali Nepal haikutaka msaada kwa sababu haikutaka mkanganyiko unaoweza kutokea wakati timu kubwa zinaelekezwa katika maeneo tofauti," alisema Chhetri. Awali, Nepal ilikataa msaada wa kimataifa kwa hofu kuwa kuwasili kwa vikosi vingi vya uokoaji kungeleta mkanganyiko katika operesheni hizo. Mkasa huo ulianza Jumatano asubuhi baada ya sehemu ya barafu katika milima ya Himalaya kuyeyuka kutoka urefu wa takriban mita 5,200. Barafu hiyo ilishuka kwa kasi kwa zaidi ya mita 1,200, ikikusanya mawe na vifusi kabla ya kutumbukia katika Mto Lende. Mafuriko yaliyofuata ulisomba maeneo ya Rasuwa, Nuwakot na Dhading nchini Nepal, na kusababisha kina cha Mto Trishuli kupanda kwa mita tisa ndani ya dakika 30. Mto Trishuli uliongezeka kina kwa takriban mita tisa ndani ya dakika 30, na kusababisha uharibifu mkubwa katika maeneo yaliyo karibu. Uchunguzi wa Shirika la Utafiti wa Jiolojia la Amerika, USGS, ulidai kuwa tetemeko la ardhi ndilo lililosababisha mkasa huo. Hata hivyo, uchunguzi wa baadaye ulionyesha kuwa mawimbi ya mtikisiko yaliyorekodiwa yalitokana na maporomoko ya ardhi yaliyosababishwa na kuyeyuka kwa barafu. Waokoaji jana waliendelea na shughuli za kuwatafuta manusura na waliotoweka, huku matumaini yakipungua kutokana na muda uliopita tangu mkasa huo utokee. Wakazi katika maeneo yaliyo hatarini wameonywa kuwa tayari kwa uokoaji. Nepal hupokea mvua nyingi wakati wa msimu wa monsoon, lakini wataalamu wameonya kuwa mabadiliko ya hali ya hewa yanaongeza hatari ya kuyeyuka kwa barafu na kutokea kwa mafuriko makubwa.

read more
T

taifaleo.nation.co.ke

@taifaleo Sun, 30 Aug 2026 07:55:20

Uchaguzi wa 2027 utakuwa ghali zaidi katika historia ya Kenya

UCHAGUZI Mkuu wa 2027 unatarajiwa kuwa ghali zaidi katika historia ya Kenya, huku makadirio yakionyesha kuwa serikali, vyama vya kisiasa na wagombea watatumia zaidi ya Sh272 bilioni katika mchakato mzima wa uchaguzi. Kiasi hicho kinajumuisha bajeti ya Sh74.8 bilioni ambayo Tume Huru ya Uchaguzi na Mipaka (IEBC) imekadiria kwa ajili ya kuendesha uchaguzi huo pamoja na takriban Sh197.35 bilioni ambazo wagombea wanaweza kutumia katika kampeni zao iwapo watazingatia viwango vya matumizi vilivyowekwa na tume hiyo. Kwa miaka mingi, uchaguzi nchini Kenya umejulikana kwa nyimbo, kauli mbiu na kampeni za kuvutia. Hata hivyo, matumizi makubwa ya fedha yameibua maswali kuhusu vipaumbele vya taifa wakati sekta muhimu kama afya, elimu na kilimo zinaendelea kukabiliwa na changamoto za ufadhili. Kiasi cha Sh272 bilioni ni zaidi ya nusu ya fedha zilizotumiwa kuendesha kaunti zote 47 nchini katika mwaka wa kifedha uliomalizika Juni 2025, ambazo zilikuwa Sh470.7 bilioni. Pia fedha hizo zinaweza kulipa kikamilifu madeni ambayo serikali za kaunti zinadaiwa ya zaidi ya Sh156 bilioni. Kwa mtazamo mwingine, kiasi hicho ni kikubwa kuliko bajeti za baadhi ya sekta muhimu katika uchumi. Kwa mfano, sekta ya afya ilitengewa Sh177.2 bilioni, elimu ya juu Sh163.9 bilioni na elimu ya msingi Sh136.6 bilioni katika bajeti ya hivi karibuni ya serikali. IEBC inasema gharama kubwa ya uchaguzi inatokana na teknolojia ya uchaguzi, vifaa vya kutambua wapigakura, mifumo ya kutuma matokeo, karatasi za kura zenye vipengele vya usalama pamoja na ongezeko la idadi ya wapigakura. Tume hiyo inalenga kusajili wapigakura milioni 28.5 kufikia mwaka 2027, ikilinganishwa na milioni 22.1 waliopiga kura mwaka 2022. Ongezeko hilo litahitaji vituo vya kupigia kura 55,393 kutoka vituo 46,229 vilivyotumika mwaka 2022. Kwa upande wa wagombeaji, viwango vipya vya matumizi ya kampeni vinaonyesha kuwa kinyang'anyiro cha kisiasa kitahitaji fedha nyingi zaidi. Mgombea urais ataruhusiwa kutumia hadi Sh6.1 bilioni, kutoka Sh4.7 bilioni mwaka 2022. Wagombeaji wa ugavana, useneta, ubunge na uwakilishi wa wanawake pia watatumia mabilioni ya fedha katika kampeni zao. Mbunge wa Likuyani, Innocent Mugabe, anasema kiwango cha matumizi kilichowekwa na IEBC ni cha chini ikilinganisha na hali halisi ya kampeni. "Nilitumia takriban Sh50 milioni mwaka 2022. Ukiwa na nia ya kushinda, lazima utumie fedha zaidi," alisema. Kwa mujibu wa IEBC, mipaka ya matumizi ya kampeni inalenga kuhakikisha uchaguzi unakuwa wa haki, uwazi na uwajibikaji, na kwamba matokeo ya uchaguzi yanaamuliwa na wapigakura badala ya nguvu ya fedha. Hata hivyo, baadhi ya viongozi wamehoji jinsi sheria hizo zitakavyotekelezwa, wakisema bado Kenya ina mfumo mkubwa wa matumizi ya fedha taslimu ambao ni vigumu kufuatilia. Iwapo makadirio ya sasa yatatimia, uchaguzi wa 2027 utaweka rekodi mpya kama uchaguzi wa gharama kubwa zaidi kuwahi kufanyika nchini Kenya.

read more