T

taifaleo.nation.co.ke

@taifaleo Sat, 29 Aug 2026 09:15:35

Mzozo wa Seneti na magavana waanika changamoto za ugatuzi

Miaka 16 baada ya Kenya kupitisha Katiba ya 2010, mizozo kati ya magavana na Seneti imeibua  maswali kuhusu mipaka ya ugatuzi. Swali kuu ni moja: Serikali za kaunti zinawezaje kuwa huru huku zikimulikwa kuhusu matumizi ya pesa za umma? Mzozo mkuu  ulizuka Februari 2026 baada ya baadhi ya magavana kususia wito wa Seneti. Magavana walidai baadhi ya maseneta walikuwa wakiwaitisha mamilioni ya pesa ili kuwapendelea katika masuala ya ukaguzi wa hesabu. Maseneta walipinga madai hayo. Mzozo huo ulitatuliwa baadaye, lakini uliweka wazi mvutano kati ya uhuru wa kaunti na mamlaka ya Seneti ya kusimamia matumizi ya fedha za umma. Magavana zaidi ya 30 walikutana Kilifi baada ya magavana saba kukosa kufika mbele ya kamati mbili za Seneti Februari 9. Magavana wa Nandi Stephen Sang na Siaya James Orengo walikuwa wameitwa mbele ya Kamati ya Seneti ya Hesabu za Kaunti. Magavana wa Laikipia Joshua Irungu, Muthomi Njuki wa Tharaka-Nithi, Irungu Kang'ata wa Murang'a, Issa Timamy wa Lamu na Cecily Mbarire wa Embu  walitarajiwa kufika mbele ya Kamati ya Uwekezaji wa Kaunti na Fedha Maalum. Kamati hizo zilikuwa zikichunguza ripoti za Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali, Nancy Gathungu, za mwaka wa fedha 2024/25. Magavana walidai baadhi ya maseneta walikuwa wakiwaitisha kati ya Sh9 milioni na Sh12 milioni ili wapate msaada katika masuala ya ukaguzi. Mwenyekiti wa Baraza la Magavana Ahmed Abdullahi alisema magavana hawapingi uwajibikaji. Alisema walikuwa wakipinga matumizi mabaya ya mamlaka ya Seneti. "Imetosha. Ikiwa tutalazimika kurudi kortini kutafuta tafsiri ya maana ya usimamizi huu na magavana kufika mbele ya kamati, tutafanya hivyo," alisema. Seneta wa Homa Bay Moses Kajwang alipinga madai hayo. Aliwataka magavana kuwasilisha ushahidi katika taasisi husika. Alisema Katiba imepatia Seneti mamlaka ya kuchunguza ripoti za Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali na kumwita mtu yeyote kutoa ushahidi. "Uwajibikaji si hisani kwa Seneti; ni wajibu kwa umma," alisema. Kifungu cha 96 cha Katiba kinapatia Seneti jukumu la kumulika kaunti na kulinda ugatuzi. Seneti pia hushiriki katika kutunga sheria zinazohusu kaunti na kusimamia matumizi ya fedha zinazotumwa kwa serikali za kaunti. Lakini ugatuzi hauzuii uwajibikaji. Kifungu cha 174 kinataja matumizi ya mamlaka kwa uwajibikaji, ushiriki wa wananchi na kujitawala kuwa miongoni mwa malengo ya ugatuzi. Seneti pia ina mamlaka ya kumwita mtu kutoa taarifa au ushahidi chini ya Kifungu cha 125. Hata hivyo, Kifungu cha 189 kinataka Serikali ya Kitaifa na serikali za kaunti kushirikiana na kuheshimu mamlaka ya kila upande. Hivyo, kaunti haziwezi kutumia uhuru wao kukwepa uchunguzi halali. Vilevile, Seneti haiwezi kutumia usimamizi kuingilia majukumu yaliyopewa kaunti. Mvutano kama huo ulijitokeza pia wakati Seneti ilipochunguza mkataba wa ushirikiano kati ya Serikali ya Kitaifa na Kaunti ya Nairobi. Mkataba huo ulitiwa saini Februari 2026. Kamati ya Seneti ilipendekeza usitishwe kwa muda, ikisema baadhi ya vipengele vilionekana kuhamisha majukumu ya kaunti badala ya kuwa ushirikiano. Gavana Johnson Sakaja alitetea mkataba huo. Alisema Nairobi ina majukumu ya kitaifa na kimataifa ambayo yanahitaji usaidizi mkubwa kutoka Serikali ya Kitaifa. Mizozo hii inaonyesha changamoto inayoendelea katika mfumo wa ugatuzi. Magavana wanataka uhuru wa kaunti uheshimiwe. Seneti inataka kuhakikisha pesa za umma zinatumika ipasavyo.

read more
T

taifaleo.nation.co.ke

@taifaleo Sat, 29 Aug 2026 08:55:01

Uzinduzi wa sare mpya ya polisi wazua maswali kuhusu zabuni ya Sh3b

SARE mpya ya polisi imezinduliwa huku kukiwa na maswali kuhusu zabuni inayokadiriwa kugharimu hadi Sh3 bilioni. Rais William Ruto alizindua sare hiyo jana katika hafla ya kuhitimu kwa maafisa wapya katika Chuo cha Kitaifa cha Polisi Kiganjo, Nyeri. Sare hiyo mpya ina shati au blauzi ya samawati hafifu na suruali ya samawati iliyokolea. Takriban maafisa 60,000 wa zamu ya kawaida wanatarajiwa kuvaa sare hiyo. Kulingana na taarifa zilizomo katika Idara ya Polisi, seti moja ya sare inakadiriwa kugharimu Sh25,000. Seti hiyo inajumuisha shati au blauzi, suruali, koti, fulana, kofia, sweta, soksi, mkanda na koti la mvua. Sare ya sherehe inakadiriwa kugharimu Sh30,000, bila kujumuisha viatu vinavyogharimu kati ya Sh3,000 na Sh5,000 kwa jozi. Hata hivyo, Idara ya Polisi imekuwa kimya kuhusu kampuni zilizoshinda zabuni na gharama kamili ya mkataba. Inspekta Jenerali wa Polisi Douglas Kanja hakujibu maswali kuhusu mshindi wa zabuni hiyo. Vyanzo vimedai kuwa zabuni hiyo iligawanywa katika sehemu kadhaa na kila sehemu kupewa kampuni tofauti. Miongoni mwa kampuni zilizotajwa ni Nalitex Ltd ya Nairobi, ambayo rekodi za Huduma ya Usajili wa Biashara zinaonyesha inamilikiwa na Selpha Chesimi Temoi. Kamati ya Bunge kuhusu Utawala na Usalama wa Ndani pia haikushirikishwa katika mchakato huo. Wabunge wa kamati hiyo walisema walifahamu kuhusu sare hizo walipotembelea Kiganjo Agosti 21. Mmoja wao alisema kamati inapanga kumwita IG Kanja na maafisa wake kueleza kuhusu zabuni hiyo. Sare mpya inalenga pia kuongeza uwajibikaji. Majina ya maafisa na nambari zao za utumishi zimeshonwa moja kwa moja kwenye sare na haziwezi kuondolewa. Sare ya samawati iliyotumika tangu 2018 ilikosolewa kwa rangi yake, ubora wa kitambaa na kutoshirikisha maafisa wa ngazi za chini katika mchakato wa kuichagua. Sare mpya ilionyeshwa kwa mara ya kwanza mwaka 2023 na aliyekuwa Inspekta Jenerali Japhet Koome. Seneta wa Nairobi Edwin Sifuna amekosoa mabadiliko hayo, akisema serikali inapaswa kuangazia mageuzi ya polisi badala ya mabadiliko ya sare. "Tusidanganywe na vitu vinavyong'aa. Tunataka mageuzi ya polisi, si sare," alisema Sifuna.

read more
T

taifaleo.nation.co.ke

@taifaleo Sat, 29 Aug 2026 07:55:13

Wabunge waliochaguliwa kwa tikiti huru wataka kuwa na usemi bungeni

ABUNGE watakaochaguliwa kwa tiketi huru katika uchaguzi mkuu wa mwaka 2027 huenda wakapata kiongozi wao rasmi katika Bunge la Taifa pamoja na ofisi inayofadhiliwa na walipakodi, iwapo mapendekezo ya marekebisho ya Kanuni za Kudumu za Bunge yatapitishwa. Katika barua iliyoelekezwa kwa Spika wa Bunge la Taifa, Moses Wetang'ula, wabunge hao huru wanataka kiongozi wao awe na ofisi, sawa na ilivyo kwa viongozi wa walio wengi na walio wachache bungeni. "Spika anaweza, kufuatia ombi la maandishi kutoka kwa angalau wabunge huru 10, kutambua rasmi kundi la wabunge huru kwa madhumuni ya kuwawezesha kutekeleza wajibu wao katika Bunge la Taifa," inasema sehemu ya barua hiyo. Barua hiyo, iliyotiwa saini na Mbunge wa Kisumu Mashariki Shakeel Shabbir, ambaye ni mwenyekiti wa kundi la wabunge huru, pia inapendekeza marekebisho ya Kanuni ya Kudumu nambari 259(1) ili kujumuisha kiti maalum kilichotengwa kwa kiongozi wa wabunge huru. "Kutakuwa na viti maalum ndani ya ukumbi wa Bunge kwa matumizi ya kipekee ya Naibu Spika, Kiongozi wa Chama cha Walio Wengi, Kiongozi wa Chama cha Walio Wachache, wabunge wenye ulemavu na wabunge huru," inasema barua hiyo. Wabunge hao wanaeleza kuwa kutengwa kwa viti maalum kutamsaidia Spika kuwatambua kwa urahisi wanapokuwa ndani ya ukumbi wa Bunge. Aidha, wanataka uwakilishi maalum katika Kamati ya Uteuzi, ambayo husimamia kuweka wabunge katika kamati mbalimbali za Bunge, ili kulinda maslahi yao. "Hili litahakikisha kundi la wabunge huru linatambuliwa rasmi badala ya kujumuishwa kwa jumla kama ilivyo sasa," inasema barua hiyo. Kwa mujibu wao, kwa sasa wanategemea hisani ya viongozi wa walio wengi na walio wachache katika ugavi wa nafasi za kamati. "Tunapoenda kwa viongozi wa walio wengi na walio wachache, tunaambiwa hawawajibikii wabunge huru ambao hawajaegemea upande wowote. Matokeo yake ni kwamba wabunge huru huachwa nje ya kamati; kwa kweli wanabaguliwa na kupuuzwa kabisa," inasema barua hiyo. Wabunge hao pia wanataka sauti kubwa zaidi katika uundaji wa Kamati ya Hesabu za Umma (PAC), wakitaka kiti maalum kitengwe kwa mwakilishi wao. Kwa sasa, Kanuni ya Kudumu 205(4) inaeleza kwamba katika uanachama wa PAC, vyama visivyo sehemu ya serikali ya kitaifa vinapaswa kuwa na wingi wa mwanachama mmoja. Barua hiyo imeungwa mkono na wabunge wote 12 huru walio katika Bunge la Taifa. Hao ni Shakeel Shabbir, Caroline Ng'elechei (Elgeyo Marakwet), Monicah Marubu (Lamu), Joshua Mbithi (Masinga), Benard Muriuki (Mbeere Kusini), Elijah Njoroge (Gatundu Kaskazini), Ronald Karauri (Kasarani), Timothy Toroitich (Marakwet Magharibi), Fatuma Mohammed (Migori), Geoffrey Mulanya (Nambale), Kitilai Ole Ntutu (Narok Kusini) na Rahim Dawood (North Imenti). Mbunge huru ni yule anayechaguliwa bila ufadhili wa chama chochote cha kisiasa. Kisheria, mtu anayepania kugombea kama mgombea huru lazima awe amejiuzulu kutoka chama chochote cha kisiasa angalau miezi mitatu kabla ya uchaguzi. Hata hivyo, ingawa kisheria hawapaswi kuhusishwa na vyama vya kisiasa, wengi wa wabunge huru wanaochaguliwa hujiunga au kushirikiana na vyama au miungano ya kisiasa. Mara nyingi hufanya hivyo ili kupata nafasi katika kamati muhimu za Bunge na pia kusaidia serikali kupata idadi inayohitajika ya kura wakati wa maamuzi muhimu. Katika siku za hivi majuzi pia kumekuwa na wito wa kuwafadhili wagombea huru kupitia Hazina ya Vyama vya Kisiasa, sawa na vyama vya kisiasa. Mwaka jana, wakati wa mjadala kuhusu Mswada wa Marekebisho ya Sheria ya Vyama vya Kisiasa wa 2024, baadhi ya wabunge walipendekeza sheria ibadilishwe ili wagombea huru wanufaike na hazina hiyo. Mbunge wa Suba Kusini, Caroli Omondi, alipendekeza wagombea huru wanaopata angalau asilimia tano ya kura zote zilizopigwa wanufaike na fedha hizo. Alisema Katiba inaruhusu mtu kuingia katika uongozi wa kisiasa kupitia chama cha kisiasa au kama mgombea huru, na kwamba hakuna njia iliyo bora kuliko nyingine.

read more