T

taifaleo.nation.co.ke

@taifaleo Sat, 29 Aug 2026 04:55:26

Kindiki aapa kutoana jasho na ODM kutetea wadhifa wake 2027

NAIBU Rais, Profesa Kithure Kindiki Ijumaa aliambia chama cha Orange Democratic Movement (ODM), kinachoongozwa na Seneta wa Siaya Oburu Oginga, kwamba hawezi kuondolewa kirahisi, na kwamba atapambana ili kuhifadhi wadhifa wake. Kauli hiyo ilitolewa huku akimshambulia pia kiongozi wa Wiper Democratic Movement, Kalonzo Musyoka, akimtaka asahau ndoto ya urais. "Wadhifa wa Naibu Rais hauko wazi, na ODM inapaswa kuusahau," alisema Profesa Kindiki. Alizungumza katika Uwanja wa Nembure, Kaunti ya Embu, alipokutana na viongozi 20,000 wa mashinani kutoka eneo hilo. Aliambia ODM kwamba hata mwaka 2027 atakuwa mgombea mwenza wa Rais William Ruto, ambaye anatarajiwa kutetea muhula wake wa pili. "Mimi ni mtu mgumu sana na hawawezi kuniondoa katika kiti changu," alisema akiwarejelea viongozi wa ODM. Katika miezi ya hivi majuzi, mjadala kuhusu wadhifa wa Naibu Rais umeongezeka huku viongozi kadhaa ndani ya serikali jumuishi wakionyesha nia ya kuumezea mate. Miongoni mwa waliotajwa kutamani wadhifa huo ni Oburu Oginga, Mawaziri Wycliffe Oparanya na Hassan Joho, pamoja na Spika wa Bunge la Taifa Moses Wetang'ula. Akiwa Embu, Prof Kindiki alieleza imani yake kuwa Rais Ruto atashinda uchaguzi mkuu wa mwaka 2027 na kuwaonya viongozi wa upinzani kujiandaa kwa mapambano makali ya kisiasa. "Siwezi kuruhusu watu wetu watoke serikalini na kuingia upinzani. Baadhi ya wanaosema tutahudumu muhula mmoja hata hawatakuwa kwenye kura. Wanataka kutuletea watu ambao hawana rekodi yoyote ya maendeleo, hawajabadilisha maeneo yao wala kujulikana kwa maendeleo. Hatutaki kubahatisha. Tunajua tunakopeleka taifa hili," alisema. Prof Kindiki aliwataka viongozi wa upinzani kueleza rekodi zao za maendeleo. Aliwahimiza wakazi wa Embu kutovutwa na misemo ya kisiasa bali wawapime viongozi kwa misingi ya yale waliyofanya walipokuwa madarakani. Alisema serikali ya Kenya Kwanza imepiga hatua kubwa katika kaunti zote 47 tangu ilipoingia madarakani mwaka 2022 na iko tayari kutetea rekodi yake mbele ya wananchi. "Kiwango cha maendeleo tulichofikia si kile tulichokuta mwaka 2022 tulipoingia madarakani. Kazi imefanyika na wananchi wanaweza kuiona," alisema. Naibu Rais alisema yuko tayari kukutana na wananchi wa Embu na Wakenya wote kueleza mafanikio ya serikali katika sekta za kilimo, elimu, afya, miundombinu na nyanja nyingine muhimu. "Niko tayari kueleza kwa wananchi kile ambacho serikali imefanya kubadilisha nchi hii na kuwawezesha wananchi kiuchumi," alisema. Aliwataka wakosoaji wa serikali pia waeleze walichofanikisha walipokuwa katika nyadhifa za umma. "Waambie wananchi walifanya nini walipokuwa na mamlaka makubwa zamani. Ukweli ni kwamba hawana chochote cha kuonyesha," alisema. Kuhusu kilimo, Kindiki alisema serikali imeboresha bei za kahawa na maziwa. Alisema wakulima wa kahawa sasa wanapata kati ya Sh120 na Sh150 kwa kilo, huku bei ya lita moja ya maziwa ikiongezeka kutoka Sh33 hadi Sh50. Aliongeza kuwa bei ya mbolea ilishuka kutoka Sh7,000 mwaka 2022 hadi Sh3,500, baadaye Sh2,500 na sasa Sh2,000 baada ya punguzo zaidi la Sh500.

read more
T

taifaleo.nation.co.ke

@taifaleo Sat, 29 Aug 2026 02:55:57

Tahadhari pombe feki ikitamba nchini

YOTE huanza kwa chupa ya pombe ya bei nafuu, chapa inayofahamika au kinywaji kilichonunuliwa katika baa inayoaminika. Kisha huja ladha ya ajabu, kuwasha koo, kutapika, kushindwa kuamka au hata madhara mabaya zaidi. Kote nchini Kenya, watumiaji wa pombe wanaeleza visa vya kunywa vileo wanavyoshuku kuwa ni bandia au vilivyotiwa kemikali hatari. Baadhi yao waliishia hospitalini, wengine wameogopa kunywa tena huku wengine wakibadilisha kabisa aina ya pombe wanazotumia. Visa hivyo vinaendelea kuibuka katika maeneo mbalimbali nchini na hata kusambaa kwenye mitandao ya kijamii huku mamlaka zikijitahidi kudhibiti tatizo hilo. Wiki hii pekee, maafisa kutoka mashirika mbalimbali walinasa mamia ya chupa za pombe zinazoshukiwa kuwa bandia katika maeneo ya Eastleigh na Jericho jijini Nairobi. Operesheni hiyo pia ilifanikisha kukamatwa kwa stampu za ushuru zinazoshukiwa kuwa feki, chupa tupu na vifuniko vya chupa. Katika mtaa wa Eastleigh, jumla ya chupa 868 za vinywaji mbalimbali zilinaswa, huku 315 zikipatikana Jericho. Ripoti ya utafiti mwaka 2025 iliyochapishwa na Mamlaka ya Kupambana na Bidhaa Bandia (ACA) ilionya kuwa sekta ya vinywaji vya kileo inakabiliwa na changamoto kubwa ya bidhaa ghushi zinazohatarisha afya ya watumiaji na uadilifu wa soko. Kwa mujibu wa ripoti hiyo, divai ndiyo bidhaa inayoghushiwa zaidi kwa asilimia 50.12, ikifuatiwa na bia kwa asilimia 47.44. Mvinyo ulirekodi asilimia 42.68 huku vodka ikifikia asilimia 36.95. John Kamau, mkazi wa Kiambu, anasimulia jinsi alivyokumbwa na matatizo makubwa baada ya kunywa pombe katika baa moja katikati mwa Nairobi. "Pombe ilikuwa chungu kupita kiasi. Niliendelea kuinywa kwa sababu nilikuwa tayari nimelipia. Asubuhi iliyofuata nilipatwa na maumivu makali ya kichwa, tumbo kuuma na kutapika mara kwa mara. Hata kufikia Jumatatu sikuweza kwenda kazini," alisema. Kamau alisema alitumia takriban Sh3,000 hospitalini kununua dawa na tangu wakati huo ameamua kuacha pombe kabisa. Mark Pollard, mshauri wa biashara kutoka Australia ambaye amekuwa akifikiria kuhamia Kenya, alisema alitapika na kuharisha mara mbili katika mazingira yanayomfanya ashuku pombe bandia. "Mara ya pili nilikuwa nimekunywa kiasi kidogo sana cha kileo nilichonunua kutoka duka maarufu. Ndani ya muda mfupi nilianza kutapika na kuharisha kupita kiasi," alisema. Hata hivyo, alikiri kuwa hawezi kuthibitisha kwa asilimia mia moja kwamba pombe ndiyo ilisababisha matatizo hayo kwa kuwa huenda kulikuwa na sababu nyingine za kiafya au chakula. Mfanyabiashara na mwandishi wa masuala ya kitaaluma Robert Ouko Owino alisema tukio lake lilitokea Juni. "Sikuweza kufanya kazi kwa siku tatu. Nimewahi kunywa pombe nyingi hapo awali lakini nilijua hali hii ilikuwa tofauti kabisa na kawaida," alisema. Kwa mujibu wake, watu wengi waliowasiliana naye baada ya kuandika kuhusu suala hilo walisimulia walivyolazwa hospitalini na kupata matatizo ya ini au kongosho (pancreas). Jeremiah Kinuthia, mwenye umri wa miaka 28 kutoka Nairobi, alisema alilazwa katika Hospitali ya Karen baada ya kunywa pombe iliyokuwa na ladha tofauti na ile aliyozoea. "Nilianza kutokwa na jasho na kupata shida ya kupumua. Nililazimika kuwekewa maji mwilini hospitalini," alisema. Tangu tukio hilo, ameacha kutumia pombe kali na sasa hunywa bia pekee. Dkt Joseph Wahome Mukundi, mtaalamu wa sumu katika Hospitali ya Rufaa na Mafunzo ya Meru, alisema kemikali inayohusishwa mara nyingi na pombe bandia ni methanol, ambayo hutumika viwandani. Alieleza kuwa methanol hubadilika mwilini kuwa kemikali hatari zinazoweza kusababisha upofu, kuharibika kwa figo, kushindwa kwa viungo vya mwili na hata kifo.  "Mishipa ya macho inaweza kuathirika na kusababisha upofu ikiwa mtu hatapata matibabu ya haraka," alisema. Daktari huyo amewataka watengenezaji wa pombe kutumia teknolojia kama misimbo ya QR ili kuwasaidia wanunuzi kuthibitisha uhalisi wa bidhaa. Pia amewahimiza Wakenya kununua pombe katika maduka makubwa na maeneo yaliyoidhinishwa rasmi ili kurahisisha ufuatiliaji iwapo kutatokea matatizo. Kwa upande wake, Mkurugenzi Mkuu wa ACA Robi Mbugua alisema bei ya chini isiyo ya kawaida inapaswa kuwa ishara ya tahadhari kwa wanywaji.

read more