T

taifaleo.nation.co.ke

@taifaleo Sun, 20 Sep 2026 06:55:43

Hofu tele wasichana 36 wa shule moja ya Upili wakipata mimba

WADAU wa elimu pamoja na viongozi wa utawala katika Kaunti Ndogo ya Webuye Mashariki, Kaunti ya Bungoma, juzi walifanya mkutano wa dharura kufuatia ongezeko kubwa la mimba za mapema katika shule moja ya eneo hilo. Wanafunzi wasiopungua 36 wa Shule ya Sekondari ya Bakisa wamekuwa wajawazito au wameacha masomo mwaka huu baada ya kupata watoto. Kwa mujibu wa takwimu zilizowasilishwa na uongozi wa shule hiyo, wanafunzi 10 kwa sasa ni wajawazito na bado wanaendelea na masomo yao huku wakikabiliana na changamoto za ujauzito. Wengine 13 walijifungua majuzi, huku wanafunzi 13 zaidi wakiacha shule kabisa baada ya kupata mimba. Mkutano huo uliofanyika Ndivisi uliwaleta pamoja maafisa wa usalama, viongozi wa elimu, wazazi, viongozi wa kidini na wanasiasa ili kutafuta suluhu za haraka za kukabili tatizo hilo. Akizungumza katika mkutano huo, Naibu Kamishna wa Kaunti wa Ndivisi, Emmanuel Kenga, alisema umaskini uliokithiri na uzembe wa baadhi ya wazazi ni miongoni mwa sababu kuu zinazochangia kuongezeka kwa mimba za mapema. Alisema kuna wanaume wanaowalenga wasichana wadogo kwa kuwapa chakula, zawadi ndogo na fedha ili kushawishi kushiriki ngono. "Umaskini unachangia sana tatizo hili. Baadhi ya wanaume wanatumia udhaifu wa wasichana wetu kwa kuwavutia kwa pesa na mahitaji ya msingi," alisema Kenga. Aidha, alitaja matumizi yasiyodhibitiwa ya simu za mkononi na teknolojia kama sababu nyingine inayowafanya watoto kukumbana na maudhui yasiyofaa katika umri mdogo. Baadhi ya wazazi waliodhuria mkutano huo walidai kwamba wasichana wengi hushawishiwa na wanaume wanapokuwa njiani kuelekea au wakitoka shuleni. Wengine walilaumu hali ya watoto kulelewa na babu na nyanya huku wazazi wao wakitafuta ajira mijini. Viongozi wa utawala walifichua kuwa baadhi ya familia hukubali fidia kutoka kwa wanaodaiwa kuwapa mimba watoto wao badala ya kuripoti kesi hizo ili hatua za kisheria zichukuliwe. Inadaiwa kwamba kesi nyingi hutatuliwa kupitia mikutano ya kijamii au baraza za wazee kwa makubaliano ya kifedha. Mwalimu Margaret Muindi aliwataka wazazi kukoma kupokea zawadi au fedha kutoka kwa wahusika wa vitendo hivyo kwa kuwa hatua hiyo huathiri juhudi za kupata haki kwa waathiriwa. Naye Nancy Chibeu, alionyesha masikitiko yake akisema kuwa licha ya wanafunzi 36 kuathiriwa, ni kesi moja pekee ambayo imeripotiwa rasmi. Alitoa wito kwa wananchi kuwafichua wahusika ili wachukuliwe hatua za kisheria na wasichana walindwe dhidi ya unyanyasaji wa kingono.

read more
T

taifaleo.nation.co.ke

@taifaleo Sun, 20 Sep 2026 05:55:59

Mpango wa Gachagua kuwachuja wafuasi wa Ruto ulivyofeli

BAADA ya chama cha Democracy for the Citizens Party (DCP) kinachoongozwa na Rigathi Gachagua kushinda uchaguzi mdogo wa Ol Kalou mnamo Julai 2026, viongozi wengi waliokuwa wakimuunga mkono Rais William Ruto walianza kuonyesha nia ya kuhamia upande wa Gachagua. Katika uchaguzi huo, mgombea wa DCP Kamau Ngotho alipata kura 35,440 dhidi ya kura 5,450 za mgombea wa UDA Muchina Nyagah. Ushindi huo mkubwa ulitafsiriwa kama ishara kwamba eneo la Mlima Kenya lilikuwa likibadili msimamo wake wa kisiasa. Kutokana na wimbi hilo la viongozi waliotaka kuhamia DCP, Gachagua alitangaza kuwa chama chake kingepokea wanachama wapya lakini wale waliokuwa washirika wa karibu wa Rais Ruto wangepitia mchujo mkali kabla ya kukubaliwa. Hatua hiyo ilifuatia shinikizo kutoka kwa viongozi wa DCP waliokuwa na wasiwasi kuwa baadhi ya wanasiasa hao walitaka kuingia chamani ili kukidhoofisha kutoka ndani. Viongozi hao walikumbushwa jinsi baadhi yao walivyoshiriki kampeni dhidi ya Gachagua na DCP. Mnamo Agosti 2, 2026, Gachagua alitangaza kuundwa kwa kamati ya watu saba kuchunguza maombi ya viongozi waliotaka kuhama kutoka UDA kwenda DCP. Kamati hiyo ilijumuisha Maseneta John Methu, Joe Nyutu na Karungo Thang'wa pamoja na wabunge na viongozi wengine wa chama. Hata hivyo, mpango huo haukudumu. Wanachama wa DCP waliibua malalamiko wakitaka wanaotaka kujiunga na chama wapimwe hadharani katika mikutano ya kisiasa badala ya kuhojiwa kwa siri. Hali hiyo ilifanya kamati ya uchunguzi ishindwe kuanza kazi rasmi. Mbunge wa Gatundu Kusini Gabriel Kagombe alikuwa miongoni mwa walioathiriwa na mfumo huo mpya. Alimuomba Gachagua msamaha hadharani na kutangaza kwamba amechoka na Rais Ruto. Lakini aliporuhusiwa kuhutubia mikutano ya DCP katika maeneo mbalimbali, wananchi walimzomea na kukataa kumpokea. Kilichompata Kagombe kilituma ujumbe kwa viongozi wengine waliotaka kuhama. Wengi waliogopa aibu ya kukataliwa mbele ya umma na hivyo wakaamua kubaki katika UDA au kutafuta vyama vingine. Aliyekuwa mwenyekiti wa Kampuni ya Mbegu Kenya, Wangui Ngirichi, pia alikabiliwa na hali ngumu alipojaribu kujiunga na DCP. Mikutano aliyohudhuria iligeuka kuwa ya vurugu huku wafuasi wake wakikabiliana na wale wa DCP, hali iliyosababisha majeraha na kifo cha mtu mmoja. Kwa sasa, viongozi wa DCP wanasema kanuni za uchunguzi bado zipo, lakini hakuna aliyewasilisha rasmi ombi la kuchunguzwa. Hivyo basi, kamati iliyoundwa na Gachagua imebaki bila kazi. Wachambuzi wa siasa wanasema kuwa mpango wa kuwachuja wafuasi wa Rais Ruto uliporomoka kutokana na upinzani wa wanachama wa DCP wenyewe. Badala ya mchakato rasmi wa uchunguzi, wanachama waliamua kuwa wapiga kura katika mikutano ya hadhara ndio wawe waamuzi wa mwisho kuhusu nani anafaa kupokelewa katika chama hicho. Matokeo yake ni kwamba viongozi wengi waliokuwa wakipanga kuhamia DCP wameendelea kusalia katika UDA au wanasaka majukwaa mengine ya kisiasa kuelekea uchaguzi mkuu wa mwaka 2027.

read more