taifaleo.nation.co.ke
@taifaleo Sun, 20 Sep 2026 04:55:42
Oburu angali Uingereza, asubiri madaktari wampe idhini kurejea
KIONGOZI wa chama cha Orange Democratic Movement (ODM), Dkt Oburu Oginga, bado yuko nchini Uingereza akipokea matibabu huku familia yake ikisema hali yake imeimarika lakini bado hajaruhusiwa na madaktari kurejea nchini. Mwakilishi wa Wanawake wa Kaunti ya Kisumu, Ruth Odinga, ambaye ni dadake mdogo, alisema mwanasiasa huyo mkongwe anaendelea kufuatiliwa na madaktari na familia haijafanya mipango yoyote ya haraka ya kumrejesha nyumbani. Kwa mujibu wa Bi Odinga, jambo la msingi kwa sasa ni kuruhusu madaktari kukamilisha kukagua afya yake kabla ya uamuzi wowote kufanywa kuhusu safari yake ya kurejea Kenya. "Ameimarika sana, lakini hatujapanga kurejea kwake Kenya kwa sasa," alisema Bi Odinga akiwa Uingereza. Aliongeza kuwa familia haina haraka ya kumrejesha nchini kwa kuwa bado ana miadi kadhaa ya matabibu ambayo lazima ahudhurie. Bi Odinga alifafanua kuwa Dkt Oginga hajalazwa hospitalini kwa sasa. Badala yake, anaishi karibu na hospitali anayohudumiwa ili iwe rahisi kuhudhuria ukaguzi na miadi ya madaktari. "Hajalazwa. Tunaishi karibu na hospitali, kwa hivyo ni rahisi kwake kuonana na madaktari wakati wowote anapohitajika," alisema. Familia hiyo imesisitiza kuwa afya ya mwanasiasa huyo mwenye umri wa miaka 83 ni muhimu zaidi kuliko majukumu yake ya kisiasa. Kwa sababu hiyo, hawataki kuharakisha kurejea kwake kabla madaktari kuthibitisha kuwa yuko katika hali nzuri. Habari hizo zinajiri huku Dkt Oginga akiendelea kushiriki shughuli mbalimbali kwa njia ya mtandao akiwa Uingereza. Wiki hii alichapisha ujumbe kwenye mitandao ya kijamii akieleza kuwa yeye na mkewe, Mama Judy, walimpokea Balozi wa Kenya nchini Uingereza, Maurice Makoloo, katika makazi yao. Alisema walijadili jinsi ya kuimarisha uhusiano kati ya Kenya na Uingereza, kusaidia Wakenya wanaoishi ughaibuni pamoja na kuchangia maendeleo ya taifa kupitia uwekezaji na ujuzi wao.
read moretaifaleo.nation.co.ke
@taifaleo Sun, 20 Sep 2026 03:55:09
Ziara ya Nyanza ilivyomkweza Raila Jnr katika siasa za taifa
NYOTA ya kisiasa inaonekana imeanza kumng'aria Raila Jnr, mwanawe marehemu Waziri Mkuu Raila Odinga akionekana kujitosa kwenye siasa mzimamzima kwa kuungana na Rais William Ruto katika ziara ya siku tano eneo la Nyanza. Raila Jnr aliandamana na Rais Ruto alipoanza ziara yake Kaunti ya Kisumu, akaenda naye katika Kaunti ya Siaya kisha akafululiza na kiongozi wa nchi hadi Kaunti ya Migori. Ni mkutano wa Kaunti ya Homa Bay, siku ya mwisho ya ziara ya Rais mnamo Alhamisi ndiyo alikosa kwa sababu familia ilikuwa ikizindua kamati ya maadhimisho ya mwaka mmoja tangu kifo cha 'Baba' Nairobi. Hadhi ya Raila Jnr ilionekana kuwa juu wakati wa mkutano wa viongozi waliochaguliwa katika eneo la Luo Nyanza mnamo Jumapili kwenye ikulu ya Kisumu. Baada ya wabunge na maseneta kutoka kaunti zote nne kutambulishwa, Kiongozi wa wachache Junet Mohamed alimwalika Raila Jnr ahutubu. Hii inaweza kufasiriwa kuwa huenda alipewa hadhi ya juu kwa kuwa baada ya kumaliza hotuba yake, Bw Mohamed aliwaalika magavana kisha Rais akapewa nafasi ya kuongea. "Mheshimiwa karibu sana Kisumu na mimi kama kijana wa baba nasema kuwa mlikuwa na ndoto sawa na Raila si kwa eneo la Nyanza pekee bali pia Kenya mzima," akasema Jnr huku akishangiliwa na umati ambao ulisikika ukisema 'wewe ndiye baba aliyebaki'. "Watu wetu kile ningependa kuwaambia ni kwamba Baba alituambia tukae pamoja na tufanye hivyo kwa kusalia ndani ya ODM," akaongeza akiwa ameandamana na shangazi yake Tabby Osewe. Mnamo Jumatatu, Jnr aliandamana na Rais Ruto katika kufungua miradi mbalimbali katika Kaunti ya Kisumu ikiwemo barabara ya Chiga-Rabuor na miradi mingine katika eneobunge la Muhoroni. Familia ya Baba yaunga Ruto Mnamo Jumanne, Junior aliandamana na Rais katika kutathmini na kuzindua miradi mbalimbali ikiwemo daraja la Dho Goye, kukagua uwanja wa Jaramogi mjini Siaya miongoni mwa miradi mingine. "Mheshimiwa Rais nakukaribisha hapa Siaya na nina kuku ambaye Mama Ida amenipa nikupee. Hapa sisi tunakuunga mkono kupitia chama cha ODM na kama familia ya baba tuko nawe hadi 2027," akasema. "Huku ni nyumbani, mimi na ami yangu Dkt Oburu Oginga tunakuunga. Kama watu wa Siaya endelea kutuhudumia na miradi ijae huku kwa sababu tuko nawe hadi mwisho," akasema baada ya kualikwa na Rais. Ziara ya Migori nayo ilionekana kusisimua zaidi kwa sababu Jnr alishangiliwa huku akisema ana ndoto ya kisiasa ya babake ambayo lazima ayatimize. "Mimi pia ni Raila na baba aliacha chama kikubwa na si cha wazee pekee bali watu wote. Kwa sasa tuko ndani ya Serikali Jumuishi na hata eneo letu pia nalo lazima liendelee," akasema akiwa Migori. Kwenye mahojiano na Taifa Leo baada ya ziara hiyo ya Nyanza, Jnr alisema kuwa analenga kutia bidii katika siasa na kujitafutia umaarufu badala ya kutumia jina la familia. "Siwezi kuketi tu kwa sababu mimi ni mwana wa Raila, lazima pia nionyeshe juhudi na kujifunza kutoka kwa wanasiasa wazoefu ambao watanishika mkono. Mimi pia sasa ni mwanasiasa," akasema akisisitiza kuwa pia ataendeleza kampeni yake katika eneobunge la Kibra. Analenga kumbandua mbunge wa sasa Peter Orero ambaye alikuwa mwandani wa marehemu babake na anahudumu muhula wake wa kwanza. Aliyekuwa mbunge Imran Okoth pia anasaka kiti hicho Jnr, 46, akiingia bungeni mwaka ujao, atakuwa anafanya hivyo kwa umri sawa na alivyofanya babake mnamo 1992. Marehemu Raila alichaguliwa mbunge wa Langata kupitia Ford Kenya huku babake akiwahi nafasi kama hiyo kule Bondo. Kwa mujibu wa mchanganuzi wa masuala ya kisiasa Javas Bigambo, ni wazi Rais Ruto ameamua kumshika Jnr mkono na kumtambisha baada ya dadake Winnie kutoonekana kujihusisha sana na masuala ya uongozi. "Winnie ni mbunge wa EALA na hata mwanzoni alionekana kujihusisha sana kisiasa kuliko Jnr. Hata hivyo, Jnr ameonyesha wazi yuko tayari kushikwa mikono na kufanya kazi na Rais,'' akasema Bigambo "Baada ya kuidhinishwa na Mama Ida awanie kiti cha ubunge wa Kibra, inaonekana ameamua kujitosa mzimamzima katika siasa na kupigania nafasi yake. Yupo pazuri kuwa mrithi wa siasa za ufalme wa Jaramogi," akaongeza.
read moreRight Column Content