T

taifaleo.nation.co.ke

@taifaleo Wed, 26 Aug 2026 11:25:55

MAONI: Kiti cha Mwakilishi wa Kike kimeongeza sauti ya wanawake bungeni?

NAFASI ya Mwakilishi wa Wanawake katika Bunge la Kitaifa iliundwa kuongeza sauti za wanawake katika chombo cha kutunga sheria. Lakini nafasi hii inapokuwa kiti cha kudumu cha mwanasiasa mmoja, tunapaswa kujiuliza ikiwa bado inatimiza dhima yake pana. Mwanamke anapopewa nafasi ya kuingia Bungeni kupitia kaunti, anapata uzoefu, mwonekano na mtaji wa kisiasa. Kwa nini asitumie jukwaa hilo kuwavisha wengine viatu na kuingia katika ushindani wa kawaida wa ubunge? Hapa ndipo uamuzi wa Esther Muthoni Passaris wa kutetea tena kiti cha Nairobi unapozua mjadala. Passaris alikuwa amedokeza nia ya kuwania ubunge wa Makadara. Lakini sasa anaonekana kurudi kwenye kiti anachokalia. Hakuna kosa la kisheria kwa yeye kufanya hivyo. Lakini kisiasa, jambo hili linahitaji kutafakariwa. Millie Odhiambo, Martha Wangari na Beatrice Elachi kwa mfano walitumia nafasi za uwakilishi wa wanawake kama jukwaa la kujijenga, kabla ya kuhamia katika maeneo bunge ya kawaida. Walipoondoka, nafasi hiyo iliweza kumpa mwanamke mwingine fursa ya kuingia Bungeni. Tatizo si Passaris pekee. Tatizo ni mfumo wa fikra. Ikiwa kila Mbunge wa Kike wa Kaunti ataona nafasi hiyo kama kiti cha kutetea milele, nafasi hiyo itageuka kuwa mwisho wa safari badala ya kuwa daraja. Usawa wa kijinsia hautafikiwa kwa kuhesabu wanawake wale wale kila baada ya uchaguzi. Utahitaji wanawake wapya kuingia, kukua kisiasa na kuchukua nafasi katika maeneo bunge ya kawaida. Mwandishi ni msomi na mtafiti wa taaluma za Kiswahili

read more
T

taifaleo.nation.co.ke

@taifaleo Wed, 26 Aug 2026 10:32:28

Benki ya KCB yadai kuna njama ya kuilaghai Sh146 bilioni

BENKI ya KCB imepiga ripoti kwa DCI ikitaka ichunguze kampuni ya Foxcapital inayodai ilituma Sh146 bilioni kwenye akaunti yake kutoka ng'ambo kuhusiana na uwekezaji wa dhamana za serikali. Benki hiyo inadai kwamba stakabadhi zilizowasilishwa na kampuni hiyo kortini kudai fedha hizo ni ghushi na inataka DCI kubaini ni nani aliziandaa, kusambaza na kuziwasilisha kortini. Mzozo unahusisha €978,675,835 (Sh146.3 billion), ambazo Foxcapital inasema ilituma kwa akaunti yao ya KCB Oktoba mwaka jana kama malipo kwa kampuni ya Uingereza, Bay Bionics Ltd, iliyotambuliwa zamani kama BB Biotech AG Limited. Foxcapital iliwasilisha kesi mapema mwezi huu ikidai kwamba KCB ilipokea fedha hizo za kigeni lakini ikakosa kuziweka kwenye akaunti yake, na kufanya Mahakama Kuu kubana hela hizo ikisubiri iamuliwe iwapo benki hiyo kweli ilipokea pesa hizo na kukataa kuzipeana kwa kampuni husika. Katika kilio chake kwa DCI kitengo cha Ulaghai wa Benki, KCB Group, kupitia Afisa Mkuu Mtendaji Paul Russo anatilia shaka stakabadhi zilizotumiwa na Foxcapital kudai pesa hizo. Stakabadhi zinajumuisha arafa za SWIFT, ripoti ya tukio ya Aprili 17, barua ya Mei 18 ya kuangazia kosa la kiuchumi na utathmini wa kiufundi wa Julai 1. KCB inasema stakabadhi zinazodaiwa kutoka UBS Switzerland AG na maafisa wa KCB sio halisi. Kulingana na malalamishi hayo, KCB iliandikia UBS Agosti 13, 2026 ikitaka thibitisho la stakabadhi na malipo. KCB inasema UBS ilijibu ikisema stakabadhi na maagizo ya malipo "hayajatoka kwa UBS Switzerland AG na kwa hivyo sio halali." KCB inasema inatilia shaka stakabadhi hizo baada ya kupata kwamba hakuna mtiririko wa malipo kama hayo kutoka kwenye mitambo yao. "Ikichukuliwa kwa pamoja, kukosekama kwa malipo hayo kwenye mitambo yetu, UBS Switzerland AG kukana stakabadhi na kiapo cha Ushahidi kutoka kwa maafisa wa KCB pamoja na stakabadhi za kutiliwa shaka kunaipa KCB kuamini kwamba kuna njama ya kuilaghai Sh146 bilioni inayoendeshwa na Foxcapital," KCB inasema.

read more
T

taifaleo.nation.co.ke

@taifaleo Wed, 26 Aug 2026 10:01:06

Home Boys ndio mabingwa ligi ya 'Weka Panga chini'

KLABU ya Home Boys FC kutoka mtaa wa Gadeni ndiyo iliyotawazwa bingwa wa michuano ya ligi ya 'Weka Panga Chini' kisiwani Lamu. Hii ni baada ya kuilaza timu ya Real Madrid kutoka mtaa wa Wiyoni magoli 2-1 kwenye fainali kali iliyochezewa katika uwanja wa Twaifu mjini Lamu Jumapili. Ligi hiyo maalum ya mpira wa miguu ilishirikisha klabu 16 za Lamu za vijana wa chini ya miaka 18. Ilizinduliwa mapema Agosti, dhamira kuu ikiwa ni kukabiliana na uhalifu wa mapanga na dawa za kulevya miongoni mwa vijana eneo hilo. Wafadhili wakuu ni Idara ya Usalama kupitia kitengo cha Polisi wa Watalii (TPU), Bodi ya Utalii ya Lamu (LTA), Shirikisho la Kandanda Nchini (FKF) na serikali ya kaunti ya Lamu. Fainali ilishuhudia idadi kubwa ya mashabiki waliofika kushangilia timu zao. Mshindi wa kwanza (Home Boys FC) alituzwa Sh30,000 pesa taslimu, kikombe na jezi ilhali wa pili (Real Madrid FC) ikituzwa Sh20,000 na jezi. Nambari tatu iliendea klabu ya Lamu Boys FC kutoka mtaa wa Langoni kisiwani Lamu, hivyo kupokea kitita cha Sh10,000 na jezi. Mechi ya fainali ilihudhuriwa na kamanda wa polisi wa watalii (TPU) ukanda wa Pwani, Bw David Kabiru, aliyekariri wito wa vijana wa Lamu, Pwani na Kenya kwa jumla kuhubiri amani, kujiepusha na makundi ya uhalifu na dawa za kulevya. "Nimefurahia kushuhudia soka tamu hapa kisiwani Lamu. Mfahamu kwamba mshindi si klabu ya Home Boys pekee eti kwa sababu imeshinda fainali. Wote walioshiriki ligi hii ni washindi. Ninaambiwa karibu vijana 270 wameshirikishwa kwenye michuano hii. Nyote mjue ni washindi na tuendelee kushirikiana kudumisha Amani," akasema Bw Kabiru. Mwenyekiti wa LTA, Bi Fridah Njeri aliahidi ushirikiano wake na wadau wengine ili kuona kwamba ligi nyingine sawia inaanzishwa kufikia Disemba mwaka huu. "Tutahakikisha kila msimu wa likizo tunazindua ligi maalum ya soka ili tuwashughulishe vijana wetu na kuwaepusha na majanga, hasa mihadarati," akasema Bi Njeri. Naibu wa LTA, Bw Jamil Mbarak ambaye pia alihudhuria fainali ya ligi hiyo uwanjani Twaifu aliwashauri vijana kujiepusha na mizozo na hasira. "Hasira hazijawahi kusuluhisha mambo. Tujifunze kudhibiti hasira zetu. Tujiepusha na mizozo na badala yake tupendane na kuhubiri amani ili Lamu iendelee kuwa kivutio bora cha watalii," akasema Bw Mbarak. Katibu wa kamati andalizi, ambaye pia ni Mwakilishi wa Vijana katika FKF, Lamu, Bw Athman Farid, maarufu Pirezi, aliwapongeza wanasoka wote walioshiriki ligi hiyo kwa kudumisha nidhamu kipindi chote cha wiki tatu ambapo ligi imekuwa ikiendelea. Kwenye ligi hiyo, kiungo Mohamed Ali kutoka klabu ya Lamu Boys FC ndiye aliyetawazwa mfungaji bora akiwa na magoli 7 ilhali kipa bora akawa ni Mohamed Farid kutoka Real Madrid FC. Mchezaji aliyeibuka bora na mwenye nidhamu zaidi ni Abdallah Abdulmalik kutoka Real Madrid FC ilhali mchezaji aliyetawazwa kuwa mwenye kipaji cha kutegemewa ni Daniel Chome kutoka timu ya Dragon Junior FC. Wote walituzwa pesa taslimu na vyeti vya kutambua juhudi zao.

read more