T

taifaleo.nation.co.ke

@taifaleo Wed, 08 Jul 2026 10:12:38

Chama cha Uanahabari chawasha taa ya vipaji Kairi Boys

CHAMA cha Uanahabari katika Shule ya Upili ya Kairi Boys, Gatundu Kaskazini, Kaunti ya Kiambu, kinaendelea kuwa chombo muhimu cha kuwakuza wanafunzi kitaaluma na kitalanta huku kikiwafungulia milango katika fani zinazohusiana na lugha na mawasiliano. Pamoja na kukuza vipaji vya wanafunzi katika sanaa hizo anuwai, chama hicho pia kinawapa msukumo wa kujitosa katika ualimu, tafsiri, upigaji picha na uhariri wa vitabu, video na filamu. Isitoshe, kinalenga kuimarisha umilisi wa Kiswahili na Kiingereza ili kuwajenga wanafunzi wenye uwezo wa kujieleza kwa ufasaha kimazungumzo na kimaandishi. [caption id="attachment_189899" align="alignnone" width="2560"] Baadhi ya walimu wa Shule ya Upili ya Kairi Boys iliyoko Gatundu Kakazini, Kaunti ya Kiambu, walipojumuika kwa picha ya pamoja.[/caption] Wanachama hukutana baada ya vipindi vya masomo mchana kutwa ili kujadili mikakati ya kuendeleza chama na kukipa nguvu zaidi. Aidha, chama kinatarajia kuanzisha kitengo cha uigizaji na kuzindua jarida rasmi la shule mwaka ujao, hatua itakayowapa wanafunzi jukwaa maridhawa la kuonyesha ubunifu wao katika uandishi na sanaa nyinginezo. Mafanikio ya chama tayari yanaonekana. Wanafunzi wanaoshiriki shughuli zake kikamilifu wamekuwa wakifaulu vyema katika mitihani ya Kiswahili na Kiingereza huku wakionyesha kujiamini zaidi katika mawasiliano na shughuli tofauti za shule. Mlezi wa chama, Bi Doreen Kathurima, anaungama kuwa chama hicho kimechangia pakubwa maendeleo ya wanafunzi na kimekuwa chanzo cha mabadiliko muhimu shuleni. "Mbali na kupiga jeki shughuli za Idara ya Lugha, chama hiki kinakuza maadili na kuboresha matokeo ya KCSE. Pia tumeshuhudia maendeleo makubwa katika ulumbi, utunzi wa mashairi na utangazaji wa habari miongoni mwa wanachama," anaeleza. [caption id="attachment_189900" align="alignnone" width="2560"] Wanafunzi wa Shule ya Upili ya Kairi Boys wakifuatilia kwa makini matukio na mawasilisho mbalimbali wakati wa hafla ya kielimu waliyoiandaa. PICHA ZOTE | RICHARD MAOSI[/caption] Mwalimu Mkuu, Bw Anthony Mwaria, anakiri kuwa chama hicho kinawaandaa wanafunzi kwa ajili ya maisha ya baadaye. "Chama hiki ni jukwaa linaloamsha hamu ya wanafunzi kujitosa katika ulingo wa uanahabari na taaluma nyingine zinazofungamana na lugha. Vilevile kinawalea na kuwakuza ipasavyo ili wawe watafiti na waandishi wabunifu wenye uwezo wa kushindana kimataifa," anasema. Kwa upande wake, Mkuu wa Idara ya Ushauri Nasaha, Bi Norah Biyaki, anasisitiza kuwa nidhamu na kujituma kwa wanafunzi ni msingi wa mafanikio ya chama. "Tunawahimiza wanafunzi kuwa na ari ya kujifunza, nidhamu ya hali ya juu na moyo wa kujituma ili waweze kufaidika kikamilifu na fursa tofauti zinazotolewa na chama hiki," akasema Bi Biyaki katika kauli inayotiliwa mkazo na Naibu Mwalimu Mkuu, Bw Michael Ngari. Kupitia shughuli zake, Chama cha Uanahabari shuleni Kairi Boys kinaendelea kuwajenga wanafunzi kuwa wataalamu, viongozi na wasanii wa kesho.

read more
T

taifaleo.nation.co.ke

@taifaleo Wed, 08 Jul 2026 10:30:12

Misri wafokea Fifa kwa 'ukora' katika mechi dhidi yao na Argentina

KOCHA wa Misri Hossam Hassan amesema hana nia ya kutazama mechi zilizosalia za Kombe la Dunia akisema refa alichangia timu hiyo kubanduliwa na Argentina mnamo Jumanne usiku. Katika mechi nyingine, Uswizi walibandua Colombia 4-3 kupitia mikwaju ya penalti na kufuzu robo fainali. Timu hizo zilikuwa zimeagana sare tasa muda wa kawaida na ule wa ziada kabla ya kuamuliwa na mikwaju ya penalti. Sasa Argentina na Uswizi zitachuana katika robo fainali wikendi hii huku Misri na Colombia zikiaga kombe. Misri walikuwa wakiongoza 2-0 zikiwa zimesalia dakika 11 mechi iishe katika raundi ya 16 dhidi ya Argentina. Kwa masikitiko walifungwa mabao matatu na ikabidi waage mashindano hayo ya hadhi ya soka. [caption id="attachment_189904" align="alignnone" width="2560"] Mshambuliaji nyota wa Argentina Lionel Messi ashangilia kufunga bao la kusawazisha dhidi ya Misri katika mechi ya 16-bora uga wa Atlanta, jimbo la Georgia, Amerika, Julai 7, 2026. Argentina ilishinda mechi 3-2. Picha|Reuters[/caption] Mkongwe Lionel Messi aling'ara katika mechi hiyo na kutumia uweledi wake kuhakikisha Argentina inatinga robo fainali. Hassan alilalamika kuwa walionewa na hana nia ya kutazama mechi zilizosalia za kombe la dunia. "Naenda nyumbani na sitatazama mechi hizo kwa sababu kilichotutendekea si haki. Tulistahili kupewa penalti, bao letu lilikataliwa na sijui kwa nini lilikataliwa," akasema akionekana mwenye hasira. Egypt walifunga bao dakika ya 62 kupitia Mostafa Zico lakini VAR iliangalia na kutambua kuwa kulikuwa na mpira wa ikabu kwa Argentina kuelekea kufungwa kwa bao hilo. Pia Misri walilia kwamba walistahili kupewa penalti baada ya Hamdy Fathy kuangushwa ndani ya kijisanduku. Hasira yao ilipanda kwa kuwa baada ya tukio hilo kwa kuwa Argentina waliendelea kucheza na kufunga bao dakika ya 92 kupitia Messi. "Mimi huwa sipendi kushindwa na kama kupoteza kwangu kumechangiwa na refa jinsi ilivyofanyika hivi leo, nawaambia tu mashabiki wetu wasikasirike. Tulicheza vizuri sana na kushindwa kwetu kumechangiwa na refa," akaongeza. Hassan alisema alifurahi kuwa wachezaji wake walifuata mwongozo wake mchezoni na waliwalemea Argentina. Misri wamekuwa wakitumia mbinu ya kulinda ngome yao mchezoni lakini dhidi ya Argentina walikuwa wakivamia hasa kupitia mipira mirefu na pia pembeni. Pia mnyakaji wao Mostafa Shoubir alionyesha uweledi wa juu baada ya kuokoa mikwaju hatari ya Argentina. "Najivunia sana wachezaji wangu kwa sababu wengi wao wanacheza kwenye Ligi Kuu ya Misri nao wapinzani wetu walikuwa na wachezaji wanaoshiriki ligi za kifahari za Ulaya," akaongeza. Colombia nao watajilaumu wenyewe baada ya nyota wa Bayern Luis Diaz na wenzake kukosa nafasi kadhaa za kufunga na kumaliza mchezo mapema. Kipa wa Uswizi Gregor Kobela aliokoa penalti ya Cucho Hernandez baada ya ile ya Davinso Sanchez kugonga mtambapanya kwa Columbia. Manuel Akanji pia alikosa penalti kwa upande wa Uswisi.

read more
T

taifaleo.nation.co.ke

@taifaleo Wed, 08 Jul 2026 08:58:01

Jinsi ya kulima maparachichi ya masoko ya ng'ambo  

KILIMO cha maparachichi kimekuwa miongoni mwa biashara zenye faida kubwa nchini Kenya kutokana na kuongezeka kwa mahitaji ya matunda hayo katika masoko ya ndani na nje ya nchi. Masoko ya kimataifa, yaani ng'ambo, yamekuwa yenye mvuto mkubwa kwa maparachichi, maarufu kama avokado. Bara Uropa, nchi za Milki ya Kiarabu (UAE) na Asia ndio wanunuzi wakuu wa avokado za Kenya. Ili kupata mavuno bora, mkulima anapaswa kuanza kwa kuchagua miche bora iliyothibitishwa kutoka kwa vitalu vinavyoaminika, anashauri Daniel Mwenda, mtaalamu. "Aina maarufu zinazopendekezwa ni Hass na Fuerte kutokana na ubora wa matunda na soko lake," Mwenda anasema. Maparachichi hustawi katika maeneo yenye mvua ya wastani hadi nyingi, udongo wenye rutuba na usiotuamisha maji. Kabla ya kupanda, Mwenda anasema hatua ya kwanza ni kuandaa shimo lenye ukubwa wa karibu sentimita 60 kwa 60 na kuchanganya udongo wa juu na samadi 'iliyooza' vizuri. "Miche ipandwe kwa nafasi ya mita saba hadi nane kati ya mti na mti ili kutoa nafasi ya ukuaji," anashauri mtaalamu huyo. [caption id="attachment_189894" align="aligncenter" width="300"] Maparachichi ya John Mburu, mkulima kutoka Gatundu Kusini, Kaunti ya Kiambu yakipimwa uzani. Picha|Sammy Waweru[/caption] Miaka ya mwanzo, ni muhimu kumwagilia miche maji hasa wakati wa kiangazi, kuweka nyasi za matandazo (mulching) ili kuhifadhi unyevuunyevu na kupunguza magugu, pamoja na kuondoa matawi yaliyokauka au kuathirika na magonjwa. John Mburu ni mkulima wa avokado Gatundu Kusini, Kaunti ya Kiambu na anasema amekumbatia matumizi ya mbolea asili na fatalaiza. "Mahitaji ya mbolea kwenye udongo, mkulima anapaswa kushirikisha mtaalamu ili upimwe kwenye maabara kujua virutubisho vinavyohitajika," mkulima huyo anasema. Wakulima wanapaswa pia kufuatilia wadudu na magonjwa, na kukabiliana na athari hizo kwa mujibu wa vigezo na dawa zilizoidhinishwa kwa minajili ya mazao yanayouzwa nje ya nchi. "Matumizi ya mbinu bora za usimamizi wa mazao, ikiwemo usafi wa shamba na ushauri wa maafisa wa nyanjani, husaidia kupunguza hasara," mtaalamu Mwenda anahimiza. [caption id="attachment_189895" align="aligncenter" width="300"] Mfanyakazi katika kampuni ya Soko Fresh, Thika akikagua avokado zinazooshwa ili kuuzwa nje ya Kenya. Picha|Sammy Waweru[/caption] Mparachichi huanza kuzaa baada ya miaka miwili hadi mine – hilo likitegemea aina ya mche na usimamizi wa shamba. Matunda yanapaswa kuvunwa kwa uangalifu kwa kutumia vifaa vinavyofaa ili kuepuka majeraha yanayoweza kupunguza ubora wake. Kwa wakulima wanaolenga soko la nje, ni muhimu kufuata viwango vya ubora kama GlobalG.A.P., kuhakikisha matunda yanachambuliwa vizuri na kuhifadhiwa katika mazingira yanayodumisha ubora wake.

read more