T

taifaleo.nation.co.ke

@taifaleo Wed, 08 Jul 2026 11:18:55

Wakazi Mbeere walia kuondolewa transfoma 'baada ya kura'

WAKAZI wa eneo bunge la Mbeere North, Kaunti ya Embu, wamelalamikia kuondolewa kwa transfoma za umeme miezi minane tu baada ya serikali kuwaunganishia umeme kupitia mpango wa Last Mile Connectivity na Stima Mashinani. Wakazi hao wanasema walipata umeme kwa mara ya kwanza wakati wa uchaguzi mdogo wa Novemba 27, 2025, lakini sasa wanahofia kurejea gizani baada ya Kampuni ya Kusambaza Stima Kenya (KPLC) kuanza kuondoa transfoma bila maelezo ya kina. Faith Kithaka wa kijiji cha Muramba asema maafisa wa KPLC waliondoa transfoma katika eneo lao wiki mbili zilizopita na hawajairejesha. Wakazi wanasema kuondolewa kwa transfoma hizo kumekatiza shughuli zao za kila siku na kuwarudisha katika maisha ya kutumia mishumaa na taa za mafuta. "Tuliishi gizani kwa miaka mingi. Serikali ilituunganishia umeme wakati wa uchaguzi mdogo, lakini kabla hatujafaidika kikamilifu, transfoma zimeondolewa," alisema Bi Kithaka. Katika kijiji cha Njarange, hali ilikuwa sawa huku wakazi wakishuhudia maafisa wa KPLC wakiondoa transfoma nyingine. Julius Njeru wa kijiji cha Rwanjeru alisema kukosekana kwa umeme kumeathiri biashara na masomo ya watoto. "Biashara zimeathirika na watoto hawawezi kusoma usiku kwa sababu stima zimekatika," alisema. Baadhi ya wakazi walikumbuka jinsi viongozi wa serikali na wanasiasa wa chama cha UDA walivyozunguka eneo hilo wakati wa uchaguzi mdogo wakiahidi maendeleo iwapo wangemuunga mkono mgombea wa chama hicho. "Tuliwapigia kura na tukaletewa umeme. Sasa miezi michache baadaye wanaondoa transfoma. Hii si haki," alisema mkazi mmoja. Wengine walidai kuwa transfoma hizo zinapelekwa Ol Kalou, ambako kutafanyika uchaguzi mdogo Julai 16, ili kuvutia wapigakura. Wakazi walitishia kuandamana iwapo vifaa hivyo havitarejeshwa haraka. Hata hivyo, Mbunge wa Mbeere North, Leo Wamuthende, alipuuza madai hayo akisema baadhi ya watu wanapotosha umma kwa maslahi ya kisiasa. "Nimeona taarifa zinazodai serikali inaondoa transfoma katika Mbeere North. Madai hayo si ya kweli na yanalenga kupotosha wananchi," alisema. Alifafanua kuwa KPLC inaendesha mpango wa kawaida wa kukarabati transfoma, hasa zile za zamani, ili kuboresha uthabiti wa huduma ya umeme. Meneja wa KPLC Kaunti ya Embu Vincent Okello, pia alikanusha madai kuwa transfoma hizo zinapelekwa Ol Kalou kwa sababu za kisiasa. Alisema kampuni hiyo "haijihusishi na siasa" na kueleza kuwa baadhi ya transfoma ziliharibiwa na wahalifu huku nyingine zikiharibika kutokana na hitilafu za kiufundi. "Katika Mbeere North na Runyenjes, transfoma tatu ziliharibiwa na ziliondolewa kupelekwa Nairobi kutengenezwa," alisema. Hata hivyo, baadhi ya wakazi walitilia shaka maelezo hayo wakisema baadhi ya transfoma zilizoondolewa ni mpya na hazikuwa na hitilafu zozote. "Transfoma hazikuharibiwa wala kuvurugwa. Tunataka tuambiwe ukweli kuhusu zilikopelekwa," alisema mkazi mwingine.

read more
T

taifaleo.nation.co.ke

@taifaleo Wed, 08 Jul 2026 10:12:38

Chama cha Uanahabari chawasha taa ya vipaji Kairi Boys

CHAMA cha Uanahabari katika Shule ya Upili ya Kairi Boys, Gatundu Kaskazini, Kaunti ya Kiambu, kinaendelea kuwa chombo muhimu cha kuwakuza wanafunzi kitaaluma na kitalanta huku kikiwafungulia milango katika fani zinazohusiana na lugha na mawasiliano. Pamoja na kukuza vipaji vya wanafunzi katika sanaa hizo anuwai, chama hicho pia kinawapa msukumo wa kujitosa katika ualimu, tafsiri, upigaji picha na uhariri wa vitabu, video na filamu. Isitoshe, kinalenga kuimarisha umilisi wa Kiswahili na Kiingereza ili kuwajenga wanafunzi wenye uwezo wa kujieleza kwa ufasaha kimazungumzo na kimaandishi. [caption id="attachment_189899" align="alignnone" width="2560"] Baadhi ya walimu wa Shule ya Upili ya Kairi Boys iliyoko Gatundu Kakazini, Kaunti ya Kiambu, walipojumuika kwa picha ya pamoja.[/caption] Wanachama hukutana baada ya vipindi vya masomo mchana kutwa ili kujadili mikakati ya kuendeleza chama na kukipa nguvu zaidi. Aidha, chama kinatarajia kuanzisha kitengo cha uigizaji na kuzindua jarida rasmi la shule mwaka ujao, hatua itakayowapa wanafunzi jukwaa maridhawa la kuonyesha ubunifu wao katika uandishi na sanaa nyinginezo. Mafanikio ya chama tayari yanaonekana. Wanafunzi wanaoshiriki shughuli zake kikamilifu wamekuwa wakifaulu vyema katika mitihani ya Kiswahili na Kiingereza huku wakionyesha kujiamini zaidi katika mawasiliano na shughuli tofauti za shule. Mlezi wa chama, Bi Doreen Kathurima, anaungama kuwa chama hicho kimechangia pakubwa maendeleo ya wanafunzi na kimekuwa chanzo cha mabadiliko muhimu shuleni. "Mbali na kupiga jeki shughuli za Idara ya Lugha, chama hiki kinakuza maadili na kuboresha matokeo ya KCSE. Pia tumeshuhudia maendeleo makubwa katika ulumbi, utunzi wa mashairi na utangazaji wa habari miongoni mwa wanachama," anaeleza. [caption id="attachment_189900" align="alignnone" width="2560"] Wanafunzi wa Shule ya Upili ya Kairi Boys wakifuatilia kwa makini matukio na mawasilisho mbalimbali wakati wa hafla ya kielimu waliyoiandaa. PICHA ZOTE | RICHARD MAOSI[/caption] Mwalimu Mkuu, Bw Anthony Mwaria, anakiri kuwa chama hicho kinawaandaa wanafunzi kwa ajili ya maisha ya baadaye. "Chama hiki ni jukwaa linaloamsha hamu ya wanafunzi kujitosa katika ulingo wa uanahabari na taaluma nyingine zinazofungamana na lugha. Vilevile kinawalea na kuwakuza ipasavyo ili wawe watafiti na waandishi wabunifu wenye uwezo wa kushindana kimataifa," anasema. Kwa upande wake, Mkuu wa Idara ya Ushauri Nasaha, Bi Norah Biyaki, anasisitiza kuwa nidhamu na kujituma kwa wanafunzi ni msingi wa mafanikio ya chama. "Tunawahimiza wanafunzi kuwa na ari ya kujifunza, nidhamu ya hali ya juu na moyo wa kujituma ili waweze kufaidika kikamilifu na fursa tofauti zinazotolewa na chama hiki," akasema Bi Biyaki katika kauli inayotiliwa mkazo na Naibu Mwalimu Mkuu, Bw Michael Ngari. Kupitia shughuli zake, Chama cha Uanahabari shuleni Kairi Boys kinaendelea kuwajenga wanafunzi kuwa wataalamu, viongozi na wasanii wa kesho.

read more
T

taifaleo.nation.co.ke

@taifaleo Wed, 08 Jul 2026 10:30:12

Misri wafokea Fifa kwa 'ukora' katika mechi dhidi yao na Argentina

KOCHA wa Misri Hossam Hassan amesema hana nia ya kutazama mechi zilizosalia za Kombe la Dunia akisema refa alichangia timu hiyo kubanduliwa na Argentina mnamo Jumanne usiku. Katika mechi nyingine, Uswizi walibandua Colombia 4-3 kupitia mikwaju ya penalti na kufuzu robo fainali. Timu hizo zilikuwa zimeagana sare tasa muda wa kawaida na ule wa ziada kabla ya kuamuliwa na mikwaju ya penalti. Sasa Argentina na Uswizi zitachuana katika robo fainali wikendi hii huku Misri na Colombia zikiaga kombe. Misri walikuwa wakiongoza 2-0 zikiwa zimesalia dakika 11 mechi iishe katika raundi ya 16 dhidi ya Argentina. Kwa masikitiko walifungwa mabao matatu na ikabidi waage mashindano hayo ya hadhi ya soka. [caption id="attachment_189904" align="alignnone" width="2560"] Mshambuliaji nyota wa Argentina Lionel Messi ashangilia kufunga bao la kusawazisha dhidi ya Misri katika mechi ya 16-bora uga wa Atlanta, jimbo la Georgia, Amerika, Julai 7, 2026. Argentina ilishinda mechi 3-2. Picha|Reuters[/caption] Mkongwe Lionel Messi aling'ara katika mechi hiyo na kutumia uweledi wake kuhakikisha Argentina inatinga robo fainali. Hassan alilalamika kuwa walionewa na hana nia ya kutazama mechi zilizosalia za kombe la dunia. "Naenda nyumbani na sitatazama mechi hizo kwa sababu kilichotutendekea si haki. Tulistahili kupewa penalti, bao letu lilikataliwa na sijui kwa nini lilikataliwa," akasema akionekana mwenye hasira. Egypt walifunga bao dakika ya 62 kupitia Mostafa Zico lakini VAR iliangalia na kutambua kuwa kulikuwa na mpira wa ikabu kwa Argentina kuelekea kufungwa kwa bao hilo. Pia Misri walilia kwamba walistahili kupewa penalti baada ya Hamdy Fathy kuangushwa ndani ya kijisanduku. Hasira yao ilipanda kwa kuwa baada ya tukio hilo kwa kuwa Argentina waliendelea kucheza na kufunga bao dakika ya 92 kupitia Messi. "Mimi huwa sipendi kushindwa na kama kupoteza kwangu kumechangiwa na refa jinsi ilivyofanyika hivi leo, nawaambia tu mashabiki wetu wasikasirike. Tulicheza vizuri sana na kushindwa kwetu kumechangiwa na refa," akaongeza. Hassan alisema alifurahi kuwa wachezaji wake walifuata mwongozo wake mchezoni na waliwalemea Argentina. Misri wamekuwa wakitumia mbinu ya kulinda ngome yao mchezoni lakini dhidi ya Argentina walikuwa wakivamia hasa kupitia mipira mirefu na pia pembeni. Pia mnyakaji wao Mostafa Shoubir alionyesha uweledi wa juu baada ya kuokoa mikwaju hatari ya Argentina. "Najivunia sana wachezaji wangu kwa sababu wengi wao wanacheza kwenye Ligi Kuu ya Misri nao wapinzani wetu walikuwa na wachezaji wanaoshiriki ligi za kifahari za Ulaya," akaongeza. Colombia nao watajilaumu wenyewe baada ya nyota wa Bayern Luis Diaz na wenzake kukosa nafasi kadhaa za kufunga na kumaliza mchezo mapema. Kipa wa Uswizi Gregor Kobela aliokoa penalti ya Cucho Hernandez baada ya ile ya Davinso Sanchez kugonga mtambapanya kwa Columbia. Manuel Akanji pia alikosa penalti kwa upande wa Uswisi.

read more