T

taifaleo.nation.co.ke

@taifaleo Mon, 24 Aug 2026 03:55:41

Uhuru: Ruto au kiongozi yeyote hafai kujilazimisha kwa Wakenya

RAIS Mstaafu Uhuru Kenyatta na Rais William Ruto wameendeleza mvutano wao wa kisiasa huku wakitofautiana kuhusu uchaguzi wa 2027, nafasi ya upinzani na maendeleo ya serikali. Akizungumza Jumapili katika maadhimisho ya miaka 23 ya kifo cha aliyekuwa Makamu wa Rais Michael Kijana Wamalwa, Milimani, Trans Nzoia, Bw Kenyatta alisema hana nia ya kurejea mamlakani baada ya kuhudumu kama rais kwa miaka 10. Alisema Wakenya ndio wataamua atakayekuwa rais 2027 na hakuna kiongozi anayepaswa kuwalazimisha kumuunga mkono. "Wakenya wataamua wanayemtaka kuwa Rais 2027. Hakuna mtu atakayewalazimisha kumuunga mkono upande wake. Tutafute kura kwa amani na uadilifu," akasema. Bw Kenyatta pia alitetea uhuru wa kisiasa na haki ya viongozi wa upinzani kufanya mikutano ya kisiasa, akilaani vurugu zilizotokea Homa Bay wakati wa mikutano ya viongozi wa Linda Mwananchi. Aliwataja Kalonzo Musyoka, Fred Matiang'i, Edwin Sifuna na Rais Ruto kama baadhi ya viongozi ambao Wakenya wanaweza kuchagua kati yao katika uchaguzi ujao. Viongozi wa upinzani waliohudhuria hafla hiyo, akiwemo Bw Musyoka, Dkt Matiang'i, Martha Karua, Charity Ngilu na Justin Muturi, walisema wako tayari kuunda muungano wenye nguvu wa kumng'oa Ruto madarakani. Bw Musyoka alisema upinzani unafanya mipango ya kuunda muungano utakaomfanya Ruto kuwa rais wa muhula mmoja. Kwa upande wake, Dkt Ruto aliwashutumu viongozi wa upinzani kwa kutumwa kupinga miradi yote ya serikali badala ya kutoa sera mbadala. Alisema wapinzani wanapiga kelele kuhusu "must go", "one term" na "Kasongo", lakini hawana ajenda ya maendeleo. Rais alisema serikali yake inapaswa kuhukumiwa kwa miradi na huduma inazowaletea Wakenya, badala ya misingi ya ukabila. Akiongea katika Kaunti ya Taita Taveta, Rais Ruto alisema serikali imetenga Sh10 bilioni kushughulikia changamoto za ardhi na kuwaondoa maskwota Pwani.  Pia alitaja ukarabati wa reli ya Voi-Taveta yenye urefu wa kilomita 129 kama mradi unaolenga kukuza biashara, utalii na ajira.  Kule Kitale, Bw Kenyatta alimsifu marehemu Bw Wamalwa kama kiongozi mzalendo aliyependa maslahi ya taifa kuliko siasa za chuki. Aliyekuwa waziri Musikari Kombo alisema Bw Wamalwa alikuwa kiongozi mwadilifu aliyekufa bila utajiri wa kutatanisha. Aliyekuwa waziri Noah Wekesa alijitolea kuongoza jopo litakalosaidia upinzani kuunda muungano wa pamoja, akisema bila mgombea mmoja itakuwa vigumu kumshinda Ruto 2027.

read more
T

taifaleo.nation.co.ke

@taifaleo Mon, 24 Aug 2026 12:06:42

WALIOBOBEA: Burudi Nabwera alivuma kisiasa wakati wa Kanu

BURUDI Nabwera alikuwa miongoni mwa wanasiasa wasomi zaidi waliohitimu kutoka taasisi mashuhuri za Uingereza wakati wa ukoloni. Elimu hiyo ilimwezesha kuelewa mifumo ya ubepari wa Magharibi na ujamaa wa Mashariki, maarifa yaliyomsaidia katika siasa na diplomasia baada ya Kenya kupata uhuru. Baada ya uhuru, Rais wa kwanza wa Kenya, Jomo Kenyatta, alimteua kuwa balozi nchini Amerika. Chini ya Rais Daniel arap Moi, Nabwera alipanda kutoka kuwa Katibu Mkuu wa KANU hadi kuwa Waziri katika Ofisi ya Rais, moja ya nyadhifa zenye ushawishi mkubwa serikalini. Alizaliwa mwaka 1924 na kusomea Maseno School, Chuo Kikuu cha Makerere nchini Uganda na London School of Economics. Akiwa Maseno, alikutana na Jaramogi Oginga Odinga, ambaye baadaye alikuwa Makamu wa Kwanza wa Rais wa Kenya. Wengine waliosoma hapo ni Masinde Muliro na Wycliffe Wasia Awori, ambao baadaye walikuwa miongoni mwa wabunge wa kwanza wa Kenya katika Baraza la Kutunga Sheria (Legco). Akiwa Makerere, Nabwera alikutana na wasomi kama Bethwel Ogot, Thomas Odhiambo, Josephat Karanja, aliyewahi kuwa Makamu wa Rais chini ya Moi, pamoja na mshairi wa Uganda Henry Muwanga Barlow, mwandishi wa shairi maarufu Building the Nation. Katika kitabu chake How it Happened, Nabwera alisema watu hao walimhimiza na kumsaidia kujenga taaluma yake ya baadaye. Katika uchaguzi wa kwanza wa kitaifa baada ya enzi ya Kenyatta mwaka 1979, Nabwera alishindwa na Joshua Angatia katika kiti cha ubunge cha Lurambi North. Wakati wa utawala wa Kenyatta, alikuwa mwanasiasa mwenye ushawishi na Waziri Msaidizi wa Mashauri ya Kigeni. Moi alitaka kuwatumia wanasiasa wakongwe pamoja na rafiki yake Moses Mudavadi kukabiliana na siasa kali za Martin Shikuku, Lawrence Sifuna na Waziri Elijah Mwangale, ambaye rais hakumwamini. Baada ya Mwanasheria Mkuu Charles Njonjo kuporomoka kisiasa kufuatia uchunguzi kuhusu madai ya "uhaini", Moi alianza kupanga upya KANU. Alimteua David Okiki Amayo kuwa mwenyekiti na Nabwera kuwa Katibu Mkuu wa tatu wa chama hicho. Katika kipindi hicho, Nabwera alijenga sifa ya kuwa mwanasiasa mkali, akitangaza sera za chama na kutishia wanachama waliokiuka maagizo kwa hatua za kinidhamu au kutimuliwa. Alipata umaarufu mkubwa mwaka 1986 baada ya kuonekana kwenye runinga ya taifa, Voice of Kenya (VoK), na kutangaza kwamba KANU ilikuwa tayari kuwasamehe wanasiasa waliofahamika kama "watu wa Njonjo". Kauli hiyo ilizua hasira ndani ya KANU kwa sababu wakati huo ilikuwa mwiko kufikiria kuwasamehe wanasiasa waliokuwa wamehusishwa na Njonjo. Moi alikuwa amemshutumu Njonjo kwa kupanga njama na nchi ya kigeni kuangusha serikali. Rais alianzisha tume ya uchunguzi iliyoongozwa na Jaji Cecil Miller, ambayo hatimaye ilimsafisha Njonjo. Hata hivyo, wanasiasa kadhaa waliodaiwa kuwa washirika wake walikuwa tayari wameanguka kisiasa. Kauli ya Nabwera ilipewa uzito mkubwa na vyombo vya habari, lakini ndani ya Ikulu na miongoni mwa viongozi wakuu wa KANU haikupokelewa vyema. Baadhi yao walimshutumu kwa kuwa mfuasi wa Njonjo. Muda mfupi baadaye, aliondolewa kama Katibu Mkuu na nafasi hiyo ikachukuliwa na Mudavadi. Akiwa Waziri wa Nchi katika Ofisi ya Rais, Nabwera alikuwa na ushawishi mkubwa kuliko hata Katibu Mkuu wa KANU. Ofisi yake katika Harambee House ilitembelewa na wafanyabiashara, watu waliokuwa wakitafuta ajira na mabroka wa kisiasa waliotaka apelekee ujumbe wao kwa Rais Moi. Hata hivyo, kosa lake kubwa lilikuwa kushindwa kutofautisha masuala ya serikali na chama. Ushindi wake wa moja kwa moja katika eneo bunge la Lugari katika uchaguzi wa 1988 wa mlolongo, ulimfanya aamini zaidi nguvu za KANU. Katika uchaguzi wa 1992, alishindwa na Apili Wawire wa FORD-Asili. Kabla ya kuondoka Bungeni, Nabwera alihamishiwa Wizara ya Habari ambako aliendelea kutetea KANU. Alifanya mabadiliko katika taasisi za habari akilenga kuhakikisha zinaunga mkono chama hicho kabla ya uchaguzi wa vyama vingi wa 1992. Aliondoa Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Utangazaji la Kenya (KBC), zamani VoK, James Kangwana, pamoja na bodi yake kupitia ilani ya serikali na kuwaweka watu alioamini walikuwa waaminifu kwa KANU. Nabwera pia alikosoa Benki ya Dunia kwa masharti yake makali ya misaada kwa Kenya, akipinga hasa pendekezo la kupunguza idadi ya wanafunzi waliojiunga na vyuo vikuu.

read more