T

taifaleo.nation.co.ke

@taifaleo Thu, 19 Nov 2026 07:55:33

Chama cha CHAWAKAMA-KENYA kinavyopeleka Kiswahili jukwaa la kimataifa

CHAMA cha Wanafunzi wa Kiswahili katika Vyuo Vikuu vya Afrika Mashariki (CHAWAKAMA-KENYA) kimezidisha juhudi za kukiendeleza Kiswahili na kukipa nafasi katika ulimwengu wa utandawazi kupitia makongamano yanayowaleta pamoja wanazuo, watafiti na wadau wa lugha hii adhimu. Mbali na kukuza Kiswahili, chama hiki kimekuwa jukwaa muhimu la kuwaunganisha wanafunzi wa vyuo vikuu, kuibua vipaji, kujenga mitandao ya kitaaluma na kuhamasisha ubunifu. Pia, kimechangia kuzalisha viongozi, waandishi, wahariri, watafiti na wakalimani watakaokipeperusha Kiswahili katika majukwaa ya kimataifa. Mwelekeo huo ulidhihirika Novemba 6–7 mwaka huu, wakati CHAWAKAMA-Kenya kilipoandaa kongamano la kikanda katika Chuo Kikuu cha Laikipia, lililoongozwa na kaulimbiu ya 'Kiswahili na Utandawazi'. Kongamano hilo liliwakutanisha wanafunzi kutoka vyuo mbalimbali, vikiwemo Rongo, Laikipia, Masinde Muliro, Kisii, Daystar, Kabianga, Murang'a, Turkana na Kaimosi. Washiriki walijadili nafasi ya Kiswahili katika kuzalisha maarifa, kuwasilisha uvumbuzi na kutatua changamoto za jamii. Kongamano lilifunguliwa rasmi na Prof Guyo Sarr Huka, Naibu Makamu Mkuu wa Chuo Kikuu cha Laikipia anayesimamia masuala ya kitaaluma. Katika tukio hilo, kamati andalizi ikiongozwa na Mwenyekiti Clinton Ageta na mlezi wa chama Prof Sheila Wandera, ilizindua bidhaa zenye nembo ya CHAWAKAMA-Kenya, zikiwemo mashati-tao, chepeo, kalamu, bango na vitabu vilivyoandikwa na wanachama. Ubunifu wa wanachama ulijitokeza pia kupitia Kishazi TV, runinga ya mtandaoni iliyorusha matukio ya kongamano mubashara na kusambaza maudhui yake kupitia mitandao ya kijamii. Kongamano lilipambwa na michango ya wataalamu mashuhuri wa Kiswahili, akiwemo Dkt Moses Wasike (Mgeni Rasmi), Dkt Riro Matinde, Prof James Ontieri, Dkt Nixon Sangili na Dkt Sussy Nandama, miongoni mwa wengine. Mafanikio hayo yalitokana na ushirikiano wa CHAWAKAMA-Kenya, Idara ya Masomo ya Kibinadamu na Maendeleo, uongozi wa Chuo Kikuu cha Laikipia na Chama cha Kiswahili cha Laikipia (CHAKILA). Chama hicho kinaongozwa na Clinton Ageta (Mwenyekiti), Granton Mdogo (Naibu Mwenyekiti), Doreen Mukami (Katibu Mkuu), Griffin Amakala (Naibu Katibu Mkuu), Diana Mirriam (Mhazini), Velma Natang'a (Afisa wa Uhusiano Mwema), Micah Sikolia (Katibu Mtendaji) na Okimba Lester (Afisa Mwenezi). Wahariri ni Luke Shikoli, Kweyu Remjo, Augustine Wekesa, Winjoy Gacheri na Zdame Zuhura, huku Samson Nyamosi na Denis Chumo wakihudumu kama Maafisa wa Nidhamu. Kwa hakika, CHAWAKAMA-Kenya kinaendelea kuthibitisha kuwa mustakabali wa Kiswahili unategemea ubunifu, ushirikiano na juhudi za kizazi kipya.

read more
T

taifaleo.nation.co.ke

@taifaleo Thu, 19 Nov 2026 06:55:00

Korti yaambiwa aliyetoweka alionyesha dalili za ugaidi

MWANAMUME mwenye umri wa miaka 26 aliyetoweka mjini Mombasa mwezi uliopita aliwahi kushtakiwa kwa kosa la kusajili watu kujiunga na kundi la kigaidi, lakini baadaye akaachiliwa huru na mahakama, imebainika. Stakabadhi zilizowasilishwa katika Mahakama Kuu ya Mombasa zinaonyesha kuwa Ismail Yusuf Mohamed alikabiliwa na mashtaka yanayohusiana na ugaidi Januari 2022, miaka minne kabla ya kutoweka kwake. Mohamed alishtakiwa katika kesi ya uhalifu iliyokuwa mbele ya Mahakama ya Hakimu Malindi. Hata hivyo, katika uamuzi uliotolewa Agosti 11, 2023, mahakama ilimuachilia huru baada ya kubaini kuwa upande wa mashtaka haukuthibitisha tuhuma zilizokuwa dhidi yake. Kesi hiyo ya awali imeibuka katika ombi lililowasilishwa na shirika la kutetea haki za binadamu la Vocal Africa, ambalo linaitaka polisi kueleza aliko Mohamed aliyetoweka kwake Oktoba 31 mwaka huu. Katika hati ya kiapo iliyowasilishwa mahakamani, mkurugenzi mkuu wa shirika hilo, Bw Hussein Khalid, alisema Mohamed aliondoka nyumbani kwao eneo la Bondeni, Mombasa, kwenda kununua chakula cha jioni lakini hakurejea. Kwa mujibu wa hati hiyo, Mohamed alitekwa nyara mwendo wa saa tano usiku nje ya mgahawa wa Bondeni Carmel's Joint, kando ya Barabara ya Abdel Nasser, na watu waliokuwa wakimfuatilia kwa gari aina ya pickup. Ombi hilo linadai kuwa, video za kamera za CCTV zinaonyesha wanaume hao wakishuka kwenye gari hilo, kumkamata Mohamed na kumwingiza kwa nguvu katika gari jeupe aina ya Toyota Land Cruiser kabla ya kuondoka naye. "Mahali alipo Mohamed na hali yake ya maisha hazijulikani, na pia hapatikani kwa simu yake ya mkononi," alisema Bw Khalid katika hati ya kiapo. Shirika hilo linasema familia ya Mohamed iliripoti kutoweka kwake katika Kituo cha Polisi cha Mombasa Central, chini ya nambari ya OB 67/31/10/2026, lakini polisi hawajawafahamisha aliko wala hatua walizochukua katika uchunguzi. Aidha, juhudi za familia kumtafuta katika vituo mbalimbali vya polisi katika Kaunti ya Mombasa hazijazaa matunda. Vocal Africa iliomba mahakama kumwamuru Inspekta Jenerali wa Polisi Douglas Kanja kumfikisha Mohamed mahakamani, akiwa hai au mfu, mbali na kueleza aliko. Pia imeomba mahakama iwaite Bw Kanja, Mkurugenzi wa Idara ya Upelelezi wa Jinai (DCI) Mohamed Amin na Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Ujasusi la Kitaifa (NIS) Noordin Haji kueleza kuhusu kutoweka kwake. "Utekaji na kutoweka kwa mtu bila kujulikana aliko ni mojawapo ya ukiukaji mkubwa zaidi wa haki ya mtu kuwa huru unaotambuliwa chini ya sheria za kimataifa," anasema Bw Khalid. Shirika hilo linasisitiza kuwa kila mtu ana haki ya kusikilizwa kwa haki na kufanyiwa taratibu za kisheria, bila kujali kosa analotuhumiwa kutenda. Katika maagizo yaliyotolewa Novemba 17, Mahakama Kuu ilithibitisha kuwa ombi hilo lina dharura na kuwaamuru washtakiwa kuwasilisha majibu yao kufikia Novemba 18. Mahakama pia ilimwamuru Inspekta Mkuu wa polisi kuhakikisha Mohamed anafikishwa mbele ya Mahakama Kuu au Mahakamani Novemba 19 saa nne asubuhi. Inspekta Mkuu na DCI pia waliamriwa kuhifadhi na kuwasilisha rekodi za kamera za CCTV, mifumo ya kufuatilia magari, mawasiliano ya simu za mkononi, taarifa za mipakani, rekodi za vituo vya kulipia ushuru barabarani na taarifa za mfumo wa kutambua nambari za usajili wa magari, zinazohusiana na kutoweka kwa Mohamed kuanzia Oktoba 30, 2026.

read more