T

taifaleo.nation.co.ke

@taifaleo Wed, 21 Oct 2026 08:55:27

Mishale ya Serikali kwa Sifuna yaongezeka

SENETA wa Nairobi, Edwin Sifuna amekuwa mlengwa wa matamshi makali kutoka kwa viongozi wa serikali ya Kenya Kwanza, huku akizidisha juhudi za kujijenga kisiasa kuelekea kwenye uchaguzi mkuu wa mwaka wa 2027. Baada ya Rais William Ruto, Mkuu wa Mawaziri Musalia Mudavadi ndiye wa hivi punde kumkosoa Sifuna, akitilia shaka uwezo wa vuguvugu lake la Linda Mwananchi kuongoza taifa. "Wapo wanaokuja na chama ambacho hakijamaliza hata miezi sita, wakidai ndicho kitakachotoa dira. Tusikubali aina hiyo ya pata-potea ya kisiasa," alisema Bw Mudavadi. Akizungumza katika kanisa la ACK, Jimbo la Kapsabet, Nandi, Jumapili, Bw Mudavadi alisema, "Wanaofikiria kuwa wanaweza kupandishwa juu kwa parachuti na kupewa uongozi nchini Kenya, ninawaambia kuwa parachuti hiyo itakatika wakiwa angani," akaonya. Kauli hiyo ilijiri siku chache baada ya Rais Ruto kumshambulia Bw Sifuna na washirika wake wa kisiasa. Dkt Ruto amedai Seneta Sifuna na chama chake (The Equitable Party) kuwa hawana mwelekeo, huku akikejeli juhudi zao za kuchangisha fedha kutoka kwa wananchi. "Mwenyewe hana kitu, chama chake hakina kitu. Halafu anaanza kuwaomba kina mama shilingi kumi kumi. Chama hicho kimekwama kwenye baa," alisema Rais Ruto. Ingawa Rais amekuwa akiwakosoa pia viongozi wengine wa upinzani, wakiwemo Kalonzo Musyoka, Fred Matiang'i, Rigathi Gachagua na rais mstaafu Uhuru Kenyatta, mashambulizi dhidi ya Bw Sifuna yamejitokeza kwa uwazi zaidi katika siku za hivi karibuni. Bw Sifuna, ambaye aliwahi kuwa katibu mkuu wa chama cha ODM, sasa anajaribu kupanua ushawishi wake nje ya chama hicho huku akipigia debe Linda Mwananchi kuwa vuguvugu la kisiasa linalolenga kuleta mabadiliko katika uongozi wa nchi. Akizungumza katika ibada ya Jumapili katika kanisa la Jesus Teaching Ministry, Donholm, Nairobi, Sifuna alijibu wakosoaji wake kwa kusema kuwa uongozi haupaswi kuamuliwa na umri, utajiri au muda ambao mtu amekuwa katika siasa. "Tutaingia katika nyumba zenu, tutaingia katika maeneo yote ya taifa hili, na kijana ambaye amechaguliwa kwa muhula mmoja pekee kama seneta ataweka historia ya kuwa rais katika taifa hili la Kenya," alisema Bw Sifuna. Aliongeza kuwa Wakenya hawapaswi kufungwa na dhana kuwa ni lazima mtu awe na umri fulani au kiwango fulani cha utajiri ili aweze kuwa rais. "Watu wamezoea kuwa siasa za Kenya lazima ziendeshwe kwa njia fulani: lazima uwe na umri fulani, lazima uwe na pesa kiasi fulani," alisema. Aliwataka wafuasi wake kueneza ujumbe wa Linda Mwananchi kote nchini, akieleza kuwa vuguvugu hilo linaweza kuongoza taifa licha ya kuwa limekuwepo kwa muda mfupi. "Rais William Ruto, utaelewa manifesto yetu tu. Ulituambia tukupeleke pole pole, tutakupeleka pole pole lazima kitaeleweka!" alisema Bw Sifuna. Mwanachama wa Linda Mwananchi, Brian Weke pia alimjibu Rais Ruto kwa kugeuza kejeli ya "kutokuwa na kitu" kuwa hoja kuhusu kile anachodai kuwa msimamo wa kiongozi wao dhidi ya ufisadi na dhuluma. "Sifuna ni 'Bw Kutokuwa na Kitu.' Hana ufisadi, hana wizi wa mashamba, hajapiga vijana wetu risasi wala kuwanyanyasa Wakenya," alisema Bw Weke. Katika mjadala huo, mchambuzi wa masuala ya kisiasa, Prof Tom Namwamba anatathmini kuwa Bw Sifuna anajitokeza kuwa mshindani wa wanasiasa wa muda mrefu, hasa katika eneo la Magharibi mwa Kenya. Kwa mujibu wa Prof Namwamba, kukosa uzoefu mkubwa wa uongozi wa kitaifa si kikwazo kinachomzuia mtu kuwa rais, kwa kuwa uamuzi wa mwisho hufanywa na wapigakura. Alitolea mfano wa rais wa zamani wa Amerika, Barack Obama, aliyehudumu kama seneta wa jimbo la Illinois na baadaye kuchaguliwa kuwa rais mwaka wa 2008. "Ni wananchi wanaochagua. Wakimchagua Sifuna, wakosoaji wake ni nani kupinga uamuzi huo?" alisema Prof Namwamba. Hata hivyo, mfano huo hauondoi changamoto zinazowakabili wanasiasa wanaotaka kujenga uungwaji mkono wa kitaifa, ikiwemo kuunda kikosi, kuimarisha miundo ya chama na kuweka sera zinazoweza kuvutia wapigakura katika maeneo mbalimbali ya nchi. Umaarufu wa Seneta wa Nairobi pia umejitokeza katika tafiti za maoni ya wananchi kuhusu uchaguzi wa urais wa 2027. Utafiti wa Infotrak wa Julai 2026 ulimweka Rais Ruto mbele kwa asilimia 32, akifuatwa na kiongozi wa Wiper Kalonzo Musyoka kwa asilimia 13. Seneta Sifuna na aliyekuwa Waziri wa Usalama Fred Matiang'i walishika nafasi moja kwa asilimia 12 kila mmoja. Kwa upande mwingine, utafiti wa Trends and Insights for Africa (TIFA) uliofanywa Juni 2026 ulimpa Rais Ruto asilimia 24 ya uungwaji mkono kitaifa, huku Bw Sifuna akipata asilimia 15. Utafiti huo pia ulionyesha kuwa asilimia 44 ya wafuasi wa ODM waliohojiwa walimtaja Bw Sifuna kuwa chaguo lao la kugombea urais kwa tiketi ya chama hicho, ikilinganishwa na asilimia 20 waliomtaja Rais Ruto. Kulingana na Prof Namwamba, matokeo hayo yanaonyesha Bw Sifuna ana uungwaji unaostahili kutiliwa mkazo katika mjadala wa kisiasa, ingawa kura za maoni pekee haziwezi kuamua matokeo ya uchaguzi. Changamoto yake ni kugeuza uungwaji huo kuwa mtandao wa kisiasa unaovuka mipaka ya Nairobi na ngome za jadi za ODM, huku akijenga chama chenye uwezo wa kushindana katika maeneo mbalimbali ya nchi. Kadiri uchaguzi wa 2027 unavyokaribia, mvutano kati ya Sifuna na viongozi wa Kenya Kwanza unaendeleza mjadala kuhusu nafasi ya wanasiasa wapya, uzoefu wa uongozi na uwezo wa kujenga uungwaji mkono wa kitaifa katika siasa za Kenya.

read more
T

taifaleo.nation.co.ke

@taifaleo Wed, 21 Oct 2026 07:55:41

Mwanawe Mackenzie asema ameridhishwa na hukumu

MWANA wa mhubiri tata  Paul Nthenge Mackenzie, Dan Mackenzie, ameeleza kuridhika kwake na hukumu iliyotolewa dhidi ya baba yake ya kupatikana na hatia ya kuua watoto 190 katika msitu wa Shakahola kati ya Januari 2021 na Septemba 2023. Dan alisema hana sababu ya kuhuzunika kwa sababu ya mtu ambaye mafundisho yake yalimfanya aache shule akiwa Darasa la Saba na kujitafutia riziki kwa kuendesha bodaboda. Kijana huyo mwenye umri wa miaka 24, alisema hukumu hiyo imewaletea faraja familia zilizopoteza wapendwa wao katika mkasa huo, akisisitiza kwamba yeye mwenyewe alikuwa miongoni mwa walioathiriwa na mafundisho ya babake alipokuwa mtoto. "Ni faraja kwetu na kwa waathiriwa waliopoteza wapendwa wao Shakahola. Haki imetendeka. Ilikuwa kipindi kigumu kwetu na kwa waathiriwa. Sasa tumepata faraja na tunasubiri hukumu ya adhabu," alisema. Dan, ambaye amejitenga na mafundisho ya kidini ya babake, alisema hakuhuzunishwa na uamuzi wa Jaji Diana Kavedza kwa sababu hakushiriki katika uhalifu huo. "Sihuzuniki kwamba babangu amepatikana na hatia. Niko sawa na nimetulia kwa sababu sikuhusika. Ana hatia," alisema katika Mahakama Kuu ya Mombasa, ambako Mackenzie na washtakiwa wenzake 28 walipatikana na hatia katika mashtaka yote 191 ya mauaji. Hukumu hiyo ilimkumbusha Dan masaibu aliyopitia utotoni alipolazimishwa kufunga akiwa na umri wa miaka 12. Kukataa kwake kufunga kulizidisha uhasama kati yake na babake, na hatimaye akalazimika kuacha shule akiwa Darasa la Saba. Baadaye alianza kuendesha bodaboda mjini Malindi, kazi anayoendelea kufanya hadi sasa. "Tulianza kufunga nilipokuwa na umri wa miaka 12. Nilikataa. Babangu alinikatia tamaa na kuniambia nijitegemee. Hivyo ndivyo nilivyoishia kuendesha bodaboda mjini Malindi," alisema. Dan pia alisimulia jinsi waumini wa kanisa hilo walivyompiga kwa karibu saa tatu kwa kukataa kuhudhuria ibada. Alimtaja Smart Mwakalama, naibu wa Mackenzie, kuwa miongoni mwa waliohusika. "Nimeathiriwa na mambo ambayo babangu amekuwa akifanya huko Shakahola. Ndiyo maana sikuishia msituni, kwa sababu nilikuwa nimechoshwa naye. Nililazimishwa kufunga kwa wiki moja nilipokuwa na umri wa miaka 12. Waumini hao, akiwemo Smart Mwakalama, walinipiga kwa karibu saa tatu ili tu nihudhurie ibada," alisema. Mwakalama, mwanzilishi mwenza wa kanisa la Good News International Ministries (GNI), alielezwa kuwa mratibu muhimu wa usafirishaji wa wafuasi kutoka tawi la Furunzi mjini Malindi hadi msitu wa Shakahola. Dan alisema alitambua uzito wa yaliyokuwa yakitendeka Shakahola baada ya babake kukamatwa Aprili 2023 na kesi kuanza kusikilizwa mahakamani. "Hapo ndipo nilipogundua kwamba mambo aliyokuwa akitufanyia utotoni ndiyo aliyokuwa akifanya msituni," alisema. Pia alifurahia kuokolewa kwa ndugu zake watano, dada watatu na wavulana wawili, waliokuwa wakiishi na nyanya yao katika nyumba ya familia eneo la Furunzi tangu Mackenzie alipokamatwa. Dan alisema aliripoti hali yao kwa polisi, hatua iliyosababisha msako na kuokolewa kwao. "Natumai sasa watakuwa na maisha mazuri," alisema. Wakati wa ziara ya Mahakama Kuu nyumbani kwa Mackenzie mwezi Juni, Dan aliambia mahakama kwamba ndugu zake walikuwa wamezama katika mafundisho ya babake na kwamba misimamo mikali ya kidini ilikuwa imekita mizizi katika familia. Alitoa ushahidi huo katika kesi nyingine inayohusiana na mkasa huo, ambapo Mackenzie na wengine wanakabiliwa na mashtaka ya mauaji kama uhalifu dhidi ya binadamu kuhusiana na vifo vya watu 53 katika kijiji cha Kwa Bi Nzaro. Licha ya matendo ya babake, Dan alisema majirani zake wanaelewa kwamba hakuhusika na uhalifu huo.

read more