T

taifaleo.nation.co.ke

@taifaleo Fri, 21 Aug 2026 03:55:22

Mapanga 500 na silaha zingine zilisambaziwa wahuni Homa Bay, polisi wafichua

TAKRIBAN vijana 500 walilipwa kuziba barabara kuwazuia wafuasi wa Linda Mwananchi kuingia Homa Bay wakati wa mkutano wao Jumapili iliyopita, huku polisi wakifichua kuwa mapanga 500 na silaha nyingine zilisambazwa kabla ya ghasia hizo. Ripoti ya kijasusi iliyotayarishwa baada ya polisi kunasa silaha hizo imeibua wasiwasi kuhusu kiwango cha maandalizi yaliyofanyika kabla ya mkutano wa Agosti 16. Kamanda wa Upelelezi wa Jinai (DCI) wa Kaunti ya Homa Bay Jimmy Kisobo alisema polisi wanaendelea kuchunguza matukio yote yaliyotokea kabla, wakati na baada ya mkutano huo. Alisema baadhi ya silaha zilisambazwa angalau siku moja kabla ya mkutano huo. "Baadhi ya vijana si waaminifu kwa waliowafadhili kuzua vurugu. Wengine walioshiriki mapigano walishirikiana na maafisa na kutueleza idadi ya silaha zilizotolewa," alisema Bw Kisobo. Kulingana na polisi, uchunguzi umebaini kuwa hadi vijana 500 walihusika katika vurugu zilizotokea katika maeneo mbalimbali wafuasi wa Linda Mwananchi walipokuwa wakielekea Homa Bay. Polisi pia wanachunguza matamshi ya baadhi ya viongozi wa Orange Democratic Movement (ODM) waliokuwa wameapa kumzuia Gavana wa Siaya James Orengo na Seneta wa Nairobi Edwin Sifuna kuingia Homa Bay. Wakati huo huo, polisi walisema wafuasi wa Linda Mwananchi walikuwa wamechochea vijana kukabiliana na upinzani wowote ambao wangekutana nao njiani. Maafisa wa usalama waliweka vizuizi kadhaa barabarani na kukagua magari yaliyokuwa yakielekea Homa Bay kabla ya mkutano huo. Operesheni hiyo ilisababisha polisi kunasa silaha na kuwakamata baadhi ya washukiwa. Wakati wa mkutano huo, vijana wenye silaha kutoka pande mbili walikabiliana huku wanasiasa wakielekea katika maeneo mbalimbali ya mikutano. Polisi walisema matukio kadhaa ya uhalifu yaliripotiwa kabla ya mkutano huo na baada ya wafuasi wa Linda Mwananchi kuondoka Homa Bay. Maafisa katika eneo hilo walisema baadhi ya vijana wameanza kujitambulisha na wanasiasa fulani na mara nyingi hutoa ulinzi kwa viongozi wanaowaunga mkono wakati wa mikutano ya kisiasa. Polisi walionya kuwa makundi kama hayo yanaweza kuhusika katika vurugu joto la kisiasa linapopanda. Bw Kisobo pia alisema polisi wanamtafuta Khassim Abdi, ambaye amehusishwa na ghasia hizo na ambaye hakutii agizo la kujisalimisha. Msemaji wa Huduma ya Kitaifa ya Polisi Muchiri Nyaga alisema Abdi aliamriwa kuripoti katika makao makuu ya DCI katika kaunti baada ya vurugu hizo. Hata hivyo, kufikia Alhamisi hakuwa ametii wito huo, hali iliyosababisha mahakama kutoa kibali cha kukamatwa kwake. Polisi pia wanachunguza uvamizi katika biashara mjini Homa Bay kabla ya mikutano hiyo. Miongoni mwa zilizolengwa ni Homa Bay Tourist Hotel, ambako mali ya thamani ya zaidi ya Sh300 milioni iliharibiwa. Washambuliaji waliingia hotelini wateja wakila na kuwalaumu kwa kutounga mkono serikali ya sasa. Bw Kisobo alisema mtu aliyelengwa katika tukio hilo ni mwanasiasa anayewania kiti cha ubunge. "Mwanasiasa huyo alijaribu kueleza kuwa anaunga mkono serikali na alikuwa ameonyesha nia ya kuwania kwa tiketi ya UDA. Lakini Abdi, ambaye pia anadai kuunga mkono tutam, hakutaka kusikia maelezo hayo," alisema. Mwanasiasa huyo, ambaye ana leseni ya kumiliki bunduki, alidaiwa kutoa bastola yake na kufyatua risasi hewani ili kuwatawanya vijana hao na kuzuia uharibifu zaidi. Gavana wa Homa Bay Gladys Wanga, hata hivyo, alikanusha kuhusishwa na ghasia hizo. "Hakuna tukio hata moja ambapo nimehusishwa na vurugu au ghasia katika kampeni zangu. Hatujawahi kufanya hivyo na hatuwezi kuanza sasa," alisema. Alisema hayo akitoa pole kwa familia ya Noreen Nalangwa, raia wa Uganda aliyefariki Jumapili baada ya kugongwa na gari lililokuwa likienda kwa kasi wakati wa vurugu zilizohusishwa na mkutano wa Linda Mwananchi. Gavana huyo aliwataka vijana na wanasiasa waliotembelea eneo hilo kujizuia na kuepuka uchochezi. Ghasia hizo zilisababisha vifo vya watu wawili na uharibifu wa mali, ikiwemo hoteli ya Homa Bay Tourist na ofisi za kanisa la Seventh Day Adventist (SDA). Raia, polisi na wanahabari kadhaa walijeruhiwa, huku biashara katika baadhi ya maeneo ya Homa Bay Town zikifungwa kutokana na ghasia.

read more
T

taifaleo.nation.co.ke

@taifaleo Fri, 21 Aug 2026 02:55:42

Gachagua aapa kutembea Emurua Dikirr licha ya vitisho

NAIBU Rais Rigathi Gachagua ameapa kutembelea Emurua Dikirr, Narok, leo Ijumaa licha ya vitisho kutoka kwa viongozi wa eneo hilo. Chama chake cha Democracy for Citizens Party (DCP) kimesema Bw Gachagua atatumia ziara hiyo kuwashukuru wakazi waliounga mkono chama hicho katika uchaguzi mdogo wa ubunge uliofanyika hivi majuzi. Pia, anatarajiwa kuzungumzia masuala ya ardhi na kile anachodai ni kushindwa kwa serikali kulinda haki za wakazi kuhusu ardhi. Mvutano kuhusu ziara hiyo umeongezeka huku viongozi wanaounga mkono serikali na wale wa upinzani wakibadilishana kauli kali. Katika uchaguzi mdogo wa Emurua Dikirr, mgombea wa DCP Vincent Rotich alipata kura 10,760, huku mgombea wa UDA David Keter akishinda kwa kura 18,266. Bw Gachagua amesema kura hizo ni ishara kwamba chama chake kinaanza kupata uungwaji mkono katika eneo linalochukuliwa kuwa ngome ya Rais William Ruto. Nitakuwa Emurua Dikirr Agosti 21 kuzungumza na watu walioniamini na kuunga mkono chama cha DCP licha ya changamoto zote," alisema. Bw Gachagua pia atatembelea familia ya aliyekuwa Mbunge wa Emurua Dikirr Johana Ng'eno katika kijiji cha Mogindo kutoa rambirambi, miezi mitano baada ya kiongozi huyo kufariki katika ajali ya helikopta. Jumatano, Bw Gachagua alizungumza kwa simu na mama wa marehemu, Mama Mary Temas, na kumthibitishia kwamba angemtembelea leo. Pia amesema atatumia ziara hiyo kuzungumzia kifo cha Bw Ng'eno na kucheleweshwa kwa ripoti ya uchunguzi wa ajali hiyo. Ajali hiyo ilitokea Februari 28, 2026 katika kijiji cha Chepkiep, kaunti ya Nandi. Watu sita walifariki. Waliofariki ni Bw Ng'eno, rubani George Were, mpiga picha Nick Kosgei, afisa wa Huduma ya Misitu Kenya Amos Kipngetich Rotich, mwalimu Carlos Robert Kibet Keter na afisa wa itifaki wa Serikali ya Kaunti ya Narok Wycliff Kiprotich Rono. Serikali iliahidi kutoa matokeo ya uchunguzi, lakini ripoti hiyo bado haijatolewa hadharani na Mamlaka ya Usafiri wa Anga Kenya (KCAA). Bw Gachagua na marehemu Ng'eno walikuwa washirika wa karibu kisiasa kabla ya mchakato wa kumuondoa Bw Gachagua kama Naibu Rais kuanza. Wakati huo, Bw Ng'eno alikuwa miongoni mwa wabunge waliosemekana kuwa hawakuunga mkono kwa dhati juhudi za kumtimua Bw Gachagua. Mbunge Keter amemuonya Bw Gachagua kutotembelea Emurua Dikirr, akisema ziara yake inaweza kuvuruga amani. "Nataka kumuonya Bw Gachagua asikanyage Emurua Dikirr kwa sababu hajaribishwi hapa. Aelekeze nguvu zake kwingine kwa kuwa hapa ni eneo la UDA," alisema. Mbunge huyo pia alimlaumu Bw Gachagua kwa kuwakosoa mara kwa mara wanachama wa jamii ya Kalenjin katika mikutano ya kisiasa huku akitafuta uungwaji mkono wao kuelekea uchaguzi wa 2027. Naibu Gavana Koech pia alisema ziara hiyo haitakuwa rahisi. "Imekuwa wazi kwamba Bw Gachagua amejaribu uvumilivu wetu. Hatuwezi tena kukaa kimya. Hawezi kututukana halafu aje katika eneo letu kutafuta uungwaji mkono," alisema. Lakini Bw Gachagua amepuuzilia mbali vitisho hivyo. Amesema amekuwa mwathiriwa wa mashambulizi zaidi ya 25 ambayo amedai yalifanywa na makundi yanayoungwa mkono na serikali pamoja na maafisa wa polisi. "Mpaka sasa nimeshambuliwa zaidi ya mara 25. Hii haijapunguza kasi yangu. Niko tayari kukabiliana na mengi zaidi," alisema akiwa Murang'a. Amesema hakuna vitisho vitakavyomzuia kutembelea Emurua Dikirr. "Wacha watuletee vurugu. Nimepata taarifa kwamba wanapanga kufanya hivyo, lakini hilo halitatuzuia. Tutaendelea na ziara yetu bila woga," alisema. Kiongozi wa Wengi katika Seneti Aaron Cheruiyot na Seneta wa Uasin Gishu Jackson Mandago wamesema Bw Gachagua ana haki ya kutembelea Rift Valley. Bw Cheruiyot alisema jamii ya Kipsigis haiwafukuzi wageni na kwamba Bw Gachagua atakaribishwa kama mwanasiasa mwingine. "Katika utamaduni wetu kama jamii ya Kipsigis, hatuwafukuzi wageni. Tunawakaribisha wafanye shughuli zao na waondoke kwa amani. Tutajitokeza kukusalimia, lakini usifikirie kwamba hiyo itakuletea kura mwaka ujao," alisema. Bw Mandago alisema jamii ya Rift Valley haitakubali kuchochewa kufanya vurugu kwa misingi ya siasa.

read more