T

taifaleo.nation.co.ke

@taifaleo Thu, 20 Aug 2026 03:55:59

Ndoa baridi za magavana na manaibu wao uchaguzi 2027 ukibisha

MAGAVANA kadhaa wanaowania muhula wa pili wanakabiliwa na kibarua kigumu cha kutafuta manaibu wapya baada ya uhusiano wao na waliowasaidia kushinda uchaguzi wa 2022 kuvurugika. Takriban magavana 10 wamejipata katika hali hii huku uchaguzi wa 2027 ukikaribia, na sasa wanatafuta washirika wapya watakaowasaidia kuhifadhi viti vyao. Mzozo wa hivi majuzi kati ya Gavana wa Kericho Erick Mutai na naibu wake Fred Kirui umeongeza orodha ya magavana waliokosana na manaibu wao. Wengine wanaotafuta manaibu wapya ni magavana wa Trans Nzoia George Natembeya, Elgeyo Marakwet Wisley Rotich na Siaya James Orengo. Magavana wa Homa Bay Gladys Wanga, Kisii Simba Arati na Uasin Gishu Jonathan Bii pia wametofautiana na manaibu wao. Gavana wa Machakos Wavinya Ndeti na Abdi Guyo wa Isiolo pia wamewahi kuwa na uhusiano baridi na manaibu wao. Kati ya magavana 29 wanaowania muhula wa pili, ni 19 ambao hawajawahi kuripotiwa kukosana na manaibu wao tangu walipochaguliwa mwaka 2022. Kaunti hizo ni Nairobi, Kakamega, Busia, Migori, Nakuru, Nyamira, Samburu, Turkana, Kiambu, Murang'a, Nyandarua, Makueni, Embu, Meru, Mandera, Taita Taveta, Kilifi, Kwale na Mombasa. Lakini uhusiano mzuri wa sasa haumaanishi kwamba magavana hao wataendelea kuwa na manaibu hao, hasa wakati wanasiasa wanapopanga upya ushirikiano kuelekea 2027. Kikatiba, kila anayewania ugavana anapaswa kumteua mtu wa kuwa mgombea mwenza ambaye huwa naibu gavana. Uhusiano kati ya magavana na manaibu wao umekuwa ukigubikwa na migogoro, maslahi ya binafsi, makubaliano yaliyovunjwa na wakati mwingine kuvumiliana. Huko Kericho, Bw Mutai alitangaza Jumanne kwamba amekata uhusiano wa kisiasa na Bw Kirui, akimlaumu kwa kuhusika katika majaribio mawili ya kumng'atua. Alisema sasa atashirikiana na waziri wa Fedha na Mipango ya Kiuchumi wa kaunti Jackson Rop, ambaye anatoka eneo la Kipkelion Magharibi sawa na Bw Kirui katika uchaguzi wa 2027. Bw Kirui alidai awali kuwa wawili hao walikubaliana kugawana nyadhifa za serikali ya kaunti kwa uwiano wa asilimia 60 kwa 40, lakini mpango huo haukutekelezwa. Bw Mutai alinusurika majaribio mawili ya kumtimua, mwaka 2024 na 2025, baada ya Seneti kuyakataa. Huko Elgeyo Marakwet, uhusiano kati ya Bw Rotich na naibu wake Grace Cheserek pia umeharibika. Mzozo wao uliibuka hadharani hivi majuzi baada ya Bi Cheserek kumkabili gavana wakati wa hafla ya uzinduzi wa Biblia iliyotafsiriwa kwa lugha ya Kimarakwet. Huko Trans Nzoia, Bi Philomena Kapkory amekuwa akizozana na Bw Natembeya tangu 2023, akidai kutengwa katika maamuzi na usimamizi wa serikali ya kaunti. Siaya pia imekumbwa na mzozo kama huo, huku Naibu Gavana William Oduol akidai uhusiano wake na Bw Orengo umedorora kabisa. Na katika kaunti ya Homa Bay, Bw Wanga alimtimua naibu wake Oyugi Magwanga baada ya kumuunga mkono mgombea huru katika uchaguzi mdogo wa Kasipul badala ya mgombea wa ODM. Kisii pia ilishuhudia Naibu Gavana Robert Monda akiondolewa kupitia mchakato wa kumtimua mwaka 2024 baada ya mzozo wa kisiasa na Bw Arati. Na katika kaunti ya Uasin Gishu, Naibu Gavana John Barorot alijiuzulu mwaka 2024 na nafasi hiyo ikachukuliwa na MCA Evans Kapkea. Tangu kuanzishwa kwa serikali za ugatuzi mwaka 2013, ni manaibu gavana 15 pekee ambao wamewahi kubaki na wakubwa wao katika uchaguzi uliofuata. Hii inaonyesha ugumu wa "ndoa" ya kisiasa kati ya magavana na manaibu wao, ambayo mara nyingi huvunjika kabla ya kufika mwisho wa muhula.

read more
T

taifaleo.nation.co.ke

@taifaleo Thu, 20 Aug 2026 04:55:02

Wataalamu waeleza kwa nini kuna baridi kali Nairobi mwezi huu wa Agosti

KWA Wakenya wengi, Agosti umekuwa mwezi wa kuvaa nguo nzito, kujifunika blanketi na baridi kali isiyo ya kawaida asubuhi. Nairobi na maeneo ya nyanda za juu katikati mwa nchi yamekuwa yakishuhudia hali hiyo hadi mchana, jambo linalowafanya wengi kujiuliza ni kwa nini ilhali msimu wa kiangazi unakaribia kufika mwisho. Lakini wataalamu wa masuala ya hali ya hewa wanasema baridi ya Agosti si jambo lisilo la kawaida bali ni sehemu ya mfumo wa kawaida wa msimu unaochangiwa na mabadiliko ya tabianchi katika sehemu ya Kusini mwa Dunia. Mtaalamu wa Hali ya Hewa katika Mamlaka ya Huduma za Hali ya Hewa Kenya (KMSA), Christine Maswi, alisema Agosti ni miongoni mwa miezi yenye baridi zaidi nchini. "Kwa kawaida, Agosti huhesabiwa kuwa mwezi wa baridi kwa sababu uko katika msimu wa baridi nchini, wakati upepo kutoka kusini-mashariki huleta hewa baridi na yenye unyevunyevu kutoka Bahari Hindi," alisema. Kulingana naye, hali ya hewa ya muda mrefu huchunguzwa kwa kutumia takwimu zilizokusanywa kwa angalau miaka 30 ili kubaini hali inayochukuliwa kuwa ya kawaida katika eneo fulani na msimu fulani. Chanzo cha baridi hiyo kinaanzia maelfu ya kilomita kusini mwa Kenya, ambako kwa sasa ni majira ya baridi. Joto linaposhuka katika sehemu hiyo, mifumo huimarika. Mifumo hiyo huathiri upepo kuelekea kaskazini na kuleta hewa baridi Afrika Mashariki. Mifumo miwili muhimu ni St Helena High, iliyoko upande wa kusini-magharibi mwa bara la Afrika katika Bahari ya Atlantic na Mascarene High, iliyoko upande wa kusini-mashariki wa bara hilo, karibu na Madagascar. Mifumo hiyo huwa muhimu zaidi wakati wa majira ya baridi katika sehemu ya Kusini ma Dunia. Kwa hivyo, mifumo hiyo inapokuwa na nguvu, husaidia kusukuma hewa baridi kuelekea Kenya. "Kadiri mifumo hii inavyoimarika, husukuma hewa baridi kutoka kusini. Ndiyo maana Nairobi, nyanda za juu katikati mwa nchi na sehemu za mashariki mwa Kenya zinaweza kuwa na baridi kali hasa Juni, Julai na Agosti," Bi Maswi alisema. Maeneo yanayoathirika ni pamoja na Machakos, Makueni, Kitui na Taita Taveta, ambako wakazi hupata asubuhi zenye baridi na wakati mwingine hali hiyo huendelea kwa siku nzima. Mchakato huo pia unahusishwa na mahali ilipo Ikweta. Hewa yenye joto karibu na Ikweta hupanda, na hivyo kutoa nafasi kwa hewa baridi kutoka kusini kuingia. Hata hivyo, nguvu za mifumo hiyo hubadilika kutoka siku moja hadi nyingine. Hilo ndilo linalofanya hali ya hewa ya Agosti kuwa isiyotabirika wakati mwingine. "Siku moja inaweza kuanza kwa baridi kali kabla joto mchana, huku siku inayofuata ikiwa na mawingu na baridi siku nzima," alisema. Utabiri wa KMSA wa Juni, Julai na Agosti ulionyesha kuwa maeneo ya nyanda za juu mashariki mwa Bonde la Ufa, yakiwemo Nairobi na sehemu za nyanda za chini kusini-mashariki, yangeshuhudia hali ya baridi na mawingu hadi nusu ya kwanza ya Septemba. Hata hivyo, utabiri mpana wa nchi ulionyesha uwezekano wa joto kuwa juu ya wastani.

read more
T

taifaleo.nation.co.ke

@taifaleo Thu, 20 Aug 2026 02:55:58

Ndimi za moto za wanasiasa zaanza kuwaka na kuzua hofu ya chuki, ukabila na ghasia

KENYA inaelekea Uchaguzi Mkuu wa 2027 huku ndimi za moto za wanasiasa zikianza kuwaka, hali inayozua hofu ya kuibuka kwa siasa za chuki, ukabila na ghasia. Tume ya Kitaifa ya Uwiano na Utangamano (NCIC) imeanza kuchunguza matamshi ya viongozi mbalimbali ambayo inasema yanaweza kuchochea migawanyiko ya kikabila, ghasia au kuvuruga amani nchini. Miongoni mwa viongozi walioangaziwa na tume hiyo ni aliyekuwa Naibu Rais Rigathi Gachagua, ambaye ameagizwa kufika mbele ya NCIC Agosti 27 kuelezea kuhusu matamshi aliyotoa katika mikutano ya kisiasa kaunti za Vihiga, Kisii na Meru. Bw Gachagua, ambaye sasa anaongoza chama cha Democracy for Citizens Party (DCP), atahojiwa kuhusu muktadha, nia na athari zinazoweza kusababishwa na kauli hizo. NCIC imesema matamshi hayo yanaweza kuwa ya ubaguzi au ya kuchochea. Tume imeambatanisha agizo hilo na nakala za matamshi inayochunguza. Afisa Mkuu Mtendaji wa NCIC Daniel Giti ameonya kuwa iwapo Bw Gachagua hatafika mbele ya tume, huenda akakamatwa na kuwasilishwa mbele ya tume. Uchunguzi huo unafanyika huku wanasiasa wakizidisha kampeni za mapema kuelekea uchaguzi wa 2027, mikutano ya kisiasa ikigeuka kuwa majukwaa ya mashambulizi makali dhidi ya wapinzani. Katika tukio moja linalochunguzwa, Bw Gachagua anadaiwa kutoa matamshi katika mkutano Luanda, Vihiga, Juni 12 ambayo tume inasema yanaweza kuchochea mgawanyiko wa kikabila. Pia anahojiwa kuhusu kauli alizotoa katika Uwanja wa Gusii, Kisii, Februari 23, ikiwemo zilizomhusu Mbunge wa Nyaribari Chache Zaheer Jhanda. Ziara yake ya Meru mwishoni mwa Julai pia inamlikwa na NCIC baada ya tume kusema baadhi ya matamshi aliyotoa yanaweza kuchukuliwa kuwa ya kuchochea vurugu na kulenga jamii fulani. Lakini Bw Gachagua si mwanasiasa pekee anayechunguzwa. Gavana wa Busia Paul Otuoma pia ameitwa na NCIC kujibu madai ya kuchochea hisia dhidi ya wafanyabiashara kutoka maeneo mengine ya nchi katika mkutano wa hadhara huko Bulanda Junction mnamo au karibu na Juni 27. Mbunge wa Homa Bay Town Peter Kaluma anakabiliwa na uchunguzi kama huo kuhusu matamshi aliyotoa kabla ya mkutano wa Linda Mwananchi uliofanyika Homa Bay Agosti 16. Bw Kaluma aliitwa kufika mbele ya tume Jumatano. Wanasiasa wengine wanaochunguzwa ni Waziri wa Afya Aden Duale, Waziri wa Utumishi wa Umma Geoffrey Ruku, Mbunge wa Mukurwe-ini John Kaguchia, Mbunge wa Sirisia John Waluke na Naibu Gavana wa Mandera Ali Mohamud. NCIC ilitangaza Julai 28 kuwa imeanza kuchunguza matamshi yaliyohusishwa na baadhi ya viongozi hao, akiwemo Bw Duale, Bw Ruku, Bw Otuoma na Bw Waluke. Wengine ni Mbunge wa Kipipiri Wanjiku Muhia na Mbunge wa Nakuru Town East David Gikaria. Mwenyekiti wa NCIC Kepha Omae alisema mazingira ya kisiasa nchini yanaendelea kuwa makali huku matamshi ya uchochezi, vitisho na siasa za kikabila yakizidi. "Tunaona mazingira ya kisiasa yanayozidi kuwa makali ambapo matamshi ya uchochezi, kulenga jamii fulani, vitisho na kuwachochea vijana vikiwa jambo la kawaida," alisema. Hata hivyo, alisema NCIC haiwezi kukimbilia kufikisha kesi kwa Mkurugenzi wa Mashtaka ya Umma (DPP) bila kuwa na ushahidi wa kutosha. "Hauwezi kupeleka faili kwa DPP achukue hatua bila ushahidi wa kutosha. Ndio maana kesi nyingi huishia hapo," alisema. Bw Omae alisema wachunguzi wa tume hulazimika kusafiri hadi maeneo ambako matamshi hayo yalitolewa, kubaini muktadha wake na kutafuta mashahidi walio tayari kutoa taarifa rasmi. Alisema tatizo kubwa ni kwamba Wakenya wengi huwa wepesi kuripoti matamshi yanayowaudhi lakini husita kuwa mashahidi. "Wakenya ni wazuri katika kuripoti na kulalamika lakini wanapotakiwa wawe mashahidi na hata kuweka malalamiko yao kwa maandishi hawataki kwa sababu wanafikiri wataitwa mahakamani," alisema. NCIC imesema imefanikisha hukumu tano huku kesi nyingine tatu zikiwa mahakamani. Hata hivyo, hakuna mwanasiasa aliyepatikana na hatia katika kesi hizo. Malalamiko yaliyohusu mwanaharakati wa haki za binadamu Khelef Khalifa, Mbunge wa Tigania East Mpuru Aburi na chifu mkuu Wilson Kaloi yalikataliwa na DPP kwa sababu ya kukosa ushahidi wa kutosha. Kesi ya mbunge Peter Salasya nayo ilisitishwa baada yake kuomba msamaha. Uchunguzi wa sasa umeibua mjadala kuhusu iwapo taasisi za serikali zinachukua hatua mapema ya kutosha kuzuia matamshi hatari kabla hayajageuka kuwa vurugu. NCIC imekuwa ikichunguza pia matukio ya nyuma tangu uchaguzi wa 2022. Wakati wa uchaguzi mdogo wa Ol Kalou, Mbunge wa Kipipiri Wanjiku Muhia na Bw Gikaria walitozwa faini ya Sh1.5 milioni na Sh2.5 milioni mtawalia na Tume Huru ya Uchaguzi na Mipaka (IEBC) kwa kukiuka kanuni za maadili ya uchaguzi. Huku hayo yakijiri, baadhi ya wanasiasa wamejikuta wakilazimika kuomba msamaha baada ya matamshi yao kuzua hasira. Katibu Mkuu wa UDA Hassan Omar alikabiliwa na wito wa kujiuzulu mwezi Mei baada ya matamshi yake kutafsiriwa na wakosoaji kuwa yalilenga jamii fulani. Baadaye aliomba msamaha. Gavana wa Nyeri Mutahi Kahiga pia aliomba msamaha na kujiuzulu kama naibu mwenyekiti wa Baraza la Magavana baada ya matamshi yake kufuatia kifo cha aliyekuwa Waziri Mkuu Raila Odinga Novemba 2025 kuzua ukosoaji. Wakati huo huo, Bw Duale anaendelea kuchunguzwa kuhusu matamshi aliyotoa katika hafla ya umma eneo la Lafey, Mandera. Waziri huyo amekana kufanya kosa akisema matamshi yake yalipotoshwa na kutolewa nje ya muktadha. Mwakilishi wa Wanawake wa Murang'a Betty Maina pia ameangaziwa na NCIC kutokana na matamshi aliyotoa dhidi ya Bw Gachagua.

read more