T

taifaleo.nation.co.ke

@taifaleo Tue, 18 Aug 2026 11:12:50

Gachagua awasilisha rufaa ya kurasa 121 kupinga kutimuliwa kwake

ALIYEKUWA Naibu Rais Rigathi Gachagua jana aliwasilisha rufaa katika Mahakama ya Rufaa kupinga uamuzi wa Mahakama Kuu uliothibitisha kuondolewa kwake mamlakani na Seneti mnamo 2024. Rufaa hiyo, yenye kurasa 121, inapinga uamuzi wa Juni 8, 2026 uliotolewa na Majaji Eric Ogola, Anthony Mrima na Frida Mugambi. Miongoni mwa hoja kuu ni madai kwamba Mahakama Kuu "ilibadilisha uamuzi wa mwisho wa maandishi na kuufanya kutofautiana na uamuzi uliotolewa hadharani mahakamani." Bw Gachagua anadai vifungu vinne vilivyosomwa baada ya aya za 484, 488, 503 na 508 viliondolewa katika uamuzi wa maandishi licha ya kusomwa hadharani na kupeperushwa moja kwa moja kwenye runinga. "Kwa kubadilisha uamuzi isivyofaa, mahakama imemnyima hoja nzito za mahakama zilizotolewa katika vifungu vilivyosomwa baada ya aya za 484, 488, 503 na 508," akasema. Pia anapinga uamuzi wa Mahakama Kuu wa kuunga mkono kuondolewa kwake licha ya majaji kubaini kuwa Seneti ilikiuka haki zake za kikatiba wakati wa mchakato huo. Majaji walibaini kuwa haki yake ya kusikilizwa na kuchukuliwa hatua za kiutawala ilikiukwa baada ya Seneti kukataa kuahirisha kikao alipougua na kushindwa kukamilisha utetezi wake. Bw Gachagua anasema ukiukaji huo ulipaswa kufanya uamuzi wa Seneti kuwa usiofaa. "Mahakama Kuu ilikosea kimsingi kisheria kwa kushindwa kubaini kwamba uamuzi wa Seneti wa kumuondoa mamlakani ulikuwa batili na usio na nguvu za kisheria," akasema. Anapinga pia msimamo kwamba uamuzi wa Seneti kuhusu kutimuliwa kwake hauwezi kuchunguzwa na mahakama, akisema mahakama zinaweza kuingilia mchakato huo iwapo Katiba imekiukwa. Pia anasema mahakama ilikosea kuzingatia hoja ya uwezekano wa kuwepo kwa Naibu Rais wawili iwapo angewarejeshwa mamlakani, kwani alikuwa amebadilisha ombi lake na hakutaka kurudi ofisini bali alitaka kutimuliwa kwake kubatilishwe na apewe fidia. Pia anapinga mchakato wa Seneti, akisema uchunguzi ulikuwa wa lazima na kamati maalum ilipaswa kuundwa. Ushirikishaji wa umma ni hoja nyingine. Bw Gachagua anasema Seneti haikuwashirikisha wananchi baada ya kupokea ripoti ya Bunge la Kitaifa. Pia anapinga mchakato wa uteuzi na kuidhinishwa kwa Kithure Kindiki kuwa Naibu Rais. Zaidi ya hayo, anasema mahakama ilishindwa kuamua kuhusu haki yake ya kulipwa hela za kustaafu. Anapinga fidia ya Sh50 milioni, akisema haikutosha. Bw Gachagua anaiomba Mahakama ya Rufaa itangaze uamuzi wa Seneti wa Oktoba 17, 2024 kuwa kinyume cha Katiba, batili na usiokuwa na nguvu za kisheria.

read more
T

taifaleo.nation.co.ke

@taifaleo Tue, 18 Aug 2026 10:39:35

MAONI: Walimu waonyeshe mfano wa nidhamu hata wanapotumia mitandao ya kijamii

KANUNI za kuimarisha nidhamu miongoni mwa walimu ni hatua inayofaa, hasa katika enzi hii ambapo mitandao ya kijamii imekuwa sehemu muhimu ya maisha ya kila siku. Mwalimu si mfanyakazi wa kawaida. Yeye ni mlezi, mshauri na kioo cha jamii. Kwa hivyo, mwenendo wake shuleni na nje ya shule unaweza kuwa na athari kubwa kwa wanafunzi na jamii kwa ujumla. Mitandao ya kijamii imeleta fursa kubwa za mawasiliano, kujifunza na kubadilishana mawazo. Lakini pia inaweza kuwa chanzo cha mienendo inayodhalilisha hadhi ya mwalimu. Lugha chafu, matusi, picha zisizofaa, ulevi wa kujionyesha hadharani na matusi dhidi ya watu wengine vinaweza kumfanya mwalimu apoteze heshima anayopaswa kuwa nayo mbele ya wanafunzi na wazazi. Mwalimu anayewafundisha wanafunzi kuhusu heshima, nidhamu na uwajibikaji hawezi kuhubiri maadili hayo darasani halafu akafanya kinyume chake kwenye mitandao. Hata hivyo, kanuni hizo hazipaswi kutumiwa kuwanyamazisha walimu au kuwanyima haki yao ya kutoa maoni. Mwalimu ni raia mwenye haki ya kujieleza. Kinachohitajika ni mipaka ya wazi kati ya uhuru wa kujieleza na tabia inayokiuka maadili ya taaluma. Walimu pia wanapaswa kuelewa kwamba kile wanachoweka mtandaoni kinaweza kubaki huko kwa muda mrefu. Chapisho moja la hasira au picha isiyofaa linaweza kusambaa kwa maelfu ya watu ndani ya dakika chache na hatimaye kuathiri heshima ya mwalimu, shule na hata taaluma nzima. Kwa upande mwingine, mamlaka zinazowasimamia walimu zinapaswa kuhakikisha kanuni hizo zinatumika kwa haki. Nidhamu haimaanishi adhabu kali pekee. Walimu wanahitaji pia kuelimishwa kuhusu matumizi salama na yenye uwajibikaji ya mitandao ya kijamii. Ni muhimu kuwe na mafunzo ya mara kwa mara kuhusu maadili ya taaluma katika mazingira ya kidijitali. Walimu wafundishwe namna ya kulinda faragha yao, wanafunzi na taasisi wanazofanyia kazi. Hatua hiyo ni muhimu kwa sababu jamii inawatazama walimu kama vielelezo. Watoto hujifunza si kutokana na vitabu na masomo pekee, bali pia kutokana na tabia za watu wanaowaongoza. Mwalimu ni kioo cha jamii. Kioo hicho kinapaswa kuonyesha maadili tunayotarajia watoto wetu kuiga.

read more